Friday, 7 January 2011







Mbunge wa zamani kutoka chama cha Labour hapa Uingereza,David Chaytor (pichani juu),leo amelala usiku wa kwanza akiwa jela kama mfungwa baada ya kuhukumiwa kifungo cha miezi 18 kutokana na kukutwa na hatia ya ubadhirifu wa fedha za umma takriban pauni 20,000 (takriban shilingi 45 milioni za Tanzania).Ubadhirifu wa fedha hizo za umma ni kutokana na matumizi mabaya ya fedha za posho kwa wabunge.


Wakati hayo yakijiri hapa,huko nyumbani Waziri wa Nishati na Madini,William Ngeleja alivunja mzizi wa fitina kwa kutangaza hadharani kuwa hatimaye serikali italipa shilingi 95,000,000,000 (bilioni tisini na tano) kwa kampuni ya kifisadi ya Dowans kufuatia hukumu ya kiini macho iliyotoa ushindi kwa kampuni hiyo licha ya rundo la utata linaloendelea kuizunguka.



Ngeleja,bila haya wala uoga,alieleza kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (Frederick Werema) ameridhia hukumu hiyo ya miujiza kabisa na ushauri wake wa kitaalam (ya sheria) ni kuilipa kampuni hiyo.

Wote,Ngeleja na Werema ni wateuliwa wa Rais Jakaya Kikwete,ambaye kwa makusudi kabisa aliepuka kuzungumzia suala la Dowans katika hotuba yake ya kukaribisha mwaka mpya 2011.Ni dhahiri kuwa Kikwete ameridhia Dowans ilipwe na ndio maana Ngeleja na Werema wanatoa maamuzi yao bila hofu wala aibu. Na kama umesahau,ni Kikwete huyuhuyu aliyeahidi wakati wa kampeni zake kuwa ana dhamira ya kuboresha maisha ya Watanzania.Nadhani labda alichomaanisha ni kuboresha akaunti za mafisadi kwa mgongo wa walalahoi.

Napata shida kutumia lugha ya kistaarabu kushangazwa na uwendawazimu huu!Hivi hawa viongozi wetu wamerogwa na mafisadi au ni matokeo ya kupokea fadhila za mafisadi kupita kiasi kwamba sasa wanalazimika kulipa fadhila hizo kwa gharama yoyote ile?Hizi sio tamaa za kawaida tulizozowea kuziona kwa watawala wetu.Hiki ni kichaa hatari ambacho pasipo hatua za haraka kinaweza kupelekea nchi nzima kuuzwa,kisha akina Werema wakaja kutuambia gharama za kuzuia kuuzwa kwa nchi yetu ni kubwa kuliko uamuzi wa kukubali nchi iuzwe.

Blogu hii ilifanya kila ilichoweza kuhamasisha wapiga kura waiepuke CCM na mgombea wake Kikwete.Sio kwamba blogu hii ilifanya utafiti wa kina kubaini athari za kuirejesha CCM madarakani bali taarifa kuhusu uhuni wa chama hicho,sambamba na kilivyojipa jukumu la kuwa kichaka cha kuhifadhi mafisadi,zilikuwa bayana kwa kila mwenye macho.Hivi kuna Mtanzania asiyefahamu kuwa ujio wa kampuni ya kijambazi ya Richmond (iliyopelekea ujambazi mwingine wa Dowans) ulikuwa na baraka za Kikwete pamoja na swahiba wake Lowassa na "kubwa la maadui" Rostam Aziz?





Ndio maana majuzi baada ya aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema,Dkt Wilbroad Slaa,kurejea kauli yake kuwa Kikwete ni mmiliki wa Dowans,hasira za mkuu huyo zikaishia kwa kuamuru polisi wake kutoa kipigo kwa raia wasio na hatia huko Arusha na kupelekea vifo kadhaa (Polisi wanadai wameua watu watatu tu lakini tangu lini wauaji wakaaminika?).


Na kama adhabu ya Kikwete kwa Chadema na wana-Arusha haijatosha,kaamua kuwadhihaki Watanzania wote kwa kuidhinisha Dowans ilipwe mabilioni hayo,huku swahiba wake Rostam akidhihaki Watanzania kwa kudai hizo bilioni kadhaa ni fedha kiduchu tu kwake.Huwezi kumlaumu kwani kaiweka serikali mfukoni na anaendesha nchi kwa remote control.

Blogu hii iliwaasa wapiga kura kuhusu madhara ya kumpatia Kikwete miaka mitano mingine baada ya awamu yake ya kwanza kugubikwa na ufisadi wa kutisha.Lakini hata kwa viwango vilivyozoeleka vya ufisadi hakuna aliyetarajia kuwa hata kabla miezi mitatu haijapita tangu arejee madarakani,Kikwete angediriki kuruhusu Watanzania wenzie wabakwe kiuchumi kwa mtindo huu wa Dowans.Lakini kwa vile Katiba tuliyonayo inampa madaraka mithili ya mungu-mtu,na kwa vile anafahamu fika kuwa Watanzania ni wepesi wa kusahau na ndio maana wengi wao wakampigia kura licha ya maumivu aliyowasababishia tangu aingie madarakani Desemba 2005,ameruhusu ujambazi huu wa mabilioni ya fedha za walipa kodi pasi soni.

Tusipochukua hatua za haraka tutashtukia tumefikishwa mahala ambapo hatutokuwa na namna ya kurekebisha mambo.Kama less than three months tangu Kikwete arejee madarakani tumeshashuhudia Dowans ikizawadiwa mabilioni kama asante ya kututapeli,na tumeona hasira za Kikwete kwa ukatili na mauaji yaliyofanywa na polisi wake (kisa kasutwa kuwa analea ufisadi),ni wazi kuwa hali itazidi kuwa mbaya na yawezekana ikawa ya kutisha kabla Kikwete hajamaliza muda wake hapo 2015 (assuming hatachakachua Katiba kutaka aongezewe muda).

Moja ya hatua inayoweza kuzaa matunda ni kufikisha kilio chetu kwa nchi wahisani.In addition to malezi anayotoa Kikwete kwa mafisadi,sasa tuna jambo jingine zito ambalo linaweza kuvuta hisia za wahisani,nalo ni ukiukwaji wa haki za binadamu kama ilivyodhihirika huko Arusha.



Kwa kuanzia,blogu hii inamwomba kila mzalendo anayeishi katika nchi mfadhili kwa Tanzania,kuwasiliana na mbunge wake na kumwomba afikishe kilio cha wanyonge wa Tanzania.Toa chapa ya picha za matukio ya Arusha pamoja na habari zinazobainisha ukiukwaji wa haki za binadamu,na ufisadi,kisha mfahamishe mbunge huyo kuwa hii ndio hali halisi ya Tanzania chini ya utawala wa Kikwete.Kama utahitaji maelezo zaidi ya namna ya kuwasilisha ujumbe wako kwa mbunge wa sehemu unayoishi,usisite kuwasiliana nami.

KWA USHIRIKIANO WETU,TUNAWEZA KUPAMBANA NA UTAWALA DHALIMU AMBAO LICHA YA KUUA RAIA WASIO NA HATIA HUKO ARUSHA,UNATOA ZAWADI YA SHILINGI BILIONI 95 KWA DOWANS KANA KWAMBA HIYO NDIO RAMBIRAMBI KWA WALIOUAWA NA POLISI HUKO ARUSHA.

3 comments:

  1. Ingekuwa wa-Tanzania ni watu makini katika kusoma vitabu wangekuwa wanasoma angalau maandishi ya Mwalimu Nyerere, ambaye miaka ya mwisho ya maisha yake, alitutahadharisha kuhusu CCM.

    Lakini wa-Tanzania ni wavivu, hata hawajui hayo. Matokeo yake ni kama walivyotamka wahenga, kwamba asiyesikia la mkuu huvunjika guu.

    Kuhusu jinsi Mwalimu Nyerere alivyoigopa CCM, soma hapa.

    ReplyDelete
  2. Mimi ni mwana harakati na mkereketwa na mageuzi, na ni mmoja wa watu ambao sikubaliani na sera za ccm, ila nimesoma profile yako na unatueleza kuwa unasoma kuhusu waislam na vikundi vya kiislam vya nchini tanzania, na wewe ni mkiristo sasa kwa upande wangu mimi sikuelewi ya kwamba ni kwa nini unasoma kuhusu waislam wa tanzania wakati sio dhehebu lako kwanini usingesomea mambo ya wakristo kwa kuwa wewe ni mkristo?

    ReplyDelete
  3. Anonymous,kwani ni dhambi kwa Mkristo kusoma kuhusu Uislam?Kwanini usiangalie hoja/makala zangu badala ya imani yangu?

    ReplyDelete

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget