Kwanza kabla hujasoma makala hii ningekushauri usome makala ya Bwana Omar Ilyas katika blogu yake,makala iliyobeba kichwa Chadema Ishinde kwa Kushindwa.
Natumaini baada ya kuisoma tunaweza kuelewana kwanini ninatofautiana na uchambuzi wa Bwana Ilyas.Katika paragrafu ya kwanza tu,mwandishi ameshahitimisha kuwa Chadema ina safari ndefu ya kushinda kuwa mtawala mbadala.Anaandika "...ili CHADEMA kushinda katika safari ndefu iliyonayo kama mtawala mbadala kinapaswa kushindwa sasa." Hata hivyo,katika makala hiyo hakuna mahala ambapo mwandishi ameweka sababu za kwanini safari hiyo ya Chadema iwe ndefu,au kwanini anaona hivyo.
Pengine jingine linaloweza kuzua taswira tofauti ya mtizamo wa Bwana Ilyas kwa Chadema ni ukweli kwamba kwa ujumla 'uhuni waliofanya Chadema' unaweza kabisa kufunikwa na 'uhuni mwingine mkubwa' uliofanywa na kiongozi wa CCM,Mbunge Ismail Aden Rage kupanda jukwaani akiwa na bastola.Kwa hakika alichofanya Rage ni zaidi ya uhuni,kwani hata kama anamiliki silaha hiyo kihalali,haiingia akilini kwa mbunge huyo kupanda jukwaani akiwa na silaha-na hakufanya jitihada yoyote kuificha.
Na 'uhuni' mwingine wa kuchefua ni ukweli kwamba hadi sasa hatua pekee iliyochukuliwa dhidi ya Rage ni tamko la Waziri wa Mambo ya Ndani kwamba mbunge huyu anastahili kuhojiwa.Hebu pata picha aliyepanda jukwaani angekuwa Mbunge wa Chadema au CUF!Ni dhahiri muda huu angekuwa lupango,na uchunguzi wa kama anamiliki silaha kihalali au la ungefanyika wakati akiwa rumande.
Tukibaki kwenye hoja hiyo hiyo ya 'uhuni' hivi kuna uhuni mkubwa na mchafu zaidi ya ule wa kiongozi mwandamizi wa CCM (na de facto mratibu wa kampeni za chama hicho huko Igunga),Mwigulu Mchemba kutembea na mke wa kada mwenzie wa CCM?Huu sio tu uhuni bali ni ukosefu wa maadili usioelezeka.
Angalau Chadema wanaweza kutoa excuse (ambayo inaweza isikubalike) kuwa chama hicho na viongozi wake si wakomavu wa kisiasa (kwa maana ya uzoefu) lakini tunawezaje kuelezea uhuni wa viongozi wa chama ambacho si tu ni chama tawala lakini pia kina uzoefu unaoweza kuzidi jumla ya umri wa vyama vyote vinavyoshiriki kampeni hizo?
Japo Bwana Ilyas amebainisha kuwa hawezi kutaja "mlolongo wa matukio ambayo yamepelekea baadhi ya watu kuiangalia Chadema kwa jicho la tahadhari badala ya matumaini" kwa hakika shutuma nzito anazoelekeza dhidi ya chama hicho zilipaswa kuambatana na mlolongo huo wa matukio,japo in a point form (yaani kwa kutaja pasipo kufafanua).
Naomba kuweka bayana kwamba two wrongs do not make a right.Hapa ninamaanisha kuwa 'uhuni' wa Rage na wa Waziri (katika kudili na uhuni wa Rage) haupunguzi 'uhuni' wa Chadema.
Lakini pia Bwana Ilyas anakosea kuchukulia tukio hilo lililofanywa na wafuasi wa Chadema wakiongozwa na wabunge wawili tu kuwa ni taswira nzima ya 'uhuni' wa Chadema.Mchambuzi yeyote makini hawezi kuhitimisha kuwa kitendo cha Rage kupanda na silaha jukwaani au kitendo cha Mchemba kutembea na mke wa kada mwenzie wa CCM kuwa ni picha halisi ya nidhamu mbovu ya CCM.
Lakini pia naomba ifahamike kuwa Chadema wanatambua fika mwenendo wa mambo ambapo sheria huonekana zimevunjwa pale tu wapinzani (au walalahoi) wanapokwenda kinyume na taratibu.Bwana Ilyas anafahamu fika kuwa laiti Chadema wangeamua kutoa taarifa kwa vyombo husika kuhusu 'uhuni' wa Mkuu wa Wilaya 'aliyekwidwa' kwa kukiuka taratibu za uchaguzi kusingefanyika lolote.Ushuhuda wa hili ni namna tuhuma za waziwazi za vitendo vya rushwa kwenye mchakato wa ndani wa CCM kupata wagombea wake kwenye nafasi za udiwani na ubunge katika uchaguzi mkuu uliopita ambapo tulishuhudia TAKUKURU ikichezeshwa sandakarawe,na wananchi kumwagiwa mchanga wa macho kwa baadhi ya wahusika kukamatwa.Labda Bwana Ilyas anaweza kutupa takwimu ni watuhumiwa wangapi walikwisha adhibiwa kisheria kutokana na vitendo hivyo.
Siungi mkono matumizi ya nguvu katika kudai haki,lakini ni ukweli usiopingika kuwa mara nyingi tawala dhalimu hazitowi haki pasipo kutumia msuli.Diplomasia ni njia bora zaidi ya kudai haki au kuendesha majadiliano.Lakini kwa bahati mbaya- na naamini Bwana Ilyas anajua hilo-mara kadhaa diplomasia imekuwa kikwazo katika upatikanaji wa haki kwa haraka.Ndio maana hata Wapalestina walipowasilisha ombi lao la uanachama wa umoja wa mataifa waliweka bayana kuwa WAMECHOSHWA na danadana za haki yao kuchezewa kama privilege flani.
Laiti sheria,kanuni na taratibu zingezingatiwa,Mkuu wa Wilaya mhusika katika tukio hilo asingezifinyanga,na kwa maana hiyo asingekutana na hasira za wana-Chadema wanaodai haki yao.Marehemu Kighoma Ali Malima aliweka wazi mtazamo wake kuhusu namna haki inavyoapaswa kudaiwa.Alisema: "HAKI HAITOLEWI KAMA ZAWADI.INACHUKULIWA AU KUDAIWA,HATA KWA NGUVU INAPOBIDI."
Maandiko Matakatifu ya Waislamu (dini ambayo naamini Bwana Ilyas ni muumini wake yanasema hivi (roughly) kuhusu jambo baya: "lisemewe vibaya...lichukiwe...na ikibidi liondolewe hata kwa nguvu." (Ninasistiza kuwa nukuu hiyo ni roughly).Sijui kwa Bwana Ilyas kama kuna jambo baya na amelichukia lakini bado lipo,amelikemea lakini linazidi kukua,hatofikia hatua ya kuliondosha hata kwa nguvu ikibidi?
Hicho ndicho kilichofanywa na Chadema.Wlilazimika kumkwida Mkuu wa Wilaya kwa vile aliamua kwa makusudi kupuuza sheria za uchaguzi na haki za vyama vingine vinavyoshiriki kwenye uchaguzi huo mdogo.Ni kweli ingependeza iwapo diplomasia ingetumika,lakini huwezi kuwa na fair play kwenye soka katika mechi ambayo timu pinzani ina wachezaji 15,yaani licha ya wale 11 wa kawaida,pia yumo refa,washika vibendera wawili na kamisaa.Au hakuna haki itakayopatikana katika kesi ambapo mshtaki au mshtakiwa pia anafanya kazi ya uendesha mashtaka,yeye huyhuyo ni mzee wa baraza,na pia ni hakimu/jaji.
Pasipo kuitihumu waziwazi,Bwana Ilyas anaihusisha Chadema na ukabila-yaani Uchagga.Amemtaja Mzee Edwin Mtei na mwenyekiti wa sasa Freeman Mbowe.Kwa makusudi kabisa,amekwepa kutaja safu nzima ya uongozi wa juu wa Chadema unaojumuisha (pasipo kufuatilia mpangilio maalum) Mchaga (Mbowe),Muha (Zitto Kabwe) na Mmbulu (Dkt Slaa).
Busara ndogo tu ingeweza kumsaidia Bwana Ilyas kubaini kuwa ushindi walioupata Chadema katika majimbo mbalimbali kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka jana haukutokana na ukabila.Je John Mnyika alishinda ubunge huko Ubongo kwa vile kuna Wachagga wengi?Vipi kuhusu Halima Mdee huko Kawe?
Pengine katika kuonyesha chuki yake kwa Chadema,Bwana Ilyas anaituhumu Chadema kuwa iliwezesha Mbowe (Mchagga na Mkristo) kupata uenyekiti kwa kutumia mbinu (ambazo hata hivyo ameshindwa kuzibainisha).Kwani ndugu yangu huyu ambaye ninamheshimu vya kutosha hataki kumwangalia Mbowe kama MTANZANIA na badala yake anaangalia kabila lake (UCHAGGA na dini yake UKRISTO).Huu ni ubaguzi wa waziwazi.Ni sawa kwake kuinyooshea kidole Chadema kwa kujaza Wachagga na Wakristo lakini haoni tatizo kwa kwa CUF au CCM kuwa na idadi kubwa ya Waislam kwenye ngazi za juu za uongozi wa vyama hivyo.
Bwana Ilyas,hivi hata katika karne hii bado unajadili wasifu wa watu kwa vigezo vya dini na kabila,badala ya kuangalia sifa walizonazo kiuongozi?Na kuna ubaya gani kwa chama kujaza watu wa kabila au dini moja ilhali kinawatumika wananchi ipasavyo?Je msukumo wa Chadema uliopelekea serikali ya Rais Jakaya Kikwete kushughulikia bei ya sukari kuna uhusiano gani na ukristo au uchagga?
Bwana Ilyas anaendeleza tuhuma zake dhidi ya Chadema na kudurufu madai kuwa chama hicho kinalea udini.Anadai (nanukuu)"...Kama vile hilo halitoshi, tukielekea katika uchaguzi wa rais na wabunge wa mwaka 2010 ambao CHADEMA ilionyesha muamko mkubwa katika medani za siasa nchini, CHADEMA ama kwa kudhamiria, kutokudhamiria au kwa kulazimika, wakafanya kosa jingine ambalo badala ya kuwanasua katika kiwingu cha ukabila na udini wakajikuta wanajisimika ndani ya wingu la Udini."
Katika uchambuzi fyongo,Bwana Ilyas anadai kuwa Chadema imekuwa ikitafuta uungwaji mono na Kanisa Katoliki.Lakini anajikanganya pale anapoweka wazi kwanini inawezekana kuhisi Chadema na Kanisa Katoliki ni "damu damu" anaposema, "Hili lilikuja ama kutokana na kanisa hilo kama watanzania wengine kuchukizwa na maovu na usaliti wa Chama cha Mapinduzi (CCM)..." Kwa hiyo ni wazi kuwa chuki ya Kanisa Katoliki dhidi ya maovu yaliyokuwa yanafanywa na CCM ilishabihiana na ajenda za kupinga maovu zilizotawala kampeni za Chadema.Huu nao ni udini?
Lakini anageuka tena na kuirushia kombora Chadema kwa kudai "...au kutokana na dalili za uwezekano wa ushindi wa uhakika wa mgombea Urais wa CHADEMA ambaye ni kiongozi wa kiroho na aliyekuwa mtumishi wa ngazi za juu wa chombo nyeti cha kanisa hilo." Hivi Bwana Ilyas anataka kutuambia kuwa hadi leo hafahamu kuwa Dkt Willbrod Slaa si kiongozi wa kiroho?Aua ameamua wka makusudi kuwaiga Daily News na Habari Leo walioamua kumtambulisha Dkt Slaa kama PADRE?
Ni kweli,kiongozi huyo wa Chadema aliwahi kuwa Padre (na upadre si uhalifu kiasi cha kujenga negative connotation) lakini aliamua kuacha nafasi hiyo na kujikitka kwenye siasda.Kuendelea kumwita kiongozi wa kiroho ni sawa na kumtambulisha Kikwete kama kiongozi wa jeshi japo alishaacha uanajeshi zamani hizo.
Bwana Ilyasa anafanikiwa vizuri kuweka tatizo lake la UDINI (ambao ironically anautumia kuishutumu Chadema) anapodai "Kitendo cha viongozi wa kanisa la Katoliki kuanzisha na kuendeleza mpambano mkali wa majukwaani na katika alteri za kanisa kuwashutumu viongozi wa chama tawala cha CCM na serikali yake inayoongozwa na Rais na Mwenyekiti Muislamu, kabla na hata wakati wa uchaguzi huo kilijenga mtazamo wa kuwa kanisa hilo na hivyo wafuasi wake walipaswa kuiepuka CCM na wagombea wake na hivyo kuashiria kuwa CHADEMA ndio chaguo lao."
Naomba kumfahamisha Bwana Ilyas kuwa mtazamo huo ni wa makengeza.Kanisa lilikuwa na linaendelea kukemea maovu bila kujali yanafanywa na muumini wa dini gani.Kwani wakati Kanisa linaikemea CCM kuhusu ufisadi,Waziri Mkuu wa serikali ya CCM hakuna Mkristo?Ina maana Bwana Ilyas anataka kutuaminisha kuwa Kikwete (Muislam) ndio CCM?Au kwa lugha nyingine,tunaposhutumu ufisadi ndani ya CCM tunaushutumu Uislam kwa vile tu mwenyekiti wa chama hicho ni Muislam?Na Bwana Ilyas anasemaje kuhusu Muislam Zitto Kabwe anapokemea ufisadi akiwa ndani ya 'chama cha Wachagga na Wakristo Chadema'?
Bwana Ilyas anaendelea kuuthibtishia umma jinsi udini unavyomkwaza kufanya uchambuzi usio wa kibaguzi kwa kuwashutumu Chadema kumdhalilisha "mwanamama wa Kiislam na hijabu yake." Hapati shida kuepuka kuzungumzia wadhifa wa mwanamama huyo bali inakuwa rahisi kwake kumtambulisha kwa dini yake na vazi lake la kidini.Ni hivi,si Uislam au hijab itakayompendeza Laah pasipo kutenda yale atakayo kama ambavyo si upadre au kutembea na Rozari Takatifu kutakakomfanya Mkristo afikie uzima wa milele.Kama DC huyo alikuwa mcha Mungu halisi basi angefuata maagizo ya kidini ya kutii mamlaka za dunia.Angezingatia taratibu za uchaguzi zinasemaje badala ya kukurupuka na vikao vya kizushi ambavyo kimsingi vililenga kuitengenezea CCM mazingira ya ushindi.
Pamoja na mazingaombe yanayoendelea kuhusu dhana ya kujivua gamba ndani ya CCM, Bwana Ilyas anadiriki kukisifu chama hich akidai kuwa hiyo ni hatua ya kwenda mbele kufuatia matokeo yasiyoridhisha sana katika uchaguzi mkuu uliopita.Ninapenda kuamini kuwa ndugu yangu huyu ana uwezo kubwa wa kujenga hoja lakini amnakwazwa na hisia binafsi.Hilo gamba lililowishavuliwa na CCM ni lipi?Kujiuzulu kwa Rostam Aziz?Ni Rostam huyuhuyu aliyesafishwa na Kikwete kwenye kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana na ambaye leo anatumika kuipigia debe CCM huko Igunga?
Na kama kujivua gamba,vipi mbona Mzee wa Vijisenti Chenge na mwenzie Lowassa bado wapo madarakani huku tukiendelea kusikia kauli za kujikanganya kuhusu suala zima la CCM kujivua gamba?
Nimalizie makala hii kwa kumsihi Bwana Ilyas kwamba ili aweze kuiangalia Chadema vizuri anapaswa kuweka kando hisia zake za udini.Na kama anataka kutumia hoja za udini basi asichelee kuzungumzia pia namna CCM inavyowatumia baadhi ya Waislam kwa manufaa ya kisiasa (na hapa wa kulaumiwa ni Waislam haohao ambao mwaka 2005 waliingizwa mkenge na akina Kikwete kwa kuwaahidi Mahakama ya Kadhi huku dandana zikiendelea hadi leo).
Ushindi wa Chadema ni ushindi kwa kile asiyependa kuona Tanzania ikiendelea kuwa shamba la bibi kwa mafisadi.Chadema,pamoja na Bwana Ilyas kuituhumu kuwa inakumbatia udini na ukabili,imewatumikia vyema Watanzania katika muda mfupi tu ambapo imeweza kuibua ujambazi mkubwa dhidi ya taifa letu (EPA,Richmond,Buzwagi,Deep Green,Meremeta,nk).
Bwana Ilyas anapaswa kutambua pia kuwa laiti Chadema ingekuwa chama cha udini isingepiga kelel kuhusu umafia wa Richmond ambao mhusika mkuu alikuwa Edward Lowassa,mkristo ambaye amekuwa akimwaga mamilioni ya shilingi makanisani.Kadhalika,Chadema ingekalia kimya ufisadi wa Kiwira au namna Ikulu ilivyogeuzwa sehemu ya biashara na Rais Mstaafu Benjamin Mkapa,Mkatoliki ambaye hakosekani kanisani kila Jumapili.
Na kelele za Chadema kuhusu umuhimu wa marekebisho ya Katiba hazikuangalia maslahi ya Wakristo bali Watanzania kwa ujumla.Kuihukumu kwa hoja mfu za udini,ukabila na uhuni hakuna tofauti na harakati za makusudi za mafisadi kumhukumu kila anayepigania haki ya Mtnzania kuwa ni mhaini,anayetaka kuvuruga amani na utulivu (wa mafisadi kufanya ulafi wa kuifilisi Tanzania,I suppose) na kukwaza harakati za kumpatia Mtanzania ukombozi wa pili.
Kama alivyoniambia msahiliwa mmoja kwenye utafiti vitendo wa kozi yangu kimasomo, "haya mambo ya Ukristo na Uislamu sana sana ni huko mijini tu,ambako napo watu wanatumia dini kama mbinu ya kumudu maisha.Huku vijijini uhaba wa maji haubagui Mkristoa au Muislam.Mgao wa umeme pia hauchagui madhehebu.Kisima cha maji kilichopom msikitini kinahudumia wanakijiji wote pasipo kuuliza kama huyu ni Hamisi au John.Vyama vya ushirika vinapotukopa mazao yetu haviangalii kama flani ni Mkristo au Muislam.Pengne matokeo ya darasa la saba au sekondari yakitoka na Waktisto wengi wamefaulu na watoto wetu wa Kiislam wamefeli ndio kidogo unaweza kusikia watu wanahoji,lakini kimsingi watoto hao,paspo kuangalia madhehebu yao wanasoma katika mazingira magumu kabisa-sakafuni na walimu wao-pasipo kuangalia madhehebu yao-wametawaliwa na manung'uniko."
Tusiwape excuse mafisadi kwa vile tu wanaongozwa na Muislam au Mkristo.Tunaweza kutofautiana katika jinsi tunavyopiga kelele kuhusu ufisadi lakini kimsingi waathirika wa dhambi hiyo ni sote.Lakini kwa vile mafisadi hawana tofauti na wakoloni waliotubagua kwa misingi ya rangi na dini,wataendelea kutumia kete za ukabila na udini kutufarakanisha ili wazidi kutufisadi.Hata hivyo sote tunajua kuwa fedha wanazotufisadi haziendi misikitini au makanisani bali zipo kwenye akaunti zao za vijisenti huku Ughaibuni,huku nyingine zikitumika kuongeza idadi ya mahekalu yao na misururu ya magari yao ya kifahari pamoja na kukuza idadi ya nyumba ndogo zao.Wahanga wao ni mimi na wewe,regardless ya tofauti zetu za kidini au kikabila.
Let's agree to disagree!
Nimependa jinsi ulivyojibu kwa hoja na mifano hai.. NASIKITIKA HATA WASOMI NAO WANAINGIA KWENYE MITEGO YA UDINI.. ninaona umoja wetu unavyoangamia.. na SERIKALI YA AWAMU YA NNE HAIWEZI KUJIKOSHA KWA HILI... inasikitisha sana kuona ni chama kikongwe ndicho kinachochea UDINI nchini kwa manufaa yao ya muda... UTAWAONGOZA NANI BAADA YA KUWAGAWANYA...
ReplyDeleteHabari za siku.
ReplyDeleteKama mwanablogu kutoka Tanzania,nakuomba kushiriki kuchangia Mchakato wa KUFUFUA JUMUWATA(Jumuiya ya Wanablogu Tanzania).
Tafadhali naomba ufungue hii kurasa ya
http://blogutanzania.blogspot.com/
kisha upendekeze jinsi ya kufufua JUMUWATA.
Ahsante.
Luiham Ringo.
Niliona uchambuzi huu wa ndugu yangu, mwanazuoni mwenzangu Omar Ilyas katika ukuta wake wa Facebook,na nilichangia kwa kifupi kama ifuatavyo...Kaka, hongera kwa makala inayochambua kwa mapana matukio haya. Nakubaliana kwa kiasi kikubwa na uchambuzi huu, lakini nachelea kusema kuwa kuna baadhi ya maeneo umekuwa "subjective" hasa unataja udini na ukabila. Kwa mtazamo wangu sidhani viongozi fulani kutoka kabila au dini fulani kuongoza ama kwa kupokezana madaraka ama kupisha mwingine katikati yao kunafanya chama kuonekana cha ukabila (if I have understood you well). Tanzania tumejegwa kwa misingi ya kuheshimiana na kuishi pamoja (regardless tofauti zetu za kikabila na kidini) kwa muda mrefu sasa. Na hii imetuletea hesima kubwa ndani na nje ya nchi yetu. Tunachokishuhudia sasa ni baadhi ya watu kuanza chokochoko (kwa manufaa wanayoyajua wao) na kuhusianisha udini na ukabila. Siwatetei CHADEMA wala CCM hapa (maana mimi si mwanachama wa chama chochote cha siasa), ninachotaka kusema ni kuwa sidhani kama tumefikia hatua ya kutumia udini au ukabila kwa ajili ya ku-achieve our political ambitions.
ReplyDelete