Twajifunza nini na vurugu hizi za Tottenham, London?
Uskochi
10 Aug 2011
Toleo na 198
WIKI iliyopita nilibahatika kuwasiliana na mtu ninayeamini (japo si kwa asilimia 100) kuwa ni Rais Kikwete kwenye mtandao wa twitter, lakini kabla sijaeleza alichonijibu, imenipendeza kuanza na suala lililoteka vyombo vya habari vya Uingereza mwishoni mwa wiki; yaani vurugu zilizochochewa na kitendo cha polisi kumuua kijana mmoja mwenye asili ya Afrika jijini London.
Muda huu ninapoandika makala hii kuna vurugu kubwa zinazoendelea kwenye kitongoji cha Tottenham, Kaskazini mwa jiji la London hapa Uingereza. Eneo hili linaweza kufahamika kwa wapenzi wa soka huko nyumbani kwani ni makazi ya klabu maarufu inayoshiriki Ligi Kuu ya hapa, Tottenham Hotspurs.
Vurugu hizo ambazo zimeshasababisha uharibifu mkubwa wa mali; huku maduka kadhaa yakiporwa na magari na makazi yakichomwa moto, zimetokana na tukio lililojiri Alhamisi iliyopita ambapo kijana mmoja Mwingereza mweusi, Mark Duggan, aliuawa kwa kupigwa risasi na polisi.
Hadi sasa zaidi ya polisi 26 wameshajeruhiwa na zaidi ya watu 40 wametiwa mbaroni. Taarifa za vyombo vya habari zinaonyesha uwezekano wa vurugu hizo kuendelea zaidi; hasa kwa kuzingatia ukweli kuwa kuna mahusiano duni kati ya mamlaka kwa jumla; hususan polisi na wakazi wa eneo hilo ambalo wengi ni weusi; yaani ni Waafrika au wenye asili ya Afrika.
Vurugu hizi za sasa zinarejesha kumbukumbu ya zile zilizotokea mwaka 1985 katika eneo la Broadwater Farm katika kitongoji hicho hicho cha Tottenham. Kama ilivyo sasa, vurugu za mwaka huo zilichangiwa kwa kiasi kikubwa na mahusiano mabovu kati ya askari polisi ambao wengi wao ni Wazungu na vijana Weusi wa eneo hilo. Lakini chanzo halisi kilikuwa vifo vya Weusi wawili vilivyosababishwa na polisi.
Wakati takriban kila anayezungumzia vurugu hizi za sasa analaani uharibifu unaoendelea kufanyika, mamlaka husika zimekuwa zikilaumiwa kwa kile kinachotafsiriwa kama kupuuzia matatizo yanayowakabili wakazi wa eneo hilo. Kadhalika, kama ilivyo kwenye matukio mengi kati ya polisi na jamii ya Weusi, suala la ubaguzi wa rangi limejitokeza tena ambapo polisi wanaotuhumiwa kuwanyanyasa na kuwabagua wakazi Weusi wa eneo hilo.
Kama ambavyo Jeshi la polisi huko nyumbani linavyolaumiwa kwa kuendekeza rushwa na unyanyasaji, kwa hapa polisi wanalaumiwa sana kwa kile kinachotafsiriwa kama ubaguzi wa rangi uliokubuhu.
Takwimu zinaonyesha kuwa jijini London, uwezekano wa Mweusi kusimamishwa na kupekuliwa na polisi ni mara nane zaidi ya Mweupe. Kwa bahati mbaya, kiwango cha uhalifu miongoni mwa jamii za Weusi nacho ni kikubwa mara kadhaa ya kile cha watu Weupe.
Ukiweka pembeni takwimu na matukio mbalimbali, ukweli unabaki kuwa jamii za watu Weusi katika maeneo mengi ya nchi hii zinakabiliwa na matatizo mengi ambayo kwa wengine yanawapa sababu ya kujihusisha na uhalifu au vitendo vingine vya uvunjifu wa sheria.
Moja ya matatizo yanayoisumbua London ni magenge ya uhalifu ambapo wengi wa wanaojihusisha na magenge hayo ni Weusi. Katika kile kinachoweza kuelezwa kama mzunguko hatari (vicious circle), kushamiri kwa uhalifu miongoni mwa jamii za Weusi kunasababisha vijana wengi kutembea na silaha kama sehemu ya kujihami. Na hilo linachangia matumizi ya silaha hizo katika vurugu na uhalifu.
Wachambuzi wengi wanaeleza kuwa kinachotokea Tottenham ni ishara tu ya hali inavyoweza kutokea maeneo mengine ya Uingereza; huku wakinyooshea kidole umasikini miongoni mwa jamii za Wasio Weupe (Non-Whites) kama kichocheo kikuu cha matatizo hayo.
Pengine katika kuelezea tukio hili inaweza kuwa mwafaka kuelezea kile ambacho pengine wengi huko nyumbani hawakifahamu kuhusu hali halisi ya maisha ya huku Ughaibuni.
Kwa hakika, moja ya matatizo makubwa yanayowakabili watu wanaotoka katika makundi madogo ya jamii (kwa mfano Weusi) ni ubaguzi (wa rangi na katika nyanja nyingine za maisha). Kubwa zaidi ni ubaguzi wa rangi.
Ukiangalia picha zinazoonyeshwa kwenye runinga na vyombo vingine vya habari hapa Uingereza, unaweza kudhani maisha huku Ughaibuni ni “tambarare.” Kinachosaidia madhila ya huku kutofahamika sana huko nyumbani ni tabia ya baadhi ya wenzetu tunaoishi nao huku kujaribu kadri wawezavyo “kuchora picha ya maisha katika nchi ya maziwa na asali” (land of milk and honey).
Wengi wao wanaofanya hivyo kwa minajili tu ya kujikweza kwa wenzao waliopo huko nyumbani. Ndio maana baadhi ya wenzetu wapo bize kuweka picha kwenye intanetikuonyesha “jinsi wanavyofaidi maisha”. Naomba nieleweke kuwa simaanishi kuwa maisha ya huku si mazuri (kutegemea uzuri huo unaelemea suala gani).
Kuna mengi tu yanayoweza kumfanya mtu asahau kabisa adha zinazoikabili sehemu yake ya asili ya kuzaliwa. Licha ya kuwepo tatizo la ubaguzi, mamlaka na taasisi mbalimbali zinafanya jitihada kubwa kuenzi haki za binadamu sambamba na kudumisha utawala bora.
Ni rahisi kulaumu kuhusu ubaguzi wa rangi, lakini ukweli ni kwamba serikali za nchi nyingi za Magharibi (kwa mfano) zinafanya jitihada kubwa kutatua matatizo ya wakazi wa nchi husika bila kujali asili yao.
Kwa ujumla, matatizo mengi yanasababishwa zaidi na migongano ya kijamii japokuwa kiundani migongano hiyo inaweza kuwa na vyanzo vyake kwenye maeneo ya siasa na uchumi. Kadhalika, mgongano wa kiutamaduni ni miongoni mwa vyanzo vya maelewano duni; hususan katika maeneo yenye mjumuiko wa watu kutoka tamaduni mbalimbali.
Kuna mambo kadhaa ya msingi tunayoweza kujifunza kutokana na vurugu hizi zinazoendelea kwenye kitongoji cha Tottenham. La kwanza ni jinsi ubaguzi unavyoweza kuzaa migongano katika jamii. Kwa bahati mbaya (au makusudi kabisa) watawala wetu huko nyumbani hawaonekani kuguswa na ubaguzi unaozidi kushamiri katika jamii yetu.
Mifano ni mingi, lakini rahisi ni pale kibaka anavyosota rumande kwa maelezo kuwa uchunguzi wa kesi yake haujakamilika; huku kigogo aliyekusanya rushwa kwenye Idara anazoongoza akipewa likizo ya kuchunguzwa (huku akiendelea kupokea mshahara na marupurupu yake lukuki).
Au kwa nini iwe rahisi kuwatupa rumande wezi wa kuku, lakini majambazi waliofanikisha wizi wa EPA kwa kutumia kampuni hewa ya Kagoda wakiendelea kuheshimiwa; achilia mbali kutochukuliwa hatua?
Na majuzi nilibahatika kumuuliza Rais Jakaya Kikwete swali hili kupitia mtandao waTwitter ambapo naye ni mshiriki akitumia jina@jmkikwete . Swali langu kwake lilikuwa hili: “@jmkikwete mheshimiwa hivi kuna uwezekano wa sie wananchi kufahamishwa mmiliki wa Kagoda kabla hujamaliza muhula wako wa pili 2015?”
Baada ya muda naye akanijibu, “@Chahali ni jambo lililo wazi kwamba kipo chombo tunachokiamini chenye kusimamia suala hili na mengine ya aina hiyo kwa taifa letu.”
Binafsi, sikuridhishwa na majibu ya Rais na nikamfahamisha bayana kwa Tweet hii kwake, “@jmkikwete hali halisi mtaani ni tofauti na mtizamo wenu watawala.Ufisadi unashamiri,watawala mnatuhadaa kuna vyombo tunavyoviamini.” Hakunijibu!
Hatuombei yanayotokea Tottenham muda huu yatokee huko nyumbani lakini tutakuwa tunajidanganya kuendelea kuimba ngonjera za “Amani na utulivu” huku mamilioni ya Watanzania wakiendelea kuishi kwa umasikini wa kutupwa na watawala wao wakiishi katika utajiri mkubwa.Utajiri wa halali si tatizo lakini sote tunajua kuwa utajiri wa wengi wa viongozi wengi ni matokeo ya wizi wa fedha za umma.
Lakini inakera zaidi kuona wakati taasisi zinazopewa mabilioni ya fedha kuutumikia umma kwa uadilifu zikiboronga, viongozi wenye mamlaka ya kuzikemea au kurekebisha mwenendo wao wanataka kutuaminisha kuwa taasisi hizo zinaaminika na zinatekeleza majukumu yake ipasavyo.
Wakati moja ya matatizo yanayoisumbua Uingereza (na kupelekea vurugu kama hizi za Tottenham) ni ubaguzi wa rangi, huko nyumbani tunakabiliwa na ubaguzi mbaya zaidi ambapo japo takriban sote tuna asili moja na tunahusiana kwa karibu, kuna wenzetu wanaotumia dhamana tuliyowapa kutuongoza kutunyanyasa na kutubagua kwa misingi ya wenye nacho dhidi ya wasio nacho.
Watawala wanaweza kuendelea “kutoa likizo kwa watoa rushwa ili wachunguzwe”, kuacha watuhumiwa wa ufisadi wajiuzulu kwa heshima (huku wakipongezwa kwa uongozi wao uliotukuka), kuwaandama wazalendo wanaoibua kashfa zinazolitafuna taifa letu, kuendelea kuzienzi kampuni za kijambazi kama Kagoda kwa kutowataja wamiliki wake, na vitendo vingine vinavyochefua. Japo hatuombei, lakini kuna siku wanyonge hawa wanaopuuzwa watasema inatosha. Mnyonge hana cha kupoteza zaidi ya nira aliyotundikwa na wanyanyasaji.
Badala ya kuendeleza ngonjera za “amani na utulivu” ni muhimu kwa watawala wetu kuanza kufanyia kazi vilio vya wanaowatawala. Tusipoziba ufa tutajenga ukuta.
0 comments:
Post a Comment