Tuesday, 28 June 2011

Na Luqman Maloto
Kikombe cha Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Masapile ‘Babu Ambi’ ni janga la kitaifa, hali halisi ni mbaya na madaktari wametahadharisha.

Kitendo cha idadi kubwa ya wagonjwa wa kisukari na ukimwi kuacha kutumia dawa za kurefusha maisha na baadhi yao kuanza kufariki dunia mmoja baada ya mwingine, imeelezwa kuwa hali itakuwa mbaya baadaye.

Kwa mujibu wa madaktari waliozungumza na gazeti hili, watu wengi wanaokunywa kikombe cha Babu Ambi, wanadharau dozi za dawa za kisukari na ukimwi kwa imani kuwa tiba ya Loliondo inaponya.
Mbali na madaktari, ipo ripoti kuwa kila kukicha watu wanapoteza maisha pande mbalimbali za nchi, ikielezwa kwamba sababu ya vifo ni wagonjwa kuacha kutumia dozi za kurefusha maisha walizopewa hospitalini baada ya kunywa kikombe cha Babu Ambi wa Samunge, Loliondo.

“Wanakosea sana, hivi sasa watu wanakufa lakini mbele ya safari watapukutika zaidi. Tunapokea watu wakiwa mahututi, wapo ambao wanakufa lakini wengine tunafanikiwa kuokoa maisha yao na kuwaanzishia dozi,”  alisema daktari mmoja wa Hospitali ya Taifa, Muhimbili (jina tunalo) na kuongeza:

“Taifa litapata msiba mkubwa baadaye kwa sababu watu wengi watakufa. Mamilioni ya watu wameshatibiwa Loliondo. Hivi kati ya hao, watu milioni moja ikiwa wanaumwa kisukari na ukimwi, wakiacha tiba inakuaje?
“Ni ruhusa watu kwenda Loliondo kwa sababu ni ngumu kuingilia imani za watu, lakini ni vizuri watu wakapokea ushauri wa kitaalamu ambao tunawapa. Wasithubutu hata siku moja kupuuza wala kuacha tiba za hospitali.”

Daktari mwingine wa Muhimbili (jina linahifadhiwa) alionya kuwa taifa linakabiliwa na mtihani mkubwa kwa sababu hata baadhi ya viongozi hawataki kuamini wanapoambiwa ukweli kwamba kikombe cha Babu Ambi hakijathibitika kuwa kinaponya.

“Hapa tunamuomba Rais Jakaya Kikwete (pichani) aingilie kati. Tunatakiwa kujua ni watu wangapi wamekwenda Loliondo, waliopimwa baada ya kunywa kikombe tuambiwe hali zao. Hapo tutapata jawabu kama Babu anapaswa kuendelea kuruhusiwa kutoa tiba au afungiwe,” alisema daktari huyo.

Aliendelea kusema: “Leo nazungumza lakini inaweza kuonekana ni mzaha, ukweli ni kuwa tiba ya kikombe cha Babu ni janga zaidi ya ajali ya MV Bukoba. Vifo vingi vinatokea, watu wenye ukimwi watakufa zaidi kwa sababu wameacha dawa za kurefusha maisha.”
MV Bukoba ni meli iliyopata ajali Mei 21, 1996 karibu na Bandari ya Mwanza na kuua watu 900.

Kutokana na takwimu hiyo, daktari huyo alisema: “Mamilioni ya watu wamekwenda Loliondo, wengi wanaacha kutumia dawa, ni matokeo gani yanangojewa? Loliondo ni janga zaidi ya MV Bukoba, ukweli upo hivyo. Tusubiri matokeo, wagonjwa wengi wanakuja kupima, tunawabaini bado hawajapona lakini wanatuambia wametoka Loliondo.

“Mimi ni daktari, kuna kasoro Wizara ya Afya katika kulifanyia kazi suala la Loliondo. Wanalichukulia kawaida wakati linabeba watu wengi. Kuna watu wamejipa matumaini hewa, wanamwaga fedha kwenda kunywa kikombe lakini hakuna kupona. Rais Kikwete aingilie kati.”

Mbali na madaktari hao walioomba hifadhi ya majina yao gazetini, Daktari Leopold Mwinuka wa Munufu Clinic alishauri wagonjwa kutoacha dawa za hospitali, hasa wale wenye kisukari.

Saidi Mohamed ambaye ni daktari mstaafu aliliambia gazeti hili: “Kuna rafiki yangu alitaka kwenda Loliondo nikamshauri asifanye hivyo. Kwenda Loliondo ni kujitafutia matatizo zaidi, wengi wakitoka huko wanaacha kutumia dozi walizoelekezwa hospitali, hivyo wanazidiwa kabisa. Sijaona mtu aliyepona. Nina mifano ya watu watano waliopoteza maisha.”

Kwa upande wa Mchungaji wa Kanisa moja, Kibaha Pwani, Godfrey Mtani alisema kuwa suala la Loliondo wamelitazama kwa maono ya kiroho na kubaini kuwa wote waliokunywa kikombe inawezekana wakafariki dunia baada ya miaka miwili.
Wakati huo huo, Makongoro Oging’, aliyekuwa Kahama mkoani Shinyanga anaripoti kuwa watu tisa waliokunywa kikombe cha Babu Ambi wa Loliondo wameangua kilio baada ya kupima na kugundua kuwa bado wana virusi vya ukimwi.

Dk. Timoth Mhezzi wa Kituo cha Mhezzi kinachojihusisha na ushauri na kupima virusi vya ukimwi kwa hiari, Kijiji cha Kakola, Kahama alisema, wagonjwa hao tisa walifika kituoni hapo mwezi uliopita kupima afya zao lakini walimwaga machozi walipopewa majibu kuwa Loliondo haikuwasaidia kitu.

“Baadhi ya wagonjwa hao walianza kububujikwa machozi baada ya kugundua hawajapona, huku  wengine walidai kwamba walitumia fedha zao nyingi kwenda Loliondo bila mafanikio,” alisema Mhezzi.


CHANZO: Global Publishers

0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget