Tumeuona wa madaktari, lakini mingi yaja
NI sababu zipi zinazomsukuma mwanafunzi kuchagua mchepuo fulani wa masomo anapopewa nafasi ya kufanya hivyo?
Pengine kwa wanafunzi wengi sababu ya msingi ni jinsi mchepuo huo unavyoweza kupelekea kufikia malengo ya taaluma au ajira tarajiwa.
Lakini kwa wengine, sababu inaweza kuwa uwezo wao kimasomo, yaani kama wanaweza kumudu mchepuo husika au la. Binafsi, nilikuwa na ndoto za kuwa tabibu (daktari). Nilipokuwa kidato cha kwanza hadi cha nne niliwekeza nguvu kubwa kwenye masomo ya elimu ya viumbe na kemia. Na niliyamudu vema masomo hayo ambayo niliamini yangeweza kufanikisha dhamira yangu ya kuwa tabibu.
Hata hivyo, ndoto yangu ilipata pigo kubwa baada ya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne, ambapo japo nilipata alama A katika kemia na C katika baiolojia, nilifeli katika fizikia kwa kupata alama F, huku nikaambulia D kwenye hisabati.
Kwa maana hiyo, japo nilipata daraja la kwanza na kuchaguliwa kuingia kidato cha tano, uwezekano wa kusoma mchepuo “wa udaktari” wa PCB (Fizikia, Kemia na Baiolojia) ulikuwa hafifu.
Kabla ya kuanza masomo ya kidato cha tano nilipewa ushauri kuwa licha ya kushindikana kuchukua mchepuo wa PCB kuna uwezekano wa kuchukua mchepuo mwingine (unaoikwepa fizikia) wa CBG unaojumuisha Kemia, Baiolojia na Jiografia.
Lakini katika kile nilichokitafsiri kama haikuwa majaliwa yangu kuwa tabibu, licha ya shule kuwa na uhaba wa mwalimu wa jiografia nilipoangalia mtaala wa kemia niligundua ina mada kadhaa zilizojumuisha hisabati na maeneo mengine yenye ugumu kama wa fizikia, hususan katika physical chemistry.
Kufupisha maelezo, nilifikia uamuzi wa kuchukua mchepuo wa HGL (Historia, Jiografia na Lugha ya Kiingereza), ambao niliumudu na miaka kadhaa baadaye ulinisaidia kuchukua michepuo ya Elimu ya Jamii (Sosholojia) na Stadi za Siasa katika ngazi ya chuo kikuu.
Miongoni mwa mada za mwanzo kabisa za Elimu ya Jamii kuna mada ya kanuni za sosholojia (sociological theories).Na moja ya kanuni hizo ni ile inayoiangalia jamii kama mfumo kulingana na kazi za kanuni, desturi, mila na vikundi katika jamii. Kanuni hiyo ijulikanayo kama functionalism inaviangalia vipengele hivyo kama namna mwili unavyofanya kazi kwa ushirikiano wa viungo mbalimbali. Katika miili yetu, moyo unaletewa damu na mapafu na mapafu yanategemea damu inayosukumwa kwake na moyo.
Kadhalika, mfumo wa fahamu unaletewa ujumbe na viungo kama macho, ngozi, pua, nk lakini ili viungo hivyo viweze kupelekea ujumbe husika vinategemea ufanisi wa ubongo.
Kwa kifupi, ni vigumu-na pengine haiwezekani kabisa-kudai kiungo fulani katika mwili ni muhimu zaidi ya kingine. Vyote ni muhimu na kila kimoja kinakitegemea kingine katika utendaji kazi wake. Ni ushirikiano wa viungo mbalimbali ulikuwezesha wewe msomaji kuwa unasoma makala hii muda huu. Macho yaliona gazeti kwa muuzaji na kupelekea ujumbe kwenye ubongo ambako maamuzi yalifanyika ulinunue. Ubongo pia ulitumia maelekezo kwa mkono kutoa fedha mahali ilipowekwa (baada ya kukumbuka mahali husika), sambamba na kutofautisha kati ya fedha (ya kunulia gazeti) na funguo za ofisini au nyumbani.
Na pengine muda huu unatabasamu kwa ‘kukumbushwa jinsi mwili unavyofanya kazi na ufanisi wa ushirikiano wa viungo mbalimbali’, tabasamu hilo ni ushirikiano wa viungo mbalimbali mwilini.
Pengine hadi kufikia hapa nimekuchanganya na huelewi makala hii inaelekea wapi. Lengo la makala hii ni kuzungumzia mgogoro unaoendelea kati ya madaktari na serikali huko nyumbani.
Hadi wakati ninaandika makala hii, kulikuwa na taarifa kwamba mgomo huo unaelekea kusambaa katika hospitali mbalimbali. Kadhalika, kuna taarifa kwamba manesi nao wametoa tishio la kugoma iwapo serikali haitayapatia ufumbuzi matatizo ya madaktari yaliyosababisha mgomo huo.
Inawezekana wakati unasoma makala hii mgomo huo utakuwa umeshamalizika lakini kuna kila dalili kuwa hata kama madaktari watamaliza mgomo wao au/na manesi hawatogoma, kitakachokuwa kimemalizwa ni dalili tu za tatizo na wala si kupatikana kwa tiba yake.
Nilipotoa maelezo ya kanuni ya functionalism kwenye Sosholojia nililenga kuonyesha jinsi taaluma/ajira mbalimbali katika jamii zilivyo na umuhimu sawa na jinsi ushirikiano kati ya fani ya taaluma/ajira hizo unavyoleta ufanisi kwa manufaa ya jamii husika.
Je, wabunge ambao taarifa zinaeleza kuwa wameongezewa posho kutoka shilingi 75,000 kwa siku ni muhimu zaidi kuliko madaktari? Jibu la wazi ni hapana, kama ambavyo madaktari si muhimu zaidi ya walimu au viongozi wa dini si muhimu zaidi ya wanausalama.
Wote hawa ni muhimu kwa jamii na kwa namna moja au nyingine, ushirikiano wao (wa moja kwa moja au vinginevyo) ndio unaotuwezesha Watanzania kuwa hai.
Labda nifafanue. Ili tuwe salama, tunawategemea wanausalama. Lakini ili wanausalama waweze kutimiza majukumu yao ipasavyo wanapaswa kuwa na afya salama pia, na hapo unaona umuhimu wa watumishi wa afya (madaktari, manesi, nk).
Lakini ili mtu awe daktari au nesi ni lazima afundishwe, na hapo tunaona umuhimu wa walimu. Lakini mwalimu nae akiugua ni lazima aende kwa daktari. Hata hivyo, ili daktari aweze kufanya kazi zake ipasavyo ni lazima mazingira ya hospitali (na nchi kwa ujumla) yawe salama, na hapo tunarejea kwenye umuhimu wa wanausalama wetu.
Kadhalika, ingekuwa vurugu isiyoelezeka kama kila daktari, mwalimu, mwanausalama, nk angeenda bungeni kuwakilisha maslahi ya jamii yake au kuwa waziri au kiongozi serikalini. Na ndiyo maana licha ya kuepusha vurugu ya aina hiyo na pengine kuepusha uhaba wa wanataaluma kwenye fani husika, unakuwa na mtu mmoja kama waziri au mbunge mwenye jukumu la kuongoza na kuwakilisha makundi mbalimbali katika jamii.
Lakini viongozi au wawakilishi hao si muhimu zaidi ya wanaowaongoza au kuwawakilisha. Waziri hawezi kabisa kutimiza wajibu wake iwapo yeye mwenyewe ni mgonjwa na hakuna daktari wa kumtibu, au kuwa na wasaidizi ambao hawajatia mguu shuleni kwa vile hakuna walimu. Kadhalika, ili waziri atie mguu ofisini sharti nchi iwe salama, na hapo anatambua umuhimu wa wanausalama.
Kwa wabunge wetu pia, kuwa kwao bungeni kunategemea sana taaluma na nyanja nyingine katika jamii, achilia mbali nani waliowapigia kura kuingia bungeni. Japo picha inayojengeka baada ya ongezeko la posho za wabunge ni kama wapo kwa maslahi yao binafsi, ukweli unabaki kuwa hawawezi kuwa wawakilishi wa hewa. Wanawakilisha wananchi ambao wanaojumuisha watu wenye taaluma na majukumu mbalimbali katika jamii.
Kama daktari ni muhimu kama mbunge, kwanini basi kundi hili dogo (lakini linalosaka kila aina ya nguvu katika jamii ikiwa ni pamoja na kuitwa ‘waheshimiwa’) lipendelewe kwa marupurupu yasiyoendana kabisa na hali ngumu ya uchumi wetu? Kama waheshimiwa wabunge ni muhimu kama madaktari, manesi, walimu na watumishi wengine, kwanini basi wapewe shilingi 200,000 kwa siku huku watumishi wengine wakiwa na mahitaji lukuki ambayo yamekuwa yakipuuzwa na serikali?
Hivi kuwaongezea posho wabunge kutasaidiaje afya za Watanzania? Je, ongezeko hilo la posho litasaidiaje kuinusuru sekta ya elimu inayokwazwa na mishahara kiduchu ya walimu, uhaba wa nyumba na vitendea kazi huku wanafunzi wakisoma katika mazingira magumu?
Je, ni vipi ongezeko hilo la posho za wabunge litawasaidia askari polisi kuepuka vishawishi vya rushwa ambavyo kwa kiasi kikubwa vinachangiwa na maslahi duni?
Lakini tatizo kubwa zaidi linalosababishwa na ongezeko la posho za wabunge ni hili: kama serikali ina uwezo wa kutoa nyongeza ya posho kwa wabunge inamaanisha kuwa fedha si tatizo kwake.
Ninaandika hivi kwa sababu sidhani kama kuna mtu yeyote (ukiondoa wabunge wetu) anaamini kuwa maslahi ya wabunge wetu ni duni. Hatujawahi kusikia kuna mbunge ametishia kujiuzulu au kugoma kwa vile kipato chake cha mamilioni hakitoshelezi mahitaji yake, na wala hakuna mbunge aliyekonda kwa vile mshahara wake haumwezeshi kumudu gharama za chakula. Sana sana tunashuhudia vitambi vya baadhi ya waheshimiwa wetu vikizidi kuongezeka sambamba na kasi ileile ya malalamiko kuwa “maslahi ya wabunge ni duni.”
Hakuna anayependa kuona madaktari wakigoma hasa kwa vile wahanga wakubwa wa migomo ya aina hiyo ni walalahoi wasioweza kwenda India (au kwingineko) kupata matibabu. Na tungependa sana kuiunga mkono serikali katika maelezo yake ya kila siku kuwa haina fedha za kuboresha maslahi ya watumishi wake lakini tutaonekana wendawazimu tukifanya hivyo wakati serikali hiyohiyo inayodai iko hoi kifedha inamudu matumizi makubwa yasiyo ya lazima kwa kuwaongezea posho wabunge.
Sipendi kubashiri hili lakini kuna uwezekano mgomo wa madaktari ni mwanzo tu wa mlolongo wa migomo mingine ya watumishi katika sekta mbalimbali za umma huko mbele. Japo sina hakika serikali itamudu vipi mzigo wa posho za wabunge, kilicho wazi ni kwamba kelele za makundi mbalimbali ya jamii pamoja na wananchi kwa ujumla kupinga ongezeko hilo la posho kimepuuzwa na serikali, na kwa kuzingatia uzoefu itakuwa miujiza kama serikali itabadilisha uamuzi huo usiozingatia hali halisi ya nchi yetu (hasa kwa vile ilikuwa na fursa ya kukataa maombi ya wabunge lakini ikaamua kuyaendekeza).
Nihitimishe makala hii kwa kuitahadharisha serikali kuwa ‘imefungua kopo la minyoo’ kwa kutoa nyongeza ya posho kwa wabunge katika kipindi ambacho watumishi wa sekta mbalimbali za umma wanaelekea kuishiwa na uvumilivu wa kusubiri ahadi hewa za kuboreshewa maslahi yao.
Wakati nyongeza hiyo ya posho kwa wabunge inaweza kuwaongezea nguvu ya kuiunga mkono serikali (hata pale maslahi ya wanaowakilishwa na wabunge hao yanapowekwa shakani) hali itakuwa mbaya pindi harakati za watumishi wa umma kudai maslahi bora zinatakapomaanisha migomo zaidi.
0 comments:
Post a Comment