Mawaziri wa kiume nchini Zimbabwe wapo mbioni kutahiriwa kama sehemu ya mkakati wa serikali ya nchi hiyo kuhamasisha njia hiyo inayoaminika kupunguza maambukizi ya Ukimwi.
Tafiti zinaonyesha kuwa tohara kwa wanaume inasaidia kupunguza uwezekano wa maambukizi ya Ukimwi (wakati wa tendo la ndoa) kwa takriban asilimia 60.Hata hivyo,wataalamu wa tiba wanaonya kuwa tohara hiyo sio njia mbadala ya hatua nyingine za kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.
Zimbabwe ilianzisha kampeni kubwa mwaka juzi ikiwalenga angalau wanaume milioni 1.2 katika jitihada za kupambana na maambukizi mapya ya ugonjwa huo.
Vituo vinavyoendesha zoezi hilo vimeeleza kuwa watu wengi wamekuwa wakijitokeza na wanaonyesha kukubaliana na hatua hiyo.
Lakini sasa kuna mpango wa kuwalenga wanasiasa wa ngazi za juu ikiwamo mawaziri,wabunge na madiwani ili nao watahiriwe.
Naibu Waziri Mkuu Thokozani Khupe ameeleza kuwa hatua hiyo inaendana na mkakati wa serikali kupambana na Ukimwi.
"Utafiti umeonyesha kuwa wanaume waliotahiriwa wana nafuu ya maambukizi ya Ukimwi pungufu kwa mara nane,na kama viongozi serikalini tunapaswa kuongoza kwa kuonyesha mfano ili tunaowaongoza watambua umuhimu na faida ya tohara," Khupe alilieleza gazeti la Sunday News la Bulawayo.
"Lengo letu ni kuwa na vifo sifuri kutokana na Ukimwi.Tunaweza tu kufanikiwa iwapo viongozi wataonyesha mfano.Watu wanapaswa kuelewa kuwa Ukimwi upo na haipaswi kudhani kwamba kuzungumzia tohara ni mwiko."
Zimbabwe ni moja ya nchi zilizoathiriwa vibaya sana na janga la Ukimwi huku kiwango cha maambukizi kikiwa miongoni mwa vikubwa zaidi duniani.
Hata hivyo,kiwango cha maambukizi kimepungua kwa kasi,takriban kwa nusu kutoka asilimia 29 ya Wazimbabwe wote mwaka 1997 hadi kufikia asilimia 16 mwaka 2007.
Watafiti wanaeleza kuwa wananchi wameanza kukubali kubadili tabia za ngono kutokana na kukua kwa uelewa kuhusu vifo vinavyotokana na Ukimwi na hofu ya kuambukizwa virusi vya ugonjwa huo.
"Nchi chache sana duniani zimeshuhudia kupungua kwa maambukizi,na katika Afrika,Zimbabwe ilionekana kama sio rahisi kumudu kupunguza maambukizi," Simon Grason wa chuo cha Imperial jijini London alieleza katika ripoti ya hivi karibuni.
CHANZO: Nimetafsiri habari hii kutoka gazeti la New Zimbabwean (bonyeza kiungo kuisoma katika lugha ya Kiingereza)
0 comments:
Post a Comment