Sunday, 14 March 2010


Wana-Msimbazi mmeweka rekodi nzuri na inayostahili pongezi.Tunataraji mtatafsiri rekodi hiyo kwa kufanya vema katika michuano ya kimataifa.Penye nia pana njia.
POINTI za Simba sasa zimetosha na imeibuka bingwa wa soka Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mwaka 2009/2010, lakini ikiwa ni mara ya 17 kwa klabu hiyo kutwaa ubingwa huo.

Hatua hiyo inatokana na ushindi wa mabao 2-0 iliyoupata jana dhidi ya Azam kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam katika mchezo wa ligi hiyo uliokuwa mkali na wa kusisimua ambao ni wa raundi ya 20.

Kutokana na matokeo hayo, Simba imefikisha pointi 56 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote katika ligi hiyo, ambapo Yanga iliyofikisha pointi 45 ikishika nafasi ya pili ikishinda michezo yake mitatu iliyosalia itafikisha pointi 54.

Chereko, nderemo na vifijo vya mashabiki wa Simba vilitawala Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam mara baada ya filimbi ya mwisho ya mwamuzi Ibrahim Kidiwa ambayo iliashiria mwisho wa mechi kati yao na Azam.

Baada ya mpira kumalizika wachezaji wa Simba walizunguka uwanja wakiwapungia mikono mashabiki wao, ambao wengi wao walikuwa wamevalia fulana zenye maneno Simba Bingwa 2009/2011, huku wakiwa wanaonekana wenye furaha isiyo kifani baada ya kutwaa ubingwa huo, huku wakiwa na rekodi safi ya kutopeza mechi yoyote kwenye ligi hiyo na ikiwa imetoka sare mara mbili tu kati ya mechi 20 ilizocheza.

Mabao mawili yaliyofungwa moja katika kila kipindi na mshambuliaji Mkenya wa timu hiyo, Mike Barasa ndio yaliyoiwezesha Simba kuwavua rasmi ubingwa watani zao wa jadi, Yanga, huku ikiwa imesaliwa na mechi mbili mkononi ikiwemo ile dhidi ya watani zao hao itakayochezwa Aprili 11 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Bao la kwanza la Simba lilifungwa dakika ya saba kwa kichwa na Barasa ambaye aliunganisha krosi ya Mkenya mwenzie Hillary Echesa na kuwafanya mashabiki wa Simba kushangilia baada ya kuenea kwa maneno ya uzushi kuwa mnajimu mmoja alitabiri Simba ingepoteza mchezo na isingeweza kutwaa ubingwa.

Baada ya bao hilo Simba ambao walionekana kupania, walilisakama lango la Azam na dakika mbili baada ya bao hilo, Ulimboka Mwakingwe alipiga krosi ndani ya eneo la hatari lakini Musa Hassan ‘Mgosi’ akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga alishindwa kumiliki mpira huo, hivyo kupoteza nafasi hiyo. Huku Simba wakionekana kutandaza kandanda safi na kufanya washangiliwe na mashabiki wao waliofurika uwanjani hapo kushuhudia timu yao ikitwaa ubingwa baada ya kuukosa kwa takribani miaka mitatu, walianza kupooza mashambulizi na hivyo kuanza kutoa nafasi kwa Azam ambao walionekana kutawala sehemu ya kiungo kipindi cha kwanza.

Kutokana na udhaifu huo Azam walipeleka mashambulizi kadhaa, langoni mwa Simba na katika dakika 35 washambuliaji John Bocco, Danny Wagaluka walishindwa kupachika bao kufuatia krosi ya Malika Ndeule, baada ya Bocco kuikosa na kipa Juma Kaseja kuuwahi kabla ya kumfikia Wagaluka.

Bocco alikosa bao pale shuti lake alilopiga akiwa kwenye ukingo wa eneo la hatari na kudakwa na Kaseja, dakika mbili baadaye mshambuliaji huyo alijaribu tena shuti kali ambalo lilimtoka Kaseja kabla hajaliwahi na kulidaka tena.

Kipindi cha pili kilianza kwa Azam kufanya mabadiliko ya kuwaingiza Ally Manzi na Mau Ally badala ya Said Sued na Wagaluka.

Mabadiliko ambayo yalionekana kuongeza uhai katika safu ya ushambuliaji ya Azam na kuleta sekeseke kadhaa kwenye safu ya ulinzi ya Simba ambayo ilikuwa ikiongozwa na Kelvin Yondani na Juma Nyosso, kwani Manzi alionekana kumsumbua beki wa kushoto, Juma Jabu.

Simba ilifanya mabadiliko yake ya kwanza dakika ya 55 kwa kumtoa Ulimboka Mwakingwe na nafasi yake kuchukuliwa na Uhuru Selemani na dakika ya 57 nusura Mohamed Banka apachike bao la pili baada ya kupiga shuti kali la adhabu ambalo liligonga mwamba wa juu na kurejea uwanjani huku, kipa Vladimir Niyonkuru akiwa ameshapoteza hesabu, lakini walinzi wake waliokoa.

Dakika ya 60 Azam walijibu shambulio hilo pale Manzi alipomtoka Jabu na kupiga krosi safi ambayo Bocco alichelewa kuinganisha wavuni, dakika mbili baada ya Azam kukosa bao hilo, Uhuru Seleman alitoa pasi ya kubetua kwa Barasa aliyekuwa kwenye eneo la hatari ambaye bila ajizi aliukwamisha mpira wavuni na kuipatia Simba bao la pili.

Yanga iliyokuwa ikitetea ubingwa huo, yenyewe imetwaa kombe hilo mara 21.

CHANZO: Habari Leo.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget