Thursday, 1 March 2012

Kama hakuna polisi anayetaka kuua, je, kuna raia anayependa kuuawa?

KWA mara nyingine tena, Watanzania tumeshuhudia unyama wa Jeshi la Polisi ambao wiki iliyopita waliwapiga risasi na kuwaua raia mjini Songea. Kosa pekee la wananchi hao ni kutumia haki yao ya kikatiba kuandamana.
Ni rahisi kuwalaumu askari waliofyatua risasi zilizoua iwapo tutapuuza kanuni za utendaji kazi wa watumishi wa vyombo vya dola. Ifahamike kuwa moja ya kanuni muhimu kwa askari ni nidhamu kwa uongozi wa juu, sambamba na kutekeleza amri na maagizo ya viongozi pasipo kuhoji.
Kwa hiyo ni muhimu kuyaangalia matukio yanayowahusisha watendaji wa vyombo vya dola na utekelezaji wa ‘amri halali’ zinazotolewa na viongozi husika. Kwa vyovyote vile, askari walioua huko Songea hawakufanya hivyo kwa vile walikuwa na hamu ya kuua au wasingeua usalama wao ungekuwa hatarini bali walikuwa wanatekeleza amri ‘halali’ za viongozi wao.
Suala jingine linalostahili kupigiwa mstari ni mtiririko wa amri kutoka kwa viongozi kwenda kwa watekelezaji, sambamba na mawasiliano kati ya ngazi za chini za vyombo vya dola (kwa mfano polisi) na makao makuu yao.
Katika mazingira ya kawaida tu, pindi hali ya usalama inapochafuka hadi kufikia hatua ya kumhusisha Kamanda wa Polisi wa Mkoa, ni dhahiri kwamba ‘wakubwa’ makao makuu ya Jeshi la Polisi walifahamishwa kila kinachoendelea katika eneo la tukio.
Kwa hiyo basi wakati tunaelekeza lawama zetu kwa polisi walioua Songea tusisahau kudadisi juu ya nani aliyetoa amri kwa askari hao.
Taarifa zilizopo hadi sasa ni kwamba zaidi ya wananchi 50 wameshafikishwa mahakamani kutokana na ‘vurugu’ hizo za Songea. Lakini wakati hilo likitokea, tunaambiwa kuwa ni askari wanne tu waliokamatwa kwa ‘tuhuma za kutumia risasi za moto.’
 Kwa nini wananchi ambao wenzao waliouawa wawe wameshafikishwa mahakamani kwa ‘kosa la kufanya vurugu’ lakini walioua waishie kukamatwa tu.
Na kuna uhakika gani kama wamekamatwa kweli ilhali hata majina yao hayajawekwa hadharani? Na hata kama madai hayo ni kweli (kuwa askari hao wamekamatwa) kuna uwezekano gani wa haki kutendeka katika mazingira ya polisi kukamata polisi wenzao waliokuwa wanaotekeleza amri ‘halali’ ya jeshi hilo?
Kingine kinachovunja moyo na kuchukiza ni mkanganyiko katika kauli za uongozi wa jeshi hilo. Kamanda wa Polisi mkoani Ruvuma, Michael Kamhanda, alinukuliwa akidai kuwa askari hao walikamatwa na wanaendelea kuhojiwa ili kujua kama kulikuwa na uzembe katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kadhalika alisema kuwa (namnukuu); “Kwa kuwa tukio hilo limehusisha vifo, hatuwezi kuacha hivi hivi tu ni lazima tujiridhishe kuwa askari hao hawakufyatua risasi kwa uzembe.”
Lakini katika kile kinachoweza kutafsiriwa kama ‘hukumu imeshatolewa juu ya nani alikuwa sahihi na nani mkosaji,’ Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Kamishna Paul Chagonja, alizungumza na vyombo vya habari na kuhitimisha kuwa ‘maandamano hayo hayakuwa ya amani bali ya kihuni kwani yalilenga kuvamia ofisi za serikali ikiwemo Ikulu ndogo na Ofisi ya Mkuu wa mkoa.’
Kamanda Chagonja alitetea polisi akisema; "Usifikirie polisi hawana akili. Haiwezekani watu wazima na akili zao wenye mafunzo wafyatue ovyo risasi za moto kwa raia. Hakuna askari anapenda kuua raia...lakini watu wanavamia Ikulu, ofisi ya mkuu wa mkoa, magari ya polisi hapo kuna amani kweli?"
Jambo la kutilia shaka ni kwamba, Chagonja huyo huyo ndiye kiongozi wa msafara uliotumwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema kwenda Songea kuchunguza tukio hilo. Sasa kulikuwa na haja gani ya kupelekea timu hiyo ilhali imeshathibitika kuwa waandamanaji walikuwa wahuni tu (na pengine ilikuwa sahihi kwa polisi kuwaua baadhi)?
Chagonja anasema tusifikiri kuwa polisi hawana akili lakini kauli zake zinaonyesha ni kwa kiwango gani yeye mwenyewe ana matatizo katika kuushirikisha ubongo wake na mantiki. Hivi busara ndogo tu isingemwelekeza kuwa wakati mwafaka wa yeye kutoa hukumu ni baada ya kukamilika kwa uchunguzi huo?
Kulikuwa na haja gani ya kuwatia mbaroni askari wanne ilhali sio tu walikuwa wanatekeleza maagizo ya uongozi wa Jeshi la Polisi bali pia walikuwa wanakabiliana na wahuni?
Japo Kamanda Chagonja anatusihi tusifikiri polisi hawana akili, lakini kila mwenye akili timamu anaweza kubaini nani asiye na akili katika kukurupuka huko kwa kiongozi wa ngazi za juu katika Jeshi la Polisi, kutoa hukumu kabla hata hajaanza uchunguzi wa tukio husika.
Kimsingi, Jeshi letu la Polisi limegeuka na baadhi ya matukio yakionyesha kuwa limeanza kuwa na dalili za awali za kundi la maharamia. Siku zote wamekuwa waoga kuchukua hatua dhidi ya wahalifu wakubwa (hususan mafisadi wanaosababisha ugumu wa maisha-ambao kwa namna fulani unachangia haja ya kudai haki kwa njia ya maandamano inapobidi) lakini sio tu wepesi wa kudhibiti wananchi wasio na hatia, bali wana vidole vyenye kiu ya kufyatua risasi (trigger happy).
Kila mara tunalikumbusha Jeshi la Polisi kuwa maandamano ni haki ya kikatiba ya kila Mtanzania. Hiyo kanuni ya kidikteta ya kutaka waandamanaji waombe kibali ni kinyume cha Katiba yetu inayoruhusu uhuru wa kukusanyika. Kinachopaswa kufanyika ni kwa waandamanaji kulifahamisha tu jeshi hilo kuhusu maandamano na sio kuomba ridhaa yao.
Jukumu la polisi sio kujifanya watabiri kwa intelijensia zao zenye shaka na kuhitimisha kuwa maandamano yatasababisha uvunjifu wa amani bali wanapaswa kushirikiana na waandaaji wa maandamano kuhakikisha yanafanyika kwa amani na utulivu.
Nimeandika intelijensia zenye shaka (za ovyo ovyo)’ kwa sababu zinaonekana kuwa na ‘ufanisi’ tu kwenye kuminya haki za wananchi lakini hazitumiki kukamata majambazi wanaobaka uchumi wetu kila kukicha. Jeshi la Polisi linaloshindwa kufanya intelijensia ya kubaini wala rushwa ndani yake litawezaje kudai lina intelijensia dhidi ya wananchi wasio waajiriwa wake?
Tatizo kubwa linalolikabili Jeshi la Polisi ni kasoro za kufikiri sawasawa miongoni mwa viongozi wake wa ngazi za juu katika suala la haki za binadamu. Unaposikia Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi hilo anapuuza mauaji ya raia na kuhitimisha kuwa ni wahuni tutegemee nini kwa askari wa ngazi za chini?
Kwa wadhifa wake, Chagonja ndiye mwenye dhamana kubwa ya kuwapatia askari wake uelewa wa haki za binadamu. Sasa kama mtu mwenye dhamana ya kuwafundisha kazi watendaji wake, anaongoza kwa mfano wa kupuuza haki za raia kuishi ni wazi tutaendelea kushuhudia polisi wakiendelea kuua, na kisha ‘kujibaraguza’ kwa kuunda tume ‘za kizushi’ ambazo zitatoa hukumu kabla ya kuanza uchunguzi rasmi.
Kwa asili, Watanzania ni watu wenye kuenzi sana amani japo baadhi ya wanasiasa wanatulaghai kuwa hayo ni matokeo ya wao kuwepo madarakani. Laiti mtu kama Chagonja angetumia faida hiyo ya ‘upole’ wa Watanzania angeweza kuliepusha Jeshi la Polisi na gharama zisizo na msingi, kuandaa operesheni kubwa (kana kwamba wanaenda vitani) kwa kuhakikisha kila maandamano yanapatiwa ulinzi na polisi na kuwakumbusha waandamanaji na viongozi wao juu ya umuhimu wa kukamilisha shughuli yao kwa amani.
Na si kwamba polisi hawana uzoefu katika kusikindikiza maandamano kwa amani lakini tatizo ni mtazmao wa baadhi yao wenye mwelekeo wa kiharamia, kwamba kila maandamano ni chanzo cha vurugu. Chagonja anasema hakuna polisi anayetaka kuua lakini hasemi kama kuna Mtanzania anayependa kuuawa.
Damu za wananchi wanaouawa pasipo hatia huku vifo vyao vikiombolezwa na akina Chagonja kwa kuwaita wahuni hazitapotea bure. Kila anayeingilia jukumu la Mwenyezi Mungu kutoa uhai wa mwanadamu mwenzie, atambue kuwa kuna siku atawajibika kwa mauaji hayo.
Hayo madaraka yanayowatia jeuri polisi kuua watu wasio na hatia yatawatokea puani, kwa njia moja au nyingine. Kwa vile kama mwananchi wa kawaida anakumbana na kila ugumu kupewa haki yake akiwa hai ni wazi hao wanaouawa pasipo hatia hawawezi kupata haki hiyo kwa sasa.
Lakini kwa vile maandiko matakatifu yanatufundisha kuwa mshahara wa dhambi na mauti, basi kwa hakika kila anayetoa amri ya kuua au kufyatua risasi atawajibika huko mbele ya haki kwani kila nafsi itaonja mauti.
Nimalizie makala hii kwa kulikumbusha Jeshi la polisi kuwa halina uwezo wala nguvu ya kuua kila Mtanzania anayetimiza haki yake ya kikatiba kuandamana.
Wanaweza kuua watu kadhaa kwa muda fulani, na wanaweza kuua watu wengi kwa muda mwingi lakini kamwe hawawezi kuua watu wote. Na kama ambavyo walionyanyaswa na mfumo dhalimu wa kibaguzi huko Afrika Kusini walimudu kupambana na silaha za hali za juu la polisi wa makaburu, yawezekana kabisa siku moja wananchi waliochoshwa kuuawa na polisi wetu watachukua hatua mkononi kwa staili ya ‘akuanzae mmalize.’


0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget