Jumatatu iliyopita,gazeti la Mwananchi lilikuwa na habari yenye kichwa 'DAWA YA UKIMWI YAGUNDULIWA'.Siku mbili baadaye,gazeti hilohilo lilikuwa na habari yenye kichwa 'MWAKYUSA: TUMSHUKURU MUNGU KWA DAWA YA UKIMWI'.Binafsi,niliposoma habari ya kwanza nilipatwa na mshangao kuwa inakuwaje habari nzito kama hiyo isipate uzito mkubwa kwenye vyombo vya habari vya kimataifa.Kama kawaida yangu,unapojitokeza utata kuhusu habari,nika-google 'HIV cure'.Tofauti na ilivyoripotiwa na gazeti hilo la Mwananchi,matokeo ya search yangu hayakukuwa na jibu la uhakika.
Nilishtushwa zaidi na kauli ya Waziri wa Afya,profesa wa utabibu,Davidi Mwakyusa,alivyoingia kwenye mkumbo wa 'kushangilia kupatikana kwa dawa ya ukimwi' pasipo kufanya utafiti wa kutosha.Na mahala rahisi pa kufanya utafiti wa aina hiyo ni mtandaoni.
Na pengine katika hali inayoweza kutafsiriwa kama 'kumpa darasa Profesa Mwakyusa',msomi mwezie Profesa Fred Mhalu wa Chuo Kikuu cha Tiba na Afya Muhimbili,ametoa tahadhari kuhusu habari hiyo ya ugunduzi wa dawa ya ukimwi.Msomi huyo ambaye ni Mkuu wa Idara ya Microbiology na Immunology,na ambaye amekuwa akijihusisha na tafiti kuhusu ugonjwa huo,amebainisha kuwa kilichogundulika ni protein antibody tu,na inabidi kusubiri mpaka chanjo itakayoweza "kutekenya" (stimulate) antibody hiyo itapopatikana,na kwa sasa haiwezekani kusema hatua hiyo itachukua muda gani.
Profesa Mhalu ametahadharisha pia kuwa huko nyuma kulishawahi kuwa na ripoti kama hizo lakini hazijaweza kuzaa matokeo yanayotarajiwa.Hata hivyo,alisema kuwa hatua iliyofikiwa ni ya kutia matumaini kwenye mwelekeo wa kupata tiba kamili japokuwa hawezi kutamka kwa hakika kuwa ufumbuzi wa tatizo hilo umeshapatikana.
Awali,Profesa Mwakyusa alinukuliwa akisema "Kama ni kweli dawa hiyo imepatikana, ni jambo la kumshukuru Mungu kwa kuwa Ukimwi ni ugonjwa ambao umeiathiri sana dunia."Ama kwa hakika usingetarajia kauli ya 'kimtaani' (layman's language) kutoka kwa mtu mbaye licha ya kuwa Waziri mwenye dhamana katika suala la Afya lakini pia ni msomi katika fani ya utabibu.Japo ni vizuri kumshukuru Mungu kwa taarifa za kutia matumaini kama hiyo,lakini watu wenye dhamana na hususan wasomi kwenye taaluma ya utabibu wanatarajiwa kutoa kauli zinazoelemea zaidi kwenye facts badala ya hisia za binafsi.Pengine kabla ya kutoa kauli hiyo iliyoongeza uzito katika habari husika,Waziri Mwakyusa angeweza kufanya 'quick search' kwenye simu (kama sio kompyuta) yake na kupata facts sahihi kisha kuwaeleza Watanzania ukweli kuhusu habari hiyo.
Kwa mujibu wa kiongozi wa utafiti uliopelekea habari hiyo,Dakta Garry Nabel wa Taasisi ya Taifa ya Allergy na Magonjwa ya Kuambukiza ya Marekani,protini zilizogunduliwa,yaani antibodies hizo,zinatumiwa na mfumo wa kinga ya mwili kutambua na kushambilia vimelea vya maradhi kama bakteria na virusi."Nina kuhusu chanjo ya ukimwi kwa sasa kuliko ilivyokuwa miaka 10 iliyopita",alisema mtafiti huyo katika kauli iliyopelekea msisimko wa aina yake sehemu mbalimbali duniani.
Virusi vya ukimwi hushambulia mfumo wa mwili kujikinga na maradhi na hivyo kumwacha mwathirika katika hatari ya maambukizi na maradhi.Tangu virusi hivyo vigunduliwe takriban miaka 30 iliyopita,wanasayansi wamekuwa wakihangaika pasipo mafanikio kupata tiba na kinga ili kudhibiti ukimwi.Inakadiriwa kuwa kufikia mwaka juzi kulikuwa na watu milioni 33 walioambukizwa virusi hivyo hatari.
Wakati dunia kwa ujumla ingetamani tiba ya ugonjwa huo hatari ipatikane hata leo,ni muhimu kwa wenye dhamana ya kuuhabarisha umma kuwa makini wanapotoa taarifa za kitaalamu zinazohitaji ufafanuzi makini ili kuepuka kutoa matumaini yasiyoendana na ukweli.Kwa kifupi,hadi sasa hakuna dawa ya ukimwi.Kilichogundulika ni hizo antobodies,na bado kuna hatua mbalimbali za kitabibu na kitaratibu kabla haijathibitishwa rasmi kuwa tiba au dawa ya ugonjwa huo imepatikana.
Lengo la makala hii sio kuvunja matumaini ya walioanza kuamini kuwa 'dawa ya ukimwi imepatikana' bali ni kutoa ufafanuzi ambao naamini utawasaidia walioathirika kuzingatia ushauri wa kitaalam na kwa sote kwa ujumla kujichunga kwa kuepukana na ngono zembe.
Ingawa waswahili wanasema samaki mmoja akioza basi tenga zima la samaki wawe wabichi au wakavu pia wote watakuwa wameoza.
ReplyDeleteKwa sisi wenye asili wa shughuli za uvuvi katika maji baridi tunauzoefu na haya mambo....
Nadhani sasa watu Baraza la kiswahili la Taifa nategemea watafanya tafiti zingine ili tupate msemo mwingine kwenye serikali hii ya Tanzania ya sasa na mawaziri wake.
Na mashaka na uwezo na maarifa wa hawa mawaziri tena wengine wana elimu za juu kabisa katika vyeti vyao na uzoefu wa kufundisha vyuo vikuu mbalimbali duniani.
Ombi langu wasomi watanzania washiriki katika maendeleo ya kisasa na kisomi ili kutumia maarifa waliojifunza katika tafiti mbalimbali duniani kuifanya Tanzania ipige hatua mbele na siyo kama hivi sasa.
Maoni na matamshi yanayotolewa yanakuwa hayana tofauti na mpiga ramli kwa mganga wa kienyeji.
Tuijenge Tanzania kisasa yenye watu wenye mawzo ya kisasa na maarifa yenye utafiti kamili na tuache kuongea kienyeji na kuiharibu Tanzania yetu tunayoipenda sisi wazalendo.
Na hakika haki itakuja kupatikana kama siyo hivi punde basi siku zijazo. Mungu ibariki Tanzania na watu.Mungu Ibariki Africa.