Tuesday, 20 July 2010

SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete kueleza umma wa Watanzania kwamba ongezeko la magari na kero ya msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam ni dalili ya maisha bora, wanazuoni na wanasiasa nchini wameikosoa kauli hiyo na kuilaani vikali.

Wamesema kauli hiyo ni dalili tosha kwamba CCM imekosa mwelekeo halisi ya maendeleo ya nchi hivyo haistahili kuendelea kutawala kwa kuwa haina dira ya kubali maisha ya Watanzania.

Mhadhiri katika kitivo cha Sayansi ya Siasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bw. Bashiru Ally aliliambia Majira kuwa ni aibu kwa kauli hiyo kutolewa na kiongozi wa nchi aliyebeba dhamana ya taifa zima.

Alisema ongezeko la fedha, majumba ya kifahari kwa watu wachache na foleni za magari jijini Dar es Salaam hakuwezi kuchukuliwa kama kipimo cha maisha bora kwa kuwa hivyo si vigezo vinavyopaswa kutumiwa kupima kiwango cha maendeleo katika nchi yoyote duniani.

Alisema maisha bora na maendeleo yoyote katika nchi yanapaswa kupimwa kwa kuzingatia ongezeko la watu, upatikanaji wa ardhi, siasa safi na uongozi bora mambo ambayo bado ni ya taabu na yanayozua migogoro mikubwa nchini.

"Kauli hii inanikumbusha kauli ya hayati Korimba (Horance), kuwa CCM haina dira wala mwelekeo, huwezi kupima maisha bora ya mwananchi wa Masasi au Kagera kwa kuangalia foleni za magari Dar es Salaam, laiti kama Mwalimu (Nyerere) na Sokoine (Moringe) wangekwepo leo kauli hii ingewapandisha presha," alisema Bw. Bashiru.

Alisema ni vema Rais Kikwete akaangalia uwiano wa ngezeko la foleni hizo na uboreshaji wa miundombinu hususan barabara, shule na mfumko wa bei za bidhaa na thamani ya fedha ambavyo vimekuwa vikiporomoka kwa kasi katika kipindi cha uongozi wake.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bw. Freeman Mbowe, alisema kauli hiyo inaonesha jinsi serikali ya CCM isivyokuwa na jambo la kujivunia kwa wananchi katika kipindi chote cha miaka mitano iliyopita.

Alisema kimsingi msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam inasababishwa na ukosefu wa miundombinu ambayo chimbuko lake ni uongozi mbovu ulioko madarakani.

Alisema kinachotokea Dar es Salaam si kuboreka kwa maisha ya wananchi bali ni ongezeko la tabaka kati ya walionacho na wasio nacho hasa masikini walioko vijijini hali ambayo inasababisha ongezeko la watu mijini wasiokuwa na ajira wala mahali pa kulala.

"Foleni za magari Dar es Salaam si dalili ya maisha bora, na kama ukifanya utafiti utagundua kuwa foleni kubwa ni katika baadhi ya barabara zinazoelekea kwa matajiri wachache ambao baba, mama na watoto kila mmoja ana gari lake, sasa maendeleo ya watu wachache huwezi kuyatumia kupima kiwango cha maisha ya Watanzania wengine," alisema Bw. Mbowe.

Naye Mhadhiri Mwandamizi katika Kitivo cha uchumi na Biashara Chuo Kikuu cha Dar Salaam, Profesa Humphrey Moshi, alisema si sahihi kwa rais wa nchi kupima maisha ya Watanzania wachache wengi kwa kutumia mfano wa watu wachache wenye uwezo wa magari.

Alisema licha ya ukweli kuwa ongezeko la idadi ya watu wanaomiliki magari linaweza kutumika kuonesha ongezeko la kipato kwa wananchi lakini haikuwa sahihi kwa kiongozi wa nchi kupima maisha ya Watanzania kwa kuangalia wenye uwezo wachache walioko Dar es Salaam.

Alisema Dar es Salaam ni mji wa kibiashara wenye viwanda, mashirika na taasisi karibuni zote za serikali ambazo katika shughuli za kawaida zinahitaji usafiri wa magari, hivyo kuna uwezekano kuwa foleni kubwa husababishwa na magari ya taasisi, hizo lakini si mabadiliko ya maisha ya Watanzania.

"Magari mengi si ya watu binafsi, idara nyingi za serikali ziko hapa, kuanzia ikulu, bunge, wizara zote, taasisi binafsi, mashirika ya dini, viwanda na wafanyabiashara mbalimbali ambao ndio wamiliki wa magari, sio wananchi wa kawaida, sasa huwezi kusema kuwepo kwa foleni za magari ya idara hizi ni maisha bora kwa wananchi," alisema Prof. Humpherey.

Alisema maendeleo yanapimwa kwa kuangalia maisha ya jumla si ya mwananchi mmoja mmoja, ikiwa ni pamoja na kuangalia uwezo wa kuzalisha mali wa wananchi, thamani ya fedha, kiwango cha elimu na uimara wa sekta za viwanda na kilimo, na si kuangalia msongamano wa magari yaliyokosa barabara za kupita.

Akihutubia wana CCM na wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam katika mkutano wa kuwatambulisha wagombea urais, mgombea mwenza na Rais wa Tanzania Visiwani katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Rais Kikwete alisema ongezeko kubwa la magari na kusababisha msongamano wa magari ni mijawapo ya dalili za maisha bora.

CHANZO: Majira

5 comments:

  1. Huyu mzee sijawahi kuelewa kauli zake,huwa hajui anawaambia wakina nani na akiwa kama nani au uwezo wake mdogo wa kupambanua mambo?

    ReplyDelete
  2. JK ana very low IQ,poor vision,na ameloose touch na reality. Kweli anafikiri watanzania ni wajinga kiasi hiki. Kauli zake mara kwa mara zinaonyesha mtu aliyelewa madaraka na asiyejali. Hivi kweli chama kikubwa kama hicho bado kinaimani na mtu mwenye thinking capacity ya JK? Nashindwa kulitafakari hili.I am very disappointed with my country. Inakuwaje mtu anakua anasema chochote anachojisikia bila kuwa-sensitive na maisha ya watu. Ni juzijuzi tu alisema miaka mitano ya kwanza ilikua yakujifunza urais maana uraisi hauna chuo. What a cheap shot. Uraisi ni leadership and management of people and resources. As long as you have a good plan and a team to implement hakuna kipya. Kwanini watanzania tunashindwa kuliona hili. Ni afadhali kutokupiga kura kabisa kuliko kutoa kura kwa mtu unayejua is just a "ceremonial leader' Tumechoka na maneno tunataka implementation please. Tuambie kwa takwimu mafanikio yako ya miaka mitano iliyopita hatutaki nyimbo it is ENOUGH!

    ReplyDelete
  3. Kuchanganua mambo kwa kina tunahitajika kupata changamoto ambazo zitaleta na kujenga ubunifu. Kimsingi maarifa yanajengwa na taaluma ambayo kivitendo imetoweka katika maisha ya Mtanzania wa kawaida.

    Na hata hao wenye hayo maarifa(tabaka la kati) wamebweteka na kwa hayo wanayofikiri na kuona kwamba ni mafanikio katika maisha yao binafsi.

    Viongozi waliopo madarakani kama huyu JK wanatambua udhaifu hivyo wanatumia kama kanuni yao wao kuendelea kuwa madarakani..Siasa na maendeleo yatategemea kuamka na kuwa wabunifu kwa watanzania wote.

    Watanzania wataweza kutambua kuelemea kwenye chama kimoja tuu cha kisiasa ndiyo chanzo matatizo yote tunayoona leo hata kuwa na viongozi wababaishaji na bora liende kuanzia ngazi ya mwenyekiti kijiji hadi Rais. Ndiyo itakuwa chachu ya mabadiliko ya kweli katika siasa na maendeleo ya nchi kiuchumi.

    Hivi sasa Tanzania ni ya vyama vingi katika vitabu na Katiba, Akilini mwa watanzania wengi tafsiri ya vyama kwao ni kwamba chama chochote cha siasa nje ya CCM ni waahasi tena wakipewa nchi wataleta vita..Hii ndiyo hali halisi kimtazamo katika masuala ya siasa na mfumo wa vyama vingi. Kura ya mtanzania itaanza kuwa na thamani tuu pale watakapotambua vyama vya siasa katika Tanzania ya leo ni sawa kampuni za simu Vodacom, Tigo, TTCL nk kwamba kupatikani kwa wateja wa simu kunaletwa na tija na ufanisi na siyo Jina la kampuni.

    Hivi sasa Watanzania walio wengi wanachagua na kumpigia Rais kutokana chama siasa na siyo ubora na ubunifu wa mgombea.

    ReplyDelete
  4. Nakubaliana na anon hapo juu na ndio maana utagundua vijana wengi waliochukua fomu zakugombania ubunge wengi wanechukua kwa tiketi ya ccm. Sio kwamba wanaamini sera za ccm ni safi lakini wanafikiri ndio njia rahisi yakushinda.Hii inaonyesha tunavyopenda mambo rahisi nasio yaku-struggle/work hard from the scratch. Tunapenda kutafuniwa alafu tumeze. Kwa urahisi huu sidhani kama Taifa litaendelea. Kila kitu ni ku-copy na ku-paste hamna mtu anafikiria outside the box. Kwakweli inakatisha sana tamaa.Mimi ni mwanamke lakini sioni umuhimu wa viti maalum. Kwanini wanawake wasigombanie kama wengine wanavyogombania kwenye majimbo?? Hii ni karne ya 21 lazima tu-prove tunauwezo wakufikiri nasio kupewa nafasi tu.Tukitafuta wenyewe kwanguvu zetu tutaona umuhimu/value ya jasho letu lakini sio kupewa tu. Ah! Nina wasiwasi bunge linalokuja linaweza kuwa na wabunge wenye uwezo mdogo sana wakufikiri wasiojua hata mikataba mibovu na safi inatofautishwa vipi.Huwezi kukimbilia kuongoza jimbo kama huna leadership/management skills (both for people and resources). Ubunge ni watu na kama unataka ufanisi jimboni itakubidi uwe karibu na watu uwaelewe matatizo yao, ujue research sio unaagiza tu unaletewa fake data unazi-present, ujue kutafuta wawekezaji kwenye jimbo lako,etc hiyo ndio everyday job. Hii ni hatari saana kama kuna watu wanakimbilia ubunge with no plan and vision. Kiongozi ni mzigo nasioni kwanini watu wanaukimbilia kiasi hiki naona maana ya uongozi imepotea Tanzania.

    ReplyDelete
  5. Said is very right, Mimi huwa sijisikii kumsikiliza kwani anaongea kama mtu asiyefahamu jambo lolote,Kwani washauri wake ni kina nani? Kama ni makamba na chiligati unategemea nini? Watanzania tuache utani kama ni meli inaenda mrama, tushikamane na kudai haki zetu bila hofu, Tuache woga na ushabiki wa kijinga.

    ReplyDelete

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget