Monday, 4 May 2009


WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha ameingiza serikali katika mgogoro mkubwa na wafadhili kutokana na madai ya matumizi mabaya ya madaraka, MwanaHALISI limeelezwa.

Masha anatuhumiwa kupendelea raia wa Ubelgiji, Brigitte de Floor, katika mgogoro kati yake na Wiebke Gaetje ambaye anatoka Ujerumani, jambo ambalo limeingiza serikali katika mgogoro wa kidiplomasia.

Brigitte de Floor na Wiebke Gaetje ni wajane wa Klaus Gaetje ambaye anatoka Ujerumani. Klaus Gaetje ambaye alikuwa mfanyabiashara mkoani Mwanza, alifariki dunia katika mazingira ya kutatanisha Julai 2004 huko Port Bell, nchini Uganda.

Waziri Masha anatuhumiwa na Wiebke Gaetje kuwa kikwazo katika upatikanaji wa urithi wa mume wake.

Gaetje anadai kuwa kampuni ya uwakili ya Masha, IMMMA Advocates, imehusika katika kushughulikia baadhi ya nyaraka ambazo zimesaidia “kupora mali” ya marehemu mume wake.

Miongoni mwa mali ambazo Masha anatuhumiwa kusaidia Brigitte de Floor kupora ni vivuko vitatu, viwanja vinne na “baadhi ya magari ya kampuni.”

Vivuko vinavyohusika ni Kamanga, mv Uzinza na mv Karumu. Vyote viko katika eneo la Kamanga.

Taarifa kutoka ubalozi wa Ujerumani nchini zinasema tayari serikali ya Ujerumani imelalamikia hatua hiyo ya waziri Masha ikiiita, “Matumizi mabaya ya madaraka.”

Naye Ofisa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa jijini Dar es Salaam, ambaye aliomba jina lake lisiwekwe wazi, alithibitisha kwamba “serikali ina taarifa hizo.”

Klaus Gaetje na Wiebke Gaetje walifunga ndoa tarehe 12 Oktoba 1979 nchini Ujerumani na kuzaa mtoto mmoja wa kiume, Mark Gaetje (28). Mtoto huyo na mama yake wanalalamikia Masha kushirikiana na Brigitte de Floor kutapanya mali yao.

Kwa sasa, Mark Gaetje anaishi Uholanzi na alitarajiwa kuwasili nchini juzi, Jumatatu saa nne usiku kwa ndege ya Shirika la Ndege la Uholanzi (KLM) ili kushughulikia suala hilo. Tayari mama wa Mark amewasili nchini.

Mgogoro huu uliomuingiza Masha katika kashifa nyingine, umetokana na hatua ya Brigitte de Floor, ambaye anajiita mjane wa Klaus Gaetje kudaiwa kugushi baadhi ya nyaraka ikiwamo cheti cha ndoa na wosia kwa lengo la kujimilikisha mali hizo.

Cheti cha ndoa kinachodaiwa kugushiwa ni Na. E 087887 kinachoonyesha kuwa kimetolewa 10 Oktoba 1999 wilayani Magu, mkoani Mwanza. Kimesainiwa na Msajili Msaidizi wa Ndoa, Anthony Jakonyango.

Hata hivyo, katika hati yake ya kiapo ya 5 Julai 2008 mbele ya kamishina wa viapo, Elias Kitwala, ambayo gazeti hili linayo nakala yake, Jakonyango anakana kufungisha ndoa hiyo; anasema cheti hicho ambacho waziri Masha anang’ng’ana nacho kimegushiwa.

Anasema, “Mimi nilihama Magu, 20 Mei 1999 kwenda Bukoba, mkoani Kagera. Hivyo kwa vyovyote vile, nisingeweza kufungisha ndoa Magu 10 Oktoba 1999.” Jakonyango anasema cheti cha ndoa anachodaiwa kusaini siyo halali.

MwanaHALISI limefahamishwa kwamba kwa msaada wa Masha, Brigitte de Floor amefanikiwa kumuondoa Mark na mama yake Wiebke Gaetje katika umiliki wa hisa za kampuni ya Kamanga Ferry Limited (KFL).

Katika nyaraka kadhaa ambazo ziko mikononi mwa MwanaHALISI, Masha amesaini, kama Katibu wa kampuni ya Kamanga Ferry Limited huku kampuni yake ya IMMMA Advocates ikithibitisha baadhi ya nyaraka ukiwamo wosia wa marehemu Klaus Gaetje.

Tayari wosia huo umelalamikiwa na mke wa kwanza wa Klaus Gaetje, Wiebke na mtoto wake Mark kwa hoja kwamba mke wa pili Brigitte de Floor amegushi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Idara ya Uhamiaji, Brigitte de Floor aliingia nchini kama mtalii na amekuwa akiishi nchini bila kibali cha kufanya kazi, lakini kutokana na mahusiano yake na Masha, serikali imeshindwa kumchukulia hatua.

Taarifa zinasema tayari mipango inasukwa ili kumpatia mama huyo kibali cha kuishi nchini ili kuendeleza kile kinachodaiwa na Wiebke, “urafiki wa damu na waziri Masha.”

Anasema, “Ninajua ukaribu wa familia ya Masha na de Floor. Baba yake Masha amekuwa akipewa misaada na de Floor. Tayari ameipa familia hiyo viwanja vinne ambavyo ni mali ya mwanangu.”

Katika wosia huo, Brigitte de Floor ambaye anatambulishwa kama shahidi amesaini kila karatasi, wakati saini ya marehemu inaonekana katika karatasi moja tena ya mwisho.

Aidha, familia ya Masha inatuhumiwa kumilikishwa viwanja vinne vilivyopo Kamanga, na kwamba suala hilo tayari limewasilishwa Ofisi ya Rais, kwa Waziri Mkuu, Wizara ya Sheria na Katiba, Taasisi ya Kuzuia na Kupamban na Rushwa (TAKUKURU) na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).

Wiebke Gaetje alitalikiana na mumewe, Klaus Gaetje, mwaka 1996 na baadaye Klaus alimwoa Brigitte de Floor, mtalaka mwenye watoto wa kike wawili ambao si wa Klaus Gaetje.

Hata hivyo, katika hali ambayo haijulikani chanzo chake, Masha ameridhia mali za Klaus Gaetje, zimilikiwe na watoto wa mke wake, jambo ambalo limelalamikiwa na mke wa kwanza Wiebke na mtoto wake Mark.

Brigitte de Floor anadaiwa kuhamisha fedha nyingi na kuzipeleka kwenye akaunti zake zilizoko nje ya nchi, jambo ambalo vyombo vya dola na taasisi nyingine za serikali zimearifiwa, lakini bado kimya kimetanda.

Imefahamika kuwa de Floor alitumia kampuni ya KFL kujipatia mkopo kutoka Benki ya CRDB na fedha hizo alizihamishia kwenye akaunti yake iliyopo Ubeligiji.

Klaus na Wiebke waliishi Kamanga kuanzia mwaka 1974 hadi 1994 na mtoto wao, Mark Gaetje, alilelewa kwenye eneo hilo la Ziwa Viktoria na hivyo kuusiwa na baba yake kuwa mrithi wa mali zote.

Kamanga ndipo makao makuu ya Kamanga Ferry Limited yenye vivuko vitatu vinavyofanya safari zake katika eneo hilo la ziwa Viktoria.

Baada ya kifo cha Klaus Gaetje Julai 2004, Brugitte de Floor aliamuru mwili wake uchomwe moto na kuzikwa Kamanga, tendo lililofanyika haraka na bila kushirikisha familia ya marehemu wala kuufanyia mwili uchunguzi.

“Baada ya hapo de Floor alighushi wosia wa pili wa Klaus kwa kusaidiwa na mwanasheria wake,” anasema mmoja wa watu walio karibu na Wiebke.

Tangu hapo de Floor amekuwa anadai kuwa alipewa mamlaka ya kufanya mambo yote ya KFL kwa niaba ya Mark na ametumia fursa hiyo kuwafukuza wafanyakazi wengi wa zamani na kuajiri wageni kutoka nje ya nchi.

Kutokana na hali hiyo, Mark Gaetje alilazimika kuandika barua, Oktoba mwaka jana, kwa Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Mwanza, kulalamikia hatua ya mama yake huyo wa kambo kughushi cheti cha ndoa ili kufaidi huduma za uhamiaji nchini.

Lakini pia 11 Februari mwaka huu, Mark aliandika barua kwenda kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), akilalamikia mambo manne, likiwamo la kampuni kukosa mkurugenzi baada ya aliyekuwapo kufukuzwa.

“Tangu kifo cha baba yangu sijawahi kuhudhuria kikao chochote cha bodi wala kupewa taarifa yoyote na de Floor…Isitoshe, sijawahi kupewa fedha zozote kama mkurugenzi na wala sijapokea habari kuwa de Floor ametumia kibali changu kufanya mambo kwa niaba yangu. Nakanusha kuwa sijampa ruhusa yoyote,” anasema.

Anaeleza kuwa kama kuna mabadiliko yoyote katika KFL, “Uongozi, anwani au vingine ambavyo vinaathiri kampuni na ambavyo vinadaiwa kufanyika nikiwa mshiriki kati ya mwaka 2004 na sasa, visichukuliwe umuhimu kwa kuwa vitaathiri kampuni ambayo mimi ni mkurugenzi wake,” anasema Mark.

Akizungumza kwa njia ya simu juzi Jumatatu na MwanaHALISI, Wiebke amesema tayari ubalozi wa nchi yake nchini umeomba hati ya kifo cha mumewe Klaus kutoka Uganda, kutokana na utata mkubwa uliogubika kifo chake.

Hii ni mara ya tatu mwaka huu waziri Masha kutuhumiwa kutenda kinyume cha utawala bora.

Januari alituhumiwa kuingilia mchakato wa zabuni ya vitambulisho vya taifa na Februari akatuhumiwa kufanya upendeleo kwa Mwingereza Douglas Hume Claxton kwa kufuta amri ya Mkurugenzi wa Uhamiaji ya kumfukuza nchini.


CHANZO: Mwanahalisi.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget