TUHUMA za ufisadi ambazo Dk. Willibrod Slaa amemshushia Rais Jakaya Kikwete, zimezima mbwembwe na majigambo ya “mapambano dhidi ya ufisadi” ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), MwanaHALISI limeelezwa.
Mwishoni mwa wiki, ikiwa ni wiki moja tangu CCM itangaze “kujivua gamba” la ufisadi, Dk. Slaa amemtuhumu Rais Kikwete kushindwa kusimamia rasilimali za taifa kwa kuruhusu au kunyamazia wizi wa Sh. 249 bilioni.
Fedha hizi ni zile za mfuko wa madeni ya taifa.
Aidha, Dk. Slaa amesema Rais Kikwete ameshindwa pia kusimamia matumizi ya Sh. 70 bilioni zinazodaiwa kurejeshwa na wezi waliokiri kuiba kutoka akaunti ya EPA “ambazo hadi sasa hazijulikani matumizi yake.”
“Udhaifu huu wa Kikwete na serikali yake umechangia ufisadi wa kiwango cha juu katika matumizi ya fedha za umma,” ameeleza Dk. Slaa.
Kwa mujibu wa nyaraka za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambazo Dk. Slaa amenukuu, Sh. 70 bilioni zilidaiwa kuingizwa katika Benki ya Rasilimali (TIB) na baadaye zikadaiwa kuwa zilitolewa ili kuanzisha benki ya wakulima ambayo haijaanzishwa.
Dk. Slaa alidondosha makombora hayo kwenye mkutano mkubwa wa hadhara katika uwanja wa Chipukizi mkoani Tabora, Jumamosi alasiri.
Kwenye mkutano huo, Dk. Slaa aliwataja pia rais mstaafu Benjamin Mkapa, makamu mwenyekiti mstaafu wa CCM John Malecela, katibu mkuu mstaafu wa CCM, Philip Mangula, waziri wa ujenzi, John Magufuli na ofisa wa ngazi ya juu wa mamlaka ya mapato ya taifa (TRA), Placidius Luoga kuwa wameshiriki ufisadi.
“Hawa, kwa njia mbalimbali, ama wameruhusu au wameidhinisha au wamenyamazia ufujaji wa raslimali za taifa,” Dk. Slaa aliuambia mkutano wa hadhara uliohudhuria na umati wa wananchi.
Hii ni mara ya pili kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuanika majina ya wale kinaowaita “vigogo wala nchi” kwa kuwahusisha na ufujaji wa fedha na raslimali za taifa.
Akiwa na wanasheria wa chama hicho, Mabere Marando na Profesa Abdallah Safari, Dk. Slaa alisoma jina moja baada ya jingine na kutoa maelezo juu ya ushiriki wa kila mmoja katika alichoita kufisidi taifa.
Tayari kishindo cha CHADEMA mjini Tabora kimeleta kizaazaa ndani ya CCM na kufanya nderemo za juu ya kujivua gamba kuonekana kama tamthiliya.
Haya yanatokea wakati katibu mkuu mpya Wilson Mukama anasema atapambana na “mafisadi” na kwamba atawaandikia barua kuwataka wajiondoe kwenye chama.
Naye katibu mwenezi mpya, Nape Nnauye, akinusa kishindo cha Tabora, amejiingiza katika malumbano na CHADEMA. Jumapili mjini Zanzibar, alidai kuwa CHADEMA kinatumiwa na “mafisadi” ili kumchafua Rais Kikwete na mtoto wake Ridhiwani.
Lakini kwenye mkutano wa Tabora, hakuna kiongozi yeyote wa CHADEMA aliyetaja jina la Ridhiwan, jambo ambalo limetafsiriwa kuwa Nnauye alitarajia kuona jina la mtoto huyo wa rais katika orodha ya watuhumiwa.
Wakionekana wamejipanga na kufanya kile walichokiamini, Dk. Slaa na timu yake walianza kueleza kile walichoita, “wizi mkubwa usioweza kuvumilika” uliofanywa na viongozi wa CCM na watendaji serikalini.
Alikuwa Profesa Safari aliyeanza kumtuhumu Mkapa kuwa ameingiza nchi katika matatizo makubwa kwa kuruhusu uuzaji holela wa nyumba za serikali. Alisema nyumba hizo ni sharti zirejeshwe serikalini na bila masharti.
“Tunataka nyumba hizo zirejeshwe mara moja. Iwapo hilo halikufanyika, tutatumia nguvu ya umma kuzirejesha,” alieleza Prof. Safari huku akishangiliwa.
Naye Marando alisema hakuna kiongozi yeyote ndani ya CCM, akiwamo Rais Kikwete, anayeweza kujinasua katika tuhuma za wizi wa mabilioni ya shilingi za EPA zilizokwapuliwa ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Akiongea huku akiwa na nyaraka kadhaa mkononi alizodai zilitumika kukwapulia mamilioni hayo, Marando alisema katika wizi huo, Mkapa ndiye kinara mkuu.
Aliwataja wengine waliohusika na wizi huo kuwa ni Rais Kikwete, Rostam Aziz na Edward Lowassa. Marando aliituhumu serikali kwa kushindwa kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wakuu wa wizi wa EPA, badala yake imeshitaki “vidagaa.”
“Mimi nimepata nyaraka zinazoonyesha kuwa John Kato, ndiye William Kemhondo na Francis William ni Barack Goda. Wote hawa wawili ni wafanyakazi wa kampuni ya Caspian Limited, inayomilikiwa na Rostam Aziz.
Akasema yuko tayari kuendesha kesi dhidi ya Kagoda bure na kuahidi kuwa haitafika mwaka 2015 kabla hajawatia gerezani watuhumiwa wote.
Ndipo ikafuata zamu ya Dk. Slaa. Akaanza kueleza wizi ulivyotokea na akasoma tuhuma ya kila mmoja. Akasema orodha yake ya sasa, itaongezeka kwa kadri nyaraka na ushahidi unavyokusanywa na kupitiwa na timu ya wanasheria wa chama chake.
Akiongea kwa staili ileile ya Mwembeyanga, ambako alitangaza orodha ya kwanza ya watuhumiwa 11 wa ufisadi, miaka mitatu iliyopita, Dk. Slaa alisema, “Kuna watu wananituhumu kwamba mimi namsakama Kikwete kwa kuwa ni muislamu. Mimi siangalii dini ya mtu, kabila lake wala sura yake.”
Akivuta pumzi, Dk. Slaa alisema, “Ninachoangalia ni nchi yangu. Ndiyo maana huko nyuma niliwahi kumkemea Sumaye (Fredrick Sumaye) ambaye ni ndugu yangu, kabila langu na dini moja. Lakini pale serikali ilipolegalega katika kusimamia rasilimali za taifa, nilimkemea bila woga.” Ndipo alianza:
Jakaya Kikwete: Huyu ameshindwa kusimamia rasilimali za taifa kwa kuruhusu au kunyamazia wizi wa Sh. 249 bilioni pamoja na Sh. 70 bilioni zilizorejeshwa na wanaodaiwa kuwa wezi wa EPA. Fedha hizo, kwa mujibu wa nyaraka za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), zilidaiwa kuingizwa katika Benki ya Rasilimali (TIB) na baadaye zikadaiwa kuwa zilitolewa ili kuanzisha benki ya wakulima.
Nyaraka zinaonyesha kuwa pamoja na fedha hizo kutolewa TIB, hadi sasa kinachoitwa benki ya wakulima hakijaanzishwa. Alitoa siku 90 kwa Kikwete kueleza mahali ziliko fedha hizo, vingevyo yeye na chama chake wataamini kuwa fedha hizo zilitumiwa na CCM katika uchaguzi mkuu uliopita.
“Huyu Kikwete amefadhiliwa na wezi, ndiyo maana ameshindwa kuchukua hatua kwa wezi hao,” alieleza.
Dk. Slaa amesema anatoa siku 90 kwa serikali kueleza zilipo fedha za DECI, Sh. 70 bilioni za EPA, Sh. 249 bilioni kutoka deni la taifa na mabilioni mengine ambayo yamegunduliwa na mkaguzi wa hesabu za serikali.
Katika tuhuma za Mwembeyanga, CHADEMA walimtuhumu Kikwete, kwa wadhifa wake wakati huo, kusaini “mikataba mibovu” ya madini na makampuni ya kimataifa, iliyosababisha upotevu wa utajiri mkubwa na kuifanya serikali ishindwe kuhudumia vizuri wananchi wake.
Inadaiwa Kikwete alisaini mkataba na kampuni ya SAMAX Limited iliyopewa leseni ya kuchimba dhahabu katika eneo la Lusu, wilayani Nzega, Mkoa wa Tabora, mradi ulioleta mateso kwa maelfu ya wachimbaji wadogo baada ya kuondolewa kwenye makazi yao kwa nguvu.
SAMAX iliuza mradi wake kwa Ashanti Goldfields ya Ghana kwa kiasi cha dola za Marekani 253 milioni. Nao Ashanti waliuza mgodi huo kwa kampuni ya Resolute Limited ambao ndio wanamiliki mgodi wa Golden Pride ulioko Lusu, Nzega uliofunguliwa Novemba 1998.
Kikwete anadaiwa pia kusaini mkataba na kampuni ya Kahama Mining Corporation Ltd (KMCL) ambayo ni kampuni tanzu ya Sutton Resources ya Canada.
Mara zote wananchi waliswagwa nje ya makazi yao ya miaka mingi ili kupisha wawekezaji na hawakulipwa fidia kwa mali zao. Takriban wananchi 400,000 waliokuwa wakiishi na kuchimba dhahabu katika eneo la Bulyanhulu, Kahama waliachwa bila makazi.
Baadaye Sutton iliuza KMCL na Bulyanhulu kwa kampuni ya dhahabu ya Barrick Gold Corporation ya Toronto, Canada kwa dola 280 milioni. Leo hii Bulyanhulu ni moja ya migodi tajiri kwa dhahabu katika Bara la Afrika.
Benjamin Mkapa: Anatuhumiwa kushiriki au kubariki, au kunyamazia ukwapuaji wa fedha za EPA na kubariki uuzaji wa nyumba za serikali.
Kwa mujibu wa upinzani, ufisadi mkubwa ulitendeka chini ya utawala wa Mkapa.
Aidha, Mkapa anatuhumiwa kushiriki, moja kwa moja au kwa kutumia ndugu na/au washirika wa karibu wa familia yake, kumilikisha asilimia 85 ya hisa za kampuni ya Kiwira Coal Mines Ltd., inayochimba mkaa wa mawe huko Kiwira, Mkoani Mbeya kwa kampuni ya Tanpower Resources Limited inayomilikiwa na baadhi ya watu wa familia yake.
John Malecela: Ametuhumiwa kusaidia baadhi ya watuhumiwa waliokwapua mabilioni ya shilingi katika akaunti ya EPA. Upinzani ulionyesha hata baadhi ya vimemo vya Malecela vinavyodaiwa kutumika katika kufanikisha wizi.
Dk. Slaa amesema nyaraka ambazo Marando amemkabidhi zinaonyesha kuwa Malecela alisaidia wizi kufanyika.
Philiph Mangula: Ametuhumiwa kusaidia wizi wa EPA kwa maslahi ya chama chake na wao binafsi. Dk. Slaa alisema vimemo alivyoandika Mangula vilikuwa vya kumwelekeza gavana wa benki kuu wakati huo, Daudi Balali.
John Magufuli: Ametuhumiwa kutumia madaraka ya umma kwa maslahi binafsi. Magufuli ametajwa kuwa ndiye aliyepeleka katika baraza la mawaziri waraka uliotaka serikali iuze nyumba za umma na kutumia ruhusa hiyo kujimilikisha moja ya nyumba hizo.
Mbali na yeye kujiuzia nyumba hizo, Magufuli akagawa baadhi ya nyumba za serikali kwa ndugu na jamaa zake; hata mtu mmoja “chini ya mwaka miaka 18.”
Placidius Luoga: Anatajwa kwa kuingizia serikali hasara ya Sh. 800 bilioni kwa hatua yake ya kuzuia magari ya kampuni ya Tango Transport ya mjini Dar es Salaam, kwa miaka 10 kwa kisingizio cha kutolipa kodi.
Dk. Slaa amesema hatua hiyo ilisababisha mhusika kwenda mahakamani na sasa serikali imeamriwa kumlipa mlalamikaji kiasi hicho cha fedha. Dk. Slaa ameeleza kuwa serikali imeanza kulipa na tayari imetoa Sh. 500 milioni.
Pamoja na kuingiza hasara kiasi hicho kwa serikali, Luoga bado ni mwajiriwa TRA.
Katika orodha ya Mwembeyanga iliyotaja watuhumiwa 11, Edward Lowassa alituhumiwa kuhusika na kashfa ya kampuni ya City Water iliyopewa uendeshaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA) mwaka 2002.
Mwanasheria Tundu Lissu aliyefafanua dai hilo alisema, anajua kilichomo katika mkataba huo ndiyo maana anamtuhumu Lowassa kuwa mhusika katika kadhia hiyo.
Lissu ni mmoja wa mawakili wa serikali katika shauri la City Water kwenye Mahakama ya Kimataifa nchini Uholanzi ambayo inashughulikia usuluhishi wa mgogoro unaotokana na kukatishwa kwa mkataba wa City Water.
Kabla ya kukatishwa mkataba, Citywater walikwishasababisha hasara ya dola 12.5 milioni, hivyo kuthibitisha onyo lililotolewa na Benki ya Dunia mapema juu ya uwezo duni wa kampuni hizo.
Lowassa anatajwa pia kwa kuhusika kwake na kashfa ya kampuni ya Richmond Development Corporation (RDC) iliyopewa zabuni ya kuzalisha megawati 100 za umeme wa dharura mwaka 2006.
Miongoni mwa watuhumiwa ufisadi katika orodha ya mwaka 2007, ni pamoja na Nazir Karamagi, Daudi Balali, Nimrod Mkono, Rostam Aziz, Patrick Rutabanzibwa, Gray Mgonja, Basil Mramba na Andrew Chenge.
Karamagi anatuhumiwa kukaidi maoni ya Kamati ya Ushauri ya Madini ambayo ilimtaka asisaini mkataba wa Buzwagi hadi hapo serikali itakaporekebisha sheria na sera ili ipate mapato zaidi.
Gavana Balali alituhumiwa mambo mengi ikiwa ni pamoja na kufumbia macho ufujaji wa mali za umma unaofikia Sh. 522, 459,255,000 kupitia mradi wa ujenzi wa majengo pacha ya BoT jijini Dar es Salaam na Gulioni huko Zanzibar; na hongo ya dola 5 milioni kutoka kampuni ya Skanska Jensen ya Sweden ambayo ilipigwa marufuku kushiriki zabuni ya ujenzi wa majengo ya BoT.
Balali alituhumiwa pia kuidhinisha malipo ya dola za Marekani 118,396,460.36 kwa kampuni muflisi ya Meremeta Ltd., kupitia benki ya nchini Afrika Kusini. Meremeta ilikuwa ikichimba dhahabu Buhemba, wilayani Musoma.
Gavana alituhumiwa pia kudhinisha malipo ya dola za Marekani 13,736,628.73 kwa kampuni ya Tangold Ltd., kwa madai kuwa ni ugharimiaji wa “mali na madeni ya Meremeta Ltd yaliyohamishiwa kwenye kampuni mpya ya Tangold ambayo inamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100.”
Hata hivyo, iligundulika kuwa Tangold Limited ni kampuni ya kigeni iliyosajiliwa kwa mara ya kwanza nchini Jamhuri ya Mauritius na baadaye kuandikishwa nchini Tanzania kama tawi la kampuni ya kigeni.”
Wakurugenzi wa Tangold Limited, kwa mujibu wa taarifa zilizoko BRELA, ni pamoja na Daudi Balali. Gray S. Mgonja, Andrew J. Chenge, Patrick W.R. Rutabanzibwa na Vicent F. Mrisho.
Andrew Chenge alituhumiwa, miongoni mwa mengine mengi, kuishauri vibaya serikali na kuwa mkurugenzi katika kampuni ya kigeni ya Tangold Limited iliyoshiriki na/au kufaidika na malipo haramu ya dola 13,736,628.73.
Basil Mramba alituhumiwa, pamoja na mambo mengine, kushinikiza kampuni ya Alex Stewart (Assayers) Government Business Corporation ya Washington DC, Marekani, kupewa kazi ya kukagua hesabu za makampuni ya uchimbaji dhahabu nchini.
Rostam Aziz alituhumiwa kushiriki katika ukwapuzi wa mamilioni ya shilingi kutoka BoT uliofanywa na kampuni ya Kagoda Agriuculture Limited.
Nimrod Mkono alitajwa kutokana na barua ya CAG iliyobainisha kuwa Benki Kuu ilikuwa ikilipa kampuni yake ya Mkono & Co. Advocates, malipo makubwa zaidi, kuhusiana na kesi ya Valambhia, ambamo BoT inadaiwa jumla ya Sh. 60 bilioni
CHANZO: Mwanahalisi
0 comments:
Post a Comment