Na Nova Kambota,Rais wa awamu ya tatu Mzee Benjamin Mkapa aliwahi kusema kuwa maisha bila vipaumbele ni ujinga mtupu, bilashaka hili halina ubishi kabisa taifa lolote linaloishi bila vipaumbele hugeuka taifa la wahuni, waporaji, mafisadi, wajinga,duni na zaidi huwa taifa legelege na dhaifu.Wageni mbalimbali kutoka Ulaya, Marekani ,Asia na sehemu nyingine za ulimwengu waliowahi kufika nchini huwa wanashangazwa sana na umasikini wa kutisha unaowaandama wananchi wa taifa hili. Wageni wanatushangaa sana na wataendelea kushangaa kuanzia Mlima Kilimanjaro,Mlima Meru, Udzungwa, Usambara, Ziwa Tanganyika, Victoria, Bahari ya Hindi mbuga nzuri za wanyama kama Mikumi na Ngorongoro lakini pia misitu ya kumwaga tu,mito mingi, mabonde ndiyo usiseme na ardhi yenye rutuba naya kutosha lakini bado miaka hamsini baada ya uhuru mamilioni ya watanzania bado ni masikini wa kutupwa.Kwa mtiririko huu wa mantiki hapa ndiyo inaibuka hoja kuwa watanzania hawafanani na nchi yao hata kidogo kwa maana ni watu mafukara waliozungukwa na utajiri wa kutisha , hakika kuna utofauti mkubwa kati ya watanzania na utajiri wa taifa lao, hata ukifika pale mbuga ya Ngorongoro wanyama wanacheza na kufurahi na ndege wanarukaruka kwa furaha kubwa, nenda kandokando ya bahari ya Hindi uone mawimbi yanavyopanda na kushuka kwa furaha kisha angalia samaki walivyo na furaha kisha sasa rudi katika maisha ya walalahoi wa nchi hii, kweli inahuzunisha kuona wanyama wana furaha kushinda watanzania, inauma sana!Kuna kisa kimoja cha kuhuzunisha sana ambacho nadhani watoto wetu wanapaswa kufundishwa madarasani. Inaelezwa kuwa mwaka jana 2010 wakati wa uchaguzi mkuu mwangalizi mmoja wa kimataifa kutoka nje alitembelea Tunduru akaona watu wanavyoogelea kwenye umasikini wa kutisha kisha akatupa macho kwa mbali akaona misitu mizuri na mto Ruvuma kisha akahoji kuwa inakuwaje watu hao ni masikini sana? Wananchi hawakuwa na la kujibu baadaye mzungu huyo akasema kuwa “siamini kabisa na hainiingii akilini kuwa CCM huwa inashinda kihalali kwa maana haiwezekani watu masikini kama hawa waichague CCM”Hivi nani atanishawishi kuwa CCM inashinda kihalali? Hapa uhalali unaozungumzwa sio wa kura tu bali hata wa kuwaacha watu huru, kwa maana haiwezekani watu wanakuwa masikini, wanafanywa wajinga na mifumo mibovu kiasi kwamba hawajui umuhimu wa kura halafu wanajiandikisha watu milioni 19 kupiga kura lakini siku ya kupiga kura wanajitokeza milioni 5 na CCM wanashinda! Kisha uniambie hapo kuna ushindi? Ushindi gani? wakati milioni 14 nzima hawajapiga kura? Idadi hii inaweza kubadili matokeo, kwa maana nyingine yule mwangalizi wa kimataifa yupo sahihi kabisa kuwa watanzania hawaichagui CCM badala yake inajichagua yenyewe na kujipa madaraka, ajabu sana!Watanzania wanalia kwa mengi, heri wote wangekuwa masikini lakini kuna wenzao “wajanja wachache” wanaishi kama wafalme kwa jasho la watanzania. Cha ajabu katika umasikini huu wa kutisha wa watanzania kuna baadhi ya watanzania wachache wamejigeuza “miungu watu” wamejimilikisha utajiri wote huu wakisaidiana na waporaji mabeberu kutoka Ulaya na Marekani, hawa hawajui njaa ni nini? hawafahamu masikini anafananaje? Wenyewe wanajua kuvaa suti na tai na mwisho wa mwaka wanaenda kwenye maduka makubwa ya nguo huko London na Dubai ili kuwafanyia “shopping” wake zao na watoto wao wapendwa.Nchi imekuwa ya matabaka kiasi kwamba mpaka taifa linayumba . Leo hii imefika mahali kuna watu wana nguvu za kutisha kwenye nchi mpaka mkurugenzi wa TAKUKURU anakiri kwenye mtandao wa Wikileaks kuwa Tanzania kuna “untouchables” hawagusiki hawa. Katika mazingira haya bado CCM inahubiri usawa, usawa gani? hata mtoto mdogo hawezi kushawishika kuwa kuna hata chembe ya huo usawa kwenye nchi hii, labda kidogo CCM waje na hoja ya kuwa na nchi mbili za kimatabaka kwenye taifa moja ndiyo! Kuna Tanzania ya tabaka la juu na Tanzania ya tabaka la chini.Huu ndiyo ukweli wa mambo , na matabaka haya mwanzo wake ni kuwa kuna wale walioshikilia utajiri wa taifa na wale waliotengwa na utajiri huo. Cha kusikitisha zaidi serikali inapigia chapuo mpasuko huu wa kitabaka kiasi kwamba imejenga shule za kata maalumu kwa masikini ili wakafeli na kuna mashule ya kimataifa yenye ubora haya ni maalumu kwa ajili ya watoto wao na maswahiba zao. Serikali haijaishia hapo tu sasa hivi Tanzania fedha iko juu ya sheria , nani asiyefahamu ukiwa na fedha nchi hii unaweza kupindisha sheria? Zaidi ya yote kuonyesha kuwa serikali yetu ni legelege ni jinsi inavyozitekeleza hospitali za serikali kiasi kwamba ni kama majengo tu bila dawa na ili kuonyesha kweli ubaguzi ni mfumo rasmi kwenye nchii hii hakuna “mkubwa” anaayekwenda kwenye hospitali za serikali huko ni kwa kapuku na walalahoi, ubaguzi wa kutisha!Viongozi hawaishii hapo tu kwenye juhudi zao za kuwafukarisha wananchi na kuwaibia mali zao, sasa wameanzisha soko huria la kura na wapiga kura na mnada kila baada ya miaka mitano. Hivi kwanini viongozi wasiwaache huru watanzania? Kwanini wasiwaache wakajichagulia watu wanaowaamini ni viongozi bora? Huu kama sio ujambazi wa haki za masikini ni nini? yaani hao walioko madarakani mwaka jana tu walipambana kununua kura kama sio kwenye ngazi ya chama basi kwenye uchaguzi kamili lakini ndiyo hivyo ukweli ni kuwa wamenunua kura kwa pesa nyingi na sasa wapo madarakani wanashindana kupora mali za wavuja jasho.Taifa limekosa vipaumbele , limehalalisha rushwa, uporaji na ufisadi, taifa linapepesuka kwa uhuni na tamaa za viongozi , dola imedhoofika sana hata kamanda mkuu Rais Jakaya Kikwete analifahamu hili lakini tatizo “kupe” wamejaa kuanzia huko CCM mpaka serikalini. Kile alichokitabiri Mwalimu Nyerere sasa kinatokea kweli, Mwalimu aliwahi kusema “serikali isiyojali wananchi wake haina uhalali hata kama imepigiwa kura” sitaki kuamini kuwa serikali ya CCM haina uhalali ila nashawishika kuwa haijali wala kuthamini wananchi wake hivyo kwa maana nyingine imeanza kupoteza uhalali wake.Imefika sehemu sasa watanzania wanapaswa kufanana na utajiri wa nchi yao, viongozi inabidi wafahamu kuwa watanzania hawana sababu ya kuwa masikini kama walivyo sasa. Watanzania lazima wafanywe kujivunia utanzania wao tofauti na hivi sasa ambapo kuna watanzania wanajilaani kwa kuwa watanzania yote kwasababu ya ubabaishaji wa viongozi wao ambao badala ya kuwatumikia wananchi wao wako “busy” kutumikia matumbo yao na familia zao.Lakini kama kawaida ya viongozi wetu wana tabia ya kuweka pamba masikioni hawataki kusikia bilashaka hata hili watapuuzia lakini nawapa angalizo kuwa watanzania wanafahamu kuwa hawakuumbwa walivyo bali umasikini wao umetengenezwa hivyo ni swala la muda tu lakini siku ikifika uvumilivu utakapowashinda basi watawang’oa wababaishaji wote wanaojineemesha na mali zao tena kwa njia yoyote ile, hizi ni zama za ukweli na uwazi ni wakati sahihi wa kuwa na mgawanyo sawa wa keki ya taifa…..Allutacontinua!Nova Kambota Mwanaharakati,+255717 709618Tanzania, East Africa07/07/2011, AlhamisiNaomba kura yako kwenye tuzo za blog Tanzania kwenye category ya best collaboration/group blog, best informative political blog na best political blog kunipigia kura nenda http://www.tanzanianblogawards.com/
Wednesday, 6 July 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment