Na Nova Kambota Mwanaharakati,
Mara kwa mara huwa nasema tatizo kubwa la Tanzania yetu ni kupenda kupindisha ukweli, hii imetufanya kuwa watu tusiopenda kufikiri kiasi kwamba tunalambishwa kila linalokuja “tumekuwa madodoki kila uchafu tunasomba”. Naandika hivi kwa nia ya kujenga si kubomoa, naandika hivi kwa mustakabali wa Demokrasia yetu ambayo nathubutu kusema imetikiswa kupita maelezo huko Igunga na tusipokuwa makini Taifa litadondoka siku za usoni.
Kwako Dr Kafumu ambaye umetangazwa kuwa mbunge wa Igunga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), naomba unaposhangilia ushindi wako nikiamini wewe ni msomi na mzoefu katika Nyanja za uongozi wa Taifa hili napenda usome maandishi yaliyo ukutani kisha malizia kwa kuunganisha dots za ushindi wako halafu niambie ikiwa ni kweli unaamini kuwa umeshinda kihalali? Au la niambie kile ambacho kinaitwa “changamoto za uchaguzi Igunga” ni nini kama siyo “mizengwe?”
Kama mchambuzi nisiyeegemea upande wowote nisingependa kutia mwaa mtiririko huu wa hoja zangu kwa hiyo sitaegemea upande wowote bali nitajadili kwa misingi ya hoja ili ikibidi kujibiwa pia nijibiwe kwa misingi ya hoja vivyo hivyo, nataka kuibua hoja zenye mashiko ili zitufikirishe na kutupa majibu ya kisayansi badala ya kumezwa na mawimbi ya watu wenye mkatiko wa mirija ya fikra ambao wamebaki na ushabiki badala ya hoja kiasi kwamba wanatoa majibu ya zamani kwa maswali mapya. Yafuatayo ni mambo manne ambayo yanatia doa ushindi wa Dr Kafumu;
Kwanza Tume Ya Uchaguzi;
Tume ya uchaguzi ya nchi hii haina sifa nzuri na haiwezi kuwa na sifa nzuri mpaka iwe huru, hata I gunga hali ni hivyohivyo tumesikia malalamiko dhidi ya tume hiyo lakini hasa kwa aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa uchaguzi huo ambaye pia ni mteule wa rais na bila shaka kwa kuunganisha mantiki haina shaka kuwa naye ni mwanachama wa CCM au basi anaipenda kimoyomoyo. Uchaguzi wa Igunga ukipimwa kwa mizania hii ya aina ya tume ya uchaguzi tuliyonayo ni vigumu sana kwa mtu mwenye kufikiri kwa mantiki kuridhia matokeo ya uchaguzi huo.
Pili Siasa Uchwara;
Hapa inahitaji moyo mgumu kuyasema lakini kwa vile tangu awali nilishasema kuwa lengo si kufukua makaburi bali kuweka shada la maua juu ya makaburi basi acha niseme hiki ambacho nakiita ni siasa uchwara. Kwanza kabisa jinsi serikali ya CCM ilivyoruhusu kubofywa kwa kile kinachoitwa “kitufe cha udini”, ikumbukwe kuwa hata wakati wa uchaguzi serikali bado ina jukumu la kuilinda katiba na kuhakikisha amani haivurugwi aidha kupitia mirija ya udini wala ukabila, nayasema haya kutokana na baadhi ya viongozi wa dini kuirushia makombora CHADEMA tena wakaenda mbali kwa kutoa wito kwa baadhi ya waumini wa dini Fulani kutompigia kura mgombea wa chamna hiko, lakini cha ajabu hata hiyo hoja ya DC kuvuliwa hijabu imekwama kama gazeti nguli la Mwanahalisi lilivyofunua kuwa Mama Fatuma Kimario uislamu wake una mashaka kutokana na yeye kuwa ni mke halali wa Bw Kimario ambaye ni mkristu wa madhehebu ya Kikatoliki ambapo hata mwanazuoni mashuhuri wa kiislamu nchini Sheikh Issa Ponda amenukuliwa akisema kuhusu mwanamke au mwanaume wa kiislamu kubadili dini Sheikh Ponda amesema “Hilo ni kosa kubwa sana”. Lakini cha kusikitisha kuwa wakati haya yote yanatokea CCM walikaa kimya kana kwamba “hawakuliona kosa”, je tukisema kuwa hii ilichangia Wana Igunga kupiga “kura za chuki” dhidi ya CHADEMA tutakuwa tumekosea? Haya ni maswali magumu kuhusu ushindi wa Dr Kafumu.
Jambo la pili ambalo linaangukia kwenye siasa uchwara ni pamoja na vitimbi vya rushwa na vitisho vya “kipuuzi” mfano gazeti la Dira linamtaja mwenyekiti wa mtaa wa Nkokoto huko Igunga Bw Abed Motomoto (CCM) kuwa amekutwa akigawa rushwa “live”kwa wanawake wa mtaa wake kwa lengo la kuwashawishi kumpigia kura mgombea wa CCM (Dr Kafumu), lakini kama hili halitoshi kuna hili la Mh Ismail Aden Rage kupanda na bastola ikining’inia kiunoni halafu tunaambiwa kapewa adhabu ya kulipa laki moja, sasa ladda nitumie fursa hii kumuuliza ndugu yangu Aden Rage kuwa alikuwa anamtisha nani na bastola yake? Au nani kamwambia kuwa ni utamaduni wa kitanzania kuonyeshana vyombo vya moto? Haya ni machache kati ya mengi yanayokinzana na maana ya demokrasia pia kupoteza mantiki nzima ya “uchaguzi huru na wa haki”
Tatu kuchelewesha matokeo;
Hili ni tatizo linalotia huzuni sana kiasi kwamba nashawishika kuamini kuwa “bado tuna safari ndefu”, nayasema haya kwasababu kwanza idadi ya watu waliojiandikisha ni tofauti sana kwasababu waliopiga kura ni wachache wanaokadiriwa kuwa elfu sitini (60,000) lakini cha ajabu hata kiasi hiki kichache cha kura kimechukua masaa kibao zaidi ya kumi kuhesabu, hiki kama si kiroja ni nini? Au tuamini kuwa kuna lililojificha nyyuma ya pazia hapa?
Nne Matumizi Ya Nguvu;
Nalazimika kuyaandika haya kutokana na tabia inayozidi kukua siku hizi ya polisi kutumia nguvu dhidi ya wananchi , matukio ni mengi lakini hebu tutupie macho kwenye hili sakata la Igunga ambapo nasema kulikuwa na matumizi ya nguvu yasiyo na msingi, mabomu ya machozi ya nini? Watu walitawanywa kwasababu gani? Kwa mamlaka ya nani? Na faida ya nani? Je hii ndiyo demokrasia tunayoitaka? Huu ndiyo tunaouita ushindi halali? Uhalali uko wapi hapa?
Baada ya kuona upungufu huu , sasa tuone nini ambacho Dr Kafumu anaweza kufanya ili kuienzi Demokrasia na kuwapa haki yao Wana Igunga;
1. Awe wa kwanza kulaani matumizi ya nguvu dhidi ya Wana Igunga
2. Awe wa kwanza kuhakikisha Ismail Aden Rage anachukuliwa hatua kali za kimaadili
3.Awe wa kwanza kulaani harakati zozote za wanasiasa kuingiza udini kwenye siasa
4.Awe wa kwanza kuomba radhi kwa niaba ya chama chake kwa kukaa kimya au kushabikia siasa uchwara.
5 Awe wa kwanza ndani ya CCM na Tanzania kukataa ushindi huo na kuitaka Tume kuitisha tena uchaguzi wa jimbo dogo la Igunga , hili lifanywe pasipo kuangalia gharama za zoezi hilo, bali lifanywe ili kuuonyesha Ulimwengu kuwa Dr Kafumu na CCM wameamua kusiamamia misingi ya Demokrasia pasipo kujali gharama za hatua hiyo.
Haya ni mambo ya msingi kwa Dr Kafumu kuyasoma na kuyafanyia kazi, hii itamjengea heshima sio tu ndani ya CCM bali kwa watanzania wote na Ulimwengu mzima. Tafakari! A luta Continua!
Nova Kambota Mwanaharakati,
+255717 709618
Wesneday, 5october,2011
Tanzania, East Africa.
0 comments:
Post a Comment