Thursday, 3 January 2013




HERI ya Mwaka Mpya 2013. Ni matarajio ya safu hii kuwa baada ya shamrashamra za jana Jumanne kuukaribisha mwaka huu sasa nguvu zinaelekezwa katika kutafsiri malengo mbalimbali tuliyojiwekea katika nyanja tofauti za maisha.
Awali, nilikuwa nimepanga kuwa mada ya makala hii iwe ubashiri wa masuala mbalimbali katika mwaka huu mpya. Hata hivyo, wakati ninajiandaa kufanya hivyo nilikumbana na mjadala mmoja huko kwenye mtandao wa kijamii wa twitter ambapo mwenzetu mmojaalitwiti akilaumu Watanzania walio nje kwa kulaumu tu kwenye blogu na mitandao ya jamii pasi kuchangia chochote kuleta mabadiliko huko nyumbani.
Kwanza, hii si mara ya kwanza na nina hakika haitokuwa ya mwisho kwa Watanzania walio nje ya nchi kulaumiwa kuhusu jambo moja au jingine.
Binafsi, ninaona sababu kubwa inayochangia hali hii ni mtizamo finyu kuwa Mtanzania akiishi nje ya Tanzania anakuwa kama nusu-Mtanzania (yaani hajakamilika).
Mara kadhaa nimekuwa mhanga wa mtizamo huo fyongo. Kuna nyakati nimetuhumiwa kuwa “ninachochea moto huko nyumbani ilhali nyumba-nchi yetu-itapoanza kuungua mie sintodhurika kwa vile niko nje.”
Wanachosahau waungwana hawa ni kwamba sidhani kama kuna Mtanzania aliye nje ya nchi ambaye hana ndugu, jamaa au rafiki huko nyumbani. Sasa tukikubaliana katika hilo, basi ni wazi kuwa miongoni mwetu Watanzania tulio nje ya nchi hakuna asiye na akili timamu za kutamani kuona ndugu, jamaa au marafiki zake wakiangamia kwa moto aliouwasha yeye.
Naomba kusisitiza tena: kuwa na makazi nje ya Tanzania hakumfanyi Mtanzania kuwa nusu/pungufu au kukosa haki ya kujadili mustakabali wa taifa letu ‘changa.’
Katika mjadala huo huko twitter muungwana mmoja alikwenda mbali zaidi na kudai kuwa kama sisi Watanzania tulio nje ambao ni mahiri kwa kulaumu pasi kushauri nini kifanyike (kwa mtizamo wa ndugu hao) hatuipendi nchi yetu basi tukachukue uraia Somalia!
Yaani kukemea maovu mbalimbali huko nyumbani imekuwa nongwa hadi tutakiwe kuchukua uraia wa nchi nyingine? Kichekesho ni kwamba baadhi ya waliokuwa wakitulaumu Watanzania tulio nje kwa ulalamishi ni mahiri mno wa si kulalamikia tu bali pia kukosoa masuala yaliyo nje ya huko nyumbani-hususan mwenendo wa soka la huku Ulaya.
Binafsi huwa ninawatafsiri kama armchair football managers, yaani makocha feki wa soka wanaokosoa huku wamebweteka kwenye makochi yao.
Kibaya zaidi, watu hawahawa wanaotulaumu Watanzania wenzao tulio nje kuwa ni walalamishi mno, nao ni mahiri pia wa kulalamika kila inapotokea ‘TANESCO wamechukua umeme wao.’
Kuna nyakati huwa ninatamani TANESCO wangekuwapo huko twitter kusikia laana, matusi na kila baya linalosemwa dhidi yao pindi umeme unapokatika.
Lakini kuna hoja nyingine ya msingi. Laiti wengi wa hao wanaotulaumu wangekuwa wanatimiza wajibu wao ipasavyo basi huenda sisi tulio nje tusingekuwa na cha kulalamikia.
Wengi wa waungwana hawa ni mifano hai ya tabaka la kati la Tanzania: vijana wenye elimu na uelewa wa kutosha kuhusu mwenendo wa nchi yetu lakini wengi wao wapo ‘bize’ kutaka washabihiane na tabaka tawala, jambo linalofanya tabaka la walalahoi kubaki kama yatima.
Wengi wa hawa wanaotulaumu ni watu ambao hupendelea kutwiti kwa Kiingereza zaidi ya sisi tunaoishi na Waingereza wenyewe (jambo linalotulazimisha kutumia lugha yao kila siku hata kama hatupendi). Hivi tuwe wakweli, waungwana hawa wana sababu ya msingi ya kujadiliana kwa kimombo ilhali wana lugha ya taifa inayojitosheleza vya kutosha?
Kuna kampuni moja ya simu huko nyumbani ambayo inalaumiwa kila kukicha huko kwenye mitandao ya kijamii kutokana na kinachoelezwa kuwa ni huduma mbovu. Baadhi ya wanaotulaumu Watanzania wa nje ni miongoni mwa walalamishi wakubwa dhidi ya kampuni hiyo ya simu.
Kimsingi, wakati wana haki ya kulalamikia kama wateja lakini nisichoelewa ni kwanini waendelee kubaki wateja wa kampuni hiyo wakati hawana mkataba unaowafunga. Angalau mie ambaye nimefungwa na mkataba wa miezi 24 na kampuni inayonipatia huduma ninaweza kuishia kulalamikia tu kwani nikivunja mkataba nitalipa fidia kubwa kwa kampuni hiyo.
Kwahiyo, walalamishi dhidi ya huduma mbovu za kampuni hiyo ni wazembe tu wasiotumia vema umuhimu wao kama watu wanaoiweka hai kampuni hiyo isiyowapatia huduma za kuridhisha. Laiti wangeikimbia, ni wazi ingelazimika kujirekebisha.
Kwa upande wangu, nimekuwa nikilalamika zaidi kuliko kupongeza kwa sababu kuna mengi ya kulalamikia kuliko ya kupongeza. Na Ifahamike wazi kuwa kila Mtanzania, awe ndani au nje ya nchi, ana haki na uhuru wa kulalamikia au kupongeza suala lolote lile, alimradi halazimishi wengine wafuate mkumbo.
Kwa zaidi ya muongo mmoja nilioishi hapa Uingereza nimejifunza kitu kimoja cha msingi. Pamoja na nchi hii kuwa moja ya mataifa tajiri na yaliyopiga hatua kubwa kimaendeleo, Waingereza si tu ni walalamishi pale inapobidi kulalamikia bali pia hawakubali ku-settle for lesser than they deserve (kupewa pungufu ya wanachostahili).
Na kwa wanaotulaumu Watanzania tulio nje kwa kulalamikia mambo ya huko nyumbani, pengine wangeelewa maisha ya maeneo mengi ya huku Ughaibuni yalivyo basi huenda wangetupongeza kwa angalau kuwakumbuka wenzetu huko nyumbani.
Ndiyo, hali ya uchumi kwa nchi nyingi za Magharibi kwa sasa si ya kuridhisha lakini bado kuna vitu lukuki vinavyoweza kutufanya ‘sie wageni’ kusahau kabisa adha na kero za huko nyumbani.
Lakini wengi wetu tumeendelea kuona ‘raha’ hizi za hapa hazina maana kama ndugu, jamaa na marafiki zetu huko nyumbani wanataabika.
Kingine cha msingi ni ukweli kwamba ili uweze kuona tofauti ya mwanga na kiza shurti uwe aidha kwenye mwanga au kiza. Wakati yayumkinika kusema kuwa ni rahisi kwa baadhi ya wenzetu huko nyumbani kukubali kuwa huduma mbovu, ufisadi na kero nyinginezo ndiyo hatima ya Watanzania, kwa sisi tulio nje tunapata fursa ya kubaini kwanini wenzetu wameweza na sisi tunakwama.
Na hii ni sababu ya msingi ya akina sisi tunaolalamikia matatizo ya huko nyumbani kwa sababu takriban kila siku tunakumbana na swali hili, kwa mfano, “Kwanini Waingereza wanaweza lakini Watanzania tunashindwa?” Na tunakumbana na jibu hili kila tuendako: wenzetu wametanguliza zaidi mbele maslahi ya taifa badala ya maslahi ya akaunti zao binafsi, nyumba ndogo zao, mahekalu yao na mambo mengine yanayokwaza maendeleo ya Tanzania yetu.
Nimalizie makala hii kwa kuwatakia kila la heri na baraka katika Mwaka huu 2013 nikitaraji kuwa mwaka huu utakuwa wa Watanzania kutambua haki na stahili zao na kuzidai (kwa amani) na kutokubali ku-settle for less.
Na kwa ndugu zangu wasiopenda kutuona sisi tulio nje tukilalamika, ushauri wangu kwao ni kuwa tunatumia haki zetu za kikatiba, na hawalazimishwi kuafikiana nasi.


0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget