MNYAMA AUA ZIMBABWE. Andrew Kingamkono, Harare.
MABINGWA wa soka Tanzania Bara Simba wameirarua Lengthens ya Zimbabwe mabao 2-0 katika mechi ya kuwania kombe la Shirikisho la chama cha soka Barani Afrika CAF iliyofanyika kwenye uwanja wa Rufaro,nchini Zimbabwe.
Mpira ulianza kwa kasi ambapo katika dakika ya 3 Lengthens FC 'Happy People' waliwakosa Simba.
Katika kipindi cha kwanza mabeki wa kati wa Simba Joseph Owino na Kelvin Yondani walikuwa wakijichanganya sana na kuonekana kutoelewana,ambapo kuna wakati bado kidogo wasababishe bao ila mshambuliaji wa Lengthens,Uzukamanda alipiga shuti ambalo lilidakwa na kipa wa Simba Juma Kaseja.
Katika dakika ya 32 Simba ilipata bao la kwanza lililofungwa na Mohamed Banka kwa mpira wa adhabu baada ya kupasiwa na Joseph Owino. Mpira huo wa adhabu ulitokea baada ya Ramadhan Chombo kuangushwa nje ya 18.
Simba iliandika bao la pili katika dakika ya 34 ambalo lilifungwa na Mussa Hassan Mgosi kwa kichwa baada ya kuunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Joseph Owino kutoka winga ya kulia.
Joseph Owino alipiga mpira huo wa adhabu baada ya Nico Nyagawa kufanyiwa faulo.
Lengthens ilitawala mchezo kwa muda.lakini Simba walionekana kurudi mchezoni japokuwa Lengthens walionekana kumiliki zaidi soka kwa kucheza soka ya pasi fupi fupi.
Katika dakika ya 44 na 47 Altwell Nyawima wa Lengthens FC alikosa mabao mawili ya wazi.
Mpaka mapumziko Simba ilikuwa ikiongoza kwa mabao 2-0. Lengthens katika kipindi cha kwanza ilikuwa ikipeleka mashambulizi yao katika winga ya kushoto ambapo alikuwepo beki Haruna Shamte aliyechukua nafasi ya Juma Jabu ambaye alikuwa jukwaani akishuhudia pambano,lakini beki Kelvin Yondani alifanya kazi ya ziada kuzuia mashambulizi ya Lengthens.
Kipindi cha pili kilianza ambapo kulikuwa hakuna mabadiliko ya wachezaji kwa pande zote mbili. Lengthens walianza kipindi hicho kwa kasi na walikosa mabao mawili ambapo shuti la Nhamo liligonga mwamba.
Simba ilifanya mabadiliko ambapo iliwatoa Mike Barasa na Nico Nyagawa na nafasi zao kuchukuliwa na Jabil Aziz na Ulimboka Mwakingwe. Pia Lengthens iliwatoa Steven Matsangaise,Nhamo,Mparati na kuwaingiza Mike Mhunsu,Patrick Makuwaza.
Mabadiliko hayo yaliisaidia Lengthens kurudi mchezoni ambapo katika dakika ya 72 bado kidogo Nyawima afumanie nyavu.Pia katika dakika ya 76 Nxawma alikosa bao akiwa na kipa Juma Kaseja.
Simba ilipata Shambulizi la maana katika dakika ya 83,lakini mshambuliaji Mussa Mgosi alipiga shuti ambalo lilipaa juu ya mwamba.
Kiujumla beki ya Simba inastahili pongezi kwa kucheza kwa kujituma na kuzuia kwa hali ya juu.
Katika mechi hiyo mchezaji wa Simba Haruna Shamte alipewa kadi ya njano kwa kumchezea vibaya Dylaan Chiroodza.
Simba ilifanya mabadiliko tena kwa kumtoa Ramadhan Chombo na kumuingiza Jerry Santo.
Mchezo wa Simba dhidi ya Lengthens ulihudhuriwa na mashabiki wachache kwa sababu jana ilikuwa ni siku ya kazi.
Kikosi cha Simba kilikuwa; Juma Kaseja,Haruna Shamte,Salum Kanoni,Kelvin Yondani, Joseph Owino,Mohamed Banka,Nico Nyagawa,Hillary Echesa,Mussa Hassan Mgosi,Mike Baraza na Ramadhan Chombo.
Lengthens:Makuvarara Lovemore, Mteili Richard,Mparati Tawanda,Machoma Casper,Mono Goderey, Bruce Tshuma,Richard Mteki,Patrick Nshamo,Altwell Nyawima,Asmir Ozukakamanda na Tawanda Mparati.
Mbali na mchezo huo, Caps United ya Zimbazwe itacheza na Morroca Swallows kesho wakati mabingwa wa Zimbabwe Gunners wataonyeshana kazi na Al Ahly ya Misri waliowasili hapa juzi.
CHANZO: Mwananchi.
0 comments:
Post a Comment