Thursday, 15 March 2012


Baada ya kulainika…Madaktari wamevuna au ‘wameliwa’?

HATIMAYE Rais Jakaya Kikwete amefanikiwa kuleta suluhisho katika mgogoro kati ya Serikali yake na madaktari waliopania kugoma wakidai maslahi bora na mazingira mazuri ya kazi. Kadhalika watoa tiba hao walikuwa wakiitaka Serikali iwawajibishe Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda na Naibu wake, Dk. Lucy Nkya.
Kwa upande mmoja, hatua hiyo ya Rais na madaktari ilikuwa habari njema kwa wanyonge wasio na uwezo wa kwenda India au kwingineko nje ya nchi kutibiwa.
Lakini kwa upande mwingine, habari kwamba madaktari wamesalimu amri baada ya kukutana na Rais, Ikulu, zimepokewa kwa hasira na baadhi ya wananchi ambao waliuona mgomo huo kama adhabu sahihi kwa Serikali yao ambayo kwa kiasi kikubwa inazembea kujali maslahi yao.
Binafsi, japo niliipokea taarifa hiyo ya kumalizwa mgomo kwa furaha, nafsini ninaona kama tatizo hilo limeahirishwa kwa muda tu. Wakati madaktari wanaonekana kuwa na imani kuwa Rais Kikwete atatekeleza ahadi alizowapa (pasipo kutuambia kwa nini wana imani hiyo), rekodi isiyopendeza ya Kikwete na Serikali yake katika utekelezaji wa ahadi ingepaswa kuwafahamisha madaktari hao kuzichukulia ahadi hizo za Rais kwa hadhari.
Kama nilivyowahi kuandika mara kadhaa huko nyuma, tatizo la uongozi wa nchi yetu halijawahi kuwa kwenye kutoa ahadi nzuri na zenye kutia matumaini. Viongozi wetu ni wepesi mno kuahidi mambo yaliyo ndani ya uwezo wao na hata miujiza.
Laiti madaktari wangekuwa makini, wangejiuliza kwa nini ahadi zisizoisha kuhusu utatuzi wa tatizo la mgawo wa umeme zinaendelea kuwa ahadi tu huku mgawo ukigeuka kuwa kama stahili katika maisha ya kila siku ya Mtanzania.
Kama kumbukumbu yangu iko vizuri, nadhani ahadi ya mwisho ya Kikwete kuhusu kupunguza makali ya mgawo wa umeme iliashiria tatizo hilo lingeanza kushughulikiwa Desemba, mwaka jana. Lakini ahadi kubwa zaidi ya Rais ilikuwa ile aliyotoa muda mfupi baada ya kuingia madarakani mara ya kwanza (mwaka 2005) ambayo iliishia kwa Watanzania ‘kuingizwa mkenge’ na kampuni feki ya Richmond.
Na kama Tanzania ni shamba la bibi ambapo kila mtu ana uhuru wa kuvuna asichopanda, kampuni hiyo hewa ‘ilizaa’ kampuni nyingine ya Dowans (katika mazingira yanayoleta maana ndotoni tu na si katika hali halisi). Japo inaleta uchungu mkubwa kuizungumzia Dowans na jinsi watendaji mbalimbali wa Serikali walivyosimama kidete kuitetea ilipwe japo haikutekeleza wajibu wake, sakata hilo linashabihiana na maisha ya kawaida ya Mtanzania kwenye ‘kona za uswahilini’ ambapo si jambo la ajabu kwa vibaka kukupora kisha kukupigia kelele za ‘mwizi….mwizi.’ Kinachofuatia hapo ni ‘maumivu mengine’ ya kipigo kutoka kwa wananchi walioamini hadaa za vibaka hao kuwa wewe uliyeporwa ndiye mwizi uliyewapora vibaka hao.
Waingereza wanasema the end justifies the means, yaani; ‘mwisho (wa jambo) huhalalisha njia (iliyotumika kufikia mwisho huo).’ Kwa mantiki hiyo, jitihada za Kikwete zilizofanikiwa kuwalainisha madaktari kutoendelea na mgomo zinahalalisha hatua hiyo.
Lakini suala la msingi hapa si uhalali wa hatua hiyo ya Kikwete na madaktari kuafikiana nae, au hata suala zima la mgomo. Na katika suala la mgomo ni vigumu kuona uhalali wa hatua ambayo kimsingi ingewaumiza wanyonge ambao hata pale huduma za afya zinapopatikana inawawia vigumu kumudu gharama za kupata huduma hizo.
Katika stadi za mantiki, ili jambo liwe halali ni lazima lionekane kuwa halali. Kwa mgomo huo, japo ilikuwa halali kwa madaktari kudai maslahi na mazingira bora ya kazi lakini uhalali wa njia waliyotumia kudai haki yao uliathiriwa na ukweli kwamba mgomo wao ulikuwa na madhara makubwa zaidi kwa wasiohusika (yaani wananchi wa kawaida ambao kimsingi hawahusiki na sababu za uduni wa maslahi na mazingira ya kazi ya madaktari hao).
Lakini hata tukiweka kando suala la uhalali, bado inanitatiza kuelewa madaktari wamepata nini katika mgomo wao wa kwanza na hatua yao ya majuzi kuamini ahadi za Kikwete.
Japo mgomo wa kwanza ulichangia Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Blandina Nyoni na Mganga Mkuu, Deo Mtasiwa kusimamishwa kazi, sitaki kuamini kuwa harakati hizo zilizogusa hisia na uhai wa kila Mtanzania zililenga tu kuona viongozi hao wawili wakisimamishwa (na si kufukuzwa) kazi.
Tangu mwanzo madaktari hao waliitaka Serikali kuchukua hatua dhidi ya Mponda, Nkya, Nyoni na Mutasiwa lakini hadi sasa inaonekana wazi kuwa Serikali haipo tayari kuwatoa rehani waziri na naibu wake.
Na hili liliwekwa bayana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliyeweka wazi msimamo wa Serikali kuwa “kama kugoma basi (madaktari) tu lakini Serikali haiwezi kushinikizwa kuwafukuza kazi Waziri na Naibu wake kwa mgomo.”
Nimebainisha hapo juu kuwa binafsi nahisi suala hili limeahirishwa tu kwa sababu historia ina muhukumu Kikwete linapokuja suala la utekelezaji ahadi, hata zile anazotoa pasipo haja ya kuzitoa.
Hivi madaktari wamesahau ile kauli maarufu ya Kikwete kuwa; anawafahamu wala rushwa lakini anawapa muda tu wa kujirekebisha, na wasipofanya hivyo watagundua kuwa tabasamu lake halimaanishi huruma kwa wazembe na wababaishaji?
Au madaktari wameshasahau kioja alichotoa Rais Bandari ya Dar es Salaam, alipotamka kuwa anawafahamu kwa majina wanaofanya ufisadi bandarini hapo na angeyawasilisha kwa uongozi ili wachukuliwe hatua, lakini hakufanya hivyo hadi leo.
Waingereza wana busara moja isemayo; “The minute you settle for less than you deserve, you get even less than you settled for,” yaani-kwa tafsiri isiyo rasmi- unapokubali ‘yaishe’ licha ya upungufu, utaishia kupata pungufu zaidi ya kile ulichokubali.
Licha ya ukweli kuwa wao ndio waathirika wakubwa, wananchi wengi walikuwa upande wa madaktari kwa maana ya kuunga mkono hoja zao. Mtego waliojiingiza watoa tiba huo ni huu: wakikurupuka tena kutishia kugoma kwa madai kuwa Rais Kikwete aliwalaghai, wataishia kuonekana wababaishaji wasio na msimamo, na pengine wananchi wataamua kuwapuuza na kuwaona kama ‘kundi linalotaka kuweka rehani uhai wa wanyonge.’
Lakini hata tukiamua kuamini kuwa ahadi za Rais kwa madaktari hao ni za dhati, hizo fedha za kuwatimizia madai yao zitatoka wapi? Hapa sina maana kuwa hakuna njia za kupata fedha za kushughulikia madai hayo, bali ukweli ni kwamba Serikali ya Kikwete ina rekodi nzuri ya matumizi ya anasa yasiyoendana na hali mbaya ya uchumi wetu.
Sidhani kama kuna mtu yeyote (pamoja na madaktari) anayedhani Rais yupo tayari kupunguza safari zake za nje ya nchi ili kuokoa fedha japo kidogo kuanza kushughulikia matatizo ya madaktari hao. Na sitaki kabisa kuamini Serikali ya Kikwete iko radhi kuendesha kampeni za CCM huko Arumeru Mashariki kwa ‘kuuza sera’ pekee bila kumwaga fedha kwa wapiga kura (fedha ambazo zingeweza kuanza kutatua kero za madaktari hao).
Pengine gumu zaidi katika utekelezaji wa ahadi hiyo ya Rais kwa madaktari ni ukweli kuwa, pindi Serikali ikianza kutoa fedha za kutatua matatizo ya madaktari kuna uwezekano mkubwa wa watumishi wa kada nyingine kuanza shinikizo la kudai ‘watendewe haki kama madaktari.’
Kama nilivyobainisha katika makala yangu ya wiki iliyopita, kilio cha madaktari kuhusu maslahi na mazingira bora ya kazi ni kiwakilishi tu cha tatizo linalowakabili watumishi wengine wa umma na wananchi wengi kwa ujumla.
Ni wazi kuwa kama Serikali itaamua kupunguza matumizi ya anasa na kushughulikia madai ya madaktari hao, kuna uwezekano wa watumishi wengine wa umma kupata funzo kutoka katika mgomo wa madaktari kuwa ‘ukigoma utaitwa Ikulu, na Rais atatumia nguvu zake kutatua matatizo husika.’
Mwisho, inakera kuona Serikali iliyojaa mawaziri lukuki (ambao wanaongeza mzigo wa gharama za kuwahudumia) inashindwa kupata ufumbuzi wa kundi moja la watumishi wa umma hadi kulazimu Rais aingilie kati.
Tuna Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, mawaziri na manaibu wao kibao (huwezi kukumbuka majina yao wote pasipo kuwa na orodha yao mkononi), na mlolongo wa makatibu wakuu na wakurugenzi wa wizara lakini inabidi kumsubiri Rais ndipo ufumbuzi wa tatizo upatikane.
Anayestahili lawama kubwa si watendaji hao bali aliyewateua. Sote tunafahamu kuwa Rais hakuwahi kushikiwa mtutu wa bunduki ili ateue watendaji ambao sio tu ni wengi bali wengi wao ni kama bado wapo kwenye sherehe za kujipongeza kwa kuteuliwa kwao na Rais, huku baadhi yao wakiwa kama hawajui kwa nini Rais aliwateua.
Na kwa mazingira haya ya lundo la wasaidizi wasio na msaada wa maana kwa Rais, Serikali na umma kwa ujumla, sio tu tutaendelea kushuhudia madaktari, watumishi wengine na wananchi kwa ujumla wakiingia kwenye mgogoro na Serikali kudai uwajibikaji bali pia tutasikia sana vioja kama hivyo vya Naibu Waziri aliyeibiwa hotelini katika mazingira ya kutatanisha.
Utitiri wa viongozi wasio na cha kufanya unaweza kabisa kusababisha waishie kuwa vituko ili angalau majina yao yasikike na ijulikane kuwa wapo kazini.


1 comment:

  1. Mnataka wagome tena? Uzalendo wenu upo wapi? Chuki zenu kwa Rais zisiwe sababu ya kuitakia mabaya nchi.

    ReplyDelete

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget