Mpendwa Chama Cha Mapinduzi (CCM),
Heri kwa siku yako ya kuzaliwa.Nakupongeza sana kwa kutimiza miaka 35.Laiti ungekuwa mwanadamu basi kwa umri huo huenda ungekuwa na mke na mtoto/watoto.Anyway,familia yako ni sie Watanzania ambao wakati unazaliwa (1977) hatukuwa na hiari zaidi ya kukuunga mkono na kukuabudu.
Mpendwa CCM,kinachofanya ionekane unachukiwa na wengi si wewe kama chama bali wengi wa viongozi wako.Kama ilivyokuwa kwa watangulizi wako TANU na ASP,ulipozaliwa ulidhamiria kupigania haki za wanyonge,kupambana na ukandamizaji na kujenga jamii iliyo sawa.Ulifanikiwa sana katika kipindi cha utawala wa Marehemu Baba wa Taifa Julius Nyerere.Lakini pindi alipotoka madarakani zikaanza jitihada za makusudi za kukugeuza kimbilio la maharamia wa kisiasa.
Alipofariki Mwalimu,maharamia hao wakakubadilisha kabisa na sasa unaonekana kama kichaka cha mafisadi.Zama za Mwalimu,ulikuwa mfano wa kuigwa si kwenye siasa tu bali hata katika ngazi ya familia.Uliwajali Watanzania japo baadhi ya sera zako hazikuweza kufanikiwa kwa utimilifu (hususan Ujamaa na Kujitegemea).Kilichokukwamisha zaidi ni maharamia waliojivika ngozi ya kondoo ilhali wao ni mbwa mwitu.Watu walewale waliokuwa wakihubiri usawa na kuwatetea wanyonge leo hii wamegeuka watetezi wakubwa wa mabwanyeye,makabaila na wanyonyaji wengine ambao siku hizi tunawaita mafisadi.
CCM umeporwa na walafi wasio na uchungu na nchi yetu.Wafanyabiashara wa kila aina (pamoja na wenye biashara haramu) wamekimbilia kwako si kwa vile wanakupenda bali wanasaka hifadhi ya kuendeleza uharamia wao.
Kabla ya mwasisi wako kufariki alitabiri uwezekano wa kupata mrithi wako kutokana nawe.Kwa mazingira tuliyonayo hilo ni vigumu kutokea kwani kwa kiasi kikubwa hakuna wa nafuu miongoni mwa vionhozi wako.Na siku yako ya kuzaliwa imeadhimishwa kwa kituko cha wabunge waliopatikana kwa kutumia tiketi yako kugoma kukutana na Mwenyekiti wao.Sijui kama ni hasira za sakata la posho wanazotaka waongezewe au wanachochewa na 'nguvu za giza' zinazotaka Mwenyekiti Kikwete asimalize muhula wake wa pili,au amalize kwa fedheha.
Anyway,natamani ningekuwa na muda wa kutosha kuwasilisha salamu hizi lakini naomba niishie hapa.Afterall,today's your big day na pengine sikutendei haki kwa kujumuisha masimango.
Enjoy your big day dude!
Truly yours,
Evarist Chahali
0 comments:
Post a Comment