Ya Usalama wa Taifa na teuzi za Rais Kikwete!
USKOCHI
21 Sep 2011
Toleo na 204
“KATIKA kupambana na uhalifu, hakuna njia ambayo - kama inaweza kuleta ufanisi - haitotumika. Kama inazingatia sheria, maadili, na inafanywa kwa nia nzuri, nipo tayari kuifanyia kazi...tumeajiriwa na tunalipwa kupambana na uhalifu, na hicho ndicho nitakachofanya...” .
Nukuu hii inapatikana katika hotuba ya kwanza ya Mkuu mpya wa ‘kanda kuu’ ya kipolisi ya London (Metropolitan Police) Bernard Hogan-Howe.
Hogan-Howe alishinda nafasi hiyo baada ya kuwabwaga makamanda wengine watatu kujaza nafasi iliyoachwa na Sir Paul Stephenson aliyejiuzulu kufuatia kuhusishwa kwake na skandali ya kunasa kwa siri maongezi ya simu (phone hacking) kulikofanywa na baadhi ya magazeti ya Uingereza yanayomilikiwa na tajiri mkubwa kabisa wa vyombo vya habari duniani, Rupert Murdoch.
Mkuu huyo wa Metropolitan Police alitamka bayana kuwa jukumu kuu alilonalo mbele yake ni kupambana na uhalifu na kuwahudumia waathirika wa uhalifu. Na rekodi yake kiutendaji ni ya kuvutia sana.
Akiwa Mkuu wa Polisi wa kanda ya kipolisi ya Merseyside (inayojumuisha jiji lililokuwa likisifika kwa uhalifu la Liverpool), alifanikiwa kuifanya kanda hiyo itoke kwenye nafasi ya 42 kati ya 43 ya ‘ligi ya uhalifu’ hadi kufikia nafasi ya kwanza alipotoka kwenye nafasi hiyo.
Kadhalika alifanikiwa kupunguza uhalifu kwa asilimia 29 na vitendo visivyoendana na maadili ya jamii (anti-social behaviour) kwa asilimia 25 katika kile alichokiita upolisi timilifu (total policing) na vita kamili dhidi ya uhalifu (total war on crime).
Dhamira hiyo ya Hogan-Howe inashabihiana na kauli aliyotoa Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa, Rashid Othman alipoteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kushika nafasi hiyo mwezi Agosti mwaka 2006.
Othman, shushushu mzoefu, alitoa ole kwa majambazi akisema moja ya kazi zake kuu ni kuhakikisha kuwa anaendeleaza mapambano dhidi ya ujambazi na majambazi, kazi ambayo alisema ilikuwa imeasisiwa na Rais Kikwete.
Kadhalika, aliahidi kuwa angehakikisha anaweka utaratibu mzuri wa kukutana na vyombo vya habari ili kuwapa wananchi taarifa za kiusalama ambazo wanastahili kuzipata, na wana haki ya msingi kujua serikali yao inafanya nini katika suala zima la usalama, na hiyo ingeongeza ufanisi wa katika utendaji kazi.
Wakati sina hakika ya mafanikio katika dhamira hizo za Mkuu huyo wa Usalama wa Taifa kupambana na ujambazi ‘wa asili’ (yaani ule wa kuvunja majumba au ofisi, kupora kwa kutumia silaha, nk), yayumkinika kuhitimisha kuwa hajafanikiwa kabisa kupambana na ujambazi dhidi ya mali ya umma au kwa neno maarufu “ufisadi”.
Tangu alipotoa kauli hiyo hadi sasa, tumeshuhudia mlolongo wa matukio ya ujambazi unaofahamika kwa kimombo kama ‘uhalifu wa kola nyeupe’ (white collar crime) ambapo wahusika hawatumii silaha; bali ujuzi na madaraka yao kuliibia taifa.
Sote tunakumbuka kuhusu ujambazi wa EPA, utapeli wa kampuni ya Richmond, dili za ufisadi kwenye makampuni ya Meremeta, TANGOLD, Deep Green Finance, na uhalifu mwingineo ambao umelisababishia taifa hasara ya mabilioni ya shilingi.
Ni ukweli usiopingika kuwa baadhi ya watu wanahoji Idara ya Usalama wa Taifa iko wapi wakati haya yote yanatokea. Kuvuruga mambo kabisa, taasisi hiyo nyeti ilijikuta ikihusishwa na ufisadi wa EPA ambapo mmoja wa maafisa wake waandamizi alitajwa kuwa mnufaika wa wizi huo mkubwa.
Na hapa ndipo inapofika mahala pa kuangalia ahadi za Othman wakati anateuliwa ambapo aliahidi kuandaa utaratibu mzuri wa kukutana na vyombo vya habari ili kuwapa wananchi taarifa za kiusalama.
Kwa kumbukumbu zangu, wakati pekee ambapo Idara hiyo ilizungumza na waandishi wa habari, ni pale Naibu Mkurugenzi Mkuu wake, Jack Zoka alipokanusha madai ya mgombea kiti cha urais kwa tiketi ya CHADEMA, Dkt.Willibrod Slaa, kuwa taasisi hiyo ilikuwa ikiisaidia CCM kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
Hadi leo, hakuna maelezo yoyote yaliyotolewa na idara hiyo kuhusu namna ilivyohusishwa na skandali ya fedha za EPA. Ilipaswa aidha wajitenganishe na afisa huyo mwanadamizi na kubainisha kuwa kampuni zilizodaiwa kumilikiwa naye hazikuwa na mahusiano na taasisi hiyo, na kutajwa kwake hakuhusiani kabisa na idara hiyo nyeti.
Kadhalika, haingekuwa vibaya kwa taasisi hiyo kuufahamisha umma ilikuwaje ikashindwa kubaini ufisadi huo, na pengine kuweka bayana mikakati yake ya baadaye ya namna ya kuzuia kurejea kwa matendo ya kihalifu kama hayo.
Naanika haya nikitambua kuwa kazi za taasisi hiyo zinafanywa kwa siri (kwa nia njema kabisa), lakini tatizo linakuja pale mambo yanapokwenda fyongo ambapo ni rahisi kwa wananchi kupata hisia kuwa utendaji kazi huo wa siri unatumika kuficha mapungufu au hata kufunika ushiriki wa taasisi hiyo katika ufisadi.
Si lengo la makala hii kumhoji kiongozi huyo mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa bali, kama nilivyobainisha mwanzoni, kauli yake siku alipoteuliwa inashabihiana na iliyotolewa na mkuu huyu mpya wa Metropolitan Police.
Na kwa vile ni nia ya kila Mtanzania kuona nchi yetu ikielekea kule inakopaswa kwenda, hakuna ubaya katika kukumbushana yale yote yanayoweza kutufikisha tuendako kwa usalama.
Lengo kuu la makala hii ni kuangalia namna teuzi zinavyofanywa na Rais, na pengine watendaji wengine wa serikali pasipo kuangalia iwapo teuzi hizo zitaleta ufanisi.
Wiki iliyopita, Rais Kikwete alitangaza wakuu wa mikoa wapya na waliobadilishiwa vituo vya kazi. Kadhalika, tulifahamishwa majina ya wakuu wa mikoa waliostaafu na ‘waliopumzishwa kwa muda’ (kwa matarajio ya kupangiwa kazi nyingine).
Kabla hata ya kujadili iwapo walioteuliwa walipaswa kupewa nafasi hizo, sijui inaleta picha gani pale Rais anapoamua kumteua mtu ambaye wapiga kura walimkataa katika ngazi ya jimbo. Hapa nazungumzia baadhi ya walioteuliwa kuwa wakuu wa mikoa lakini waliangushwa katika uchaguzi wa wabunge katika majimbo yao.
Tuwe wakweli: Hivi kama idadi ndogo tu ya wananchi katika jimbo imekosa imani na mgombea, na hivyo kutompa kura za kutosha za kumfanya awe mbunge, inawezekanaje kwa mtu huyo kukabidhiwa ‘urais wa mkoa’? Ndio, ukuu wa mkoa ni kama urais wa mkoa; kwani anayepewa dhamana hiyo ni mwakilishi wa Rais katika mkoa husika.
Sijui lengo ni kuwakebehi wapigakura waliomnyima ubunge kiongozi wa aina hiyo au ndio hadithi zile zile za kuteuana ‘kishkaji’ (kirafiki) lakini sidhani kama kuna maelezo stahili ya kuelezea teuzi za aina hii; hasa ikizingatiwa kuwa nchi yetu haina uhaba wa wazalendo wenye uwezo wa kushika nyadhifa.
Katika baadhi ya teuzi hizo zilizofanywa na Kikwete baada ya ya takriban mwaka mzima wa ‘upembuzi yakinifu’ zina walakini uliozoeleka wa watendaji ambao rekodi zao zina walakini. Hili halihitaji kutajwa majina; kwani mikoa iliyoboronga kimaendeleo inafahamika.
Kuwazawadia waharibifu wa maendeleo nafasi za ‘kujaribu tena mkoa mwingine’, ni sawa kabisa na kutothamini maslahi ya wananchi katika maeneo husika.
Lakini pia katika walioteuliwa kuna mbunge ambaye anaungana na baadhi ya wabunge wenye kofia zaidi ya moja -kwa maana ya kuwa mbunge na mkuu wa mikoa. Kitendo hiki ni kuwanyima kwa makusudi wananchi nafasi ya kuwa na kiongozi atakayeelekeza nguvu zake kwa jukumu moja.
Katika mazingira yakawaida, mbunge ana majukumu ya kuwatumikia wapiga kura wake. Kumpa jukumu jingine la kuongoza mkoa ni kumbembesha mzigo mzito wa ziada pasipo kujali matokeo yatakuwaje.
Kukosoa na kumlaumu pasipo kutoa ushauri si jambo jema. Nimalizie makala hii kwa kushauri kuangalia madaraka ya Rais katika kufanya teuzi mbalimbali, na kwa vile tupo kwenye mchakato wa marekebisho ya Katiba, basi, ni muhimu pia kuangalia uwezekano wa ulazima wa teuzi zinazofanywa na Rais kuidhinishwa na Bunge.
Rais kama binadamu anaweza kufanya teuzi zisizo na maslahi kwa taifa. Bunge likifanya kazi yake zaidi ya kuwa ‘mhuri wa kuidhinisha kila kinacholetwa na serikali’, linaweza kabisa kuepusha teuzi fyongo au zile zinazozidi kudidimiza nchi yetu kwenye lindi la umasikini unaochochewa na ufisadi.
0 comments:
Post a Comment