Wednesday, 3 April 2013



NIANZE makala hii kwa kutoa salamu zangu za pole kwa Watanzania waliokumbwa na janga la kuangukiwa na jengo la ghorofa zaidi ya 10 jijini Dar es Salaam, Ijumaa iliyopita.
Inasikitisha kuona uhai wa wenzetu umepotea katika mazingira ambayo kimsingi yangeweza kuzuilika.
Baada ya salamu hizo, tuelekee katika mada ya wiki hii ambayo inajadili kauli ya hivi karibuni ya Rais Jakaya Kikwete kuhusu kushuka kwa uzalendo miongoni mwa Watanzania.
Akizungumza hivi karibuni na vijana ya Taasisi ya Maendeleo ya Vijana (UVIKITA) jijini, Rais alielezea kushangazwa na tabia ya baadhi ya Watanzania kuona ufahari 'kuiponda' nchi yao, na kuwasifia wale wanaoisema vibaya, na kudai hali hiyo imetokana na wao kutojali uzalendo kwa taifa lao.
Kadhalika Rais Kikwete alidai kuwa zamani haikuwa rahisi kuwapata watu wenye tabia hiyo kutokana na utaratibu uliokuwapo. Vile vile alieleza wakati huo mtu akisema vibaya nchi yake aliwekwa katika wakati mgumu, na kwamba mabadiliko yalianza kujitokeza katika kipindi cha utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi, ambapo kiongozi huyo alikuja na “moto wake wa ruksa.”
“Mabadiliko haya yalianza na Mzee Mwinyi, enzi zetu pamoja na kipindi kuwa kigumu , hakuna aliyeisema vibaya akaachwa, sijui tumeteleza wapi? Mimi nadhani kuna mahala tumepotoka,” alisema Rais, na kuongeza, “Cha kushangaza hata wakimsikia mtu anaisifia Tanzania, wao wanapinga, na hii inatokana na wengi wao kutokuwa na moyo wa kujitolea kwa nchi yao tofauti na ilivyokuwa zamani.”
Kwanza, ninaafikiana na Rais Kikwete kuwa nchi yetu kwa sasa inakabiliwa na uhaba mkubwa wa uzalendo. Lakini pengine kabla hata ya kuanza kulijadili suala hili pengine ni vema kujiuliza swali hili: kama Rais hajui kwa nini tumefika hapa, tutarajie nini kutoka kwa mwananchi wa kawaida?
Pili, wakati ni kweli anachosema Rais kuwa kabla ya utawala wa Mwinyi haikuwa rahisi kwa mtu kuisema vibaya nchi yetu, ni muhimu kutambua kuwa zama hizo licha ya kuwa ni za siasa ya chama kimoja ambapo mtizamo tofauti na chama tawala ulikuwa sawa na uhaini, lakini pia siasa za wakati huo zilikuwa na chembe za udikteta kwa maana ya kuminya uhuru wa kutoa mawazo (freedom of expression).
Ni kweli pia kama alivyosema Rais kuwa mtu yeyote aliyejaribu kuisema vibaya nchi yetu aliwekwa kwenye wakati mgumu, lakini pia mawazo hayo hayo ambayo zama hizo yangeweza kumweka mtu katika wakati mgumu ndiyo yanayokumbatiwa hivi leo. Ni nani asiyejua kuwa baadhi ya watu tunaowaita wawekezaji leo hii ndiyo tuliowaita mabepari au makabaila zama hizo?
Wakati Rais Kikwete ana kila sababu ya kukerwa na hali hiyo ya uhaba wa uzalendo, cha muhimu zaidi si kukerwa tu bali kuchukua hatua stahili kurekebisha au kuondoa kabisa tatizo hilo. Katika uelewa wangu mdogo wa dini ya Kiislamu ninafahamu kuna mafundisho haya muhimu dhidi ya jambo baya: “ukiona jambo baya basi aidha lichukie, au likemee kwa nguvu zako zote, au ikiwezekana liondoe, hata kwa nguvu ikibidi” (nukuu hii sio rasmi).
Sasa katika kipindi hiki ambacho Rais Kikwete amebakiwa na chini ya miaka miwili kabla ya kustaafu kwake anafanya jitihada gani za kurejesha uzalendo miongoni mwa Watanzania (tukiweka kando ukweli aliokiri mwenyewe kuwa hajui kwa nini tumefika katika hali hiyo)?
Tatu, siamini kabisa kuwa kila Mtanzania anayeisema vibaya nchi yake ana makosa. Hivi ni kosa kulaumu viogozi na nchi kwa ujumla kwa kutofanya jitihada za kurejesha mabilioni yetu yaliyofichwa Uswisi na wezi ambao licha ya kufahamika lakini baadhi yao bado wapo madarakani (na pengine wakiendelea kutuibia)?
Je, ni kosa ‘kuisema vibaya’ nchi yetu pale majambazi wa EPA wanapoonewa huruma na ‘haki zao za kibinadamu’ kupewa kipaumbele, na hivyo kuambiwa walipe taratibu fedha walizotuibia, huku yule jambazi mkuu wa kampuni ya Kagoda aliyeiba zaidi ya shilingi bilioni 40 za EPA akisitiriwa na watawala ambao wamegoma katakata kumtaja hadharani (japo wengine tunamfahamu bayana)?
Na je, ni dhambi ‘kuisema vibaya’ nchi yetu wakati huu tunaomboleza vifo vya wenzetu (walioangukiwa na jengo jijini Dar Ijumaa iliyopita) ambapo mwaka 2008 kulitokea ajali kama hiyo, na aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo, Edward Lowassa aliunda tume na kutoa mapendekezo lakini yakipuuzwa, na sasa tumejikuta kwenye majonzi ambayo yangeweza kabisa kuepukika?
Ni hivi, Rais, tatizo si Mtanzania kuisema vibaya nchi yake. Tatizo ni kuisema vibaya pale inapostahili kusifiwa. Ndiyo maana hakuna Mtanzania yeyote mwenye akili timamu aliyediriki ‘kuiponda’ nchi yetu pale Taifa Stars ilipotoa ‘kipigo cha nguvu’ kwa Morocco hivi karibuni.
Kadhalika, baadhi ya tuonakerwa na ‘sifa za kutuvika kilemba cha ukoka’- kama hizo za baadhi ya taasisi za fedha za kimataifa zinazodai kuwa uchumi wetu unakua kwa kasi ilhali nchi ipo gizani kila baada ya saa na umasikini ukizidi kuongezeka- si kama hatuipendi nchi yetu bali tunakerwa na unafiki wa aina hiyo.
Moja ya sababu kubwa kabisa ya kupotea kwa uzalendo ni kuruhusu ufisadi uwe sehemu muhimu ya maisha ya Mtanzania. Hata katika ngazi ya familia tu, ni mtoto gani atakayempenda mzazi anayekwapua fedha za matumizi muhimu ya nyumbani na kwenda kuzitumia kwa anasa zake?
Nihitimishe kwa kusema kwamba japo ni jukumu la kila Mtanzania kuipenda nchi yetu (na nina hakika Watanzania wengi wanaipenda kweli nchi yao maana vinginevyo wasingevumilia jitihada za mafisadi kukomba karibu kila rasilimali tuliyonayo kila kukicha) lakini watawala wetu wana dhamana kubwa ya kuwa mfano sahihi wa uzalendo.
Kadhalika, kama kweli Rais Kikwete anakerwa kwa dhati na kushuka kwa uzalendo (na sina sababu ya kuamini vinginevyo) basi na aende mbali zaidi ya kukerwa tu au kujiuliza kwa nini hali imekuwa hivi, aanze jitihada za makusudi za kurejesha uzalendo.


0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget