Friday, 19 August 2011




Raia Mwema Ughaibuni
Walalahoi Uingereza, sawa na wa Tanzania, ni ‘bomu’
Evarist Chahali
Uskochi
17 Aug 2011
Toleo na 199
  • Lisipoteguliwa na watawala hulipuka

  • Ghasia za Tottenham ni kengele ya uamsho

KATIKA makala ya wiki iliyopita, nilizungumzia vurugu zilizotokea katika kitongoji cha Tottenham, jijini London, hapa Uingereza. Kadhalika nilijaribu kuzihusisha vurugu hizo na mazingira yalivyo sasa huko nyumbani na kutoa wito kwa watawala wetu kufanya kila wawezalo kutatua matatizo yanayowakabili Watanzania ambayo yanaweza kusababisha vurugu kama hizo.
Hata hivyo, wakati naandaa makala hiyo vurugu hizo zilikuwa zimetawala Tottenham pekee. Lakini kwa takriban siku tano tangu zianze, ziliweza kusambaa maeneo mbalimbali ya London na hatimaye kuvuka mipaka hadi miji ya Liverpool, Birmingham, Manchester na mingineyo.
Kwa bahati nzuri sie huku Scotland tumenusurika. Na katika kile kinachoweza kutafsiriwa kama uhusiano wa ‘paka na panya’ kati ya Scotland na England, Waziri Mkuu (First Minister) Alex Salmond, alitahadharisha watu walioziita vurugu hizo ‘za Uingereza’ (UK riots) na kuwakumbusha kuwa hazijaigusa Scotland, Wales au Ireland ya Kaskazini; bali England pekee. Kwa hiyo, Salmond alitaka vurugu hizo ziitwe ‘za England’ (English riots).
Baada ya takriban siku tano zilizoshuhudia uharibifu mkubwa na vifo vya angalau watu watano, hatimaye polisi walifanikiwa kuzizima japokuwa hadi sasa bado hali haijarejea kuwa shwari kabisa.
Zaidi ya watu 1,000 wameshafikishwa mahakamani na wengine kuhukumiwa. Mahakama zinazoendesha kesi dhidi ya washiriki wa vurugu hizo zimelazimika kufanya kazi hadi usiku kukabiliana na msongamano wa watuhumiwa.
Waziri Mkuu wa Uingereza (nzima), David Cameron, alilazimika kukatisha likizo yake ili kutoa tamko na kuendesha mjadala Bungeni kuhusu vurugu hizo. Takriban kila mwanasiasa aliyezungumzia vurugu hizo aliwalaani wahusika na kuhitimisha kuwa hakuna maelezo mengine zaidi ya uhalifu mtupu (sheer criminality).
Licha ya Kamisheni Huru ya Malalamiko dhidi ya Polisi (Independent Police Complaint Commission) kukiri bayana kuwa taarifa za awali kwamba kulikuwa na kurushiana risasi kati ya Mark Duggan (Mwingereza Mweusi aliyeuawa na polisi kwa risasi na hatimaye kusababisha vurugu hizo) na polisi si sahihi (marehemu alikutwa na silaha lakini hakuwafyatulia risasi polisi), ‘makosa’ hayo ya polisi yalifunikwa na shutuma na laana zilizoelekezwa kwa waliohusika kwenye vurugu hizo.
Kimsingi, vurugu hizo zilipoanza katika kitongoji cha Tottenham zilihusisha zaidi Weusi. Na hata ziliposambaa kwenye maeneo mengine ya jiji hilo bado wahusika wengi walikuwa Weusi. Hata hivyo, kadri zilivyosambaa ndivyo tulivyozidi kushuhudia picha kwenye vyombo vya habari zikiwaonyesha Weupe kadhaa wakishiriki kwenye uporaji ulioambatana na vurugu hizo.
Kwa baadhi yetu, licha ya kutopendezwa na vurugu hizo, uwepo wa Weupe ulileta ahueni kidogo; kwani ni siri iliyo wazi kwamba kila baya linalofanywa na asiye Mweupe (Non-Whites) ‘linaongeza shehena ya silaha kwenye ghala la chuki dhidi ya kila asiye Mweupe.’ Mifano ni mingi lakini hapa nitaonyesha machache.
Kwa mfano, huko Marekani ambapo mtikisiko wa uchumi unaisumbua nchi hiyo vilivyo, kuna wanaoamini kuwa tatizo ni rais Mweusi, Barack Obama. Lakini ukweli ni kwamba matatizo ya kiuchumi ya nchi hiyo yalianza zama za mtangulizi wa Obama; yaani ‘Mweupe’ George W. Bush.
Na mfano unaoweza kutoa picha halisi ya double standards (viwango vinavyokinzana) ni tukio la kinyama kabisa la kigaidi lililotokea mwezi uliopita nchini Norway ambapo mhusika, ‘Mweupe’ Anders Behring Breivik, aliwaua kinyama zaidi ya watu 70. Mara baada ya kupatikana kwa habari za kusikitisha kuhusu tukio hilo, wachambuzi walikurupuka na kubashiri kuwa wahusika wangekuwa “Waislamu wenye msimamo mkali.”
Wachambuzi hao wakajitahidi kadri wawezavyo kubainisha sababu mbalimbali zinazowafanya kuamini kuwa kuna uwezekano mkubwa kabisa kuwa wahusika ni “magaidi wa Kiislamu.”
Wakajaribu kuhusisha hasira za Waislamu dhidi ya mchora katuni wa Kidenishi aliyechora kikaragosi cha kumkashifu Mtume Muhammad S.W.A na kusababisha maandamano sehemu mbalimbali duniani. Kwa nini tukio lililotokea Udenishi lisababishe shambulizi ‘la kigaidi’ Norway? Jibu wanalo wachambuzi hao.
Wakajaribu pia kuhusisha uwepo wa majeshi ya nchi za Magharibi huko Afghanistan, na sababu nyingine kadha wa kadha; alimradi kuongeza nguvu kwenye ubashiri wao.
Bahati nzuri, kama wasemavyo Waswahili, Mungu hamfichi mnafiki. Baada ya muda si mrefu ikafahamika kuwa mhusika wa ugaidi huo alikuwa sio tu Mnorway; bali pia ni Mweupe, na tena ni muumini wa Ukristo wenye mrengo mkali (Christian Fundamentalism) na mfuasi wa siasa za mrengo mkali wa kulia (far-right politics).
Pamoja na majonzi yaliyowakumba wengi kutokana na mauaji hayo ya watu wasio na hatia, lakini taarifa kwamba mhusika hakuwa Muislamu zilileta ahueni kubwa.
Lakini kama ilivyo katika matukio mengine ya kigaidi yaliyofanywa na Weupe, ukajitokeza ‘utetezi’ kuwa Breivik (muuaji) “alikuwa ni chizi tu, na wala hakusukumwa na Ukristo wake wala itikadi yake ya siasa za chuki dhidi ya wageni na Waislamu.”
Licha ya gaidi huyo kuchapisha mtandaoni ‘ilani’ yake yenye kurasa 1,500 (siku chache kabla ya mashambulizi yake ya kigaidi) ambapo alibainisha chuki aliyonayo dhidi ya wageni na Waislamu na kuweka wazi kuwa ‘angefanya kitu fulani kikubwa kuleta ufumbuzi’, bado watetezi wake wameendelea kumtenganisha na siasa za mrengo mkali wa kulia na Ukristo wa msimamo mkali.
Tukirejea kwenye vurugu za Uingereza, tayari dalili zimeanza kujitokeza kuwa wa ubaguzi wa rangi watafanya kila wawezalo kumhusisha mtu Mweusi na vurugu hizo.
Ni kweli kuwa vurugu zilichipuka kutoka katika maandamano ya amani ya baadhi ya watu kwenye Jumuiya ya Weusi katika baadhi ya vitongoji vya London. Lakini kila aliyeshuhudia vurugu hizo zikipamba moto aliona wahusika wa rangi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Weupe.
Majuzi, mwanahistoria maarufu wa hapa, David Starkey, aliwachefua watu wengi alipodai kuwa vurugu hizo ni matokeo ya ‘Weupe kugeuka Weusi.’ Kimsingi, hoja yake ni kwamba vurugu ni kasumba ya mtu Mweusi, na Weupe wanaojihusisha na vurugu ni matokeo ya ‘maambukizo’ ya kasumba hiyo kutokana na mwingiliano wa kijamii kati ya Weusi na Weupe. Inachefua!
Kwa upande mwingine, ‘majibu’ ya watawala wa hapa wakiongozwa na Waziri Mkuu Cameron yanaonekana kuelemea zaidi kwenye kukabiliana na matokeo badala ya chanzo. Cameron amekuwa akizungumza kwa ukali dhidi ya ‘wahalifu’ waliosababisha vurugu hizo; huku akinuia kupambana nao kwa nguvu zote.
Lakini Profesa wa Historia ya Wakati Huu (Modern History), Robert Gildea wa Chuo Kikuu cha Oxford anabainisha kuwa “wanasiasa na vyombo vya habari wameongoza msafara wa kulaani walioshiriki vurugu kama wahalifu, wendawazimu na wasio na maadili. Hii ni lugha ya matabaka tawala yanapokabiliwa na vurugu za kijamii, kuwaharamisha wanaonyanyaswa kama wahalifu wa anasa dhidi ya jamii yenye amani, lengo likiwa kuwaadhibu wanyanyaswa hao na kuwatenga zaidi.
Cameron na Wahafidhina wenzake wana kila sababu ya kuwabebesha lawama ‘wahalifu’ hao; kwani baadhi ya wachambuzi wanazihusisha vurugu hizo na hatua ya serikali kubana matumizi kutokana na mtikisiko wa uchumi wa dunia, ambapo wahanga wakubwa wameendelea kuwa tabaka la walalahoi.
Kwa kuaminisha umma kuwa vurugu hizo ni uhalifu tu, Cameron na serikali yake atakuwa amefanikiwa kuepusha lawama dhidi ya hatua zinazochukuliwa na serikali yake kubana matumizi na madhara yake kwa jamii.
Kadhalika, kwa bahati mbaya au makusudi watawala wameamua kufumbia macho tatizo la ubaguzi wa rangi ambalo ndio kilio kikubwa cha jamii za Wasio Weupe, na kwa wengi ni sababu kuu ya kuibuka kwa vurugu hizo.
Vilevile, uwezekano kwamba baadhi ya walalahoi wa Uingereza wanaona kama wamesahauliwa na tabaka tawala, na hivyo kusubiri kwa hamu fursa za kuonyesha hasira zao, pia unaelekea kupuuzwa.
Kama nilivyoeleza wiki iliyopita, kuna mengi ambayo watawala wetu huko nyumbani wanaweza kujifunza kutoka kwenye vurugu hizi na jinsi watawala walivyozishughulikia.
Historia inatufundisha kuwa amani inayotawala licha ya uwepo wa lindi la ubaguzi, ukandamizwaji na umasikini, ni sawa na bomu la muda linalosubiri tu wakati lilipuke. Kama tabaka tawala Uingereza litapuuzia vyanzo halisi vya vurugu hizo (ubaguzi, umasikini, nk), basi, ni suala la muda tu kabla hatujashuhudia vurugu nyingine.
Katika mtizamo huo huo, iwapo watawala wetu huko nyumbani wataendelea kuamini katika amani ya kukosekana vurugu; ilhali kuna mamilioni ya Watanzania wasio na amani matumboni na mifukoni mwao (kutokana na umasikini), basi, nasi tunaweza kujikuta katika hali mbaya kama hii iliyojiri hapa.
Tunaweza kusema ‘Mungu aepushie mbali’, lakini tukumbuke kuwa mara nyingi Mungu huwasaidia wale wanaojisaidia wenyewe kwanza.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget