Monday, 14 January 2013



Mmoja amshangaa mwenzake kuwakamata machangudoa
*Asema anawakamata kwa sababu hana elimu ya madanguro
*Mwenzake ajibu, huyu ana miezi sita hapa, haya anayatoa wapi?

MAKAMANDA wawili wa polisi katika Kanda Maalum ya Dar es Salaam, wamekwaruzana. Makamanda hao, Charles Kenyela wa Mkoa wa Kinondoni na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo, wamekwaruzana na kurushiana maneno yasiyofaa kuhusu namna ya utendaji kazi wa Jeshi la Polisi.


Kutofautiana huko kumeibuka baada ya wiki iliyopita, Kamanda Kenyela kufanya operesheni ya kuwakamata wanawake wanaofanya biashara ya ukahaba, maarufu kama machangudoa na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Baada ya Kamanda Kenyela kuendesha operesheni hiyo, Kamanda Kiondo wa Temeke, alinukuliwa na vyombo vya habari jana, akikosoa zoezi hilo na kusema hakuna sheria nchini inayozuia mwanamke kujiuza.

Katika maelezo yake, Kamanda Kiondo alisema, operesheni hiyo ilifanywa kwa kukurupuka na kwamba kamanda huyo hajasomea elimu ya jamii juu ya madanguro.

Kwa mujibu wa Kamanda Kiondo, kama Kamanda Kenyela angekuwa anaielewa vizuri elimu hiyo, kamwe asingedhubutu kuwakamata wanawake hao bali angewapatia elimu na ushauri dhidi ya maradhi wanayoweza kuambukizwa.

Pamoja na hayo, alihoji kuna umuhimu gani wa kuwakamata machangudoa wakati hakuna sheria inayomtaka awafikishe mahakamani badala yake anayetakiwa kushitakiwa ni mtu anayetoa nyumba ili itumike kama danguro.

Naye, Kamanda Kenyela alipozungumza na MTANZANIA jana juu ya kauli za kejeli zilizotolewa na mwenzake huyo, alisema amestushwa na taarifa ya Kamanda Kiondo kwa kuwa amemdhalilisha kupitia vyombo vya habari.

“Yaani mwandishi sipati picha kama Kamanda Kiondo ambaye hana miezi sita kwenye nafasi hiyo tangu ateuliwe, anaweza kunidhalilisha juu ya utendaji wangu wa kazi, kwanza inakuwaje azungumzie mambo ya Kinondoni wakati mimi nipo?

“Kama alijua nimekosea, alipaswa kunipigia simu kwanza tushauriane kabla ya kusema kwenye vyombo vya habari au angenisema kwa wakubwa wetu ambao wangeniita na kunishauri ili nisitishe operesheni hiyo, kama kweli ninakwenda kinyume.

“Amenidhalilisha sana na unajua ni vigumu kwa kamanda kama yule kutoka kwenye himaya yake na kuzungumzia himaya ya kamanda mwingine wakati mhusika yupo.

“Kibaya zaidi anasema eti mimi sina elimu ya jamii juu ya madanguro, lakini binafsi siwezi kuona vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani au usumbufu kwa raia wengine, halafu nikakaa kimya, sitaacha kuchukua hatua.

“Ninachoweza kumwambia Kamanda Kiondo ni kwamba, sina ugomvi naye na pia sitaki malumbano naye, kazi ya kudhibiti uhalifu haihitaji mpango mmoja lazima tutumie njia mbadala kuhakikisha tunatimiza majukumu yetu ya kulinda raia na mali zao, nafikiri suala hilo linazungumzika tuache litapata suluhisho,” alisema Kamanda Kenyela akionyesha kukerwa na kauli za Kamanda Kiondo.

Kova aingilia kati 
Kutokana na malumbano hayo, Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, aliliambia MTANZANIA kwa simu kwamba atawakutanisha makamanda wa polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam ili kupata ufumbuzi wa suala hilo.

“Ni kweli suala hili limenifikia na kwa kuwa kesho (leo) kuna kikao, basi litawekwa katika ajenda ili lipate kuondoa malumbano hayo.

“Lazima tuangalie sheria zinasemaje juu ya machangudoa, sasa tutajadiliana ili kupata msimamo wa kudhibiti biashara hiyo, kwani kuna matukio mengi ya namna hiyo yapo yanafanyika lakini kwa upande wetu polisi lazima tuwe na sheria ya kudhibiti vitendo hivyo.

“Kikao cha kesho (leo) kitaangalia sana sheria kuliko maoni ya watu, tutaangalia upande wa mahakama kama sheria zipo za kuwatia hatiani wahusika wa biashara hiyo, nakuhakikishia tofauti hizi za ma RPC wawili zitakwisha na wote tutapata msimamo wa pamoja.

“Si kwamba kikao cha kesho (leo) kimeitishwa kwa sababu ya mzozo huo wa ma RPC hao, hapana, kilipangwa tangu siku nyingi lakini tushukuru mzozo huu umeibuka wakati tunatarajia kukutana,” alisema Kamanda Kova.

Kamanda Kiondo alipozungumza na MTANZANIA kwa simu, alisema alitoa kauli hiyo baada ya kupigiwa simu na waandishi wa habari wakitaka atoe ushauri juu ya operesheni inayofanywa na Kamanda Kenyela.

“Nilichokifanya ni kutoa ushauri na uzoefu wangu nilioupata wakati nikiwa masomoni nchini Afrika Kusini, ambako Serikali ya nchi hiyo ilipambana kisheria na machangudoa lakini ikashindwa kwani hata soko liliongezeka.

“Hata huku kwangu eneo la Sokota kuna machangudoa na kila ninapojaribu kuwakamata, ndipo soko linapoongezeka. Hivyo hivyo na gongo, ukiikamata inapanda bei.

“Kwa hiyo, nilichokifanya mimi ni kutoa ushauri ili itolewe elimu kwa wanawake na wanaume ili wajue madhara wanayoweza kupata pindi wanapojihusisha na biashara hiyo.

“Sasa basi ninachosema hapa ni kwamba, nguvu ya Kenyela haitaleta mafanikio bali itaongeza soko, kwani ukiwakamata wahusika maana yake unawafanya waliobaki waongeze bei na pia ieleweke kwamba, wanaokamatwa ni machangudoa wa Kinondoni tu wala siyo Dar es Salaam nzima.

“Kwa hiyo, sina maana ya kutaka kumchafua Kamanda Kenyela, niliyasema kwa nia nzuri kabisa, sina tatizo naye, naomba anielewe hivyo,” alisema Kamanda Kiondo.

 CHANZO: Mtanzania



0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget