Thursday, 4 August 2011





Raia Mwema Ughaibuni
Spika wetu na wauchapao usingizi bungeni!
Evarist Chahali
Uskochi
3 Aug 2011
Toleo na 197
MATUKIO ya kutia aibu yanayozidi kutokea katika kikao kinachoendelea cha Bunge la Bajeti huko Dodoma yanatoa picha moja ya msingi kuwa Spika Anne Makinda anaelekea kushindwa kumudu wajibu wake.
Haihitaji kuwa mchambuzi mahiri wa siasa kutambua hilo. Japo tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi Bunge letu limeshindwa kumudu uwepo wa wabunge wa vyama vya Upinzani, lakini kwa jinsi hali ilivyo sasa; chombo hicho muhimu kwa taifa kimegeuka kuwa uwanja wa vurugu.
Ninamshutumu Spika Makinda kwa sababu tangu apate wadhifa huo, amekuwa akijitahidi kadri awezavyo kuendesha Bunge kibabe; huku akitaka kuuthibitishia umma kuwa anakimudu kiti cha uspika ipaswavyo.
Lakini inawezekana kabisa kuwa chanzo cha matatizo yanayozidi kushamiri Bungeni ni madaraka makubwa anayopewa Spika dhidi ya wabunge. Sio siri kwamba madaraka ya Spika yanampa nguvu kubwa mno ndani ya chombo hicho cha kutunga sheria; huku kukiwa hakuna namna nzuri ya mwafaka ya kumdhibiti.
Kibaya zaidi, kwa makusudi, chama tawala kimeshikilia msimamo wa kuwa na Spika anayetoka moja ya vyama vyenye wabunge bungeni. Busara nyepesi tu inaweza kueleza kuwa katika mazingira ya uchanga wetu kwenye siasa za vyama vingi, Spika lazima atapendelea chama anachotoka.
Tukubali tusikubali, upendeleo ni moja ya vikwazo vikubwa vya maendeleo sio ya Tanzania pekee; bali sehemu kubwa ya nchi za Dunia ya Tatu. Ukimpa mtu madaraka pasipo kutengeneza mazingira bora ya kumdhibiti kuyatumia madaraka hayo isivyofaa, moja ya mambo ya mwanzo kabisa yanayoweza kutokea ni upendeleo.
Na laiti mtu huyo akitambua kuwa ana uhuru wa kufanya apendavyo, basi, atafanya upendeleo wa waziwazi akijua fika kuwa kufanya hivyo hakutoathiri nafasi yake.
Ni rahisi kuhitimisha kuwa Spika Makinda kazi inamshinda iwapo hatutorejea nyuma kidogo na kuangalia utendaji kazi wa waliomtangulia. Lakini kumbukumbu ndogo tu inaweza kutupa mwanga kuwa vitendo vya maspika wote baada ya kuruhusiwa mfumo wa vyama vingi, vimekuwa sio tu vya kidikteta dhidi ya wabunge wa vyama vya Upinzani; bali pia vinaweza kabisa kutafsiriwa kuwa matumizi mabaya ya nafasi hiyo muhimu.
Jingine ambalo linaweza kupoteza kabisa sio tu heshima ya nafasi ya cheo cha Spika bali pia umuhimu mzima wa kuwa na Bunge, ni mtindo wa ku-kasimu madaraka ya kuongoza vikao vya bunge kwa wabunge mbalimbali.
Hilo lisingekuwa tatizo laiti wabunge wote tulionao wangekuwa wa ina moja; yaani wanatambua kwa nini wanalipwa mamilioni ya shilingi kila mwezi kuwatumikia Watanzania.
Lakini sote tunajua kwamba asilimia kubwa tu ya wabunge wetu ni watu wasiojali kabisa jukumu la kuwatumikia wananchi waliowachagua kuwa wabunge, na badala yake wanaendekeza maslahi binafsi; huku picha zikiwaonyesha baadhi yao wakichapa usingizi kwenye vikao.
Na suala hilo la wabunge kulala linaweza kuibua mjadala mwingine kwenye maeneo mawili ya msingi. Kwanza, hivi ni haki kweli kwa mbunge kulipwa mamilioni ya shilingi kama posho; kisha akaishia kulala bungeni? Hivi huo kama sio ukupe ni nini?
Huo si uungwana hata kidogo, kwa sababu wakati mbunge anakoroma bungeni na kulipwa fedha kibao, walalahoi huko mitaani wanadamka alfajiri kusaka fedha ambazo kila kukicha zinazidi kuwa ngumu kupatikana kutokana na hali ngumu ya maisha.
Pili, kama maamuzi ya kuwatimua wabunge yanazingatia haki, kwanini basi wabunge wanaolala bungeni nao wasikumbane na “hasira za Spika” kwa kutolewa nje? Japo kusinzia au kulala si kosa, lakini katika mazingira ya kawaida tu mtumishi anayelala kazini anapaswa kuadhibiwa.
Jingine ambalo mara nyingi hujitokeza nje ya bunge, ni tabia za baadhi ya wabunge baada ya vikao vya chombo hicho kinachopaswa kuwa kitukufu kutokana na dhamana yake kwa umma.
Unaweza kudhani huu ni uzushi kwa vile hakuna chombo cha habari kinachoweza kuthubutu kuripoti hili, lakini ukweli ni kwamba tabia za baadhi ya wabunge wetu nyakati za jioni au wakati wa mapumziko ya mwisho wa wiki sio tu hayaendani na nyadhifa zao; bali pia zinakinzana na wajibu walionao kwenye familia zao.
Sote tunafahamu kwanini akina dada wanaofanya biashara za kuuza miili yao hukimbilia Dodoma kila kunapokuwa na vikao vya bunge. Jibu ni kwamba huo ni msimu wa ‘kuchuma’. Hivi kweli tunawalipa watu hawa mamilioni ya shilingi kwa ajili ya kufanya mambo kinyume na maadili?
Unaweza kutetea kuwa hiyo ni tabia ya mtu binafsi, lakini hoja hiyo inakosa uzito kutokana na ukweli kwamba, kwanza watu hao binafsi wanatumia fedha za walipakodi kufanya anasa zisizostahili, na pili, anasa hizo zinaweza kabisa kuathiri uwezo wao wa kutumikia umma kwa uadilifu.
Unadhani Mheshimiwa mbunge mwenye miadi na “dada poa” anaweza kweli kuelekeza akili yake kutuliza maswali ya msingi kuhusu matatizo yanayowakabili wapigakura wake?
Hili linaweza kuonekana kama tatizo dogo, lakini lina uzito mkubwa; kwani mtu asiye mwadilifu kwa familia yake hawezi kuwa mwadilifu kwa wapiga kura wake au taifa kwa ujumla.
Uhuni wa baadhi ya wabunge wetu umevuka mipaka hadi kufikia hatua ya kumfanya Waziri Mkuu kama mtu wa kumtania. Sikuamini macho yangu niliposoma habari kwamba baadhi ya wabunge wanafoji sahihi ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuandika vimemo feki kwamba mbunge fulani anahitajiwa kukutana na Pinda wakati si kweli.
Taarifa zilizopo ni kwamba mmoja wa wabunge wenye tabia hiyo ya kitoto ameshafahamika, lakini katika kuashiria kuwa bunge hili limekithiri mizaha, hakuna hatua itakayochukuliwa dhidi ya mbunge huyo. Kwa lugha nyingine ni sawa na kuhalalisha upuuzi aliofanya mbunge huyo.
Kuna picha kubwa zaidi kuhusu mapungufu ya bunge letu ambalo katika msimu uliopita lilipata kujigamba na kutunga kitabu chenye jina “Bunge Lenye Meno” (nami nikaandika makala bloguni kwangu nikaliita “Bunge Lenye Meno ya Plastiki”).
Wingi wa wabunge wa CCM ndani ya Bunge hilo umeshindwa kabisa kumsaidia Mtanzania wa kawaida, kwa sababu, kwa CCM na viongozi wake (pamoja na wabunge), maslahi ya chama yana umuhimu mkubwa zaidi kuliko maslahi ya nchi.
Kila mara tunashuhudia wingi wa wabunge wa CCM unavyosababisha sheria mbovu kupita baada ya wabunge hao “kupewa somo la kuwekana sawa.”
Japo tunaweza kujidanganya kuwa demokrasia inakua kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wabunge wa vyama vya Upinzani, ukweli unabaki kuwa tangu vyama vingi viruhusiwe; bunge letu limeendelea kuwa la chama kimoja. Hapa ninamaanisha kuwa wingi wa wabunge wa chama tawala unafunika kabisa uwezekano wa uwepo wa wapinzani kuleta mabadiliko yanayotarajiwa.
Kulaumu tu bila kutoa ushauri hakuwezi kusaidia kutatua tatizo lililopo. Spika Makinda na wasaidizi wake wanapaswa kutambua kuwa kuwatimua nje ya bunge wabunge wa CHADEMA na wengine wa vyama vya Upinzani pekee kunatoa picha moja tu ya uonevu kwa upande mmoja na upendeleo kwa upande mwingine.
Lakini hilo si la msingi zaidi kulinganisha na ukweli kwamba kuwatimua wabunge kwa “makosa” yanayoweza kurekebishika kwa maonyo tu kuna madhara makubwa kwa wapigakura wanaowakilishwa na wabunge hao.
Adhabu kwa mbunge ni adhabu kwa maelfu kama sio malaki ya wapiga kura wanaowakilishwa na mbunge husika. Spika anaweza kujitetea kwamba hawezi kulea tabia mbovu bungeni. Sasa iweje tabia hiyo mbaya iwe ni kwa wabunge wa Upinzani pekee?
Vipi kuhusu baadhi ya wabunge wa CCM tunaowaona kwenye picha wakiwa wamelala; huku bunge linaendelea? Na vipi kuhusu baadhi ya wabunge watoro wasiohudhuria vikao wakati tayari wameshachota malipo ya posho zao?
Nimalizie kwa kusisitiza kuwa Tanzania yetu ni muhimu kuliko maslahi ya mtu au chama binafsi. Kila mbunge, ikiwa ni pamoja na Spika, ni waajiriwa wa Watanzania. Wananchi ndio wanaowalipa mishahara yao monono na posho zao zisizoendana kabisa na umasikini wetu. Ni dhahiri wananchi hawaridhishwi na mwenendo huu wa sasa wa bunge letu.

1 comment:

  1. Good stuff!! hata wanaolala bungeni pia wafukuzwe kama sio kuonywa!! Na picha zinaonyesha waliolala wote ni wa chama changu (msiniulize chama gani).Nasikitika sana kwa hili!

    ReplyDelete

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget