Tuesday, 30 April 2013


Majuzi tumeshudhudia jinsi Mbunge wa CCM Peter Serukamba akitukana tusi baya kabisa huko Bungeni. Siku chache baadaye tukashuhudia ubabe wa kipuuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha dhidi ya wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu na Mbunge wa Chadema Godbless Lema.

Kabla kumbukumbu hizo mbaya hazijaondoka vichwani mwetu amejitokeza mtendaji mwingine wa serikali, Mkurugenzi wa Idara ya Maelezo Assah Mwambene, kuendeleza madudu yaleyale yanayozidi kuthibiths kuwa kuna ombwe kubwa la uongozi katika serikali ya Rais Jakaya Kikwete.

Jana kulikuwa na mjadala ulioanza tangu asubuhi huko Twitter kuhusu utendaji kazi wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS). Mjadala huo ulielemea zaidi kwenye jinsi taasisi hiyo inavyofanya kazi kwa kuipendelea CCM huku matishio halisi ya usalama wa taifa letu yakipuuzwa.

Kama mwananchi wa kawaida na mtumiaji wa kila siku wa Twitter nilijumuika katika mjadala huo.Kimsingi, hakukuwa na matusi wala maneno ya kuudhi bali mjadala uliotawaliwa na busara na jitihada za kushawishi mabadiliko ya uendaji kazi wa TISS.

Ghafla akajitokeza Bwana Mwambene, na kuanza kuhoji kwa nini tunaijadili TISS kiholela. Nikajaribu kumfahamisha kuwa Twitter haipo chini ya Idara ya Maelezo, na ni mtandao wa jamii ambao unaruhusu watumiaji kutoa mwazo yao angalau kwa ustaarabu.

Badala ya kuzingatia ushauri huo,Bwana Mwambene akanigeukia mie akidai inashangaza kuizungumzia TISS ambayo ilinifukuza kazi (kwa mujibu wa maelezo yake).

@isongole: @chahali jamani kama mmekosa story za kuongea ebu kaeni kimya mimi. najua baadhi yenu mlivyofukuzwa kazi mnataka ndo iwe hoja hapa

Akaendelea 

@isongole: @Chahali ukifika kuitukana taasisi iliyokufukuza kwa makosa tunayoyajua unataka tusemeje kwenye mtandao hii ndugu yangu.

Sasa utoto huu wa kutishiana vitu ukifanywa na mtu wa kawaida sawa, lakini unapofanywa na mtu aliyeteuliwa na Rais kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali inatia doa hata huyo Rais aliyefanya uteuzi huo.Kama mpuuzi huyu anajua SIRI iliyopelekea 'kunifukuzisha kazi' (kwa mujibu wake) kwanini asiiweke bayana badala ya 'kunitishia mtu mzima nyau'?

Hawa ndio wapuuzi waliopewa dhamana ya kuongoza taasisi nyeti kabisa.Hawajui tofauti ya lugha ya malumbano mtaani na lugha ya kiofisi.

(Lakini kwa upande mwingine, tutegemee nini kwa mtu aliyeonyesha u-kichwapanzi kama huu? Katika hali isiyoeleweka, Mkurugenzi wa Habari na Maelezo Ndg. Asah Mwambene alijikuta akitoboa siri hadharani, either kwa makusudi au bila kukusudia aliposema Mh. Zitto alimtahadharisha asiwe na urafiki na watu kama Mkurugenzi wa gazeti la MwanaHalisi Ndg Saed Kubenea isije kumharibia kazi. Asah alisema Zitto alimpa ushauri huo muda mfupi tu mara baada ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo kutoka kwa Clement Mshana ambaye amekwenda TBC alipokwenda bungeni Dodoma kujitambulisha kwa Waheshimiwa wabunge. )

Kwa upeo wake finyu, mteuliwa huyu wa Rais alidhani kuwa porojo zake kuwa "nilifukuzwa TISS"  zingenitisha nisiendelee kujadili masuala muhimu yanayohusu mustakabali wa taasisi hiyo na taifa kwa ujumla.

Sijui kama alitumwa na serikali kuja kufanya vitisho hivyo huko Twitter au ni kimbelembele tu cha kulind ajira yake inayopeleka mkono wake kinywani, lakini kilicho wazi ni kuwa Bwana Mwambene alitaka kuigeuza Twitter kama chombo cha habari cha Tanzania kinachofanya kazi chini ya uangalizi mkali wa serikali kupitia Idara ya Maelezo inayoongozwa na Mwambene.

Sipendi kuzungumzia maisha yangu ya zaidi ya miaka 10 kama mtumishi wa TISS (ambapo nilianza kutoka ngazi ya chini kabisa hadi kufikia ukuu wa kanda ya kiusalama). Lakini tofauti na madai ya Bwana Mwambene kuwa nilifukuzwa kazi kwa makosa anayoyajua, nililazimika kuachana na taasisi hiyo kutokana na kuandamwa mara kwa mara kwa sababu ya makala nilizokuwa nikiandika kwenye magazeti ya Kulikoni na Mtanzania na baadaye Raia Mwema (baada ya kuja masomoni huku Uingereza).

Niseme ilifika mahala kuwa ajira yangu ndani ya taasisi hiyo ilikuwa haiwezekaniki kutokana na tuhuma na hisia kuwa makala zangu zilikuwa zikiwatumikia wapinzani wa chama tawala na hisia kuwa nilikuwa nikitumikia 'taasisi zaidi ya TISS' (kosa ambalo kisheria ni uhaini).

Mwezi Oktoba mwaka 2006 nilipigiwa simu na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TISS Bwana Jack Zoka akihoji kama mie bado ni mtumishi wa serikali ya Tanzania au la, na kuniamuru niache kuandika makala za siasa hususan zile zinazoikosoa CCM. Tukio hilo lililotokea siku chache baada ya mie kuandika makala iliyokuwa ikimkosoa aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa katika jitihada zake za ku-lobby wabunge wa CCM wasijadili ishu ya Richmond. Miaka miwili baadaye, ishu hiyohiyo iliyomfanya Zoka anipigie simu ilipelekea Lowassa kulazimika kujiuzulu.

Siandiki makala hii kumshawishi Mwambene au mtu yeyote yule kuwa uamuzi wangu kuachana na TISS ulitokana na unyanyasaji dhidi yangu kwa sababu tu ya maoni yangu ya kisiasa (political opinions). Ninajivunia nilivyolitumikia taifa langu wakati huo na ninavyoendelea kulitumikia hivi sasa kupitia makala zangu.

Sijisikii aibu kutuhumiwa kuwa nilifukuzwa kazi kwa vile tu nilisimami kwenye haki.Wa kujisikia aibu angekuwa marehemu Daudi Balali (kama ni marehemu kweli) aliyekwapua mamilioni ya fedha na 'kuingia mitini' kisha tukaambiwa amefariki. Sijisikii aibu kwa vile mie si mmoja ya watumishi wa TISS ambao walitajwa kuhusiska na ufisadi wa EPA lakini hawajachukuliwa hatua hadi leo.

Kilichonikera ni mawazo ya kale ya Bwana Mwambene kudhani kuwa Twitter inaweza kuzibwa mdomo kama walivyofanya kwa gazeti la Mwanahalisi ambalo kosa lake pekee ni habari iliyomtaja Afisa Usalama wa Taifa aliyehusika na utekaji na uteswaji wa Dokta Ulimboka 

Talking about Mwanahalisi, hiki ndicho alichosema Bwana Mwambene 

@isongole: @Chahali  Mwanahalisi ilifinguwa nikiwa Mambo ya Nje lakini hata ningekuwepo ningewafungia maana walipita mipaka ya taaluma ya uandishi

Huwezi kuamini kuwa kauli hii inatoka kwa mtu ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari. Mwambene anafahamu fika kuwa laiti gazeti la Mwanahalisi lingekuwa limekiuka maadili ya uandishi wa habari kwa kuandika habari za uchochezi au kashfa basi sehemu mwafaka kwa serikali na gazeti hilo kupata haki ilikuwa mahakamani.

Mwanahalisi lilifungiwa kwa sababu moja tu: kuliziba mdomo lisiweke hadharani mkakati dhalimu unaoendelea wa kuteka na kung'oa kucha kila anayeonekana tishio kwa utawala wa kifisadi.

Majuzi walituma wazembe flani kujaribu kunidhuru (naamini bado wanaendelea na mkakati huo dhalimu ambao nina imani hautofanikiwa). Sasa wameafikia hatua ya kumtuma Msemaji wa Serikali, Mkurugenzi wa Idara ya Maelezo Bwana Assah Mwambene ajaribu kutuziba mdomo hadi kwenye mitandao ya kijamii.

Halafu Rais Kikwete anasema nchi haijamshinda ilhali watendaji wake wanafanya mabo ya kipuuzi kana kwamba ni wahuni wa vijiweni. Does it make any sense kwa Msemaji wa Serikali kuingilia maongezi ya kawaida tu ya wananchi huko Twitter na kuwalazimisha waache kuongelea 'mambo nyeti.'? Huu sio udiktrata bali upuuzi wa hali ya juu


Nimalizie makala hii kwa kumtahadharisha Mwambene kuwa hakuantawala iliyokuwa na nguvu za kutisha huku ikitumia mashuishushu kial kona kama USSR (Muungano wa Jamuhuri za Kisosahalisti za Urusi). Pamoja na nguvu kubwa za taasisi yake ya ushushushu ya KGB, haikuwezekana kuzuwia kuporomoka kwa utawala wa USSR na ukomunisti wa Ulaya Mashariki kwa ujumla.

Kuna siku CCM itaondoka madarakani, na ni wakati huo ambapo watu kama Mwambene watakuwa wanahaha kutafuta sehemu za kujificha. Huo utakuwa ni uhuru wa pili kwa wote wanaonyanyaswa sasa kwa vile tu si miongoni mwa watawala wachache, sambamba na akina sie tunaopiga kelele zinazotishia kutia mchanga kwenye keki ya taifa inayotafunwa na mafisadi.



Time will tell!



1 comment:

  1. nakala safi sana ndugu yangu usife moyo endelea kusema ukweli kwani tunahitaji watu kama wewe kwenye taifa letu. Mungu akulinde

    ReplyDelete

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget