Thursday, 29 March 2012

Zitto na urais: Haki binafsi isiyokidhi alama za nyakati

Uskochi
Zitto Kabwe
Zitto Kabwe
MAKALA yangu katika gazeti hili toleo la Novemba 2, mwaka jana ilihusu nafasi za vyama vya siasa huko nyumbani, katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Katika makala hiyo nilichambua changamoto zinazoikabili CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao, nikagusia nafasi na vikwazo dhidi ya CHADEMA na CUF ambavyo kimsingi, angalau vina nafasi (hata kama haba) ya kutoa upinzani kwa CCM, na hata kuing’oa madarakani.
Nilihitimisha makala hiyo iliyobeba kichwa ‘CCM dhaifu mtaji imara wa urais CHADEMA, CUF’ kwa ahadi ya kuendeleza uchambuzi huo. Leo nitaitupia jicho CHADEMA.
CHADEMA imekuwa ikipanda chati kwa kasi kiasi cha kuweza kubashiriwa kushika hatamu za uongozi baada ya Uchaguzi Mkuu, 2015.
Lakini, uwezekano wa CHADEMA kuingia Ikulu unategemea mazingira ya ndani na nje ya chama hicho. Tuanze na mazingira ya nje, ambayo pengine ni magumu zaidi si kwa CHADEMA pekee bali chama kingine chochote kile cha upinzani kumudu kuing’oa CCM madarakani.
Ukichambua kwa undani mageuzi ya kisiasa huko nyumbani utabaini bado tuna safari ndefu ya kimfumo na kisaikolojia.
Pamoja na uwepo wa vyama kadhaa vya siasa, mazingira ya kisiasa bado yanashabihiana kwa kiasi kikubwa na yale ya mfumo wa chama kimoja. Na tatizo hili limejikita zaidi kwenye vyombo vya dola. Kama kuna eneo moja ambalo mageuzi ya kisiasa yameshindwa kulibadili ni suala la kuvitenganisha vyombo hivyo na siasa.
Jeshi la Polisi limeendelea kuwa mithili ya kitengo cha usalama cha CCM. Tatizo sugu zaidi katika jeshi hilo linachangiwa na maslahi binafsi ya baadhi ya viongozi wake. Na tatizo hilo halipo Tanzania pekee bali ni mbinu inayopendelewa na watawala wengi wenye dhamira ya kuhodhi madaraka, kukandamiza demokrasia na kujitengenezea kinga dhidi ya maovu yao.
Sasa kwa vile utendaji kazi katika vyombo vya dola unaongozwa na kanuni ya ‘kidikteta’ ya kutekeleza amri bila kuhoji, mtawala akimteua shemeji yake kuongoza taasisi kama Jeshi la Polisi, ni wazi chombo hicho kitafanya kazi bila weledi wa kutosha.
Na japo wahusika watang’aka kwa nguvu zote, Idara yetu ya Usalama wa Taifa imeendelea kuwa nguzo muhimu ya mafanikio ya CCM kwenye chaguzi na hakuna uwezekano kwa chama kukamata uongozi wa nchi iwapo idara ya usalama ya nchi husika ‘haitaki’ (iwe kwa sababu za msingi au za kipuuzi).
Kwa vile utendaji kazi wao ni wa siri, chama kinachohujumiwa huishia kushangaa tu jinsi ‘kura zilivyoyeyuka’ pasipo kuwa na ushahidi wa jinsi hujuma husika ilivyofanyika.
Kwa hiyo-na hapa nisiume maneno- ili CHADEMA iweze kutimiza ndoto zake za kuingia Ikulu ni lazima mashushushu wetu waafiki iwe hivyo. Habari njema kidogo kwa chama hicho ni kwamba sio kwamba haiwezekani kabisa kwa Idara ya Usalama wa Taifa kuamua ‘sanduku la kura liamue mshindi halali wa uchaguzi.’
Tofauti na taasisi nyingine za dola, Idara hiyo haiendeshwi kama jeshi kamili bali ni nusu-jeshi (paramilitary). Hii inaweza kutoa mwanya kwa baadhi ya watendaji wa taasisi kama hiyo ‘kupambana’ na ile kanuni inayowabana polisi ya ‘kutekeleza amri bila kuhoji.’
Katika mazingira ya kinadharia, kama ikionekana ni wazi mwelekeo wa CCM ni tishio kwa usalama wa taifa, baadhi ya wazalendo ndani ya Idara hiyo wanaweza kuhakikisha si tu wanahujumu matakwa ya viongozi wanaotaka kuibeba CCM bali pia wanatumia ‘nguvu za giza kwenye chaguzi’ kukisaidia chama cha upinzani.
Kisaikolojia, vyama vya upinzani vinakabiliwa na vikwazo vikuu vitatu. Kwanza, uoga wa ‘Tanzania haiwezekani bila CCM’ na pili ni hofu ya ‘yale yale tuliyoshuhudia yakitokea Kenya,’ yaani machafuko. Sababu zote hizi ni mtaji mkubwa kwa CCM nyakati za uchaguzi.
Kikwazo cha tatu cha kisaikolojia ni hofu ya ‘je watu hawa ambao kimsingi asili yao ni CCM hiyo hiyo wanayotaka kuing’oa hawawezi kweli kugeuka wakipata madaraka na kuwa sawa au wabaya zaidi ya CCM?’
Ahueni kwa CHADEMA ni kwamba, kama mwelekeo wa wake utaendelea kuleta matumaini kwa Watanzania, na wakati huo huo CCM inazidi kugeuka uwanja wa mapambano ya wenyewe kwa wenyewe, basi wapiga kura wanaweza kuamua kuongozwa na chama tofauti.
Kwa bahati mbaya (au makusudi)-na haya ni mazingira ya ndani ya CHADEMA- tayari zimeanza dalili za mgogoro wa kuwania kuteuliwa kuwa mgombea urais.
Wiki iliyopita, Mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia chama hicho, Zitto Kabwe, alitangaza kuwa kuutamani urais. Pengine hoja nzito kabisa katika waraka huo uliobeba kichwa cha habari ‘Ndio, nataka kuwa Rais’ ni kauli ya Zitto kuwa (namnukuu); "Sasa kama wananchi watasema huyu Zitto anapaswa kubeba jukumu hili mwaka 2015 tuache iwe. Kama watasema hapana wewe bado mpaka mwaka 2020 au hata 2025 tuache iwe hivyo. Pia Kama hawataki kabisa tuache iwe hivyo.
Naomba ieleweke kuwa Zitto ana haki si tu kutaka urais, bali pia kutangaza dhamira hiyo katika wakati anaotaka. Lakini kimantiki, kama ambavyo mwanasiasa huyo alivyowahi kulishutumu gazeti moja kwa kuzungumzia ilichokiita ‘zimwi la urais CHADEMA’ wakati inaomboleza kifo cha mbunge wa chama hicho, Regia Mtema, ndivyo inavyoshangaza kwa Zitto kutangaza nia ya urais ilhali chama chake kikiwa katika mapambano makali dhidi ya CCM, Arumeru Mashariki
Japo msiba wa Regia hauwezi kulinganishwa na kampeni hizo za uchaguzi, lakini matarajio ya wengi ni kuona viongozi wote wa chama hicho wakielekeza nguvu zao Arumeru Mashariki ili kushinda kiti cha ubunge. Hoja ya msingi hapa si kauli ya Zitto bali timing yake.
Na japo hakuna dalili kuwa mwanasiasa huyo machachari ‘amesusia’ kampeni za Arumeru Mashariki, uamuzi wake wa wa kutangaza nia ya urais kwa wakati huu sio tu unazua mkanganyiko usiohitajika, lakini pia unaathiri nafasi ya chama hicho kufanya vizuri mwaka 2015, hasa ikizingatiwa kuwa amana kubwa ya chama hicho bado ipo kwa Dk. Willbrod Slaa.
Naishauri CHADEMA kuwekeza nguvu kukabili vikwazo vizito vya nje ya chama hicho, badala ya kuanza ndoto za nani awe mgombea.
Wakati kila mwanachama wa CHADEMA ana haki ya kutaka nafasi yoyote ile ikiwa pamoja na urais, ni muhimu kwa chama hicho kutambua kuwa, baadhi ya Watanzania wanakiangalia kwa umakini iwapo si tu kinaweza kuwa mbadala wa CCM bali kumudu kuwakwamua kutoka lindi la ufisadi, umasikini na kudumaa kwa maendeleo.
Na kama alivyoandika Zitto, sauti ya Watanzania-wana CHADEMA na wasio wanachama wa chama hicho- iwe kigezo muhimu cha kuamua nani apewe dhamana ya kuwa mgombea wake hapo 2015 kwa kuzingatia muda mwafaka, kukubalika kwake kwa umma na uadilifu wake binafsi.


0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget