Natambua kuwa CCM ni chama chenye sheria,taratibu na kanuni zake.Nafahamu pia kuwa kama chama huru (hata kama kumekuwa kikiwakumbatia mafisadi kukiendesha) kina mamlaka na uhuru wa kufanya mambo kipendavyo alimradi hakifunji sheria za nchi.
Hata hivyo,mengi ya maamuzi ya CCM-kama si yote-yanamgusa kila Mtanzania kwa vile chama hicho ndio tawala kwa sasa.Na kwa vile mfumo wetu wa siasa umeendelea kuwa wa chama kushika hatamu,kwa maana ya matakwa ya chama ndiyo yanayoiongoza serikali iliyopo madarakani,kila mwananchi mwenye mapenzi mema kwa Tanzania yetu anawajibika kuishauri,kuipongeza na hata kuikosoa CCM pale inapofanya mambo “ndivyo sivyo”.
Majuzi,chama hicho kimetangaza “kujivua magamba”.Nimeshaliongelea hilo kwa mapana,na makala yangu ya Jumatano ijayo kwenye jarida la Raia Mwema inajadili suala hilo kwa undani zaidi.Kwahiyo hapa sintingia kwa undani kuhusu uamuzi huo wa chama tawala uliopelekea vigogo wake kadhaa kuvuliwa madaraka (japo kwa kuwaheshimu,kilichofanyika ni kuvunja kamati kuu na kuingiza sura mpya kwenye nafasi mbalimbali).
Wasiwasi wangu mkubwa ni tendencies za kidikteta zinazoelekea kushamiri ndani ya CCM.Sijawahi kuwa shabiki wa Edward Lowasa,Rostam Aziz au Andrew Chenge,sio kwa vile siwapendi bali naamini kuwa matendo yao yanaikwaza sana Tanzania kupiga hatua kimaendeleo huku mamilioni ya wananchi wakigubikwa na umasikini wa kutupa.Hata hivyo,kutokuwa shabiki wao hakumaanishi kutoangalia namna walivyotendwa na CCM.
Haihitaji kuwa na uelewa wa uchambuzi wa siasa kumaizi kuwa by kujivua magamba CCM imemaanisha kuondokana na baadhi ya viongozi wake ambao kwa namna moja au nyingine wamekuwa wakihusishwa na ufisadi.Kwa lugha nyingine,magamba ni ufisadi,na ilichofanya CCM ni kujivua joho la ufisadi.
Wengi wetu tunafahamu kuwa uhasama mkubwa kati ya CCM na Dokta Wilbroad Slaa na Chadema kwa ujumla ni suala la ufisadi.Na kwa upande mwingine,umaarufu wa Slaa na Chadema umetokana zaidi na harakati zao katika kupambana na ufisadi.
Ndio maana katika majadiliano yangu ya kistaarabu huko Twitter na msanii wa Bongofleva mwenye mwamko mkubwa wa kisiasa,Hamisi Mwinjuma a.k.a Mwanafalsafaau MwanaFA,nimekuwa nimkumbusha mara kwa mara kuwa mie si mwanachama wa chama chochote kile cha siasa,achilia mbali Chadema.Kinachonifanya niafkiane na Chadema ni mtizamo,misimamo na harakati zao katika kupinga na kupambana na ufisadi.Kadhalika,sina chuki binafsi na Rais Jakaya Kikwete,serikali yake au CCM kwa ujumla bali “ugomvi” wangu nao ni jinsi wanavyokumbatia ufisadi na kupuuza vilio vya wanyonge wa Kitanzania kuhusu suala hilo.
Tunalazimika kuamini kuwa magamba yaliyovuliwa na CCM ni Lowassa,Rostam na Chenge kwa sababu kuu mbili.Kwanza,ni kwa vile kutoswa kwao kama vigogo wenye nguvu ndani ya chama hicho kumeendana na CCM kutangaza kuwa imejivua magamba.Ni wazi kuwa kama umevuliwa madaraka kisha aliyekuvua madaraka akitangaza kuwa ameondokana na uozo basi lazima utatafsiri kuwa uozo huo ni wewe uliyevuliwa madaraka.Pili,hata kabla ya CCM kuchukua uamuzi huo,wanasiasa hao wamekuwa wakituhumiwa kuhusika na ufisadi,japo mara kwa mara CCM iliwatetea huku ikidai kuwa tuhuma dhidi yao zinaweza tu kuthibitishwa na mahakama na si vinginevyo.
Na hilo la pili ndilo lililonisukuma kuandika makala hii.Si Kikwete,CCM au Kamati/Halmashauri Kuu yake wenye mamlaka ya kumtia mtu hatiani,hususan hatia yenyewe inapokuwa kubwa kama tuhuma za ufisadi.Hivi kwa mfano,Lowassa,Rostam na Chenge wakiamua kwenda mahakamani wakiituhumu CCM kwa kuwachafua kwenye jamii chama hicho kitasemaje?
Unaweza kudhani kuwa itakuwa rahisi kwa CCM kuweka hadharani ushahidi wa kusapoti tuhuma zake dhidi ya wanasiasa hao.Lakini hilo sio rahisi kwa vile,kwanza,tangu mwaka 2005 CCM hiyohiyo imekuwa ikipita huku na kule kudai kuwa tuhuma za ufisadi dhidi ya wanasiasa mbalimbali wa chama hicho (including Lowassa,Rostam na Chenge) ni porojo tu zisizo na ukweli wowote.Actaully,Mwenyekiti wa chama hicho,Rais Kikwete,ameshanukuliwa mara kadhaa akidai kuwa “kelele za mlango hazimnyimi usingizi mwenye nyumba”,akimaanisha kuwa tuhuma za ufisadi dhidi ya chama hicho na baadhi ya viongozi wake ni kelele tu zisizopaswa kuendekezwa au kuamsha tafakuri ya Watanzania.
Kana kwamba hiyo haitoshi,miezi machache iliyopita,wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana,Rais Kikwete alisimama katika jukwaa jimboni Monduli kumpigia debe Lowassa,na akasimama kwenye jukwaa jimboni Igunga kumpigia debe Rostma,na akaenda jimboni kwa Cheyo kumpigia kampeni mwanasiasa huyo.Kadhalika,siku moja kabla ya Uchaguzi mkuu,Kikwete alizungumza na waandishi wa habari na kuwatetea tena watuhumiwa wa ufisadi na kudai kuwa ni watuhumiwa tu kwa vile hawajatiwa hatiani.
Sasa kama kilichofanyika Dodoma si udikteta ni kitu gani?Kwa sababu haiingia kabisa akilini kwamba viongozi waliosfifiwa na kutetewa mwezi Oktoba mwaka jana kuwa ni wasafi na wanaopaswa kuchaguliwa tena,waonekane hawafai miezi 6 baadaye.Of course,lolote linaweza kutokea katika kipindi cha miezi 6 lakini sote tunafahamu kuwa tuhuma za ufisadi wa Lowassa,Rostam na Change hazijatokea katika kipindi hiki cha miezi 6.
Kama maovu yao yalivumiliwa huko nyuma,na wakasafishwa hadharani na Rais Kikwete,iweje basi leo wanasiasa hao wabebeshwe tuhuma hizohizo ambazo walishasafishwa nazo?Ndio maana nimesema kuwa laiti wanasiasa hao wakiamua kufungua kesi ya kudhalilishwa mbele ya jamii,CCM itakuwa na kazi kubwa sana kujinasua.
Na sio hivyo tu bali wengi wetu tunafahamu kuwa ni vigumu mno kuwatuhumu watu kama Lowassa na Rostam kwa ufisadi pasipo kumhusisha Kikwete mwenyewe.Kama Lowassa ndiye aliyesababisha na kumwezesha utapeli wa Richmond,mwenye maamuzi ya mwisho kabisa alikuwa Kikwete mwenyewe ambaye aliidhinisha matakwa ya Lowassa kupitia vikao vya Baraza la Mawaziri ambavyo Kikwete ndio mwenyekiti wake.
Kama Rostam anahusishwa na suala la EPA,Kagoda na Dowans,again Kikwete alibariki yote hayo katika wadhifa wake kama Rais wa Tanzania.Anaweza kujiteteea kuwa hakufahamu ufisadi huo wakati unatokea.Hiyo inaweza kumfanya akaishi kwa muda wa kuazima lakini baadaye atalazimika kutueleza alichukua maamuzi gani baada ya kubaini kuwa ufisadi huo ulisababishwa na swahiba wake.
Lakini kuna suala jingine kubwa zaidi ambalo ni uhusika wa watu wasio na nyadhifa ndani ya CCM.Kwa mfano,ni watu gani ndani ya Idara ya Usalama wa Taifa waliwezesha kufanikiwa kwa wizi wa EPA na Kagoda,na ujambazi wa Richmond na Kagoda?Kwanini hawajachukuliwa hatua hadi leo?Je nao si magamba?Kam jibu ni ndiyo,je ni CCM au serikali yake itakayowapa siku 90 za kuwajibika?Na watawajibikaje?Wajipeleke wenyewe mahakamani?
Vipi kuhusu Mwanasheria Mkuu Mstaafu wa Serikali Johnston Mwanyika?Vipi kuhusuMkurugenzi Mkuu wa Takukuru Edward Hosea?Je hawa nao si magamba yanayopaswa kuvuliwa?Wangekuwa ndani ya CCM wangeweza kupewa notisi ya siku 90 lakini hawa sio wanasiasa,hivyo haitowezekana kuwawajibi9sha katika namna ya akina Lowassa na Rostam.
Vipi kuhusu Rais Mstaafu Benjamin Mkapa?Kwa wadhifa wake bado ni kiongozi wa CCM.Kwanini basi iwe Lowassa,Rostma na Chenge pekee na sio rais huyo Mstaafu,sambamba na akina Mangula,Sumaye,Malecela,Mwinyi au hata Zakia Meghji,Mkuchika na Chiligati?
Na kama kujivua magamba kuna maana yoyote,kwanini basi Waziri Membe aendelee kuwa Waziri ilhali kuondolewa kwake kwenye madaraka aliyokuwa nayo kunaweza kutafsiriwa kuwa ni hatua dhidi ya mafisadi?Vipi kuhusu akian Lawrence Marsha,Daniel Yona na Basil Mramba ambao kwa sasa hawapo madarakani?Na vipi kuhusu watu kama William Ngeleja na Naibu wake Malima ambao wizara yao,kwa namna moja au nyingine,imewezesha ujambazi wa Richmond na Dowans?Vipi kuhusu watendaji kama Dr Idris Rashid na Mgonja?
Narejea tena.Siwatetei Lowassa,Rostam au Chenge wala sipingani na hatua yoyote iliyo,inayo na itakayochukuliwa dhidi yao.Lakini kama lengo la Kikwete na CCM yake ni kupambana na ufisadi kwa vitendo basi ni lazima zoezi hilo litanuliwe kwa mapana zaidi.Lakini sote tunajua kuwa sio rahisi kwa Kikwete kwenda mbali zaidi kwa vile anatambua kuwa anakalia kuti kavu.Najua fika kuwa washirika wake wanaweza kabisa kumwaga uozo wote hadharani katika staili ya “bora tufe wote”.
Jingine,na hili lina umuhimu wa ikipekee,Kikwete anatambua kuwa vyovyote iwavyo,lazima mwakani apitishwe na kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM mpaka atakapomaliza muda wake.Na sio kupitishwa na kuchaguliwa tu,bali pia anapaswa kupata ushindi wa kishindo wa asilimia tisini na kitu.Sasa kwa vile anafahamu fika kuwa asipokuwa makini, “magamba” aliyoyavua yanaweza kabisa sio tu kumpunguzia kura hapo mwakani bali pia,in worst case scenario, kumuingiza kwenye vitabu vya historia kama mwenyekiti wa kwanza wa CCM kushindwa kurejea kwenye wadhifa wake huku akiwa bado madarakani,hawezi kwenda mbali zaidi ya alivyokwishafanya sasa.
Lililo wazi ni kwamba tutashuhudia mengi.Na tayari tumeshaanza kushuhudia baadhi ya vituko.Kwa mfano,mara baada ya “CCM kujivua magamba”,magazeti yanayomilikiwa na Rostam Aziz yameanza kuonekana yakiinanga CCM na serikali ya Kikwete.Tusisahau uwezo wa “magamba” hayo kifedha na influence kubwa waliyanayo ndani ya CCM na kwenye jamii.It is a bad influence lakini still ni influence.
All in all,matarajio ya Watanzania ni kuona nchi yao ikiondokana na nira ya ufisadi.Anayedhani “CCM kujivua magamba” ni sehemu ya process hiyo basi ni vema aamke kwenye lindi la usingizi aliomo.Kinachofanyika ndani ya chama hicho ni revelation ya msemo wa Kiswahili kuwa ushirika wa wachawi haudumu.Ni vita ya kimaslahi zaidi kuliko ya maslahi kwa jamii.Na ndio maana inasemekana hata maamuzi ya Kikwete kuvunja kamati kuu na kuwatosa maswahiba zake ni baada ya kutambua walikuwa wamedhamiria kwa dhati kumwondoa yeye mwenyewe kwa kuanzia na ajenda ya kutenganisha urais na uenyekiti wa CCM taifa.
Sihitaji kukwambia nani anayeweza kutuongoza kufikia ukombozi wa kweli wa Tanzania.Matendo hukidhi haja maridhwa kuliko maneno.Na kwa kila Mtanzania mwenye uzalendo na mapenzi ya kweli kwa nchi yetu anafahamu ni nani na chama kipi kinaweza kutufikisha tunakostahili kuwepo na kuwateketeza mafisadi wote.
0 comments:
Post a Comment