Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu kesho Rais Jakaya Kikwete atakutana na kufanya mazungumzo na MAMA FRANNIE LEAUTIERA,anayetajwa kuwa ni Mtendaji Mkuu wa MFUKO PRIVATE FUND.
Nimejaribu kufanya utafiti mtandaoni lakini jina la karibu linaloshabihiana na la mwanamama huyo ni FRANNIE LEAUTIER (pichani juu)
Lakini jitihada zangu za kutafuta MFUKO PRIVATE FUND (taasisi ambayo taarifa hiyo ya Ikulu inaeleza kuwa Mama Leautiera ni Mtendaji Mkuu) hazijazaa matunda.
Je Ikulu walimaanisha Frannie Leautier lakini wakaongeza herufi 'A' kimakosa, hivyo kusomeka LEAUTIERA badala ya LEAUTIER?
Tukiamini hilo ni kosa dogo tu la kiuandishi, je MFUKO PRIVATE FUND ni taasisi gani? Na kwanini Rais akutane na Mtendaji Mkuu wake?
Unaweza kudhani maswali haya hayana umuhimu lakini kwa vile taarifa zimeshasambaa duniani kuwa tuna utajiri 'mpya' wa gesi, basi ni vema kufahamu viongozi wetu wanakutana na watu wa aina gani wanapokuwa ziarani huko nje.
Kama mnavyojua, kabla na wakati wa ukoloni akina Karl Peters walipita huko na kule kusaini mikataba ya kilaghai ya kuchukua ardhi na raslimali zetu.Siku hizi, baadhi ya viongozi wa Afrika ndio wamegeuka akina Karl Peters kwa aidha kukaribisha 'wakoloni wapya' au kuwafuata huko makwao kusaini mikataba ya kuuza nchi yetu.
Ni matarajio yangu kuwa Ikulu itajitahidi kutoa ufafanuzi kuhusu suala hili.
0 comments:
Post a Comment