Wednesday, 7 July 2010


Demokrasia katika jamii isiyojali utawala bora ni sawa na kufukia makaratasi ardhini kwa matarajio ya kuota mmea wenye matunda ya noti.Ni mithili ya kualika timu ya Taifa ya Brazil kwa mabilioni ya shilingi kisha mechi husika ituache na bili kubwa pasipo manufaa yoyote.Hebu tafakari.Mwezi Oktoba Watanzania kwa mamilioni yao watapiga kura kumchagua Rais na Wabunge.Japo shughuli hiyo ni ya siku moja tu,maandalizi yake yanagharimu mabilioni ya shilingi.Wenyewe wanasema ndio gharama ya demokrasia.Lakini baada ya uchaguzi,wengi-kama sio wote-wa tutakaowachagua watasahau kabisa kwanini tumewachagua,huku wakiwa bize kutafuta namna ya kufidia gharama walizotumia kuingia madarakani.

Zamani hizo tuliambiwa kuwa demokrasia ni pamoja na uwepo wa vyama vingi vya siasa.Takriban miongo miwili baadaye Watanzania wameshuhudia namna uwepo wa vyamahivyo vingi vya siasa ulivyoshindwa kulikwamua taifa letu kutoka kwenye lindi la umasikini.Sanasana umasikini umekuwa ukizidi kuongezeka huku wanasiasa wetu wakibadili kauli mbiu kila baada ya muhula (kwa mfano kutoka Ari Mpya,Kasi Mpya na Nguvu Mpya kuwa Ari Zaidi,Kasi Zaidi na Nguvu Zaidi).Tumeshuhudia pia mlolongo wa sera,mikakati,mpingo na vitu kama hivyo,from MKUKUTA to MKURABITA to KILIMO KWANZA.Na kwa mawazo mapya hatujambo,shughuli ipo kwenye utekelezaji.

Siku chache zilizopita nilitundika makala kuhusu utata wa kauli za Waziri wa Sheria na Katiba Mathias Chikawe na zile za Makamu Mwenyekiti wa CCM Pius Msekwa kuhusu suala la uanzishwaji Mahakama ya Kadhi.Wakati Waziri Chikawe aliahidi kuwa mahakama hizo zingeanza kazi mwakani,Msekwa alitamka bayana kuwa suala hilo haliwezekani.Hadi leo hakuna ufafanuzi uliotolewa kuhusu suala hilo ila kilicho bayana ni kuwa CCM imeamua kuachana nalo baada ya kuliingiza kwenye manifesto yake ya Uchaguzi mwaka 2005.Kwa vile sie ni mahiri zaidi wa kuhangaika na mambo kwa mtindo wa zimamoto tunasubiri liwake la kuwaka ndipo tuanze kuhangaika namna ya kudhibiti.Taasisi zenye majukumu ya kuwa proactive (yaani kuazuia majanga kabla hayajatokea) ziko busy zaidi na kuhakikisha CCM inarejea madarakani kwa ushindi wa kishindo badala ya kujishughulisha na jukumu lao la msingi la kulinda na kutetea ustawi wa taifa letu.Kwao,siasa (yaani CCM) ndio nchi na ndio kila kitu.

Majuzi umejitokeza utata mwingine wa kauli kati ya mawaziri wawili waandamizi kuhusu suala la uraia wa nchi mbili (dual citizenship).Na kichekesho ni kwamba tofauti na ule mgongano wa kauli kati ya Chikawe na Msekwa,safari hii mgongano wa kauli za mawaziri hao umejiri ndani ya jengo la Bunge katika kikao kinachoendela cha bajeti ya mwaka 2010/11.Awali,Waziri wa Mambo ya Ndani Lawrence Masha alilieleza Bunge Tukufu kuwa serikali imeamua kuwa huu sio wakati mwafaka kwa suala la uraia wa nchi mbili,na kwamba serikali anaangalia uwezekano wa kuanzisha ukaazi wa kudumu (permanent residency).Waziri Masha alieleza kuwa serikali inaandaa hoja kuhusu suala hilo la permanent recidency kwa minajili ya kuileta bungeni ijadiliwe. "Huu sio wakati mwafaka kuruhusu uraia wa nchi mbili,serikali inaangalia uwezekano wa kuanzisha ukaazi wa kudumu badala ya uraia wa nchi mbili", alisema Masha.

Wakati Masha akisema hivyo,Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe alilieleza Bunge hilohilo kuwa serikali imeridhia suala la uraia wa nchi mbili na kwamba Wizara yake iko kwenye mchakato wa kuwasilisha suala hilo kwenye kikao cha Barza la Mawaziri.Pia Membe alieleza kuwa anafanya mawasiliano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ili kupata baraka zao kutokana na suala hilo kuwa la Muungano.Akihitimisha hoja ya bajeti ya wizara hiyo, kwa mwaka wa fedha 2010/2011, Waziri Membe alisema siyo dhambi, Watanzania kutafuta riziki nje ya nchi na ni haki yao kubaki na uraia wa Tanzania.Alisema wakati umefika kwa Watanzania, kupatiwa haki yao ya msingi kwani licha ya kuwa ni manufaa kwao pia ni manufaa kwa nchi kutokana na fursa ya kuongeza pato la taifa.

Kadhalika,inadaiwa kuwa Waziri Membe aliwaeleza Watanzania waliohudhuria mkutano wa Diaspora jijini London hivi karibuni kwamba suala hilo limeshajadiliwa na baraza la mawaziri na linasubiri kuwasilishwa bungeni ili upitishwe au kupingwa na wabunge.Mimi sikuhudhuria Mkutano huo wa Diaspora kwa vile niliamini ungenipotezea muda wangu tu kwa sababu viongozi wetu ni mahiri sana katika kuahidi mambo mazuri kwenye hadhara,na hujifanya wasikivu sana lakini utekelezaji ni zero,sifuri,zilch!

Ni dhahiri kwamba mmoja kati ya mawaziri hawa anadanganya.Wakati sina la kusema kuhusu kauli ya Waziri Masha,kauli za Waziri Membe huko Bungeni na London zinaleta utata unaoweza kuyumkinisha kuwa kuna urongo wa namna flani.Je kauli ipi ni sahihi kati ya hiyo alotoa London kuwa suala hilo limeshajadiliwa na Baraza la Mawaziri na hiyo ya bungeni kuwa suala hilo bado liko wizarani huku likifanyiwa mchakato wa kulipeleka kwenye Baraza la Mawaziri?

Unajua kwanini mmoja wao anadanganya?Sababu ni kadhaa,lakini kwa ufupi,moja,ni kwa vile mdanganyifu huyo anafahamu bayana kuwa wabunge wanaoelezwa suala hilo wapo bize zaidi kufikiri namna watakavyorudi bungeni baada ya uchaguzi (sambamba na kuwazia posho zao nono za vikao vya bunge) kuliko kumkalia kooni waziri aeleze kinagaubaga.Ndio maana mwanzoni mwa makala hii nilibainisha uselessness ya demokrasia yetu.Tunapoteza mabilioni ya shilingi (sambamba na muda wetu kusikiliza porojo za "mkituchagua tufafanya hiki na kile") kuwachagua watu wa kutuwakilisha bungeni lakini wakishafika huko wanakuwa bize zaidi na maslahi yao binafsi.

Pili,anayedanganya kati ya mawaziri hao anafahamu kuwa aliyemteua hatamwajibisha.Kama kuna mtu alimudu kumzuga Rais kwa kuchomekea ishu kadhaa kwenye muswada wa sheria za gharama za uchaguzi na kisha akasalimika,kwanini basi mdanganyifu huyo katika suala hili la uraia mbili awe na hofu?

Tatu,waziri anayedanganya kati ya hao wawili anafahamu udhaifu wa Watanzania katika kudai haki zao za msingi.Kiongozi anaweza kudanganya waziwazi kwenye umati wa watu lakini bado akaishia kupigiwa makofi na vigeregere.Ule wimbo wa "Ndio Mzee" wa Profesa Jay unawakilisha hali halisi ya namna Watanzania wengi wanavyoridhia kuzugwa na wanasiasa wababaishaji.Hebu angalia namna harakati za kuirejesha tena madarakani CCM zinavyopamba moto huko nyumbani.Kwa mgeni,anaweza kudhani labda chama hicho ni kipya na hakihusiki kabisa na kashfa za ufisadi,kubebana,kubomoa uchumi wetu na madudu mengine chungu mbovu yanayoifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi masikini kabisa duniani licha ya raslimali lukuki iliyojaaliwa kuwa nazo.Binafsi naamini kuwa unyonge huo wa Watanzania umechangiwa sana na siasa za chama kimoja ambapo kiongozi alikuwa mithili ya Mungu-mtu,hakosei,lazima ashangiliwe hata akiongea utumbo,sambamba na suala la kujikomba kwa viongozi kwa matarajio ya kujikwamua kwa namna moja au nyingine.

Na kwa vile vyama vya upinzani vimetuthibitishia kuwa uwezo wao katika kuing'oa CCM madrakani ni kama haupo,basi mazingaombwe kama hayo ya Chikawe na Msekwa,na haya ya sasa kati ya Masha na Membe yataendelea kuwepo kwa muda mrefu sana.Unaweza kuhisi kama nimekata tamaa vile kwa namna ninavyoandika.Hapana,ila safari yetu ni ndefu sana,na tatizo sio urefu tu bali ni kiza kilichotanda kwenye njia yetu ambayo imejaa mashimo kadhaa.Ni sawa na kipofu kumsaka paka mweusi kwenye chumba chenye giza ilhali paka huyo hayumo chumbani humo.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget