Wednesday, 15 February 2012


Wafuateni kina Zitto, Januari Makamba

MAKALA katika toleo lililopita la jarida hili ilizua mjadala mrefu kwenye mtandao wa kijamii wa twitter kutokana na kunukuu matamshi ya Rais Jakaya Kikwete na utata kama wasifu uliopo kwenye mtandao huo ni wa Rais mwenyewe.
Katika makala hiyo niliandika kuwa “nilifanya mazungumzo yasiyo rasmi na Rais kuhusu mkanganyiko uliojitokeza kufuatia kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda juu ya nyongeza ya posho za wabunge.”
Baadhi ya wananchi hawakupendezwa na matumizi ya maneno ‘nilifanya maongezi na Rais...’ wakidai huko ni kupotosha ukweli. Pengine hali hiyo ilisababishwa na kasumba iliyozoeleka kuwa ni nadra mno kwa kiongozi (achilia mbali Rais) kufanya maongezi (hata yasiyo rasmi) na ‘mtu wa kawaida’ kama mimi.
Kwa upande mwingine, imezoeleka kuwa ‘maongezi’ ni pale tu mtu anapozungumza nawe uso kwa uso, kukuandikia barua, kukupigia simu au kukutumia SMS.
Maendeleo ya teknolojia yanayowezesha mazungumzo kufanyika kupitia mitandao ya kijamii kama twitter, facebook, google+, nk, bado ni kitu kigeni kwa wengi. Na si tu ni jambo geni kwa vile watumiaji ni wachache bali pia mazoea ya wengi wetu yanapeleka kuyaona mawasiliano ya aina hiyo kutostahili kuitwa maongezi.
Kimsingi, maendeleo katika teknolojia yamebadili kwa kiwango kikubwa jinsi habari zinavyokusanywa au/na kupatikana. Wakati kabla ya kuja kwa radio, runinga, simu, nk njia pekee ya kupata habari ilikuwa kwa kukutana uso kwa uso na chanzo cha habari, hali sasa ni tofauti kabisa.
Wakati kauli mbalimbali za viongozi wetu zinaendelea kupatikana kupitia mikutano yao na wanahabari au/na press releases, waandishi wengi wamekuwa wakifuatilia ‘kurasa’ za viongozi (na watu wengine maarufu) kwenye mitandao ya kijamii kwa minajili ya kupata habari.
Kadhalika, kuna nyakati viongozi hufanya maongezi na watumiaji wengine wa mitandao hiyo. Kwa mfano, huko twitter unaweza kumuuliza kiongozi swali (ili kufanya hivyo unapaswa kuandika jina analotumia kwenye wasifu wake likianza na tarakimu @) na yeye akakujibu.
Na hivyo ndivyo ilivyotokea kwangu. Nilimuuliza swali Rais Kikwete naye akanijibu. Sikuona ubaya wa kutumia ‘maongezi’ hayo (yasiyo rasmi) kwenye makala husika hususan kwa kuchelea kuonekana nimepandikiza maneno yangu binafsi kwenye habari hiyo.
Jambo la pili lililozua mjadala ni uhalali wa akaunti ya Rais Kikwete huko twitter. Kwa upande mmoja, baadhi ya watu walidai kuwa yote yanayoandikwa kwenye ‘ukurasa’ wa Rais hufanywa na timu yake ya mitandao ya kijamii (social media team).
Hoja hiyo inaingia akilini kwa sababu sote tunafahamu jinsi Mkuu wa Nchi anavyokuwa na majukumu mengi yanayoweza kumkwaza kufuatilia kila kinachoendelea kwenye mitandao ya kijamii, magazetini, nk. Hata hivyo, yayumkinika kuamini kuwa wasaidizi wa Rais waliokabidhiwa jukumu hilo (kama wapo) wanafanya hivyo kwa ridhaa ya Rais mwenyewe.
Hiyo ni kama jinsi taarifa mbalimbali zinapotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu au Mwandishi wa Habari wa Rais. Japo anayeandika na/au kusambaza taarifa hizo si Rais mwenyewe, ridhaa yake na ukweli kwamba kinachoongelewa kinamhusu yeye kunapelekea taarifa za aina hiyo kupokewa na umma kama kauli (au msimamo) ya Rais.
Mkanganyiko kuhusu akaunti ya Rais huko twitter unachangiwa pia na kukosekana na alama inayoashiria kuwa akaunti husika imehakikiwa na wamiliki wa mtandao huo wa kijamii (yaani kuwa verified).
Wakati Rais Kikwete anatajwa kuwa miongoni mwa viongozi wachache barani Afrika wanaoitumia mitandao ya jamii mara kwa mara, si yeye pekee ambaye akaunti yake ya twitter haijahakikiwa (kwa mfano, ya Rais Jacob Zuma na Yoweri Museveni pia zipo katika hali hiyo).
Lakini japo pengine ingependeza akaunti rasmi ya Rais inaonyesha alama ya verified na hivyo kuondoa ‘sintofahamu’ kuhusu mmiliki wake, ukweli kwamba licha ya Ikulu kutoikana, na miongoni mwa followers wake ni watu na taasisi zenye hadhi kwenye jamii (kwa mfano CCM, CHADEMA, na familia ya Kikwete mwenyewe) basi kwa sasa tunaweza kuamini kuwa akaunti hiyo ni yake.
Lengo la makala hii si kuendeleza mjadala huo ambao kwa hakika si wa muhimu kulinganisha na masuala mbalimbali muhimu kwa Taifa. Hata hivyo, unaweza kutupa fursa nzuri kutathmini nafasi ya teknolojia ya mawasiliano katika mwingiliano (interactions) kati ya watawala na watawaliwa au viongozi na wananchi.
Kuna ugumu mkubwa katika kupata taarifa rasmi kutoka taasisi za umma. Wahanga wakubwa wa tatizo hilo si waandishi wa habari tu bali pia watafiti wanaosaka takwimu kwa ajili ya tafiti zao na wananchi kwa ujumla.
Uzuri wa namna ya kutumia teknolojia kama ya mitandao ya jamii upo kwenye urahisi wa namna ya kuitumia. Mitandao kama twitter na facebook inafikika kirahisi kwa kutumia hata simu (ili mradi iwe na huduma ya intaneti).
Pasipo kujali ni kiongozi mwenyewe au wasaidizi wake wanaosimamia ukurasa husika mtandaoni, uwepo wa ukurasa huo unaweza kutoa nafasi nzuri kwa wananchi kuwasiliana na kiongozi husika, sambamba na kuepusha mkanganyiko unaoweza kujitokeza pindi kauli ya kiongozi inapowasilishwa na mtu mwingine.
Mfano hai katika hilo ni mkanganyiko uliojitokeza siku chache kuhusiana taarifa zilizohusu ongezeko la posho za wabunge.
Ninatambua kuwa kwa mwananchi wa kawaida kule kijijini (ambako uhaba wa huduma muhimu za jamii unaumiza kichwa zaidi ya suala kama intaneti) anaweza asione umuhimu wa kuhamasisha viongozi wetu kuitumia mitandao ya kijamii, ukweli ni kwamba njia yoyote itakayowezesha kuwaweka viongozi hao karibu na wananchi inapaswa kutiliwa mkazo.
Wenzetu katika nchi zilizoendelea wana sheria zinazolazimisha upatikanaji wa habari zenye maslahi kwa umma, kwa mfano, sheria ya uhuru wa kupata habari (Freedom of Information Act).
Kwa huko nyumbani, tatizo si kuwapo (au kutokuwapo) kwa sheria ya aina hiyo, bali utashi kwa upande wa watawala kuona habari zenye maslahi ya umma zinapatikana kwa wananchi pasipo vikwazo.
Sasa katika mazingira ambapo habari kutoka taasisi za umma au viongozi zinapatikana kama fadhila (badala ya kuwa haki ya msingi), kuwa na viongozi kwenye mitandao ya kijamii kunaweza kusaidia sana kupunguza ombwe hilo.
Kwa kuwa Rais Kikwete (bila kujali ni yeye mwenyewe au wasaidizi wake) anaonekana kuwa ‘muumini mzuri’ wa matumizi ya mitandao ya kijamii, anaweza kuhamasisha watendaji wake na taasisi kuiga mfano wake.
Lakini kwa vile ‘mtoto hazaliwi akatambaa’ (kwa maana itachukua muda kabla mwingiliano wa viongozi wa/taasisi za umma na wananchi kwa kutumia mitandao ya kijamii haujaenea kwa kiwango kikubwa) bado kuna nafasi ya kutumia vyombo kama blogu za Kitanzania (ambazo idadi yake inaongezeka kwa kasi) kutimiza jukumu hilo.
Kwa sasa, njia pekee ya blogu kuwasilisha habari kutoka kwa viongozi au taasisi mbalimbali ni kwa kunukuu habari kutoka vyombo ‘vya asili’ vya habari (yaani magazeti, radio na runinga).
Kibaya zaidi ni ukweli kuwa tovuti za taasisi chache za umma (zilizoona umuhimu wa kuwa na tovuti) aidha haziwekwi habari mpya mara kwa mara au zimebaki kuwa anwani tu (kwa maana hazipatikani mtandaoni).
Ukienda kwenye blogu ya Ikulu (inayoendeshwa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu) utaona habari ‘mpya’ ni mwanzoni mwa mwezi uliopita. Wakati viungo (links) ni kwa Wizara pekee, kuna video moja tu kwenye ukurasa wa video. Blogu hii ingeweza kabisa kuwa na kipengele cha maandiko ya Rais na/au Ikulu kwenye mitandao mingine ya kijamii (kama twitter na facebook), hiyo ingesaidia kuondoa mkanganyiko kama nilioubainisha awali.
Nimalizie makala hii kwa kuwapa changamoto viongozi wetu kuiga mfano wa baadhi ya wanasiasa kama Zitto Kabwe, Januari Makamba, Dk. Faustine Ndugulile, Dk. Hamisi Kigwangalla, Mo Dewji na John Mnyika (na wengineo wachache) ambao kama Rais Kikwete mwenyewe, wamekuwa mahiri katika matumizi ya teknolojia ya mawasiliano kwa kutumia mitandao ya jamii.
Licha ya kuwa nyenzo muhimu katika shughuli zao za kisiasa, mitandao hiyo inawaweka karibu zaidi na wananchi na kurahisisha upatikanaji wa habari zinazowahusu au zenye maslahi kwa umma.


0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget