Tuipende,tuichukie lakini ukweli unabaki kuwa CCM ndio chama tawala.Kwa mantiki hiyo kila Mtanzania,including sie tusiokuwa wananchama wa chama chochote kile cha siasa tunalazimika kuwa na interest na hali ya mambo ndani ya chama hicho.Afterall,tofauti zetu za kiitikadi hazimaanishi uadui kama unavyohubiriwa na akina Nape.Sote ni Watanzania,na iwe CCM,Chadema,CUF,nk vyote ni vyombo tu vya kutushirikisha katika siasa za nchi yetu kwa namna moja au nyingine.
Anyway,niende kwenye mada.CCM inakabiliwa na changamoto kubwa katika kumpata mgombea wake anayetarajiwa kumrithi Rais Jakaya Kikwete atakapomaliza muda wake mwaka 2015.Naomba kuorodhesha changamoto hizo kama ifuatavyo
MGOMBEA KUTOKA ZANZIBAR
Japo Katiba ya Jamhuri ya Muungano na ile ya CCM hailazimishi utamaduni usio rasmi wa kupokezana nafasi ya mgombea urais kati ya CCM Bara na Zanzibar,yayumkinika kuamini kuwa baada ya miaka 20 (1995-2015) ya CCM Zanzibar kutotoa mgombea kwenye nafasi ya Urais wa Muungano upande huo utakuwa unatarajia kuwa sasa ni zamu yao.Baada ya Rais Mzanzibari Ali Hassan Mwinyi,alikuja M-Bara Benjamin Mkapa aliyetawala kwa miaka 10 kabla ya kurithiwa na M-Bara mwingine Jakaya Kikwete ambaye kufikia mwaka 2015 atakuwa ametawala kwa miaka 10.
Kwa vile katika utamaduni mwingine usio rasmi ndani ya CCM mgombea atakayepitishwa mwaka 2015 (na ikitokea akashinda) anaweza kuwa madarakani kwa miaka 10 (kwa maana kuwa anatarajiwa kupitishwa tena mwaka 2020-kama ilivyokuwa kwa Mwinyi,Mkapa na sasa Kikwete), Wazanzibari wakikubali mgombea ajaye wa CCM atoke Bara itamaanisha wakose nafasi kwa miaka 30 mfululizo.
Tofauti na ccm Bara ambapo uongozi wake una sauti kuliko wanachama,kwa Zanzibar wanachama na viongozi wa kawaida wana influence kubwa ndani ya chama hicho.Wakati uongozi wa CCM Zanzibar unaweza kuridhia mgombea ajaye ataoke Bara,ni vigumu kuhisi wanachama na viongozi wa kawaida wakakubali miaka mingine 10 pasipo Mzanzibari mwenzao kushika urais kupitia CCM.
Iwapo CCM Bara watashinikiza lazima mgombea atoke Bara basi Wazanzinari wanaweza kutumia turufu ya "tunatoka nje ya Muungano" na hili linaweza kuzua sokomoko kubwa.
MGOMBEA/RAIS MUISLAM KISHA MKRISTO (na vice versa)
Utamaduni mwingine ndani ya CCM ni kuzungusha nafasi ya urais (au mgombea wa urais) kati ya Waislam na Wakristo.Baada ya miaka kadhaa ya utawala wa Mwalimu Nyerere ikaja zamu ya Muislam Mwinyi,ambaye naye alirithiwa na Mkristo Mkapa,kabla ya ujio wa Muislam Kikwete.Katika mambo ambayo CCM inapaswa sifa nyingi ni pamoja na umakini wake katika kudili na ishu nyeti ya dini (japo wanasiasa mufilisi wameanza kutumia udini kwa minajili ya kusaka mafaniko yao binafsi kisiasa).Chama hicho kimejitahidi sana kuzingatia ukweli wa mgawanyo wa kiimani miongoni mwa Watanzania ambapo Waislam na Wakristo wanatengeneza takriban robo mbili za wakazi wote wa nchi yetu (robo nyingine ni wanaofuata imani nyingine pamoja na wapagani)..
Sasa,kwa kuzingatia ukweli kuwa Kikwete ni Muislam,inatarajiwa mgombea urais wa CCM mwaka 2015 awe Mkristo ili kudumisha utamaduni huo usio rasmi.Iwapo mgombea huyo atatoka Bara,haitokuwa vigumu kumpata.Tatizo ni iwapo mgombea atatakiwa kutoka Zanzibar.Kama tujuavyo,takriban asilimia 99 ya Wazanzibari ni Waislam,na hali ni kama hiyo kwenye uongozi wa CCM visiwani humo.Uwezekano wa kumpata mgombea urais kutoka Zanzibar ambaye ni Mkristo ni mgumu pengine kuliko uwezekano wa Gaddafi kuwa mgombea urais wa Marekani kuchuana na Rais Barack Obama hapo mwakani.
Kwa mantiki hiyo,kama changamoto ya kwanza itapatiwa ufumbuzi,yaani CCM kufanikiwa kupata mgombea wake kutoka Zanzibar,tatizo litabaki kwenye changamoto ya pili,yaani kupata mgombea Mkristo kutoka visiwani humo.
CHAGUO LA KIKWETE
Ni wazi Rais Kikwete angependa kupata mrithi atakayeweza kumpa amani baada ya kustaafu.Baada ya kuonjesha ladha ya 'ujeuri' pale baadhi ya vigogo wa chama hicho wanapodaiwa kutaka kumng'oa kwenye kiti cha uenyekiti wa chama hicho kwa kigezo cha kutenganisha kofia ya urais na uenyekiti wa CCM,yayumkinika kuamini kuwa asipokuwa makini kumpata mrithi atakayehakikisha anakula pensheni yake bila usumbufu wala hofu ya kukumbana na yaliyomkuta Chiluba...
Lakini Kikwete kulazimisha chaguo lake kutategemea namna atakavyoweza kumpromoti kuanzia sasa.Wachambuzi wengi wa siasa zetu wanafahamu kuwa Kikwete hana sauti kubwa ndani ya chama hicho.Kimsingi,mtu kama Edward Lowassa ana nguvu takriban mara mbili ya alizonazo Kikwete ndani ya chama hicho.Nguvu pekee ya mwenyekiti huyo ni kutoka kwa watu wa Idara ya Usalama wa Taifa ambao licha ya kumpatia dossiers zenye "machafu" ya viongozi wenzie wa CCM,pia wanaweza kulazimisha matakwa ya Kikwete yakatimia kwa mbinu chafu za kiintelijensia.Hilo linafanyika sehemu nyingi tu duniani ambapo siasa na intelijensia zimefunga ndoa isiyo rasmi.
Lakini hili la mashushushu kuingilia siasa za ndani ya CCM linategemea zaidi siasa za ndani za Idara ya Usalama wa Taifa.Wajuzi wa mambo wanafahamu mgogoro wa chini chini ndani ya Idara hiyo kuelekea mchakato wa CCM kumpata mgombea wake mwaka 2005.Tofauti za kimaslahi miongoni mwa viongozi waandamizi wa Idara hiyo zilitishia kwa kiasi kikubwa jina la Kikwete kupitishwa,na hata alipofanikiwa kupitishwa na hatimaye kushinda urais baadhi ya viongozi waandamizi wa Idara hiyo walijikuta majeruhi.
LOWASSA NA 'PIGA UA' YAKE
Mpende au mchukie, lakini Edward Lowassa ameendelea kuwa mwanasiasa mwenye nguvu na ushawishi mkubwa ndani na nje ya CCM.Licha ya uwezo wake mkubwa wa kifedha,Lowassa amewasaidia viongozi wengi wa CCM kuwepo madarakani,iwe kwa misaada ya kifedha au kimkakati.
Japo hajaweka msimamo wake hadharani,wachunguzi wengi wa siasa wanaamini kuwa ndoto za mwanasiasa huyo kumrithi Kikwete bado zipo hai.Inaaminika kuwa chanzo cha ndoto hizo ni mkataba usio rasmi kuwa Kikwete angemwachia Lowassa jahazi la kuongoza Tanzania baada ya kumaliza miaka yake 10 ya Urais.Mahesabu yalikwenda vizuri hadi pale ilipoibuka skandali ya Richmond iliyopelekea Lowassa kuachia ngazi.Laiti hilo lisingetokea basi muda huu wala nisingeandika makala hii kwa vile ingekuwa wazi kuwa Lowassa ndiye Rais ajaye baada ya Kikwete.
Kinachomsaidia Lowassa ni jinsi anavyotumia kila nafasi ipasavyo kuhakikisha jina lake linaendelea kuwa masikioni mwa Watanzania.Mwanasiasa huyo yupo radhi hata kuwaunga mono wanasiasa wa vyama vya upinzani alimradi kufanya hivyo kunamweka karibu zaidi na wapiga kura.
Kadhalika,pamoja na kuhusishwa na ufisadi,Lowassa anakubalika kama mtu anayemudu kufanya anachoamini,jambo linalomtofautisha na Rais Kikwete ambaye anaelemewa zaidi na kutaka kuwafurahisha watu wake wa karibu.Lowassa yupo tayari aonekane mbaya ndani ya CCM lakini aishie kuonekana mkombozi kwa Watanzania.
Na katika kumtendea haki,Lowassa ana 'u-Sokoine' wa namna flani.Hasiti kutoa maamuzi na anaweza kusimamia maamuzi yake.Laiti mwanasiasa huyu asingekuwa na mawaa ya ufisadi basi Tanzania ingeweza kupata carbon copy ya Sokoine.
Kuna wanaomwona Lowassa kama mwanasiasa anayeweza kubadilika kwa sababu kuu mbili.Kwanza,utajiri mkubwa alionao unaweza kabisa kumshawishi asitumie madaraka yake kuendeleza utaratibu wa kuifanya Tanzania kuwa shamba la bibi.Japo utajiri sio kigezo cha fisadi kutotamani fedha zaidi lakini madaraka kama ya Urais yanaweza kumfanya mtu apate huruma kwa anaowaongoza.Kikwete ana huruma lakini tatizo ni kwamba huruma yake kwa mafisadi ni kubwa ziadi ya ile aliyonayo kwa walalahoi.Hilo halina mjdala na mwenyewe anajua hilo.
Kingine kinachoweza kumpa faida Lowassa ni network yake ambayo inaweza kabisa kupenya Zanzibar kuwashawishi wamuunge mkono.Ukichanganya na advantage nyingine kwamba yeye ni Mkristo (ambayo inamfanya awe eligible kwa mujibu wa changamoto ya pili hapo juu),
Lakini pengine faida nyingine aliyonayo mwanasiasa huyu ni ukaribu wake na Idara ya Usalama wa Taifa,ambayo penda usipende itacheza nafasi muhimu kwa mgombea mwana-CCM yeyote anayetaka kumrithi Kikwete.Japo sina hakika kwa sasa ukaribu huo upo katika hali gani lakini unaweza kuwa na faida kubwa kwake.
Kubwa zaidi ya yote ni ukweli kwamba Lowaasa anamfahamu Kikwete in and out.Kwa mantiki hiyo,anaweza kumwandama Kikwete hata atakapomaliza muda wake wa Urais.Na kwa vile by then Kikwete hatokuwa na nguvu za kutosha ukilinganisha na hali ilivyo sasa ambapo yeye ni mkuu wa nchi, yayumkinika kuamini kuwa angependa kuwa na maadui wachache wenye nguvu na uwezo wa kumwangamiza.Kikwete anaweza kujikuta anakabiliwa na mzimu uleule ambao yeye na wanamtandao wenzake walimsababishia Rais Mkapa.
Inafahamika kuwa Kikwete na timu yake waliweka wazi kwa Mkapa kuwa laiti asingepitishwa basi aidha angegombea (na pengine kushinda) kupitia tiketi ya chama cha upinzani.Sasa ukizingatia Kikwete hakuwa karibu kihivyo na vyama vya upinzani kwa wakati huo,ukaribu wa Lowasaa kwa wapinzani unaweza kulifanya tishio la aina hiyo kuchukuliwa kwa uzito mkubwa.Ikumbukwe kuwa nafuu pekee kwa Kikwete atakapostaafu ni kwa CCM kubaki madarakani kwani kuna kila dalili kuwa kama chama cha upinzani kikishinda basi anaweza kabisa kupandishwa kizimbani kujibu tuhuma lukuki za ufisadi.
Je CCM wanawezaje kukabiliana na changamoto hizi?Moja ya njia mwafaka ni kujaribu kuiga utaratibu wa siasa za uchaguzi nchini Marekani ambapo wananchama wenye nia ya kuwania kupitishwa kugombea urais wanatangaza dhamira zao mapema.Pamoja na faida ya kumfanya mwanachama mwenye dhamira hiyo kufahamika vema kwa wapiga kura,utaratibu huo unaambatana na hatari zake.Kwa mwananchama kujitambulisha hadharani mapema anaweza kuwapatia maadui zake wa kisiasa ammunition ya kutosha kumteketeza mapema,na ikifika wakati wa kupiga kura za kumpitisha mgombea anaweza kuwa amekwisha kabisa.
Anyway,kwa leo naomba kuishia hapa.Nitaendelea na mada hii wakati mwingine
0 comments:
Post a Comment