Monday, 10 October 2011


Nyakati za Ujamaa na Kujitegemea tulifundishwa kuwa maadui wakubwa wa maendeleo ni ujinga,maradhi na umasikini.Na tuliaswa kuhakikisha tunapambana nao kwa nguvu zote.Lakini mambo haya matatu si binadamu bali ni hali ya kimaisha.

Kibinadamu,tulifundishwa kuwa maadui wakubwa ni wanyonyaji-makupe,makabaila,mamwinyi,ma-mangi meza,na viumbe wengine kama hao.

Baada ya itikadi ya Ujamaa kuzikwa hai na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Pili,Ali Hassan Mwingi na kundi lake,utambulisho wa maadui zetu ulibaki wa kusuasua.Lakini tulipoingia kwenye siasa za vyama vingi,wakazuka maadui wapya.Kundi moja-ambalo na akina sie (waropokaji au vimbelembele-kama wanavyotuita watawala) lilikuwepo hata zama za Ujamaa.Uzuri au ubaya ni kwamba nyakati hizo haikuwa rahisi kupingana au kuwa na mawazo tofauti na watawala.Na 'vimbelembele' na 'waropokaji' waliishia jela kama si kusumbuliwa kwa muda wao wote wa uhai wao.

Baada ya mageuzi ya kisiasa na kiuchumi,kundi hili limeendelea kunyanyaswa japo kwa wakati huu sio waziwazi.Akina Marehemu Katabalo,Kolimba na wengineo ni majeruhi wa hasira za watawala na washirika wao dhidi ya kundi hili.Na hadi leo wapo wenzetu wengi tu ambao wananyanyaswa na vyombo vya dokla kwa kosa la kusema ukweli ambao watawala na washirika wao hawataki usemwe.

Lakini kundi jipya la maadui baada ya ujio wa mageuzi ni vyama vya upinzani.Pamoja na CCM kuridhia kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi,wapinzani wameendelea kujengewa picha kwenye jamii kama watu wa kuogopwa kama ukoma.Wanahujumiwa kwa fedha za walipa kodi,wanasemwa vibaya na kupachikwa majina mabaya kuliko makupe,makabaila,nk.

'Kosa' kubwa  la wapinzani ni kutaka kuwanyang'anya watawala na washirika wao fursa ya kuendelea kutukandamiza.Wanaonekana kama walafi na waroho wa madaraka (watakuwaje waroho wakati wameingia juzi tu ilhali kuna watu wanazeekea madarakani?).Hoja inayojengwa ni kwamba walikimbia CCM na kujiunga na upinzani si kwa minajili ya kuutumikia umma kwa siasa bali kutokana na tamaa,ulafi na uroho wao wa madaraka.

Ukimsikia mtu kama Nape Nnauye akiwazungumzia wapinzani unaweza kabisa kuhisi kuwa anawazungumzia Taliban au Al-Shabaab.Picha inayojengwa ni ya viumbe hatari kuliko virusi vya ukimwi.

Kwa muda mrefu CCM imekosa sauti za kusisitiza mshikamano wa kitaifa (ambapo hata wapinzani wana jukumu hilo) na badala yake nguvu nyingi zimeelekezwa katika kupanda mbegu ya chuki.Wapinzani wanaonyeshwa kama sio Watanzania,na pale inapobidi kuwakubali kuwa ni Watanzania wenzetu basi jitihada zinafanywa kujenga picha kuwa wenzetu hao wanataka kuitumbukiza nchi yetu kwenye shimo lenye kina kirefu.

'Kosa' jignine la wapinzani ni kutumia nafasi waliyonayo kupigania maslahi ya wananchi,ambao kwa kiasi kikubwa wanaendelea kutapeliwa na watu wanaolipwa mshahara kwa kazi ya kuwawakilisha-I mean Wabunge wetu.Hatuhitaji kuingia kwa undani kuhitimisha kuwa wengi wa wabunge wetu ni sawa na majambazi tu ambao wanalipwa mishahara minono pasipo kuwatumikia wapiga kura wao ipasavyo.Nasisitiza,NI BAADHI TU ya wabunge.

Sasa katika pitapita zangu mtandaoni nimekutasna na habari ifuatayo ambayo kwa hakika imenitia nguvu sana.Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM, Benno Malisa ameonyesha ukomavu wa hali ya juu kisiasa kwa kuongea masuala ambayo kwa hakika ni kwa maslahi ya taifa na si ya kichama.

Najua kuna watakaomsema vibaya-hususan ndani ya chama chake-lakini uzuri wa ukweli ni kwamba ukishawekwa hadharani,atakayeumia na aumie lakini hakuna wa kuufuta.Wapo watakaodai Malisa ameanza kumpigia debe mmoja wa wanaotajwa kutaka Urais 2015 (nadhani itakuwa ni Lowassa) na wengine wanaweza kumtuhumu kuwa huenda hata yeye (Malisa) ana nia ya kugombea urais.

Sijawahi kumsifia Malisa lakini kwa hili NINAMPA TANO.Namsihi apuuze tuhuma zote zitakazoelekezwa kwake kwa 'kosa' la kusema 'yasiyopaswa kusemwa.' Laiti tukiwa na viongozi wanaodiriki kueleza hisia zao pasi kuhofia kuwachukiza watu fulani (na wanachokiongea kuwa chenye maslahi kwa umma) basi kwa hakika tunaweza kufanya mijadala muhimu kuhusu taifa letu na kuzika chuki zisizo za msingi dhidi ya wale wanaoongea tusiyopendezwa nayo.

Nisiandike mengi,hebu soma habari ifuatayo:

UVCCM yataka CCM isiifuatefuate Chadema
Monday, 10 October 2011 22:27
Waandishi wetu, Arusha 
KAIMU Mwenyekiti wa Umoja Vijana wa CCM (UVCCM), Benno Malisa amewataka vigogo ndani ya chama hicho tawala kuacha kuingilia mambo ya chama kikuu cha upinzani nchini, Chadema hasa mgogoro wake na madiwani wa Arusha Mjini na badala yake watafute suluhu ya matatizo ya msingi yanayoikabili nchi kama mfumuko wa bei na tatizo la ajira.Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Hospitali ya Mtakatifu Thomas, Malisa alisema wapo baadhi ya watu ndani ya CCM ambao siyo wana Chadema lakini wamekuwa wakijihusisha na mgogoro wa chama hicho pinzani. 
Alisema wana CCM hao wamekuwa wakiingilia mgogoro kati ya Chadema na madiwani wake ambao tayari chama hicho kilikwishaamua kuwafukuza na kusisitiza kuwa mambo ya chama hicho pinzani yaachwe yasiingiliwe. 
Kauli hiyo ya Malisa inakuja kipindi ambacho Chadema kimekuwa kikilalamikia baadhi ya mawaziri wa Serikali kupuuza uamuzi wake wa kuwatimua madiwani wake.
Chadema imewahi kumnyooshea kidole Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi,) George Mkuchika kwamba alikuwa na ajenda ya siri baada ya kuendelea kuwatambua madiwani hao.
Pia Chadema kimekuwa kikituhumu baadhi ya makada wa CCM mkoa wa Arusha na taifa, kujaribu kuingilia uamuzi huo wa Chadema wa kutimua madiwani hao kutokana na uamuzi wao wa kuingia muafaka wa Umeya wa Arusha. 
Kaimu Mwenyekiti huyo wa UVCCM, alisema si sahihi kwa CCM kutumia hata vyombo vya serikali kudhoofisha demokrasia kwa vyama vya upinzani akionya kwamba
mwisho wa siku matokeo yake hayatakuwa mazuri kwa taifa. 
Alisema demokrasia inapaswa kuachwa ichanue kwa vyama vya upinzani ili kujenga ustawi mzuri wa nchi.

“Nitumie nafasi hii kumuomba Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), kaka yangu (Godbless) Lema kuwa mstari wa mbele katika kuleta umoja na mshikamano hapa mjini na kumaliza tofauti za UCCM na UCDM (U - Chadema) ili wakazi wa Arusha wapate maendeleo. Sasa uchaguzi umekwisha tujenge nchi yetu.” 
Alisema CCM kinapitia katika wakati mgumu hivi sasa na kuonya kwamba badala ya kuisimamia Serikali wapo wanaohangaika kutafuta wachawi na kutuhumu watu. 
“Tuache kabisa. Hili jambo halisaidii chama wala taifa letu, kumekua na dhana na fikra potofu juu ya ushindi wetu wa 2010 matokeo yale na tuliyoyaona Igunga ni funzo kwetu na hasa vijana,” na kuongeza kuwa vijana wengi wameanza kukosa imani na CCM kwa sababu: 
“Tunashindwa kuwaonyesha kuwa tuna majibu ya matatizo yao. Tumebaki tunaimba historia na kumtaja Baba wa Taifa na kutumia nukuu zake bila kuwapa matumaini vijana kuwa Tanzania yao itakua njema, watapata elimu nzuri, afya na itakua ya uhakika.” 
Alisema vijana wanataka kusikia uchumi umekua, ajira zinapatikana, fursa za kujiajiri zipo, mikopo inapatikana na kusisitiza: “Tusipotoa matumaini haya na kuyafikia 2015, wapiga kura milioni sita wapya watatukataa, uelewa wa vijana wa Kitanzania sasa umekua mkubwa. Wanajua haki na wajibu wao tuache kufanyia siasa maisha ya Watanzania.” 
Wanaotaka urais 2015
Akizungumzia mbio za urais kwa mwaka 2015 ndani ya CCM, Malisa aliwataka makada wa chama hicho wanaotaka kuwania nafasi hiyo kuacha kuwagawa vijana na kuvuruga chama akisema kufanya hivyo ni hatari kwa uhai wa chama. 
“Wapo baadhi ya watu wanaopita wenzangu msiishi kwa kutarajia madaraka ya kupewa wapo wengine wanapita wanakusanya CV za vijana na kuwaahidi vyeo vya U-DC. Msipotoshwe na wala msifungwe fikra kwa sababu mmepewa ahadi ya kuteuliwa U DC. Tuna bahati mbaya wapo ambao mpaka leo wanaishi kwa kusubiri U DC wamegeuka kuwa ndiyo mzee na watumwa kifikra, tuukatae utumwa huu UVCCM.” 
“Tusiwe ndiyo mzee. Nawaagiza wenyeviti na makatibu wa mikoa na wilaya zote Tanzania, wafuatilie katika halmashauri zao kujua mipango ya maendeleo inayohusu vijana na kufuatilia utekelezaji wake wakiona hakuna utekelezaji, watumie kamati za siasa za wilaya kuwabana wenyeviti wa halmashauri. Nazitaka wilaya zote zifuatilie zituletee taarifa juu hili jambo. Tusikubali kuwa ndiyo mzee lazima tusimamie maslahi ya Vijana.” 
Alisema huu si wakati Serikali ya CCM kukaa likizo badala yake ifikirie namna ya kufikia matarajio ya Watanzania. 
Dowans
Akizungumzia suala la mitambo ya Dowans Malisa alisema: “Watu waliosababisha hasara wawajibike, walitudanganya. Kama taifa leo tumeshindwa kesi mitambo ile waliyosema haifai leo inatumika na kampuni ya Symbion. Wanatufanya Watanzania mazuzu. Walisema heri tukae giza wakati wao wanatumia majenereta na wanalipiwa na Serikali huku wakinunua aspirini kwa mamilioni.” 
“Leo wanajifanya wazalendo. Nilitarajia wawajibike walidanganya taifa, Serikali ikavunja mkataba. Wakasema mitambo haifai mibovu leo imenunuliwa na Wamarekani na wanatuuzia umeme... wanafiki wametufikisha hapa niwaombe UVCCM na vijana wa vyama vyote tuungane hawa wawajibike.” 
Watunishiana misuli na polisi
Kabla ya kuhutubia, Malisa na msafara wake waliingia katika mgogoro na vyombo vya dola, baada ya kufanya maandamano na mikutano ya uzinduzi wa matawi mapya ya UVCCM ambayo awali, yalizuiwa na polisi kabla ya kuruhusiwa baadaye. 
Mamia ya vijana wa CCM walianza kukutana kuanzia asubuhi katika Ofisi za UVCCM mkoani hapa, lakini walipoanza matembezi walizuiwa na polisi mbele ya Jengo la CCM Mkoa. 
Sababu ya kuzuiwa inaelezwa kuwa ni mgogoro ndani ya chama hicho katika Wilaya ya Arusha. Viongozi wa umoja huo wanadaiwa kupinga ziara ya viongozi hao wa kitaifa. Hata hivyo, maandamano hayo yaliendelea baada ya mazungumzo baina ya polisi na viongozi hao wa UVCCM huku wakikubaliana njia za kupita. 
Lakini, mara baada ya kukamilika kwa uzinduzi wa matawi hayo viongozi wa umoja huo walionyesha kukerwa kwao na hatua ya polisi na baadhi ya viongozi wa chama hicho kutaka kuzuia kazi hiyo. 
Habari hii imeandikwa na Mussa Juma,Peter Saramba na Moses Mashalla


CHANZO: Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget