na Mwandishi Wetu
WATANZANIA wapatao milioni 8.4 wanashinda na njaa au kulala njaa ili kukabiliana na ukali wa maisha, utafiti umeonyesha.
Kwa mujibu wa utafiti wa Synovate uliofanyika kati ya Septemba na Desemba 2009, wananchi wanaahirisha milo kwa sababu hali ya kiuchumi ya Watanzania milioni 20 imezidi kuwa mbaya.
Mbali na wale waliopunguza bajeti zao (asilimia 43), na wale walioamua kuacha kula baadhi ya milo kwa siku (asilimia 21), watu milioni 11.2 (wanaowakilishwa na asilimia 28 ya wahojiwa), walisema hawajachukua hatua zozote dhidi ya kuongezeka huko kwa gharama za chakula wakati watu milioni 1.6 (asilimia 4) walisema wamekopa kutoka kwenye benki za biashara na hawajui jinsi ya kurejesha mikopo hiyo.
“Idadi ya wale waliosema kuwa hali zao za kiuchumi zimebakia vile vile ilikuwa ni watu milioni 16.8, ambao ni asilimia 42 ya wahojiwa.
“Ni watu milioni 1.4 sawa na asilimia 4 tu ya waliohojiwa, ndio waliosema maisha yao yameboreka, huku watu wengine milioni 2 sawa na asilimia 5 ya waliohojiwa wakisema hawajui,” alisema meneja huduma wa Taasisi ya Synovate, Jane Meela.
Kwa mujibu wa utafiti huo, idadi ya waliosema hali zao za kiuchumi zimekuwa mbaya zaidi ilikuwa kubwa zaidi kwa upande wa wanawake kuliko wanaume, wakati wanaume kidogo walisema hali zao za kiuchumi zilibakia vile vile.
Kwa kuzingatia kipimo cha maendeleo ya jamii, kisiasa na kiuchumi (SPEC), wananchi milioni 17.2 pia wamelazimika kupunguza matumizi yao ya vitu vya nyumbani kutokana na kupanda kwa gharama za mahitaji ya msingi.
Matokeo hayo yalitolewa na meneja utafiti na mawasiliano wa taasisi hiyo, Abdallah Gunda na meneja huduma, Meela, katika mkutano wao na wanahabari uliofanyika juzi jijini Dar es Salaam.
“Makali ya maisha nchini yamefikia hatua mbaya zaidi tangu utafiti wetu uliopita, na mwenendo wa sasa unatisha,” alisema Meela.
Alisema kinachoonekana ni kuwa watu maskini wameendelea kutokomea kwenye umaskini, huku kukiwa na watu wachache tu wanaoona kuwa hali za maisha yao zimekuwa bora.
Meela alisema serikali inahitaji sera na mikakati iliyojengwa na matokeo ya tafiti kama hizo kufanya gharama za maisha ziwe nafuu kwa kila mtu.
Utafiti huo ulihusisha sampuli nasibu za idadi ya watu 2,000 waliopatikana katika mikoa yote 21 ya Tanzania Bara, na visiwa vya Unguja na Pemba.
Alisema matokeo ya sampuli hizo yalipangwa katika jedwali na kufanyiwa upembuzi uliozingatia makadirio ya idadi ya watu milioni 40 nchi nzima ili kupata takwimu zilizokaririwa katika ripoti hiyo.
Matokeo hayo yanaonekana kuakisi hali halisi yakilinganishwa na mwenendo wa hivi karibuni wa mfumuko wa bei za vyakula.
Takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonyesha kuwa mfumuko wa bei nchini umebaki katika tarakimu mbili.
Hali ilikuwa mbaya zaidi mwaka jana mwezi Agosti, ambapo ulifikia asilimia 18.9, mwezi mmoja tu kabla ya kufanyika kwa utafiti huo wa Synovate.
Kiwango hicho kilishuka hadi kufikia asilimia 17.3 Septemba na kupanda hadi asilimia 18.1 Oktoba, na tangu wakati huo kimekuwa kikishuka na kupanda kati ya asilimia 14.5 na 17 kwa miezi iliyofuatia.
Wachumi wamekuwa wakitumia kigezo hiki kuthibitisha jinsi serikali ya awamu ya nne ilivyoshindwa kuboresha maisha ya mwananchi.
Na wanaharakati wametumia kigezo hiki, na kukithiri kwa ufisadi miongoni mwa vigogo serikalini, kama kielelezo cha Serikali ya Rais Kikwete kushindwa kutimiza ndoto zake za ‘maisha bora kwa kila Mtanzania.’
Naye Gunda alisema tatizo la rushwa na hongo ndilo lililotajwa kuwa sugu kwani linaathiri wengi nchini na lilipewa asilimia 53, likifuatiwa na tatizo la umaskini lililopewa asilimia 42, gharama za vyakula, asilimia 39, uhaba wa chakula na njaa, asilimia 38.
Tatizo la ajira, ukimwi na VVU, maji, kupanda kwa gharama za maisha, afya, umeme, ukame, barabara, elimu, kilimo, kutokuwepo kwa usalama na matumizi ya dawa za kulevya pia vilitajwa kama miongoni mwa matatizo makubwa nchini.
Utafiti huo umebainisha kuwa rushwa na umaskini ni matatizo yanayowaathiri zaidi wanaume kuliko wanawake.
CHANZO: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment