Wednesday, 28 July 2010

Ni dhahiri kwamba kila Mtanzania mzalendo na mwenye uchungu na nchi yetu anatamani kuona mambo yakibadilika huko nyumbani.Nchi yetu ina takriban miaka 50 tangu ipate uhuru mwaka 1961.Ukiondoa uvamizi wa nduli Idi Amin mwaka 1978-79,nchi yetu imeendelea kuwa na sifa ya kipekee ya amani na utulivu huku tukishuhudia "nyumba za majirani zetu zikiteketea".Chama tawala CCM kimekuwa kikijigamba kuwa amani na utulivu huo ni matokeo ya sera zake nzuri na uongozi uliotukuka.Haihitaji kuwa mwanafunzi wa siasa kama mie kufahamu kuwa amani na utulivu tulionao unasababishwa na uvumilivu wa Watanzania.Na ni uvumilivu huo huo unaowafanya CCM watuone wajinga,watupelekeshe watakavyo na waifilisi nchi yetu huku tukifahamu fika namna ya kuwadhibiti.Imetosha.Uvumilivu una mwisho,na mwisho huo ni sasa.

Na hata hilo suala la amani na utulivu lina utata kinamna flani.Wachambuzi wa siasa wanabainisha kuwa kutokuwa na machafuko au vita si viashiria kamili vya amani na utulivu.Hebu jiulize msomaji mpendwa,wazee wetu wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wana amani gani wakati fedha zao ziliibiwa na wajanja (mafisadi)  katika serikali ya CCM?Je wakulima wanaokopwa na vyama vya ushirika kila unapojiri msimu wa mavuno wana amani gani wakati wanashuhudia namna mavuno yao yanavyorutubisha vitambi vya mafisadi wa vyama vya ushirika?Mabaamedi wana amani gani katika mishahara ya kijungujiko wanayopewa (na inayokatwa kila siku kila glasi au chupa inapovunjika)?Watoto zetu au wadogo zetu wana amani gani wanaposoma kwenye shule zisizo na madawati huku walimu wao wakinyong'onyea kutokana na mazingira duni ya kazi?Na je watumishi wa umma wana amani gani ilhali wanapodai haki zao wanaishia kudharauliwa kuwa kura zao hazihitajiki (as if mishahara yao ni fadhila kwa kumchagua kiongozi)?

Na madereva wa daladala na mabasi ya mikoani wana amani gani ilhali askari wa usalama barabarani wanawakamua kila siku kana kwamba rushwa ni sehemu ya sheria za usalama barabarani?Na huko magerezani kuna Watanzania wangapi wasio na amani kwa vifungo vya kubambikizwa kesi,kushindwa kutoa rushwa kwa polisi au hakimu au uonevu pasipo sababu?Na dada na mabinti zetu wenye sifa stahili za kupata ajira wana amani gani ilhali kila wanapofanya maombi ya kazi wanakumbana na masharti ya "ngono kwanza,kisha ajira"?Na wagonjwa wetu wana amani gani wanapolazwa sakafuni katika wodi za hospitali mbalimbali (na hii ilimtoa machozi Supamodo Naomi Campbell)?

Mtanzania ana amani gani wakati kila siku anashuhudia namna nchi yake inavyozidi kuhujumiwa na mafisadi?Wanaoamini katika utawala wa sheria wana amani gani wanaposhuhudia mtu kama Lowassa anapewa air time kwenye televisheni ya taifa inayoendeshwa kwa fedha za walipa kodi (na mahijiano hayo hayafanyikii gerezani)?Yani fedha za walipa kodi zinatumika kusafisha watuhumiwa wa ufisadi!

Na walalahoi wana amani gani wanaposhuhudia serikali waliyoiweka madarakani,na iliyoahidi maisha bora kwa kila Mtanzania,ikielekeza nguvu kubwa katika kukumbatia mafisadi huku viongozi wa serikali hiyo wakiishi maisha ya kifahari kana kwamba Tanzania ni nchi ya "dunia ya kwanza"?Na wasafiri wanaotegemea huduma za Reli ya Kati au Tazara wana amani gani wakati usafiri wao unategemea kudra za Mwenyezi Mungu ?

Yapo mengi ya kueleza kuhusu namna CCM inavyofanya kila jitihada ya kubomoa hata kile kidogo kilichobaki kwenye "amani na utulivu".Ni dhahiri kuwa chama hiki kimevimbiwa madarakana na hakijali kuona Tanzania ikielekea kwenye korongo lenye kina kirefu.CCM inaweza kufanya kila hila ili ibaki madarakani kama ilivyowazuga Waislamu mwaka 2005 kuwa ingewapatia Mahakama ya Kadhi,lakini baada ya ushindi wa "kishindo" kwenye uchaguzi mkuu uliopita suala hilo limeendelea kuwa ngonjera tu huku akina Msekwa wakisema hili,Pinda akisema lile na Chikawe akiongea vile.Huku ni kuchochea vurugu.

Tanzania haiwezi kupiga hatua katika mfumo wa sasa wa kifisadi ambapo madaraka yanatolewa kwa minajili ya ushkaji huku watawala wakijiona miungu watu wenye uwezo wa kufanya watakayo hata kama yanapelekea kuhatarisha "amani na utulivu" wetu.

It's high time to say enough is enough.Na namna pekee ya kuwaadhibu CCM ni kuwanyima kura katika uchaguzi mkuu ujao.Binafsi,nina imani kubwa na Dokta Wilbroad Slaa,mgombea urais kwa tiketi ya Chadema.Ameonyesha ukomavu wa hali ya juu katika kutetea hali zetu na kupambana kwa dhati dhidi ya ufisadi.Nafasi adimu kama hizi huwa hazijirudii.Tukifanya kosa la kuiacha CCM madarakani hapo Oktoba tutaishia kujilaumu.Nia tunayo,sababu tunazo (tena elfu kidogo) na uwezo tunao (siku ya kupiga kura).Mnaopewa rushwa ili muichague CCM pokeeni kwa vile rushwa hiyo ni fedha mlizoibiwa.Wato rushwa hao hawana uwezo wa kushinikiza muwapigie kura hasa ikizingatiwa kuwa hamkuwaomba wawahonge na wanachowanhonga is in fact fedha zenu wanazowaibia kwa ufisadi.

Inawezekana ukitimiza wajibu wako

1 comment:

  1. Nyongeza Mzee Ughaibuni!

    Hawa CCM na serikali yake wapo tayari kufanya lolote kuhakikisha wanapunguza nguvu ya hoja kutoka kwa wazalendo wa kweli kama hapo siku za zilizopita mtu ambaye alikuwa mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tena kwa muda mrefu hata pia kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya. Sasa huyu Mh Jenerali Ulimwengu alipokuwa anatekeleza shughuli za kizalendo kweli, watu wasiyo wazalendo wa Tanzania wakaanza njama nyingi na kubwa zaidi na la kushangaza kwa kuhamua kumfunga mdomo kwa kumfutia uraia..

    Kimsingi Jenerali ulimwengu ndiye raia na mzalendo wa kweli, na kamwe siyo hao wageni ambao hawana uchungu na nchi yetu.

    ReplyDelete

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget