DCI Manumba amewasiliana na Wizara ya Afya ya nchi gani?
Sumu ya Dk. Mwakyembe
Mwakyembe, Sitta wajiuzulu kutumikia Serikali wanayoituhumu
MIONGONI mwa matukio ya kukumbukwa ya Bunge lililokuwa chini ya Spika wa zamani, Samuel Sitta ni tuhuma kwamba mmoja wa wabunge alifanya vitendo vya ushirikina.
Japo suala hilo lilimalizwa kimya kimya, ukweli unabaki kuwa lilikuwa ni la kuaibisha na pengine kudhihirisha upungufu mkubwa kwa baadhi ya watu tuliowakabidhi jukumu la kutuongoza.
Na kama ilivyozoeleka kwenye masuala mengi yenye utata, Watanzania hawakuwa na jinsi ya kudai ukweli kuhusu suala hilo. Kwa upande mmoja huwezi kuwalaumu hasa ikizingatiwa kuwa, wengi wao wanahangaika tangu mawio hadi machweo kuhakikisha ‘mkono unakwenda kinywani.’ Kwa upande mwingine, watawala wetu wamejitengenezea mazingira ambayo mwananchi wa kawaida hawawezi kudadisi ‘upuuzi’ wao (kama huo wa madai ya ushirikina bungeni).
Lakini pengine kikubwa zaidi ni ukweli kwamba kama hadi leo hii watawala wetu wamegoma kabisa kutuambia kuhusu wahusika wakuu wa ujambazi wa mchana kweupe (daylight robbery) katika skandali za EPA (hasa nani anayemiliki kampuni iliyoiba fedha nyingi ya Kagoda), Richmond, Meremeta, Tangold na nyinginezo, basi ni dhahiri hawakuona haja ya kujihangaisha na ‘jambo dogo’ kama hilo la tuhuma za ushirikina bungeni .
Busara zinatukumbusha kuwa ‘usipoziba ufa utajenga ukuta.’ Tabia ya kuyapuuza masuala yanayopaswa kushughulikiwa ipasavyo sasa imeanza kuzua sokomoko mpya ambayo imeendelea kutawala vichwa vya habari kwa siku kadhaa sasa. Ninazungumzia sakata linalowahusu Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, kwa upande mmoja, na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Robert Manumba, kwa upande mwingine.
Unaweza kulipanua sakata hilo na kumjumuisha Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta (ambaye amejitokeza kuwa mtetezi mkuu wa Mwakyembe) na Jeshi zima la Polisi chini ya uongozi wa IGP, Said Mwema.
Tuhuma kwamba Mwakyembe amenyweshwa sumu zilianza kama mzaha. Kadri siku zilivyozidi kwenda, suala hilo lilianza kupata uzito hasa baada ya tamko la wazi lililodai kwamba Idara ya Usalama wa Taifa ilikuwa na mpango wa kumuua.
Sijui nchi yetu imefika mahali gani kiasi naibu waziri na mbunge anaituhumu taasisi muhimu na nyeti ya dola kuwa ina njama za kuondoa uhai wake lakini wahusika waliipuzia. Lakini kama nilivyobainisha hapo awali kuwa, masuala mengi yenye kugusa hisia za umma yamekuwa yakimalizwa kienyeji, hazikufanyika jitihada zozote aidha kukanusha madai hayo ya Mwakyembe wala hatua madhubuti za kuyachunguza.
Mwananchi wa kawaida anaweza kujiuliza, “Hivi kama mashushushu wanaweza kupanga njama za kumuua kiongozi wa kitaifa anayetoka chama tawala CCM; je, hali ikoje kwa viongozi wa vyama vya upinzani? Na je, kama usalama wa vigogo unatishiwa na chombo kinachopaswa kulinda usalama wa nchi, hivi kuna usalama kweli kwa walalahoi?”
Pengine suala hilo lilipuuzwa kwa matarajio lingekufa kifo cha asili na kusahaulika akilini mwa Watanzania. Hali ya Mwakyembe ikazidi kuwa mbaya na swahiba wake, Waziri Sitta, akapita huku na kule kuukumbusha umma kuwa mafisadi wakishirikiana na vyombo vya dola ndio waliomdhuru naibu waziri huyo ambaye pia ni mbunge wa Kyela (CCM).
Kama mchezo wa kuigiza vile, Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha, akaingizwa kwenye sakata hilo pale alipomtaka Waziri Sitta kuwasilisha ushahidi wa madai yake kuwa Mwakyembe amenyweshwa sumu.
Lakini katika kile kinachoweza kuashiria kuwa nchi yetu inaendeshwa kwa mtindo wa ‘bora liende,’ Nahodha pia alidai kuwa hajawahi kusikia suala hilo (japo yeye ndiye mwenye dhamana ya jeshi la polisi na usalama wa raia), na kuwataka waandishi wa habari wamuulize Sitta aliyetoa tuhuma hizo.
Hatimaye Sitta naye akamjibu Waziri mwenzake (Nahodha) kwa kubainisha kuwa hatapeleka ushahidi wa madai aliyotoa kuwa Mwakyembe alilishwa sumu kwa kuwa polisi tayari wanao ushahidi.
Awali, Nahodha alidai kuwa “...masuala yote yanayohusu uchunguzi hayawezi kuzungumzwa katika vyombo vya habari...ni mambo ambayo hufanyika kwa umakini mkubwa...” na hatimaye DCI Manumba akathibitisha kauli hiyo ya bosi wake (kufanya mambo kwa umakini) kwa kukurupuka na kudai Mwakyembe hajalishwa sumu. Pia, aliwataka wananchi kupuuza madai ya Sitta, akidai kuwa Jeshi la Polisi liliwasiliana na Wizara ya Afya ambayo ilithibitisha ilitoa taarifa kuwa Mwakyembe hakulishwa sumu.
Kauli hiyo ya Manumba ikawaibua Mwakyembe na Sitta ambao walishusha tuhuma nzito dhidi ya Manumba na Jeshi la Polisi kwa ujumla. Mwakyembe alikwenda mbali zaidi na kudai jeshi hilo lilimtuma ‘askari mtuhumiwa wa dawa za kulevya na ujambazi’ kufuatilia taarifa za (Mwakyembe) kutishiwa maisha yake.
Katika kile kinachoashiria kuwa ‘sinema’ hii inaweza kuendelea kwa muda mrefu, muda mfupi kabla sijaandika makala hii Waziri wa Afya, Dk. Hadji Mponda, ameikana kauli ya Manumba kuwa wizara hiyo ilitoa uthibitisho kwa polisi kuwa, Mwakyembe hajalishwa sumu.
Ni vigumu kuwasilisha sakata hili katika mtiririko unaoleta maana kwa sababu staili inayotumiwa na wahusika ni mithili ya ‘piga nikupige.’ Lakini kilicho wazi ni ombwe kubwa kabisa la uongozi kuanzia kwa Rais Jakaya Kikwete mwenyewe.
Kwa vyovyote vile Kikwete anashuhudia mtifuano huu unaoweza kabisa kupoteza imani ya wananchi kwa Serikali yake na taasisi kama Jeshi la Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa, lakini amekaa kimya kana kwamba mambo hayo yanatokea Somalia na si Tanzania anayoiongoza.
Yeye ndiye aliyewateua Mwakyembe na Sitta, japo uteuzi huo ulionekana na baadhi ya wachambuzi wa siasa za nchi yetu kama mbinu ya ‘kuwadhibiti wanasiasa hao wanaotajwa kuwa ni makamanda wa vita dhidi ya ufisadi.’ Wanaodai hivyo wanapigia mstari kanuni ya uwajibikaji wa pamoja ambayo kama inazingatiwa, haitarajiwi mawaziri wanaotumikia ‘kabineti’ moja kupingana hadharani.
Kama Mwakyembe aliituhumu Idara ya Usalama wa Taifa kuwa ilikuwa na njama za kumuua, na kimsingi kiongozi mkuu wa taasisi hiyo nyeti (sponsor) ni Rais mwenyewe, hiyo inaweza kuzaa tafsiri kuwa Rais ni sehemu ya njama hizo. Kwa hiyo ni wazi kwamba laiti umakini ungetumika tangu mwanzoni mwa sakata hii, Rais Kikwete angeweza kuchukua hatua za aidha kumwajibisha Mwakyembe (kwa vile haiwezekani waziri anayeituhumu taasisi inayoongozwa na Rais kufanya kazi kwa ufanisi na Rais huyo) au kuitisha uchunguzi wa kina wa ili suala hilo kupatiwa majibu sahihi na hatimaye kulimaliza kabisa.
Lakini kwa upande mwingine, ninashindwa kabisa kuwaelewa Mwakyembe na Sitta. Japo ninaguswa na maradhi yanayomsibu Mwakyembe lakini sielewi kwa nini yeye na Sitta wanaendelea kuitumikia Serikali ambayo kimsingi wanaituhumu kuhusika na suala hilo la kulishwa sumu. Idara ya Usalama na Jeshi la Polisi si tu ni taasisi muhimu za Serikali bali pia zote zipo chini ya Rais ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu.
Na kama Mwakyembe alikuwa na uhakika kwamba Idara ya Usalama ina mpango wa kumuua kwa nini hakumwomba Rais aingilie kati, hasa baada ya kubaini (kwa mujibu wa maelezo yake) kuwa Jeshi la Polisi lilikuwa linachukulia tuhuma zake kama mzaha?
Kwa upande wa Idara ya Usalama wa Taifa, ninaamini ukimya wao unachangia kulikuza suala hili. Tuhuma kutoka kwa naibu waziri kuwa taasisi hiyo ina njama za kumuua si ndogo. Sasa kama walidiriki kukana madai yaliyowahi kutolewa na aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya CHADEMA, Dk. Willbrod Slaa kuwa Idara hiyo ilishiriki kumhujumu katika Uchaguzi Mkuu uliopita, kwa nini ikalie kimya tuhuma kuwa inataka kumuua kiongozi asiye na hatia?
Ikumbukwe kuwa kuna nyakati taasisi za intelijensia katika nchi mbalimbali hulazimika ‘kummaliza mlengwa’ (termination) alimradi kufanya hivyo ni kwa maslahi ya nchi. Hilo lipo ndani ya mamlaka wanayokabidhiwa na taifa husika. Naomba ieleweke kuwa hapa simaanishi kuwa Idara yetu ya Usalama wa Taifa nayo inajihusisha na vitendo vya aina hiyo, lakini kwa vile mbinu hiyo ‘inakubalika katika mazingira ya utendaji kazi wa taasisi za aina hiyo,’ kunyamazia tuhuma za Mwakyembe kunaweza kusababisha hisia kuwa ni za kweli.
Jeshi la Polisi nalo lina maswali kadhaa ya kujibu. Kwanza, lini watatoa matokeo ya uchunguzi wao kuhusu tuhuma za Mwakyembe kuwa Idara ya Usalama ilikuwa na njama za kumuua? Pili, kama jeshi hilo limeshatamka bayana kuwa wananchi wapuuze madai ya Waziri Sitta kuwa Mwakyembe amelishwa sumu, kwa nini halijamchukulia hatua ‘kwa kutoa tuhuma nzito kama hizo’? Na tatu, DCI Manumba alipata taarifa kutoka ‘Wizara ya Afya ya nchi gani kuwa Mwakyembe hajalishwa sumu’ (kwani Waziri Mponda ameshang’aka wizara yake kuhusika na hilo)?
Nimalizie makala hii kwa kutoa hadhari kwamba hiki kinachoonekana kama ‘mchezo wa kuigiza’ kinaweza kuwa na madhara makubwa huko mbele.
Wanaozembea kwa kukaa kimya kwa matarajio kuwa suala hili litapotea tu kama masuala ya Kagoda, Meremeta na Tangold wanajidanganya na hatma yake inaweza kuwa mbaya na isiyoweza kurekebishika.
0 comments:
Post a Comment