DCI Manumba katika kashfa; Adaiwa kumkingia kifua mbunge asikamatweSunday, July 3, 2011, 12:03Habari, Mtanzania*Adaiwa kumkingia kifua mbunge asikamatweNa Kulwa KarediaMKURUGENZI wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Robert Manumba, amedaiwa kumkingia kifua Mbunge wa Busega, Dk. Titus Kamani (CCM) asikamatwe.Uamuzi wa kukamatwa umekuja baada ya mbunge huyo kuhusishwa na njama za kutaka kumuua aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Dk. Raphael Chegeni.Habari zinadai kuwa, DCI Manumba amekuwa akimkingia kifua mbunge huyo, licha ya Jeshi la Polisi kutangaza azma ya kumkamata kwa nguvu kutokana na ukaidi wa kutotii amri ya jeshi hilo.Kwa mujibu wa chanzo hicho cha habari, DCI Manumba amekuwa akimkingia kifua mbunge huyo kwa kuwa wanatoka wilaya moja ya Magu, mkoani Mwanza.Taarifa hizo ziliendelea kudai kuwa, tayari Dk. Kamani alikwisha jisalimisha polisi mkoani Mwanza mwishoni mwa wiki kwa mahojiano zaidi.Akizungumza na MTANZANIA Jumapili, Manumba alikanusha shutuma hizo na kueleza kuwa tangu mbunge huyo ahusishwe na sakata hilo, hajawahi kumkingia kifua kwa namna yoyote.“Kwanza nikwambie ukweli, suala hilo ndilo kwanza nalisikia kwako, sielewi kinachoendelea… kama kuna mambo Dk. Kamani amefanya taratibu zote za kisheria zitafuatwa.“Sijawahi hata siku moja kumkingia kifua, kesi yao naamini inashughulikiwa kwa mujibu wa sheria za nchi, sasa iweje mimi nijiingize kwenye kitu ambacho sihusiki?” alihoji DCI Manumba.DCI Manumba alisema yeye hapaswi kuzungumzia kwa undani suala hilo kwa kuwa si msemaji wa polisi na kwamba anayefaa kuhojiwa ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Saimon Sirro.“Sasa hayo mengine unayosema mimi si msemaji, nakuomba umtafute RPC Sirro yeye ndiye anayeweza kuzungumzia zaidi suala hilo kwa kuwa limetokea kwake,” alisema.DCI Manumba alikiri kutoka eneo moja na mbunge huyo, ingawa alisema hiyo si sababu ya kumkingia kifua. “Ni kweli huyu ni mbunge wangu na mimi ni mpiga kura wake, lakini hii si sababu ya kufanya nizuie polisi wasifanye kazi yao, hakuna mtu aliye juu ya sheria, hatutoki kijiji kimoja…narudia mimi ni mpiga kura wake, …nawashauri wale wote wanaohusishwa na tukio hili, waendelee na mambo yao, mimi sihusiki hata chembe katika hili,” alisema DCI Manumba.Alisema upelelezi ndiyo njia pekee itakayomkomboa mbunge huyo kama ana hatia au la.“Unajua hatufanyi kazi kwa kukurupuka, upelelezi unaoendelea ndiyo njia pekee itakayoamua kama nani ana kesi ya kujibu, tungoje tuone,” alisema.Mapema wiki hii, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Simon Sirro, aliwaambia waandishi wa habari kuwa mbunge huyo alijisalimisha na kutoa maelezo yake kuhusiana na tuhuma zinazomkabili.Alisema mbunge huyo alifika na kuhojiwa mwishoni mwa wiki na baada ya hapo aliachiwa, huku polisi wakiendelea na upepelezi zaidi kabla ya kumpandisha kizimbani.Habari zinasema mbunge huyo, alijisalimisha kituo cha polisi Juni 25, mwaka huu na kuhojiwa usiku kabla ya kuondoka kuelekea Dodoma kuendelea na vikao vya Bunge. Akiwa mkoani Shinyanga, gari lake liligonga mtu na kuua papo hapo.Mei 31, mwaka huu, inaelezwa kuwa Jeshi la Polisi mkoani Mwanza, liliandika barua Ofisi ya Bunge kutaka Dk. Kamani aende Mwanza kwa ajili ya mahojiano dhidi ya tuhuma zinazomkabili.Barua hiyo yenye namba MZR/CID/SCR/105/2011/4 ilitumwa kwa Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila ikimtaka Dk. Kamani kwenda kujibu kesi yenye namba ya usajili MW/IR/2607/2011-MR-CC.28/2011.Dk. Kamani atakuwa mshitakiwa wa tano iwapo atafikishwa mahakamani, baada ya watu wanne ambao ni Dismas Zacharia Ndaki, Erasto Kazimili Kombe, Queen Joseph Bogohe na Ellen Joseph Bogohe, ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Mwanza.
CHANZO: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment