Matokeo ya Uchaguzi Mkuu hapa Uingereza yametuacha baadhi yetu tukiwa na majonzi baada ya chama tawala cha Labour kuambulia nafasi ya pili (viti 258) huku chama cha wahafidhina (Conservatives) waikibuka mshindi kwa kupata viti 307 (japo ni pungufu ya viti 19 kwa viti 326 vinavyohitajika kuunda serikali ya peke yao).Chama cha kiliberali (Liberal Democrats) kimeshika nafasi ya tatu kwa kuambulia viti 57.
Kila mwenye majonzi kutokana na matokeo mabaya kwa Labour ana sababu zake binafsi.Zangu ni za kibinafsi zaidi (na mambo binafsi yanapaswa kubaki binafsi).Lililo bayana ni kwamba Labour haikushindwa kwa vile ni chama kibaya au kimeboronga wakati wa utawala wake.Hapana.Tofauti kati ya hawa wenzetu na akina sie na CCM yetu ni kwamba haitoshi kuwa umefanya vizuri tu bali watu wanataka vizuri zaidi kama sio vizuri kabisa.Bahati mbaya kwa Labour ni mtikisiko wa uchumi wa dunia ambao kama ulivyoathiri sehemu nyingine ulimwenguni,umepelekea idadi kubwa tu ya Waingereza wakiwa hawana ajira sambamba na ugumu wa wastani wa hali ya maisha.Kwa lugha nyingine,hali hiyo ya uchumi (ambayo kimsingi haikusababishwa na Labour) imechangia chama hicho kuangushwa na wahafidhina.
Hadi dakika hii haijafahamika nani atakuwa Waziri Mkuu kutokana na kanuni na taratibu za uchaguzi za hapa.Tofauti na huko nyumbani ambapo wingi wa kura unatafsiri ushindi wa moja kwa moja kwa chama husika,kwa hapa ili chama kiweze kuunda serikali kinapaswa kushinda viti 326.
Nitachambua zaidi baadaye kuhusu uchaguzi huu na namna Watanzania wanavyopaswa kujifunza kwa ajili ya uchaguzi wetu hapo Oktoba mwaka huu.Ila kuna habari ya 'kuliwaza' inayokihusu chama cha kibaguzi cha BRITISH NATIONAL PARTY (BNP) ambapo mwenyekiti wake Nick Griffin ameshindwa kumuangusha mgombea wa Labour,Margaret Hodge, katika eneo la Barking lililopo mashariki mwa jiji la London.
Habari njema zaidi ni kwamba BNP imepoteza viti vyote 12 ilivyokuwa inashikilia kwenye manispaa ya Barking and Dagenham jijini London.Pengine hili linaweza kutafsiriwa kama tamko la Waingereza dhidi ya siasa za kibaguzi.BNP ilitumia suala la uhamiaji kama ajenda yake kuu kwenye uchaguzi huo lakini ni dhahiri kuwa matokeo hayo yatafikisha ujumbe kwao kuwa watu wenye akili timamu hawaafikiani na ushenzi wa wabaguzi hao.
Mengi,baadaye.Kwa sasa tusubiri matokeo ya majadiliano ya simu katika ya mgombea wa wahafidhina,David Cameron na kiongozi wa waliberali Nick Clegg yanayotarajiwa baadaye leo kuangalia uwezekano wa ushirikianio kati ya vyama hivyo.Wakiafikiana,Cameron atafanikiwa kuwa Waziri Mkuu.Lakini kama Clegg ataamua kushirikiana na Labour basi Gordon Brown ataendelea kushikilia wadhifa wake.
0 comments:
Post a Comment