Maelezo yafuatayo ni ya Mheshimiwa John Mnyika,Mbunge wa Ubungo wa tiketi ya Chadema.Nayawasilisha kama yalivyo:
Hatua nilizochukua kuhusu barabara ya Kibangu-Makoka na fidia ya Riverside
Nilichukua hatua kuhusu barabara Kibangu-Makoka na Januari nilikwenda Makuburi kuchangia matengenezo ya barabara husika , leo nimemweleza diwani kazi iharakishwe na kuhusu fidia ya wananchi wa Riverside Manispaa imenihakikishia kuwa italipwa mwezi Machi 2012; kesho nitakuwepo tena Makuburi kwa ajili ya kufuatilia masuala ya maji.
Kazi ya mbunge ni kuwakilisha wananchi na kuisimamia serikali. Kama sehemu ya wajibu huo nilitumiwa SMS na baadhi ya wananchi wa Kibangu na Makoka katika kata ya Makuburi kuhusu ubovu wa barabara ulioongezeka mara baada ya mafuriko ya mkoa wa Dar es salaam. Pamoja na kuwa barabara hii ni ya ngazi ya mitaa kwa maana ya halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, nilichukua hatua ya kuunganisha nguvu pamoja na diwani na wananchi kwa ujumla.
Izingatiwe kwamba kuhusu barabara hii nilitimiza wajibu wa uwakilishi baada ya kukutana na wananchi wa eneo husika mwaka 2010 na kunitaka niipe kipaumbele katika bajeti, kwa kushirikiana na diwani tulifanya hivyo na hatimaye barabara hii imetengewa fedha takribani milioni 100 kwa ajili ya kufanyiwa matengenezo na Manispaa ya Kinondoni katika mwaka huu wa fedha 2011/2012.
Hata hivyo, baada ya kupokea malalamiko ya siku za karibuni nilifika tena tarehe 7 Januari 2012 na kufanya mkutano na wananchi katika shule ya msingi Mabibo/Makuburi kwa ajili ya kuanza harambee ya kuunganisha nguvu ya wananchi kufanya ukarabati wa dharura wakati ambapo matengenezo makubwa ya Manispaa yakisubiriwa.
Katika mkutano huo paliundwa kamati ya wananchi wenyewe na sisi wengine tulichangia fedha na kamati ikapaswa kuwaona wadau wengine zaidi ili kazi iweze kufanyika kwa haraka. Kamati ilikuwa ni ya wananchi wenyewe lakini tulikubaliana kwamba iangaliwe kwa karibu na Diwani na Mwenyekiti wa Mtaa husika ili kuhakikisha kwamba fedha zinatumika vizuri na kazi inafanyika kwa ufanisi.
Hata hivyo, kamati haikuweza kuanza kazi kwa wakati kwa kuwa walipaswa kupata utambulisho toka kwenye mamlaka husika lakini kukawa na vikwazo kwenye ngazi ya serikali za mitaa.
Kwa maelezo niliyopewa na diwani ni kwamba pamekuwa na mvutano baina yake na Mwenyekiti wa Mtaa wa Kibangu kwa kuwa mwenyekiti husika amekuwa akinufaika na ukusanyaji wa fedha za “KITENGO”, ambazo ana hofu kwamba mchakato huu wa kuwashirikisha wananchi unaweza kutishia maslahi hayo. Diwani amenieleza kuwa kufuatia hali hiyo mwenyekiti huyo amekuwa akitumia baadhi ya vijana kupinga harakati hizo za maendeleo suala ambalo lilimlazimu diwani kuitisha wenyeviti wa mitaa yote ya kata bila kujali vyama kwenye kikao cha kamati ya maendeleo ya kata (WDC) kufanya maamuzi ya pamoja.
Mwanzoni mwa mwezi huu wa Februari wamekaa kikao husika, wenyeviti wengine wamehudhuria na kubariki kazi hiyo iendelee isipokuwa mwenyekiti wa Kibangu ambaye alitoka kwenye kikao kwa kususia.
Wenyeviti wengine na diwani wamekubaliana kuendelea na utekelezaji wa kazi hiyo ya matengenezo ya barabara, kazi ilichelewa kidogo kuanza baada ya mabadiliko ya mtendaji kata kufanyika kwenye kata ya Makuburi.
Leo tarehe 29 Februari 2012 nimemweleza diwani aendelee kusimamia kwa karibu suala hili ambalo liko kwenye ngazi yake ili ukarabati wa barabara ufanyike kwa haraka, na amenijulisha kwamba tayari walishaanza na maeneo korofi zaidi ili kupunguza adha ya usafiri.
Nimemwambia Diwani aongeze nguvu zaidi ili pamoja na michango ya wananchi kufanya ukarabati katika kipindi hiki cha mpito mpaka pale Manispaa ya Kinondoni itakapokuwa na fedha na kukamilisha mchakato wa zabuni wa matengenezo yaliyotengewa fedha.
Kwa upande mwingine, kumekuwepo na tatizo la miaka mingi la njia ya kwenda Makoka kwenye eneo la Riverside kumegwa na Mto Kibangu kwa kiwango cha barabara kutopitika na hivyo wananchi wenye magari kuzunguka umbali mrefu. Mara baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa Ubungo nilifanya uchambuzi wa Hansards za miaka ya nyuma na kuiandikia serikali itekeleze wajibu wa kuwalipa fidia wananchi husika ili njia mbadala kuweza upatikana, suala hili nimelifuatilia kwa karibu kwa nyakati mbalimbali kwa mamlaka zote zinazohusika.
Tarehe 26 Januari 2012 nilifanya mazungumzo ya kikazi na wawakilishi wananchi toka Makuburi pamoja na Meya na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni na hatimaye nikafanikisha wananchi hao kukutana na watendaji wa Manispaa na fedha zao za fidia kutengwa.
Hata hivyo, kabla ya kukabidhiwa fedha hizo baadhi yao wamekataa kiwango ambacho walikuwa wamekubaliana awali kwa maelezo kwamba thamani za nyumba zao zimepanda baada ya serikali kuchelewa kuwalipa kwa miaka mingi, hawajaridhika na kiwango cha riba kilichowapa nyongeza kwa miaka husika kwa kutozingatia bei ya soko.
Nimeendelea kufuatilia suala husika kupitia mikutano ya baraza la madiwani tarehe 25 Februari na 28 Februari 2012 na Manispaa imeahidi kufanya majadiliano nao tena kuweza kutoa nyongeza inayowezekana ili malipo yafanyike mwezi Machi. Nimemwelekeza diwani afuatilie kwa karibu utekelezaji na iwapo akikwama anijulishe ili niweze kuchukua hatua za kuingilia kati.
Natoa mwito kwa wakazi wa Makuburi kuendelea kutoa ushirikiano wa dhati kwa diwani katika kuhakikisha kwamba masuala husika yanafanyika kwa wakati, na iwapo hatua za kibunge zinahitajika msisite kunijulisha. Maslahi ya Umma Kwanza.
0 comments:
Post a Comment