Michango kwa ajili ya Barabara ya Maziwa-External Mandela, kifusi sasa; lami itafuata
Kwa watumiaji wa Barabara ya Mkato ya Maziwa mpaka External Barabara ya Mandela; tuunganishe nguvu ya pamoja kuwezesha matengenezo ya dharura ya kuweka kifusi wakati tukiendelea kufuatilia barabara husika ijengwe kwa kiwango cha lami.
Watendaji wa Manispaa ya Kinondoni wametueleza kuwa barabara ya External haiwezi kupitishwa grader kusawazishwa kwa kuwa ina mabaki ya lami; hivyo suluhisho ya muda mfupi linapaswa kuwa ni kuweka kifusi.
Manispaa imekubali kutoa malori kwa ajili ya kubeba kifusi; hata hivyo wameeleza kuwa hakuna bajeti ya kununua na kusambaza kifusi kwa haraka. Jana tarehe 20 Machi 2012 nilimjulisha Diwani wa Kata ya Ubungo Boniface Jacob akutane na kamati ya wananchi iliyoanza jitihada mbalimbali kuangalia nini tunachoweza kufanya kwa kuunganisha nguvu ya umma.
Diwani amenijulisha kwamba gharama zinazohitajika kuweka na kusambaza kifusi ni milioni moja; nimeshampatia 10% ambayo ni sawa na laki moja kazi iendelee. Nawaandikia kuwaomba watumiaji wa Barabara hiyo ambayo ni ya mkato na yenye kupunguza foleni, tuunganishe nguvu za pamoja kukamilisha matengenezo yanayoendelea.
Wasiliana na Diwani 0712239595 kwa ajili ya maelezo na maelekezo ya kuwasilisha mchango wako; ukishaunganisha nguvu yako tafadhali tujulishe kupitia mbungeubungo@gmail.com ili kuhakikisha uwajibikaji.
Mtakumbuka kuwa gazeti la Habari leo la tarehe 18 Machi 2012 katika ukurasa 5 lilikuwa na habari “Wataka Ubungo-Mandela kutengenezwa”, Habari hiyo imeeleza kuwa “Wakazi wa Ubungo katika Manispaa ya Kinondoni, wamemuomba mbunge wa Jimbo hilo John Mnyika, kushughulikia tatizo la Ubovu wa Barabara inayounganisha eneo la Ubungo Maziwa na Barabara ya Mandela ambayo kwa kipindi kirefu imekuwa kero”.
Kufuatia habari hiyo kwa kazi waliyonipa wananchi ya kuwawakilisha na kuisimamia serikali na vyombo vyake katika kuwezesha maendeleo nilitoa wiki moja kwa halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kutimiza wajibu wa kushughulikia ubovu wa barabara husika.
Nikaeleza kuwa iwapo baada ya wiki moja Manispaa itakuwa haijaanza kuifanyia matengenezo barabara iliyolalamikiwa basi nitachukua hatua za kuunganisha nguvu ya umma kuwezesha matengenezo yanayohitajika.
Kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi kazi za utekelezaji ziko chini ya vyombo vya serikali kuu na serikali za mitaa; kazi ya mbunge ni kuvisimamia vyombo husika kuwezesha maendeleo.
Wananchi wa kata ya Ubungo na maeneo mengine ya Manispaa ya Kinondoni wanalipa kodi na kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012 kumetengwa fedha za matengenezo ya barabara hivyo ni wajibu wa Manispaa kutumia mafungu hayo kwa haraka kufanya ukarabati au kama Manispaa haina fedha itangaze kufilisika ili vyanzo vingine viweze kutumika.
Hivyo, kama katika kipindi hicho cha wiki moja nilieleza iwapo Manispaa itakuwa haijatoa kauli ya lini matengenezo ya barabara husika yataanza nitawajibika kwa kutumia nafasi yangu ya ubunge kuunganisha wananchi na wadau wa maendeleo katika eneo husika kuweza kuanza kushughulikia ubovu wa barabara husika kwa dharura kwa kutumia vyanzo vingine vya fedha nje ya kodi.
Aidha, wakati tukichukua hatua za dharura za kufanya matengenezo ili kupunguza kero , suluhisho muhimu zaidi ni kupanua daraja la External katika Eneo la Ubungo Kisiwani ili kupunguza msongamano wa magari na kujenga barabara husika kwa kiwango cha lami.
Kwa kutambua umuhimu wa suala hili nilichukua hatua mbalimbali za kibunge kuanzia mwanzoni mwa mwaka 2011 ili barabara husika iweze kupandishwa hadhi na kujengwa kwa kiwango cha lami kwa haraka zaidi kwenye mwaka wa fedha 2011/2012 kuliko ilivyopangwa awali.
Niliziandikia mamlaka husika hususan Wizara ya Ujenzi na TANROADS kuzingatia barabara tajwa katika bajeti kwa lengo la kuchangia katika kupunguza msongamano, Wizara ya Ujenzi awali ilisema serikali kuu haiwezi kushughulikia barabara hiyo kwa kuwa iko chini ya Manispaa ya Kinondoni. Lakini, nikaendelea kuchukua hatua zaidi kwa njia za kibunge na za uwakilishi wa wananchi na hatimaye TANROADS ikaingiza barabara hiyo katika vipaumbele vyake na sasa imetengewa fedha za ujenzi wa kiwango cha lami kiasi cha shilingi bilioni 1.2.
Hivyo, nichukue fursa hii pia kutoa mwito kwa TANROADS kutoa taarifa kwa umma kuhusu hatua iliyofikiwa katika kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami kuanzia mwaka huu wa 2012 ili kupata suluhisho la kudumu zaidi la kuondoa kero ya ubovu wa barabara husika na kuchangia katika kupunguza msongamano katika Jimbo la Ubungo.
Aidha, pamoja na kiwango hicho cha fedha kilichotengwa na TANROADS, tarehe 5 Machi 2012 Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam alieleza kuwa amewasilisha maombi mengine kupitia Mfuko wa Barabara (Road Fund) kwa ajili ya ujenzi wa daraja kubwa zaidi katika barabara hiyo kwenye eneo la Ubungo Kisiwani/External.
Hivyo, ni muhimu watendaji wa Mfuko wa Barabara (Road Fund) nao wakaeleza hatua ambayo imefikiwa katika kushughulikia maombi hayo kwa lengo la kuchangia katika kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam.
Nitumie nafasi hii pia kurudia kutoa mwito kwa Wizara ya Ujenzi kueleza kwa wananchi hatua iliyofikiwa katika kupandisha hadhi barabara za Dar es salaam za kupunguza msongamano na kutumia nyongeza ya mapato iliyopatikana kwenye ushuru wa barabara kuanza kujenga barabara hizo kwa kiwango cha lami mwaka huu wa 2012. Maslahi ya Umma Kwanza.
John Mnyika at 12:1
0 comments:
Post a Comment