Makala hii ilitarajiwa kuchapishwa katika tole la wiki hii la jarida la Raia Mwema.Sina hakika kama ilichapishwa au la kwa viletovuti ya gazeti hilo haipatikani mtandaoni hadi muda huu
Kuna msemo miongoni mwa Wamarekani Weusi kwamba unaweza kumtoa Mtu (Mmarekani) Mweusi kutoka ghetto lakini huwezi kutoa ghetto ndani ya Mtu Mweusi. Kwa kifupi kabisa, ghetto ni makazi ambayo kwa tafsiri isiyo rasmi ni kama ‘uswahilini.’
Kadhalika, katika mazingira yetu tunaweza kabisa kusema unaweza kumtoa mshamba kutoka kijijini lakini huwezi kuondoa ukijijini ndani ya mshamba. Hapa neno mshamba halina maana ya kudharau watu ambao hawakuzaliwa mijini, mie nikiwa mmoja wao.
Wakati nikiwa kijana mdogo kulikuwa na mtizamo kuwa ushamba (kwa maana ya kutozaliwa mjini) ni kama ugonjwa flani hususan kwenye mikusanyiko kama mashuleni au hata vijiweni (mijini).Ninakumbuka wakati ninasoma Tabora Boys’ High School, rafiki yangu mmoja aliomba nimpatie albamu yenye picha zangu.
Nyingi ya picha hizo, kama si zote, nilipiga katika mjini mdogo wa Ifakara, ambapo katika suala la mjini na kijijini, inaangukia kundi la pili. Si kwamba Ifakara ni kijiji au sehemu iliyojaa mashamba lakini pia Ifakara si mjini kama Dar es Salaam. Kwahiyo kwa minajili ya makala hii, tuafikiane kuiita Ifakara kijijini.
Basi picha hizo kwa rafiki yangu huyo ambaye sio tu alikulia mjini bali pia alizaliwa “hospitali ambayo kila mtoto wa mjini kazaliwa,” (nikimaanisha hospitali ya Ocean Road) zilizua vicheko miongoni mwa wanafunzi wengine ambao walikuwa wanatokea Dar. Sikujilaumu kwa uamuzi huo wala sikuona aibu. Kwako ni kwako hata kukiwa porini.
Nilifika Dar kwa mara ya kwanza nilipokuwa kidato cha pili (katikati ya miaka ya 80).Nakumbuka jinsi lafidhi yangu ya Ifakara ilivyogeuzwa chanzo cha vichekesho kila nilipokwenda kwenye magenge ya maongezi (vijiweni).Lakini sikuona aibu kwa sababu lafidhi ya ‘kishamba’ si ugonjwa.
Nilipokuja Uingereza mara ya kwanza nikakumbana na tatizo kama hilo, ambapo lafidhi ya Kiingereza change ilikuwa imetawaliwa sana na Kiswahili, kiasi kwamba mara nyingi nilipoongea na wenyeji wa hapa waliuliza mara mbili mbili nilichokuwa nakiongea. Miaka 10 baadaye, lafidhi yangu haijabadilika sana.
Ahueni niliyopata kwa huku Scotland ni ukweli kwamba lafidhi ya Kiingereza cha Waskochi inawasumbua hata Waingereza wenzao wa sehemu nyingine (kwa mfano England).Lakini kikubwa zaidi kwa hapa ni ukweli kwamba lafidhi yako ni kitu cha kujivunia, ni sawa na utambulisho wako.
Msimamizi (Supervisor) wangu wa kwanza wa kozi yangu ambaye alikuwa mzaliwa wa Wales (na hivyo kujikuta anahangaika na lafidhi za Waskochi) alinitia hamasa kwa maelezo haya, “ukiongea huku una lafidhi flani basi inamaanisha una lugha au utamaduni zaidi ya mmoja, na hiyo ni faida kwako.”
Lengo la makala hii si kuchambua lafidhi au lugha bali kuzungumzia nafasi ya tabaka la kati ambalo kwa kiasi kikubwa linapatikana mijini, hususan jijini Dar. Katika jamii ya kinadharia, tunaweza kuwa na matabaka makuu matatu: tabaka la juu (Upper Class),tabaka la kati (Middle Class) na tabaka la chini (Lower Class).Kwa kifupi, kinachotenganisha matabaka hayo ni nguvu yao katika jamii (au power kwa kimombo).Kwa mantiki hiyo, tunaweza kuigawa jamii katika makundi ya ‘wenye nguvu’ (the powerful) na ‘wasio na nguvu’ (the powerless).
Ugumu uliopo katika kuielezea dhana ya matabaka katika jamii inatokana na ukweli kwamba takriban kila fani inayaangalia matabaka kwa mtizamo wake. Japo kuna mwingiliano, lakini dhana ya matabaka inaweza kueleweka tofauti kati ya fani ya siasa, uchumi, elimu jamii (Sociology), nk. Hapa nitaizungumzia dhana hiyo kwa mtizamo wa jumla pasipo kuelemea fani moja.
Ukiingia kwa undani sana utakuta kati ya matabaka hayo matatu kuna matabaka madogo madogo kwa namna hii: tabaka la kati la juu (Upper Middle Class), tabaka la kati la chini (Lower Middle Class), na tabaka la wafanyakazi (Working Class).Labda nitumie mchoro kama hivi: Tabaka la Juu→Tabaka la Kati la Juu→Tabaka la Kati la Chini→Tabaka la Wafanyakazi→Tabaka la Chini. Hii ni kwa mujibu wa mchanganuo wa kitaaluma wa matabaka wa karibuni zaidi (mwaka 2005) na ni kwa mujibu wa mtizamo mmoja wa kitaaluma wa Marekani.
Ili tuelewane, ni muhimu kuzingatia tahadhari niliyoitoa awali kuwa mgawanyiko huu ni wa jumla-jumla kwani kuna tofauti za kimtizamo miongoni mwa wachambuzi, fani na kanuni (theories) zinazohusu mada ya matabaka.
Pengine katika kurahisisha maelezo, mfano mwepesi ni wa kijana kama mie niliyekulia kijijini, mtoto wa mkulima, kisha nikaja mjini kupata elimu ya juu, na hatimaye kupata kazi. Ukiangalia mlolongo huo unaweza kubaini kuwa, kwa namna flani, nimetoka tabaka la chini na kuingia tabaka la kati. Pengine nikagombea ubunge (hapana, sina wazo hilo) nikamudu kuingia tabaka la juu.
Kwanini tabaka la kati lina umuhimu mkubwa katika mabadiliko ya jamii? Jibu jepesi ni kwamba tabaka hilo linatarajiwa kuelewa zaidi masahibu yanayolikabili tabaka la chini. Yaani kwa kutumia mfano wetu wa mie niliyetoka kijijini, sio tu ile lafidhi yangu iliyonifanya nichekwe mjini bali pia uzoefu wangu wa kijijini kuulinganisha na wa mjini unaweza kuniweka katika nafasi nzuri zaidi ya kuwa na msaada wa namna flani kwa ‘tabaka la kijijini’ (la chini).
Lakini tatizo lililopo katika jamii yetu (na hii ni kwa jumla-jumla) ni tabaka hilo la kati kutamani kuwa tabaka la juu, na hapo hapo kulipuuza tabaka la chini. Kwa kutumia mfano, kijana aliyetoka kijijini na kuwaacha wazazi wake wakihangaika na ufukara uliozoeleka kwenye tabaka la chini, anapata ajira baada ya kuhitimu masomo, na anajaribu kuishi maisha kama yale ya vigogo au watoto wao.
Ofkoz, Wanasema ukienda Roma inabidi uishi kama Warumi. Lakini hiyo haimaanishi usahau ulipotoka. Hapa ninamaanisha kuwa hakuna ubaya kwa kijana kutoka kijijini kujaribu kuendana na maisha ya ‘kimjini’ bali tatizo ni pale anaposahau ‘wajibu’ wake (ambao si wa lazima) wa kutumia nafasi aliyonayo kuhamasisha au kuchangia kuboresha tabaka wanaloishi wazazi, ndugu, nk huko kijijini.
Naomba pia tuelewane kuwa hapa ninatumia ‘umjini’ kama aina ya maisha ya jumla (kinadharia na wakati mwingine kiuhalisia) ya wakazi wa mjini. Yaani katika dhana ya kufikirika, chaguo la makazi kwa tabaka la juu ni mjini (japo haimaanishi kila anayeishi mjini yupo kwenye tabaka hilo).
Kuna wenzetu ambao hawajawahi kufika kijijini, na kwao Tanzania ni ile wanayoishi na kuiona mijini. Lakini kama ilivyo kwa nchi nyingi masikini, idadi kubwa ya wananchi wake wanaishia vijijini. Ukiwa umezaliwa na kukulia Masaki, Upanga, Mbezi Beach, nk na sehemu yako ya kazi ikawa Mjini Kati na maeneo kama hayo (na ikatokea hajawahi kufika kijijini) basi inaweza kuwa vigumu kwako kuielewa ‘Tanzania nyingine’ huko vijijini.
Wakati nipo huko nyumbani, kila mara niliposafiri kati ya Dar na Ifakara nilikuwa ninajaribu kuangalia namna mandhari na pengine hali ya mjini ‘inavyoyeyuka’ kadri safari ya kuelekea ‘kijijini’ ilivyokuwa inashika kasi. Na Nilipofika kijijini tofauti zilikuwa ni za wazi. Kwa mfano, wakati vitu kama magari na runinga vilionekana vya ‘kawaida’ kwa kijijini viliangaliwa kwa mtizamo ‘zaidi ya wa kawaida.’
Lakini pia hata katika suala la tabia za kibinadamu kulikuwa na tofauti. Kwa mfano, wakati mwanamke kuvaa suruali mjini halikuwa jambo ‘kubwa, kwa kijijini lingeweza kuzua picha tofauti. Ninasisitiza, huu ni mtizamo wa jumla na haimaanishi hali iko hivyo kila kijiji.
Wakati Tanzania yetu inahitaji mno maendeleo na kuondokana na umasikini (hususan huko vijijini), tabaka la kati lingeweza kuwa kiungo na nyenzo muhimu kwa, aidha kushiriki au kuunga mkono harakati za tabaka la chini, au kwa vile lina ukaribu na tabaka la juu, kujaribu kushawishi-au hata kuilazimisha- tabaka la juu liangalie na/au kushughulikia matatizo ya tabaka la chini.
Mabadiliko tunayoshuhudia yakiendelea kutokea sehemu mbalimbali duniani (kwa mfano nchini Tunisia, Misri, Libya, nk) yamechangiwa zaidi na muungano wa nguvu za matabaka haya mawili-la kati na la chini. Kwa bahati mbaya (au makusudi) kwa kiasi kikubwa tabaka la kati kwetu limekuwa likitamani zaidi kuwa tabaka la juu (kitu ambacho si kibaya endapo kitasaidia kulikwamua tabaka la chini) na kulisahau tabaka la walalahoi.
Nimalizie kwa kukiri kuwa ninafahamu mada hii inaweza kuleta mkanganyiko wa aina fulani lakini lengo ni kuhamasisha tabaka la kati kuunganisha nguvu na tabaka la chini katika kuikwamua Tanzania yetu kutoka kwenye lindi la umasikini (na ufisadi) na hatimaye kila Mtanzania aone fahari ya kuwa mwananchi wa Tanzania.
Inawezekana, timiza wajibu wako
0 comments:
Post a Comment