Monday, 4 April 2011


Magufuli atamba mbele ya Rais
• Atoa onyo la bomoabomoa kwa wakazi Dar

na Bakari Kimwanga

SIKU chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kumtaka Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, aache ubabe katika kutekeleza zoezi la bomoabomoa, jana waziri huyo alitoa onyo mbele yake akiwataka wakazi wa Tegeta jijini Dar es Salaam hasa waliokuwa katika hifadhi ya barabara ya Mwenge hadi Tegeta, wahame wenyewe kabla hajachukua hatua za kuwaondoa kwa nguvu.

Magufuli aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana huku Rais Kikwete mwenyewe akiwa pembeni yake, wakati wa sherehe za uzinduzi wa mradi wa upanuzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 12.9 inayojengwa kwa msaada wa serikali ya Japan kupitia shirika lake la maendeo (JICA).

Waziri huyo makeke alisema katu hataacha kusimamia sheria namba 18 ya mwaka 2007 ambayo ilisainiwa na Rais mwenyewe ambayo inakataza watu kuingilia eneo la hifadhi ya barabara kwa kujenga makazi au kufanya biashara.

“Mheshiwa Rais, hata wakileta malalamiko kwako usiwasikilize, kwani sheria namba 18 uliyoisaini inakataza….naahidi kuisimamia na kuwepo kwa Makatapila katika eneo la Tegeta sasa ni ishara tosha kwa wakazi waliovamia hifadhi ya barabara kuondoka wenyewe kabla sijaanza kuwaondoa kwa nguvu!”

“Mradi huu utachukua miezi 27 kuanzia mwezi Februari na unatarajiwa kukamilika Mei, 2013 na utagharimu shilingi bilioni 88 na fedha zote ni msaada toka serikali ya Japan,” alisema Magufuli.

Barabara hiyo inapanuliwa kwa kiwango cha lami na itakuwa na njia nne na vituo rasmi vya mabasi 22.

Aidha, alieleza kuwa hatua ya Rais Kikwete kumteua kushika wadhifa huo ni msukumo tosha kwa yeye na wasaidizi wake kuhakikisha wanasimamia sheria na ikiwa kutatokea utata Naibu Waziri wake, Harrison Mwakyembe, kwa kushirikiana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Hebert Mrango, wanaweza kuutatua kwani wao ni wanasheria kitaaluma.

Awali akizindua mradi huo, Rais Kikwete aliiagiza wizara hiyo kukishughulikia mara moja kile alichokiita “genge la watu waliojipanga kuidhulumu serikali na wananchi” kwa kuwalipa mabilioni ya fedha makandarasi ambao ujenzi wao wa barabara ni wa kiwango hafifu na cha chini.

Pia aliiagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuacha mara moja kugawa maeneo ya wazi na badala yake iyasimamie ipasavyo maeneo hayo yakiwamo yale ya watoto kuchezea kwa kuzuia kabisa ujenzi katika maeneo hayo.

Hata hivyo agizo hilo la Rais Kikwete linaonekana limechelewa sana kwani tayari kuna tuhuma na malalamiko mengi yanayoonyesha kuwa tayari maeneo mengi ya wazi yamekwishagawiwa kwa watu binafsi wenye uwezo kinyume cha taratibu, huku ikielezwa kuwa wahusika bado hawajachukuliwa hatua.

“Tumejitahidi kupandisha bajeti ya barabara mwaka 2006; ilikuwa bilioni 470 na hivi sasa tumepanda hadi trilioni 1.3 ili kuimarisha miundombinu ya barabara za ndani.”

“Wizara na Tanroads sasa msifanye malipo kwa watu ambao ujenzi wao ni wa kiwango cha chini na msipokee barabara ambayo iko chini ya kiwango ili kuongeza ufanisi wa barabara zetu jamani,” alisema Rais Kikwete.

Alisema kukamilika kwa upanuzi wa barabara ya Mwenge hadi Tegeta kutapunguza msongamano jiji la Dar es Salaam ambao kila mara umekuwa ukisumbua wakazi wa jiji.




0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget