WAKATI Tanzania imetimiza zaidi ya miaka 20 tangu yatokee mageuzi ya kisiasa yaliyosababisha kuruhusiwa kwa siasa za vyama vingi, kuna haja ya kufanya tathmini japo fupi kwa minajili ya kuyafanya mageuzi hayo yawe na manufaa kwa nchi yetu.
Miongoni mwa machapisho mbalimbali yanayozungumzia suala la mageuzi ya kisiasa barani Afrika ni kitabu maridhawa kilichohaririwa na Profesa Adebayo Olukushi, kinachoitwa The Politics of Opposition in Contemporary Africa (yaani, Siasa za upinzani katika Afrika ya sasa).
Katika tafiti zilizofanyika kwenye nchi saba za Afrika (na ambazo zimejadiliwa katika kitabu hicho) masuala kadhaa ‘yasiyopendeza’ yalibainika. Masuala hayo ni pamoja na
Mosi, tawala zilizokuwa madarakani (wakati wa mageuzi) kuridhia kwa ‘shingo upande’ mageuzi hayo, na matokeo yake tawala hizo zimeendelea kuyakwaza, kunyanyasa wapinzani sambamba na kuwadhoofisha na ‘kuwafitini.’
Pili, uungaji mkono wa taasisi mbalimbali (za umma na za binafsi) uliondolewa kwa kila aliyeonekana kuwa karibu au kuwaunga mkono wapinzani, na hii imeathiri uwezo wa kiuchumi wa vyama vya upinzani hususan kwa wafanyabiashara kuchelea ‘hasira za watawala’ pindi wakitambulika kuwa wanawasaidia wapinzani.
Tatu, vyama tawala kupata upendeleo zaidi ya vyama vya upinzani katika maeneo mbalimbali, hususan kutoka kwa vyombo vya habari vya umma na taasisi za usalama (ambavyo licha ya kushiriki ‘kuchakachua’ matokeo ya chaguzi mbalimbali pia vimekuwa vikiwanyanyasa na kuwaonea wapinzani).
Nne, mfumo wa uchaguzi wa ‘mshindi kuchukua vyote’ (winner takes all) umekuwa kikwazo kwa wapinzani ambapo idadi ya viti wanavyoshinda kwenye chaguzi havilingani na mgawanyo wa kura.
Tano, katika kukimbilia kwao kushiriki kwenye chaguzi chini ya mfumo wa vyama vingi, vyama vya upinzani vilijinyima fursa muhimu ya kudai mabadiliko ya Katiba ambayo yangesaidia uendeshaji wa shughuli za kisiasa wakati na baada ya chaguzi.
Sita, harakati za kisiasa za vyama vya upinzani kutegemea mno misaada au uungwaji mkono kutoka nje yao.
Japo kitabu hicho kilichapishwa miaka 15 iliyopita, tafiti husika zilifanywa nchini Kenya, Zimbabwe, Niger, Nigeria, Senegal, Afrika ya Kusini na Uganda, takriban vipengele vyote nilivyotaja hapo juu vinaakisi hali ilivyo huko nyumbani.
Wakati chaguzi mbalimbali zilizofanyika huko Kenya, Nigeria na Afrika Kusini zinaweza kutoa picha tofauti kiasi na inayobainishwa kwenye kitabu hicho, yayumkinika kuhitimisha kuwa kwa Tanzania yetu hali inaelekea kubaya zaidi. Nitafafanua.
Tuweke kando tawala za Awamu ya Kwanza na ya Pili (angalau kwa minajili ya mjadala huu), Awamu zilizofuatia (ya Rais Benjamin Mkapa na ya sasa ya Rais Jakaya Kikwete) kwa kiasi kikubwa zimetawaliwa na harakati na mikakati ya makusudi si tu ya kudhoofisha siasa za upinzani bali pia kuutokomeza kabisa upinzani.
Hata hivyo, tofauti na ilivyokuwa zama za Mkapa ambaye wapinzani wataendelea kukumbuka kwa hotuba zake kali dhidi yao, sambamba na ‘kuwaponda’ mara kwa mara, ni nadra kwa Kikwete ‘kuwapiga vijembe’ wapinzani, na hata anapofanya ni rahisi kumtoa lawamani kwa hoja kuwa “huwezi kuwa kiongozi kamili wa kitaifa wa CCM pasipo angalau ‘kuwapiga madongo’ wapinzani.” Ni kama anatekeleza tu wajibu wake kwani hata ‘tone’ yake huwa sio ya mwanasiasa mwenye chuki au uadui dhidi ya wapinzani.
Lakini kama kuna zama ambazo nchi yetu imeshuhudia siasa hatari kabisa basi ni hiyo ya Mwenyekiti ‘mpole’ wa CCM Taifa, yaani Kikwete. Sasa kama Kikwete ana ‘sura mbili’ (ya upole hadharani lakini mwenye hasira anapokuwa na wasaidizi wake ndani ya CCM na serikali), au amezungukwa na watu wenye chuki kubwa dhidi ya wapinzani, ni vigumu kuhitimisha hilo kwa dhati.
Naomba nisiume maneno. Kuna wanasiasa watatu ambao wote ni wasaidizi wa karibu wa Kikwete huko CCM, wamekuwa sio tu wakijitahidi kufanya kila wawezalo kuteketeza vyama vya upinzani-hususan Chadema bali pia wanaweza kabisa kuliingiza taifa letu matatizoni kutokana na siasa zao za chuki. Hao ni Steven Wassira, Nape Nnauye na Mwigulu Nchemba.
Wassira, maarufu kama Tyson, amekuwa ‘asset’ muhimu kwa CCM dhidi ya wapinzani, pengine kwa vile alikuwa huko kabla ya kurejea CCM. Nafasi niliyonayo katika makala hii haitoshi kuorodhesha matendo kadhaa ya mwanasiasa huyo dhidi ya vyama vya upinzani, lakini kubwa, na pengine la msingi zaidi, ni kauli yake hatari kuwa Chadema itakufa kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao.
Ikumbukwe kuwa Wassira si mnajimu wala hakuna kumbukumbu zozote zinazoonyesha kuwa ana uwezo wa kupiga ramli kubashiri uhai au vifo vya vyama vya siasa. Kauli hiyo ya Wassira ina uzito mkubwa zaidi kutokana na ukweli kuwa nafasi yake serikalini inaweza kusukuma vyombo vya dola kufanikisha utabiri wake huo (ambao kimsingi ni fyongo lakini unaoweza kutimia kwa ‘nguvu za giza.’)
Nape ni mwanasiasa ambaye binafsi ninamwona kama disappointment of the century.Kabla ya kuingia kwenye siasa za ngazi za juu, mwanasiasa huyu kijana alijipambanua kama mtu mwenye maono, ujasiri na msimamo usioyumba. Pasi kuchelea matokeo, alimudu kukosoa vikwazo kwa maendeleo na ustawi wa taifa letu na kupingana waziwazi na wanasiasa wenye mitizamo fyongo ndani ya chama chake.
Kijana huyo 'alilipa gharama’ kubwa ya msimamo wake usioyumba (wakati huo) na akakumbwa na zahma kubwa ya kisiasa. Pengine kwa kutambua kuwa kosa pekee la Nape ni msimamo wake makini, Rais Kikwete ‘alimzawadia’ ukuu wa wilaya (ambapo wachambuzi wa siasa walitafsiri hatua hiyo kama sapoti ya Rais kwa mwanasiasa huyo).
Alipoteuliwa kushika nyadhifa ya juu ndani ya CCM, Nape alikuja na nuru mpya ndani ya chama kilichokuwa kikionekana machoni mwa wengi kuwa kimezama kwenye himaya ya mafisadi, akatangaza dhamira ya kihistoria ya ‘CCM kujivua magamba,’ yaani chama hicho tawala ‘kuwakalia kooni’ viongozi na wanasiasa wake wanaohusishwa na tuhuma za ufisadi. Kwa nyakati kadhaa, Mwenyekiti wake wa CCM Taifa, Rais Kikwete alionyesha kumuunga mkono Nape.
Nikiri kuwa nami ni miongoni mwa ‘tuliongizwa mkenge’ (kughilibiwa) na suala hilo la CCM kujivua magamba. Pengine kilichoniaminisha zaidi kuhusu suala hilo ni kauli za Nape na ukweli kwamba historia yake huko nyuma ilipaswa kumwaminisha yeyote anayemfahamu vema kuwa hakuwa ‘anapiga politiki’ bali alikusudia kwa dhati kukisafisha chama chake.
Pamoja na ‘hasira’ za Nape kutonifuatilia (unfollow) kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter baada ya kumwandama kwa maswali ya/hoja za kichokozi (lengo likiwa kumhamasisha arejee kwenye mstari sahihi), bado ninaamini kwa asilimia 100 kuwa mwanasiasa huyo alikuwa na dhamira ya dhati kuivua CCM magamba, na kilichomkwaza si unafiki bali ukweli kuwa ‘tofauti na nyoka ambaye uhai wake hutegemea kujivua gamba, ukimvua gamba kobe utamuuwa.’
CCM si kama kobe bali ni kama nyoka ambaye kujivua gamba ni sehemu muhimu ya uhai wake. Jitihada zozote za kukitenganisha chama hicho na mafisadi kitakuwa na matokeo ya aina moja tu: kukidhoofisha na hatimaye kukiuwa.
0 comments:
Post a Comment