Monday, 1 August 2011


Idd Simba aitabiria kifo CCM

• AKERWA NA MALUMBANO NDANI YA BUNGE

na Waandishi wetu

MWANASIASA mkongwe nchini, Idd Simba, amekitabiria kifo Chama cha Mapinduzi (CCM) endapo hakitachukua hatua za haraka kudhibiti makundi yaliyo ndani yake ambayo mengi yanatokana na baadhi wanachama kuanza mapema mbio za kukimbilia Ikulu wakitaka urais.

Idd Simba, mwenyekiti wa baraza la wazee wa mkoa wa Dar es Salaam alisema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumaliza kufungua semina ya maimamu na wanazuoni wa Kiislamu, iliyofanyika katika hoteli ya Starlight, Dar es Salaam.

Alisema makundi yaliyojengeka ndani ya CCM yamesababisha chama hicho kupoteza kuaminika na wananchi hali ambayo inahatarisha amani nchini.

Alisema kutokana na hali hiyo moja ya mkakati wa kwanza wa baraza la wazee wa mkoa wa Dar es Salaam ni kuhakikisha linadhibiti hali hiyo ili kuweka mazingira mazuri ndani ya CCM katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Igunga na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Pamoja na mambo mengine, aliwaonya wanachama wanaojiundia makundi ya mtandao kwa kuelekeza nguvu zao za kuelekea Ikulu badala ya kukisaidia chama kuwa imara mbele ya wananchi.

“Kupoteza mwelekeo kwa chama chetu kunatokana na makundi ya watu ambao wana nia ya kukimbilia Ikulu na hali hii sisi wazee wa mkoa wa Dar es Salaam kwa kushirikiana na wenzetu nchi nzima tumejipanga kuthibiti hali hii.

“Kila anayesema hivi sasa anamtolea mfano Mwalimu Nyerere, sasa hayupo nani anayeendeleza na kukienzi chama kama ilivyokuwa wakati wake? Ili kuondokana na tabaka hili sisi wazee tunajipanga kukishauri chama kama kunatokea matatizo kama ilivyo sasa wazee tuweze kushauri kwa maslahi ya chama na wanachama kwa ujumla pamoja na kujenga misingi imara ya uzalendo na siasa zilizotukuka ndani na nje ya CCM,” alisema Simba ambaye amepata kuwa waziri katika serikali ya awamu ya tatu.

Alisema ili kujenga misingi imara lazima siasa ndani ya CCM, zijengwe na watu hasa kwa kuongozwa na itikadi kama aliivyokuwa ikisimamiwa na Mwalimu Nyerere na wasaidizi wake.

“Sisi wazee na wanachama wote wa CCM tusiposimama imara kuna hatari ya chama kupoteza mwekelekeo; sasa juhudi zinazofanywa za kurudisha misingi ya chama na mwenyekiti wa taifa, Rais Jakaya Kikwete, na sekretarieti tunahitaji kusimamia na kukomesha makundi yanayokitafuna chama ndani,” alisema Simba.

Hali ya kisiasa nchini

Akizungumzia mwenendo wa kisiasa alisema hivi sasa amani imekuwa ikivurugwa na vyama vya siasa kutokana na kila chama kutanguliza utashi na maslahi ya chma husika kuliko wananchi na taifa kwa ujumla.

Alisema malumbano yanayotokea mara kwa mara bungeni, siku moja yanaweza kuwaingiza wananchi barabarani kwa kuhisi wawakilishi waliowachagua hawana tija kwao.

“Haya yanayoendelea hivi sasa bungeni ni ya kusikitisha sana kwani hivi sasa muhimili muhimu wa Bunge unayumba na hata kukosa mwelekeo kutokana na baadhi ya wabunge kuona pale ni jukwaa la kisiasa.

“Huwezi ukawa na wabunge wenye kuonyesha ufundi wa kuzungumza na kila mara mwongozo wa Spika au taarifa wakati hivi sasa Watanzania wanahitaji kutatuliwa matatizo yao na watunga sheria hao,” alisema mwenyekiti huyo wa wazee wa mkoa wa Dar es Salaam.

Amani ya nchi

Kuhusu suala hilo, Simba ambaye alikuwa waziri katika utawala wa awamu ya tatu kisha baadaye kuwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi Taifa, alisema hivi sasa amani ya nchi iko shakani kutokana na kauli za viongozi wa vyama vya siasa wanazozitoa katika Bunge na mikutano yao ya kisiasa.

“Kila mbunge au kiongozi ametanguliza maslahi yake binafsi kwa kugombea vyeo vya uwakilishi na kulumbana kupitia Bunge kuliko watu waliomchagua huku akisahau lilolompeleka pale, kwa hatua hii kuna kila dalili za kuchafua amani yetu,” alisema Simba.

CCK yasikitishwa na Bunge

Katika hatua nyingine, Chama cha Kijamii (CCK), kimesema Bunge limepoteza heshima kutokana na wabunge kusimama kutetea maslahi ya vyama vyao na kusahau wananchi ambao walichagua serikali yao kukaa madarakani.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Katibu Mkuu wa CCK, Renatus Muabhi, alisema kuwa kupoteza heshima kwa Bunge kumetokana na wabunge kuwakilisha vyama na kuacha wananchi wakiwa hawana imani na serikali yao katika kupata maisha bora.

Alilaani wabunge kutohudhuria kwa wingi bungeni hali inayosababisha wabunge wanaopitisha bajeti kuwa wachache hivyo kuwafanya wananchi wengi kukosa kuwakilishwa ipasavyo.

Dowuta yatoa tamko

Wakati huo huo, Chama cha Wafanyakazi wa Shughuli za Meli na Bandari (DOWUTA) kimesema Buge la sasa limekosa dira na kutokana na hali hiyo kuna haja ya kuwepo kwa chuo kinachofundisha uongozi kabla ya watu hao kuteuliwa katika nafasi za uongozi.

Akizungumza na Tanzania Daima, ofisini kwake mwishoni mwa wiki, Katibu Mkuu wa Dowuta, Abdallah Kibunda, alisema Bunge la sasa linatia aibu machoni mwa jamii hivyo kulifanya kukosa dira.

“Bunge la sasa ni la ghasia tu, wabunge wamejisahau kwani badala ya kujadili masuala ya maendeleo wanalumbana bila mpango wakati malumbano yalishaisha wakati wa kampeni
“Hao ni wawakilishi wa wananchi hivyo hawana budi kujirekebisha. Hata hivyo suala la uongozi linahitaji taaluma na kungekuwa na chuo ambacho moja ya sifa ni viongozi wakiwemo mawaziri, wabunge, wakuu wa mikoa na wengine kupitia huko kabla hawajateuliwa ingekuwa vizuri,” alisema Kibunda.

Alisema malumbano hayo hayawanufaishi wapigakura kwani asilimia kubwa ya wapigakura si wanachama wa CCM, CHADEMA, CUF wala TLP bali waliwapigia kura wabunge hao kutokana na kunadi sera zao kwao wakitegemea watapata maendeleo lakini kinyume chake wabunge hao wamekuwa wakilumbana siku hadi siku badala ya kupaza sauti zao bungeni kusaidia kuondoa kero za wananchi.

Alisema kwa hali hiyo wabunge hawana budi kurekebisha mara moja tabia hiyo kabla haijaleta athari zaidi.

Kwa mujibu wa katibu huyo, mkutano huo wa Bunge ni muhimu kwa sababu unajadili maendeleo ya taifa yakiwemo ya wafanyakazi katika kukuza uchumi wa taifa ili kukuza uchumi.

Alisema badala ya wabunge hao kujadili matatizo ya wafanyakazi kama vile mazingira mabovu ya kazi waliyonayo, kukatwa kodi na mengine badala yake kila mtu anafanya jambo analojisikia.

Alitoa rai kwa wabunge kufanya kazi kwa hekima, umakini na busara wawapo bungeni kwa maslai ya taifa.


0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget