Monday, 19 September 2011


Kikwete mtegoni tena
• Asaini tangazo la serikali lililochakachuliwa

na Waandishi wetu

RAIS Jakaya Kikwete amedanganywa tena na baadhi ya watendaji wake, akasaini tangazo lililochakachuliwa.

Septemba 5 mwaka huu, Kikwete alisaini tangazo la kusudio la uanzishaji wa wilaya mpya ya Butiama, lakini katika namna ya kushangaza, sasa inaonekana eneo la wilaya mpya ni Nyamisisi.

Hali hiyo inayotia fedheha kwa Rais wa nchi, imebainika juzi wakati Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipofika Butiama kuzuru kaburi la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Pinda alilazimika kuwatuliza wakazi wa eneo hili waliotaka kujua sababu za msingi za Rais kubadili msimamo wake na kuhamishia makao mapya yaliyotakiwa kuwa Butiama na kuyapeleka Nyamisisi.

Pinda alikiri bayana kuwa Rais alisaini tangazo hilo akijua kuwa kilichoandikwa ni makao makuu kuwa Butiama bila kujua eneo lililoandikwa ni Nyamisisi.

“Hata kama kuna mtu alitaka makao makuu yawe Nyamisisi, kwa kweli haikupaswa hiyo Nyamisisi kuchomekwa hivyo. Hata mngeniuliza mimi makao makuu yawe wapi, ningesema lazima yawe Butiama tu,” alisema Pinda na kushangiliwa.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amesema tangazo hilo lilikuwa na makosa kutokana na kutaja eneo la makao makuu tofauti na lile lililopendekezwa.

Pinda alisema mpango wa serikali ulikuwa ni makao makuu ya wilaya hiyo yawe katika kijiji cha Butiama ili kumuenzi Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Akijibu malalamiko ya wakazi wa Butiama, walioingia katika eneo la nyumba hiyo, wakimtaka atamke kuwa makao makuu yatakuwa Butiama, Pinda alisema:

“Hili la Butiama kwa kweli linaleta manenomaneno. Sisi serikalini tulidhani ukiwa na wilaya ya Butiama na makao makuu ni lazima yawe Butiama, ili tumuenzi Baba wa Taifa.

Hata hivyo, alisema pamoja na tangazo hilo kuchomekwa neno Nyamisisi, bado mtu aliyefanya hivyo hajafanikiwa, kwani tangazo hilo sio uamuzi wa mwisho wa kuhusu suala hilo.

Aliwataka wananchi wa Butiama kulichukulia tangazo hilo kuwa ni pendekezo tu ambalo wanapaswa kulitolea maoni yao kuhusu kulikubali au kulikataa na kwamba maamuzi ya mwisho kuhusu wapi yawe makao makuu ya wilaya hiyo yatatokana na maoni ya wananchi wenyewe.

Alisisitiza kuwa Butiama ikiwa wilaya sio tu huduma za msingi zitaboreshwa na kuwapa watu sababu ya kwenda wilayani hapo, bali pia itawapa sababu ya kwenda kuzuru nyumbani kwa Hayati Baba wa Taifa.

Pinda pia alimpa fursa mjane wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere, kutoa kauli yake kuhusu suala hilo, ambaye alisema yeye asingependa kuliingilia suala hilo.

“Hili suala halina tatizo, ninyi na wananchi wote mtakavyoamua ndivyo iwe hivyohivyo,” alisema Mama Maria.

Maswa watishia kuandamana

Katika hatua nyingine, hatua ya Rais Kikwete kuunda mikoa mipya, imezua balaa baada ya mamia ya wananchi wa wilaya ya Maswa, mkoa wa Shinyanga kuandaa maandamano iwapo serikali itaamua kuyaweka makao makuu ya mkoa mpya wa Simiyu katika wilaya ya Bariadi.

Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana katika Uwanja wa Nguzo Nane na kuhudhuriwa na mamia ya wakazi wa wilaya hiyo, wananchi hao wamedai kuwa hawako tayari kutendewa hivyo na wataandamana hata ikilazimu kupigwa risasi.

Katika mkutano huo ulioitishwa kwa ajili ya kutoa maoni ya mapendekezo juu ya nia ya serikali ya kupeleka makao makuu ya mkoa mpya wa Simiyu mjini Bariadi, wananchi hao wamesema uamuzi huo ni dharau kwao na unataka kufanywa kwa ajili ya manufaa ya viongozi wachache.

“Sisi wana Maswa tutaandamana bila kujali itikadi za vyama kama hatutasikilizwa na tuko tayari kupigwa risasi. Hatuwezi kunyang’anywa haki yetu kwa ajili ya ubinafsi wa viongozi wachache,” alisema mkazi mmoja wa Maswa, Thomas Nkola, na kushangiliwa na umati wa wananchi.

Walisema kuwa viongozi wa mkoa wa Shinyanga kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa wilaya ya Bariadi wamekuwa na desturi ya ubinafsi katika masuala yenye maslahi ya umma kitendo kilichodhihirika katika ujenzi wa barabara ya lami ya Mwigumbi –Maswa-Lamadi.

“Viongozi wetu wa mkoa wa Shinyanga na wa Bariadi wametuona sisi wa Maswa watulivu sana hivyo wanatumia mwanya huo kutuchezea.

“Mfano ujenzi wa barabara ya lami ya Mwigumbi-Maswa-Lamadi ilitakiwa ianzie Mwigumbi kuja Maswa lakini kutokana na ubinafsi wao imeanzia Bariadi kwenda Lamadi,” alisema mwananchi mwingine, Samwel Kidima.

Walisema licha ya mapenzi mema aliyonayo Rais Jakaya Kikwete ya kuanzisha mkoa huo, ni vizuri mchakato wa kupata makao makuu yake ukaanza upya kwani wa awali haukupitia katika vikao halali kama vile baraza la madiwani na kamati za ushauri za wilaya (DCC) hali ambayo imezua mgogoro mkubwa na kufanya kutokuwepo kwa mahusiano mazuri kati ya wananchi wa wilaya hizo.

“Rais Kikwete alipoamua kuanzisha mikoa na wilaya mpya alikuwa na nia nzuri sana lakini jambo la kushangaza mchakato wa kutoa mapendekezo ya makao makuu ya mkoa wa Simiyu hayakufuata utaratibu kwani ilitakiwa uanzie katika vikao vya baraza la madiwani na kamati za ushauri za wilaya ndiyo maana jambo hili limezua mgogoro mkubwa na sasa mahusiano kati ya wananchi wa wilaya ya Maswa na Bariadi si mazuri hivyo mchakato uanze upya,” alisema Edward Bunyongoli.

Walisema iwapo serikali itabaki na msimamo wake huo basi wao wataendelea kubaki katika mkoa wa Shinyanga lakini hawako tayari kukubaliana na uamuzi huo uliofanywa kwa ajili ya maslahi ya watu wachache wabinafsi.

“Kama serikali itabaki na msimamo kuwa Bariadi ndiyo makao makuu ya mkoa wa Simiyu sisi tutabaki katika mkoa wa Shinyanga kwani hatuko tayari kukubali uamuzi huo uliotawaliwa na vitendo vya kifisadi,” alisema Kulwa Nangale.

Hii si mara ya kwanza kudanganywa kwa Rais kwani ameshadanganywa zaidi ya mara 12 miongoni mwa mambo aliyodanganywa ni pamoja na ile ya kuzindua mradi wa Bwawa la Manchira lililoko wilayani Serengeti wakati tayari wananchi wamekwishafungua kesi Mahakama Kuu ya Mwanza wakidai fidia.

Kesi hiyo iliyofunguliwa ni matokeo ya viongozi wa serikali wilayani humo kuhusika kuwalipa fidia watu wasiohusika na kuwaacha walengwa waliofanyiwa tathmini.

Pia aliwahi kudanganywa kwamba daraja la Mkenda lililoko Ruvuma ambalo ni njia muhimu kuelekea Msumbiji, lilikuwa limekamilika.

Katika tukio jingine, Rais aliwahi kupewa taarifa zisizo sahihi kuhusu tuhuma za rushwa zilizokuwa zikimkababili Anatory Choya kisha akamteua kuwa mkuu wa wilaya, lakini siku siku chache baadaye akafunguliwa mashtaka na TAKUKURU.

Mwaka juzi, akiwa ziarani Mbeya msafara wa Rais ulishambuliwa kwa mawe na watu, lakini wasaidizi wake wakaja kutoa taarifa kwamba watu hao walikuwa ni wahuni na walikuwa wakimsubiri Rais kwa muda mrefu bila mafinikio.

Hata hivyo, baadaye uchunguzi huru ulibainisha kwamba tukio hilo lilikuwa na mafungamano ya kisiasa na makovu ya mchakato wa uchaguzi ndani ya CCM kwa mwaka 2005.

Mlolongo huo mrefu wa upotoshaji taarifa kwa Rais uliibuka tena katika utoaji wa magari ya misaada ambapo badala ya kupewa mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Longido alipewa wa Ngorongoro.

Tukio hilo lilimfanya mkuu huyo wa nchi kukasirika na kumzodoa mkurugenzi huyo, lakini baadaye ikabainika mkurugenzi huyo alikwenda kutokana na makosa ya maafisa wa Ikulu.

Katika mlolongo huo, tukio kubwa kabisa ni Rais kutia saini kwa mbwembwe Sheria ya Gharama za Fedha za Uchaguzi ambayo ilichomekwa vipengele nje ya Bunge kitu ambacho ni kinyume cha sheria.

Tukio hilo ambalo ni la uvunjifu wa Katiba, liliibuliwa na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, ambaye awali, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Fedrerick Werema, alikanusha.

Hata hivyo, baadaye sheria hiyo ilirudishwa bungeni na kukarabatiwa kwa mgongo wa mabadiliko ya sheria mbalimbali.

Mei mwaka jana, Rais alipewa taarifa za upotoshaji kuhusu mazungumzo ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) na serikali, kwa kuelezwa shirikisho hilo halikuhudhuria mkutano wa saa 4:00 asubuhi kama ilivyopangwa.

Hata hivyo, TUCTA wakatoa ushahidi wa barua za mwaliko wa mkutano huo wa Aprili 22 mwaka jana, ambazo zilikuwa mbili, moja ikionyesha walitakiwa kufika katika mazungumzo Hazina saa 4:00 asubuhi na nyingine saa 8:00 mchana.

Katika kuonyesha upotoshaji kwa Rais, wasaidizi hao walimpa barua iliyokuwa ikionyesha walipaswa kukutana saa 4:00 asubuhi huku ile ya saa 8:00 wakawa wameificha.

Rais akizungumza na wazee wa mkoa wa Dares Salaam aliwashambulia viongozi wa TUCTA hasa Naibu Katibu Mkuu, Nicolas Mgaya, akimwita mnafiki, mzandiki, na mchochezi.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget