Sunday, 2 October 2011


Wenzetu Zambia wameweza, sie ‘tumerogwa’ na nani?
Evarist Chahali
Uskochi
28 Sep 2011
Toleo na 205
WIKI iliyopita tumeshuhudia wenzetu wa Zambia wakiamua kukipa kisogo chama tawala baada mgombea wa kilichokuwa chama cha upinzani cha Patriotic Front, Michael Sata kuibuka mshindi katika uchaguzi mkuu wa nchini humo.
Sata, anayefahamika pia kwa jina la utani la King Cobra, alimbwaga aliyekuwa Rais na mgombea wa chama tawala cha Movement for Multiparty Democracy (MMD), Rupiah Banda.
Katika mazingira ya kawaida ya siasa za Afrika, yayumkinika kuhitimisha kuwa ni vigumu sana kwa chama cha upinzani kushinda uchaguzi mkuu. Kikwazo kikubwa ni jinsi vyama tawala barani Afrika hutumia kila mbinu kuhakikisha kuwa utawala wao unadumu milele.
Kimsingi, hakuna tatizo kwa chama kimoja kuwa madarakani muda mrefu.Tatizo ni pale uwepo madarakani wa chama hicho unavyozidi kuididimiza nchi husika katika nyanja mbalimbali za maisha.
Kanuni isiyo rasmi ya kisiasa katika bara hili inatanabaisha kuwa ‘chama tawala hakiwezi kushindwa uchaguzi,’ na ikitokea kikashindwa basi labda ni kutokana na sababu kuu tatu.
Kwanza, kuteua mgombea asiyekubalika na wengi ndani ya chama hicho na hivyo kupelekea kura za chuki dhidi yake ambazo zitamnufaisha mpinzani wake mkuu.
Pili, katika sababu inavyoweza kushabihina na hiyo ya kwanza, ni pale chama tawala kinapogubikwa na migogoro isiyoisha na hatimaye baadhi ya waandamizi ndani ya chama hicho kukimfanyia hujuma mgombea wao kwa minajili ya kukomoana.
Sababu ya tatu ni ulevi wa madaraka. Pengine mfano mwepesi ni wa nyoka chatu ambaye akishakula kiumbe mkubwa anakuwa kama mfu. Anajisahau na laiti ukimwona kichakani baada ya mlo huo unaweza kudhani amezimia kama si kufa kabisa.
Sasa, baadhi ya vyama tawala baada ya kuwa madarakani muda mrefu vinafikia hatua ya kujisahau kwanini vipo madarakani.Vinaendesha mambo kwa mtindo wa ‘bora liende.’
Lakini sababu zote hizo hapo juu zinaweza zijitosheleze kukiondoa chama tawala madarakani kwa sababu mara nyingi uwepo madarakani wa chama hicho unazinufaisha taasisi nyingine  zisizo za kisiasa, kwa mfano vyombo vya dola.
Kuna imani kwamba taasisi za usalama kama vile jeshi la polisi, idara za usalama wa taifa na hata jeshi huenziwa vya kutosha na vyama tawala kiasi cha kujenga kile kinachofahamika katika elimu-viumbe (baiolojia) kama symbiotic relationship. Huu ni aina ya uhusiano wa kutegemeana, uhai wa mmoja ni uhai wa mwingine.
Taasisi hizo za dola hujenga au kujengewa imani potofu kwamba pasipo chama tawala kuwepo madarakani basi nazo zinaweza kupoteza uhai wake.Unaweza kujiuliza kwa nini taasisi yenye watu kadhaa ikajazwa imani potofu kirahisi namna hiyo?
Jibu ni kwamba mara nyingi taasisi hizo, kama ilivyo mazoea ya siasa katika nchi mbalimbali za Afrika, huongozwa kibinafsi. Mkuu wa taasisi husika hugeuka kuwa kama mmiliki wake.
Na marais huwa makini katika kufanya teuzi ambapo kigezo kikubwa huwa utiifu wa mteuliwa kwa Rais (sio utiifu kwa mujibu wa sheria na kanuni bali kwa sababu za kibinafsi).
Kwa hiyo, viongozi wa taasisi hizo hugeuka kuwa kama kirefusho (extension) cha matakwa binafsi ya Rais katika taasisi husika. Lengo ni kuhakikisha rais na chama chake wanaendelea kuwepo madarakani; huku taasisi hizo zikipindisha utekelezaji wa majukumu yake kwa manufaa ya chama tawala.
Watendaji katika taasisi hizo huaminishwa kuwa wanachofanya ni kwa mujibu wa sheria zinazoongoza utendaji kazi wao; japo kiuhalisia wanaotekeleza matakwa binafsi ya rais na swahiba yake aliyekabidhiwa jukumu la kuongoza taasisi husika.
Katika mazingira ya kawaida ya siasa zetu, vyama vya upinzani vinapopambana na chama tawala vinakutana na mazingira kama haya ya kinadharia ambapo kesi dhidi ya mtuhumiwa mahakamani inaendeshwa na mshtak ambaye pia ndio hakimu na mwendesha mashtaka. Ni wazi katika kesi ya aina hiyo ni lazima mtuhumiwa ashindwe na mshtaki ashinde.
Au mfano mwingine rahisi (wa kinadharia pia) ni pale timu ya soka inapopambana na timu nyingine yenye wachezaji 15; yaani wachezaji 11 wa kawaida wakisaidiwa na refa, washika vibendera wawili na kamisaa. Haihitaji kuwa na ufahamu wa soka kuelewa timu gani kati ya hizo mbili itaibuka mshindi.
Kwa huko nyumbani, ushindi wa Sata si habari njema kwa chama tawala CCM, chama ambacho hakina maelezo ya msingi ya kwa nini nchi yetu yenye utajiri lukuki inaendelea kuelemewa na lindi la umasikini unaochangiwa zaidi na ufisadi (huku wahusika wakuu wa ufisadi wakiwa ni baadhi ya viongozi wa chama hicho au wanapatiwa hifadhi salama dhidi ya hatua za kisheria).
Yayumkinika kuhisi kuwa CCM wanaombea hali nchini Zambia ichukue mkondo kama ule wa Kenya pale muungano wa wapinzani ulipofanikiwa kuking’oa madarakani chama kikongwe cha KANU. Kwa bahati mbaya (au makusudi) mabadiliko ya kisiasa nchini Kenya yalianza kwa dalili mbaya za vurugu zilizopelekea vifo kadhaa vya wananchi wasio na hatia.
CCM hawakushindwa kutumia mfano wa Kenya kuhalalisha hoja yake mfu kuwa ‘wapinzani wapo kwa ajili ya vurugu tu.’
Sijui sasa watasemaje kuhusu wapinzani kuchukua serikali nchini Zambia tukitarajia yaliyojiri Kenya hayatojitokeza kwa jirani zetu hao tunaounganishwa nao na Reli ya TAZARA (ambayo nayo iko hoi bin taaban kama ulivyo uchumi wetu).
CCM pia wana hoja yao nyingine maarufu kila unapokuja uchaguzi, iwe ni uchaguzi mdogo au uchaguzi mkuu ambapo huwalaghai wapigakura kwamba wasifanye kosa kuwapa madaraka wapinzani ambao hawana uzoefu wa kuongoza.
Hoja hiyo ni fyongo kwa sababu hakuna mwananchi anayehitaji chama chenye uzoefu wa ufisadi. Ni bora kufanya majaribio na chama mbadala cha upinzani - ambacho yawezekana kabisa kikawa makini kwenye utawala wake kwa kuhofia kung’olewa kama mtangulizi wake - kuliko kuking’ang’ania chama kilichoishiwa na uwezo wa kuongoza.
Ukiona chama kikongwe kinaruhusu viongozi wake kupanda majukwaani na silaha waziwazi (kama huko Igunga), basi, ujue tukiendelea kukiweka madarakani tutafika pabaya.
Siichukii CCM; bali nachukizwa sana na jinsi kinavyowafanya Watanzania kama wapangaji katika nchi yao. Kila kukicha ni hadithi za kukera na zisizoleta matumaini, ukiweka kando tuzo lukuki anazotunukiwa Rais wetu mpendwa Jakaya Kikwete huko nje ‘kwa kazi nzuri anayofanya kuongoza taifa letu.’
Ni fahari kuona Rais akipewa tuzo lakini ni matusi makubwa kutoka kwa watoa tuzo hizo pale wanapofumbia macho sababu zinazotufanya tuendelee kuwa masikini wa kutupa. Rais Kikwete anaweza kumaliza uongozi wake akiwa na historia ya kutunikiwa tuzo nyingi zaidi pengine zaidi ya Baba wa Taifa, lakini Watanzania hawatamkumbuka kwa tuzo hizo au picha aliyopiga na rapa 50 Cent; bali aliwafanyia nini katika miaka yake 10 ya utawala.
Mazoea yana athari moja kubwa ya kumfanya mwadamu akubali mabaya kwa vile tu yamekuwepo siku zote. Mazoea kwamba siku zote tumekuwa tukitawaliwa na CCM ni miongoni mwa sababu za takriban kila baya linaloweza kukufanya umlaumu Muumba kwa kukufanya uzaliwe nchini Tanzania.
Kwa hakika, wanaomlaumu Mungu kwa matatizo yetu wanatafuta ugomvi nae tu; kwani ametupa macho ya kuona uhuni tunaofanyiwa,ametupa ubongo wa kutuelewesha kuwa chini ya utawala wa CCM tutaendelea kuwa na maisha bora kwa mafisadi; huku walalahoi wakizidi kudidimia katika lindi la umasikini.
Na  ametupa masikio kusikia jinsi tuliowakabidhi dhamana ya kutuongoza wakitufisadi na kutukejeli kwa anasa zao za safari zisizoisha huko ng’ambo, visenti kwenye akaunti zao Ughaibuni, na utitiri wa mahekalu, magari ya kifahari na mapande makubwa ya ardhi waliyohodhi.
Kama Zambia wameweza, basi, nasi tunaweza pia. Na pengine hakuna namna nzuri ya wapiga kura kutoa pongezi kwa wenzao wa Zambia zaidi ya kuanza na fundisho la kwanza kwa CCM huko Igunga.
Kwa vile uhuni wa mbunge wa CCM Ismail Aden Rage kupanda na bastola kwenye mikutano wa kampeni hautopelekea hatua zozote za kisheria (hadi muda huu ninapoandika makala hii kilichofanyika ni kauli tu ya Waziri wa Mambo ya Ndani kutaka Rage ahojiwe badala ya kukamatwa),adhabu kubwa inaweza kutolewa na wapiga kura wa Igunga kwa kuigaragaza CCM, na kuitumia salamu kuwa kama imewezekana Zambia, Igunga napo inawezekana, na kwa hakika hata 2015 inawezekana kwa mapana zaidi.
Ndio, inawezekana iwapo kila mzalendo mwenye uchungu na Tanzania yetu atakapoamua kuwa IMETOSHA!

0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget