Wednesday, 1 June 2011


Karibu msomaji mpendwa usome MAKALA YANGU YANGU KATIKA TOLEO LA WIKI HII la gazeti linaloongoza nchini Tanzania la Raia Mwema.Makala nzima hii hapa chini

Wawekezaji wavumiliwe hadi lini kwa mauaji haya?

Evarist Chahali, Uskochi
Juni 1, 2011

JUMAPILI iliyopita ilikuwa ni siku ambayo mimi na familia nzima ya Chahali tuliadhimisha mwaka wa tatu tangu mama mpendwa, Adelina Mapango, aage dunia. Kwangu na kwa wanafamilia wengine, kifo cha mpendwa huyu ni kama kimetokea jana kwani bado tumegubikwa na majonzi makubwa.

Kifo hicho cha mama kimeathiri sana maisha yangu. Nilipofika huko nyumbani kwa ajili ya kumuuguza, tayari alikuwa ameshapoteza fahamu. Matumaini yangu kuwa labda angepata nafuu japo kidogo yalikuwa yakififia siku hadi siku kwa muda wote wa miezi mitatu aliyokuwa amelazwa.

Nilitamani angalau afungue mdomo kunipa japo wosia (japokuwa sikutaka kabisa kuamini kuwa ugonjwa wake ungeweza kusababisha mauti yake) lakini haikutokea hadi anafariki.

Kipindi tunamuuguza mama wakati na baada ya msiba kiliniwezesha pia kulielewa vyema jambo moja la msingi ambalo marehemu alikuwa akilisisitiza sana wakati wa uhai wake - upendo.

Nadhani hakuna mtu katika familia yetu ambaye hakuwahi kumlaumu marehemu mama kwa “kuendekeza sana upendo”. Kuna wakati tulikuwa tunashindwa kumuelewa pale alipowathamani watu waliomtendea mabaya. Siku zote alikuwa akisisitiza kuwa kazi ya kuhukumu sio yetu wanadamu; bali ni ya Mwenyezi Mungu.

Kadhalika, alikuwa muumini wa vitendo wa mafundisho ya kiroho kwamba “huwezi kudai unampenda Mungu ambaye hujamwona; ilhali unamchukia binadamu mwenzio unayemwona”.

Nakumbuka vizuri sana mahubiri yaliyotolewa na padre kabla ya mazishi ya marehemu mama. Alitufariji kwa kutuambia kuwa japo sie tulimpenda Adelina, lakini baba yake (yaani Mungu) alimpenda zaidi, na ndio maana aliamua kumchukua.Tangu siku hiyo nimekuwa nikiitumia kauli hiyo kuwafariji wafiwa.

Kadhalika, tulipewa wosia kwamba japo tuna kila sababu ya kumlilia marehemu, lakini njia mwafaka ya kumwenzi ni kudumisha mema yake na kuzingatia mazuri yake yote yaliyopelekea msiba wake kuvuta umati mkubwa.

Kabla ya kufikwa na msiba huo, nilikuwa nimeshahudhuria misiba mbalimbali, lakini katika misiba yote hiyo sikuweza kuelewa kwa undani uchungu waliokuwa nao wafiwa. Sio kwamba sikuguswa na misiba hiyo; bali ni ukweli kwamba ni vigumu kuzielewa hisia pindi tukio linalosababisha hisia hizo halitokei kwako.Wote tunalia misibani, lakini uchungu wanaosikia watu wa karibu zaidi na marehemu ni tofauti na watu wengine.

Baada ya msiba huo wa mama, imekuwa kana kwamba kifo kimechukua maana mpya kwangu. Kila ninaposikia taarifa za vifo ninarejea uzoefu niliopitia na kupata picha ya kinachowasibu wafiwa.

Ni katika mantiki hiyo, niliposoma, hivi karibuni, taarifa za kifo cha mkazi wa Kigamboni, marehemu Lila Hassan, aliyefariki kwa kinachodaiwa kuchomwa moto na mwekezaji mwenye asili ya Kiasia, nilipatwa na uchungu kana kwamba marehemu ni ndugu yangu.

Uchungu huo uliongezwa na ukweli kwamba, nikiwa mgeni hapa Uingereza, ninaelewa wazawa wanavyopewa kipaumbele kulinganisha na sie wageni.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka eneo la tukio, marehemu alikumbana na mkasa huo baada ya kuingia eneo la hoteli ya mwekezaji pasipo kulipa kiingilio. Hivi binadamu hao wenye roho ya kinyama walishindwa kuelewa kuwa laiti marehemu angekuwa na uwezo kama wao wawekezaji asingeweza japo kufikiria kuingia eneo hilo bila kiingilio?

Kwa vile wao walimudu kuja Tanzania kutoka huko walikotoka, wakanyenyekewa kwa ugeni wao na fedha zao na kupewa hadhi ya uwekezaji, basi, wanadhani kila binadamu ana “bahati” kama hiyo?

Ninasema “bahati” kwa vile ndivyo ilivyo kwa anayetokea kuwa ‘mwekezaji’ katika nchi yetu ambapo baadhi ya wawekezaji wamegeuka kama miungu-watu kwa jinsi watawala wetu wanavyowapapatikia.

Na usidhani upapatikiaji huo unatokana na “umuhimu wa wawekezaji”; bali sana sana ni katika kuhalalisha “teni pasenti” zao na ufisadi mwingineo.

Kabla hatujasahau yaliyomkumba marehemu Lila wala kufahamu hatma ya fedhuli hao waliomchoma moto, wakazi wa kijiji cha Nyamongo, mkoani Mara, nao wameletewa majonzi.

Tofauti na tukio la Kigamboni ambapo wahusika walikuwa mwekezaji na wapambe wake, katika tukio la hivi kartibuni la huko Nyamongo (Tarime), wahusika ni Watanzania wenzetu wanaolipwa mshahara kutokana na kodi za wananchi, na-kibaya zaidi-ni watu tuliowakabidhi dhamana ya usalama wa raia.

Katika kuendeleza utamaduni wao wa “chinja chinja” askari wa jeshi letu la polisi waliwapiga risasi na kuwauwa wakazi watano wa Nyamongo kwa tuhuma za kuvamia mgodi wa dhahabu. Waliua kinyama kulinda ‘mali ya mwekezaji’, na pengine kwa maelekezo ya mwekezaji.

Kama ambavyo tulishuhudia katika vurugu zilizosababisaha mauaji ya raia watatu wasio na hatia huko Arusha (wakati wa maandamano ya wafuasi wa CHADEMA), wafiwa wamejikuta wakiongezewa machungu kwa kauli zisizo za kibinadamu kwamba waliouawa walikuwa wahalifu.

Sasa kama kweli ni wahalifu, kwa nini, basi, serikali ilitaka kubeba gharama za mazishi ya “wahalifu” hao?

Tulimsikia Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Balozi Hamis Kagasheki alivyozungumzia tukio hilo, na hatukupata shida kugundua kuwa hajisikii uchungu wowote kutokana na vifo vya raia hao.

Katika maelezo yake, waliuoawa ni miongoni mwa wahalifu waliokwenda kwenye mgodi husika wa mwekezaji kwa minajili ya kupora dhahabu.

Hivi mwanadiplomasia huyu hatumii busara japo kidogo kutambua kuwa anachozungumza ni upande mmoja tu wa tukio? Hapo ninamaanisha kuwa maelezo aliyopewa Naibu Waziri huyo ni kutoka Jeshi la Polisi ambalo ndio watuhumiwa wa mauaji hayo.

Halafu, kama Kagasheki ameshahitimisha kuwa kilichowapa ruhusa polisi wake kuua ni uvamizi wa raia hao eneo la mgodi, sasa, hiyo timu ya wataalamu iliyoundwa na IGP Said Mwema kwenda Nyamongo ilikwenda kuchunguza nini; maana Kagasheki ameshatueleza chanzo cha tukio hilo?

Kwa bahati mbaya, matukio ya kusikitisha kama haya yataendelea kutokea kwa sababu baadhi ya viongozi na watendaji serikalini hawajali thamani ya uhai wa Watanzania wenzao. Kwa akina Kagasheki, kwa mfano, kabla hata uchunguzi haujakamilika jambo la muhimu kwake ni kutetea kwa nini polisi wameua raia hao pasipo kujali vifo vya marehemu hao na maumivu yanayowakabili wafiwa.

Tukiweka kando tukio la Kigamboni na hili la Nyamongo, kuna mauaji takriban kila mwaka yanayotokea katika migodi nchini; hususan kwenye machimbo ya Tanzanite kule Mererani.

Chanzo cha mauaji hayo yanayofanywa na walinzi wa migodi hiyo kwa maelekezo ya wawekezaji, ni mivutano ya muda mrefu ya kimaslahi kati ya wawekezaji hao na ama wachimbaji wadogo au wanavijiji wa vijiji vinavyopakana na migodi hiyo.

Jambo la kusikitisha ni kwamba kila mauaji hayo yanapotokea, Serikali; hususan Jeshi la Polisi, hutetea wawekezaji hao wa kigeni; hata pale inapoonekana dhahiri kwamba hawakuwa na sababu yoyote muhimu ya kuua. Inasikitisha kwamba linapokuja suala la wawekezaji wa kigeni, Serikali inasita kuwapenda na kuwatetea raia wake.

Kama nilivyoeleza mwanzoni, “huwezi kumpenda Mungu ilhali unamchukia jirani yako” ndivyo ambavyo haiwezekani kuipenda nchi kama hakuna mapendo kwa mwananchi mwenzako. Laiti askari wepesi wa kufyatua risasi wangekuwa na upendo kwa wananchi wenzao, matukio kama ya Arusha na huko Nyamongo yasingetokea.

Na kama mwekezaji wa Kigamboni aliyemchoma moto Lila angekuwa na upendo kwa sie wenyeji wake tuliomkaribisha kuwekeza nchini, tukio hilo la kinyama lisingetokea. Vivyo hivyo kwa wawekezaji wa Mererani na migodi mkingine nchini.

Tukiweza kutafsiri upendo wa ngazi ya familia na ukoo, kisha kuuhamishia kwa majirani zetu na hatimaye wananchi wenzetu, ni dhahiri kuwa ubinafsi, ulafi, ufisadi na uhalifu mwingine dhidi ya taifa na Watanzania wenzetu kwa ujumla, utapungua kwa kiasi kikubwa.
Pamoja na makala hii,usikose kusoma makala nyingine na habari motomoto katika jarida la RAIA MWEMA  kwa kubonyeza HAPA

0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget