Dk. Slaa: Kikwete ajiuzulu
• Asisitiza anahusika na Dowans, aahidi kutoboa siri
na Janet Josiah
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilibrod Slaa, sasa amekuja na hoja mpya ya kumtaka Rais Jakaya Kikwete ajiuzulu kutokana na kuhusika moja kwa moja na sakata la Dowans iliyorithi mikoba ya Richmond.
Dk. Slaa ametoa kauli hiyo nzito jana katika mahojiano maalumu na Tanzania Daima Jumatano, ikiwa ni siku moja baada ya Ikulu kutoa taarifa ya kejeli na vijembe vya mitaani dhidi yake kuhusu sakata hilo.
Akizungumza kwa utulivu na umakini mkubwa, Dk. Slaa alisema Rais Kikwete alipaswa kujiuzulu kabla ya aliyekuwa Waziri Mkuu na swahiba wake mkubwa, Edward Lowasa, kuchukua hatua hiyo Februari 7, mwaka 2008, mjini Dodoma.
Mawaziri wengine waliojiuzulu kutokana na sakata la Richmond lililozua mjadala mkali nchini ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini wakati huo, Nazir Karamagi na Ibrahim Msabaha ambaye alikuwa waziri wa wizara hiyo kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC).
Akitoa ufafanuzi wa taarifa ya Ikulu iliyotolewa juzi na Kurugenzi ya Mawasiliano, Dk. Slaa alisema mkuu huyo wa nchi hawezi kukwepa kuhusishwa na sakata la Dowans, kwani alilijua hata kabla mitambo yake haijaingizwa nchini.
"Nataka niwatoe Watanzania wasiwasi kwamba ingawa kurugenzi ya mawasiliano imetoa taarifa ya kumsafisha Rais Kikwete na kunikashifu mimi kwa lugha ya mtaani, nawaambia alipaswa kujiuzulu kabla na anatakiwa ajiuzulu sasa, kwani anahusika moja kwa moja na uingiaji wa mkataba wa Kampuni ya Richmond na baadaye na Dowans" alisema Dk. Slaa.
Alimtaka Rais Kikwete kutambua kuwa hawezi kukaa kimya kwa kisingizio cha kuhatarisha amani na utulivu wakati wananchi wanaibiwa mabilioni ya fedha na mafisadi wachache kupitia kampuni feki ya Dowans.
Akirejea historia ya vita dhidi ya ufisadi aliyoiasisi bungeni, Dk. Slaa aliwataka wananchi wakumbuke kuwa taifa lilipokumbwa na tatizo la umeme kabla ya mitambo ya Richmond kuingia nchini, Rais Kikwete alikwenda Marekani kwa ziara ya kikazi.
Alisema aliporejea nchini, alizungumza na waandishi wa habari kuhusu tatizo hilo na kuahidi kuwa serikali yake inalifanyia kazi na siku chache baadaye, rafiki yake wa karibu, Rostam Azizi, Mbunge wa Igunga (CCM), naye alikwenda Marekani.
"Rostam aliporejea kutoka Marekani baada ya siku chache tukaanza kusikia mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura kutoka Kampuni ya Richmond inatarajiwa kuwasili. Kweli ilitua nchini katika Uwanja wa Mwalimu Nyerere na shughuli nyingine zilifungwa uwanjani hapo kupisha ushushaji wa mitambo ya Richmond" alisema Dk. Slaa.
Kwanini Rostam Asiwe na Furaha?Kuendesha Nchi ya Watu Takriban Milioni 50 kwa Kutumia Remote Control si Jambo Dogo Ati! |
Huku akisisitiza kuwa ana ushahidi wa anachokisema, Dk. Slaa alisema hata baada ya Richmond kushindwa kuzalisha umeme na kusababisha mawaziri kujiuzulu, serikali ya Kikwete iliamua kuingia mkataba na Dowans iliyorithi shughuli za Richmond na hatua hiyo Rais Kikwete pia aliijua.
"Dowans nayo ikashindwa kuzalisha umeme, mwisho Bunge katika moja ya maazimio yake liliridhia uamuzi wa kuvunja mkataba huo, lakini leo Serikali inadaiwa fidia ya sh bilioni 185, je, Rais Kikwete anaweza kukwepa kwamba hana mkono wake hapo?" alihoji.
Kutokana na hayo, Dk. Slaa alimtaka Rais Kikwete amtaje mmiliki halali wa Dowans ili kuwatoa kiu Watanzania wanaohitaji kumjua.
"Sitaacha kuzungumzia masuala yanayowagusa Watanzania na mali, hasa katika kipindi hiki ambacho Watanzania wanataka kuibiwa fedha zao, wakati wa kukaa kimya umekwisha" alisema Dk. Slaa.
Alisema hashangazwi na kejeli za Ikulu na kuwataka Watanzania kukumbuka alipoanza kuwalipua mafisadi, Rais Kikwete aliwahi kutamka kwamba kelele za mlango haziwezi kumnyima mwenye nyumba usingizi na kamwe kelele za chura hazimzuii ng ombe kunywa maji.
"Lakini baada ya sisi kuamua kupambana na Richmond, Rais Kikwete alikiri linamnyima usingizi na hili la Dowans litamnyima usingizi zaidi katika kipindi hiki cha mwisho cha uongozi wake" alisema Dk. Slaa.
Ili kumaliza kelele za Dowans, Dk. Slaa alimtaka Rais Kikwete kumtaja mmiliki wake ambaye anataka kuwaibia Watanzania mabilioni ya fedha.
Wakati Dk. Slaa akimkaba koo Rais Kikwete, mjadala wa Dowans hivi sasa umewavuruga hata viongozi wa serikali tangu ilipoamriwa ilipwe sh bilioni 185.
Aliyekuwa Spika wa Bunge lililopita, Samuel Sitta, hivi karibuni alikaririwa akiitaka serikali iache kuilipa Dowans kwa madai kuwa ni mradi wa mafisadi watatu.
Kauli hiyo ilipingwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye alisema kuwa suala la malipo ya Dowans lipo kisheria na ikithibitika serikali haiwezi kukata rufaa, italazimika kulipa mabilioni hayo.
Juzi Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu imeelezea kukerwa kwake na hatua ya Dk. Slaa kumtaja Rais Kikwete kuwa alihusika katika uzembe uliosababisha taifa kutakiwa kuilipa Kampuni ya Dowans sh bilioni 185 kama fidia.
Taarifa hiyo kali ya Ikulu iliyobeba ujumbe wenye maneno ya kebehi na ya mitaani ya kumwita Dk. Slaa mtu aliyechanganyikiwa na mzabinazabina ilisainiwa na Salvatory Rweyemamu, ambaye kabla ya kwenda Ikulu alikuwa mmoja wa wahariri watendaji, aliyekuwa akiheshimika kwa kutumia lugha fasaha na ya staha.
Rweyemamu katika taarifa yake hiyo iliyoonyesha waziwazi kuandikwa na mtu mwenye hasira, chuki na dharau ama kwa Dk. Slaa, CHADEMA na Tanzania Daima, alikwenda mbali na kumwita kiongozi huyo wa kisiasa kuwa ni mtu hatari.
Katika mahojiano maalumu na gazeti la Tanzania Daima Jumapili, mwishoni mwa wiki, Dk. Slaa alikaririwa akisema chanzo cha suala la Dowans kutakiwa kulipwa fidia limetokana na uzembe wa serikali na Rais Kikwete mwenyewe anahusika kuileta Kampuni ya Richmond ambayo baada ya kuonekana ya kitapeli iliamua kurithisha kazi zake kwa Dowans.
VYANZO: Habari kwa Mujibu wa Tanzania Daima.Picha Kutoka Vyanzo Mbalimbali Mtandaoni.
VYANZO: Habari kwa Mujibu wa Tanzania Daima.Picha Kutoka Vyanzo Mbalimbali Mtandaoni.
Jamani mwenye macho haambiwi tazama. Hivi kweli unaweza kumpigia debe mtu aliyekuwa mtuhumiwa wa Richmond nasijui so called msimaizi wa Dowans alafu useme mmiliki wake humjui? Kwani si-kiasi chakumpigia Rostam simu nakuuliza hivi mkubwa wako wa Dowans ni nani? Napata hasira mtu anapojaribu kuona watanzania wote nimapunguani. Kwakweli JK hana jinsi kipindi hiki niku-accept responsibilities ya yote yanayotokea.Huwezi kuwa kiongozi safi ukawa na wasaidizi mafisadi unless na wewe ni fisadi kiaina. Kitu kinachoshangaza kunawatu bado wanasema kidumu chama cha mapinduzi insasikitisha kwakweli. Kama CCM kuna watu safi kwanini wanakubali kuongozwa na mafisadi? Mimi siko kwenye chama chochote lakini I can't figure out the motives behind those Kikwete followers. It does not make sense at all if you real love your country.
ReplyDelete