Mkulo ‘amgomea’ Spika kujibu swali bungeni |
Tuesday, 31 January 2012 22:07 |
Habel Chidawali, Dodoma WAZIRI wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo jana ‘alimgomea’ Spika wa Bunge, Anne Makinda kujibu swali lililomtaka aeleze kama chenji iliyorejeshwa na Uingereza kutoka kwenye ununuzi ya rada, ingetumika kununua madawati kwa ajili ya wanafunzi shuleni. Hata hivyo, baadaye Mkulo alisema hakufanya hivyo makusudi, bali alikuwa hajasikia akiitwa na Spika kujibu swali hilo na kuahidi kuwa makini zaidi katika siku zijazo. Ilikuwa kichekesho bungeni baada ya Spika kumwita Waziri Mkulo kwa takriban mara nne, akimtaka ajibu swali hilo lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Martha Mlata lakini hakusimama kujibu. Kitendo hicho kiliwafanya baadhi ya wabunge waduwae huku waziri huyo akiendelea kuwa kimya. Tukio hilo lilitokea baada ya Mlata kuuliza swali hilo la nyongeza lililotokana na swali na msingi ambalo liliulizwa na Mbunge wa Musoma Mjini (Chadema), Vicent Nyerere. Katika swali hilo, Mlata alitaka kujua namna Serikali ilivyojipanga katika matumizi ya fedha hizo za rada na kama kuna mpango wowote wa kuzitumika katika kupunguza tatizo la uhaba wa madawati shuleni. Swali la msingi la Nyerere lilijibiwa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Elimu), Kassim Majaliwa. “Swali hilo naomba Waziri wa fedha ujibu, waziri tafadhali jibu swali hilo. Waziri wa Fedha… namtaka waziri ajibu si yupo?” alisema Spika Makinda lakini, Mkulo hakusimama. Makinda alisisitiza: “ Hilo swali anatakiwa kujibu waziri mwenyewe na asijibu naibu wake. Jamani Waziri wa Fedha hayupo? Vipi mbona kimya kuna nini? Haya endelea naibu waziri.’’ Wakati wote ambao Spika Makinda alikuwa akimtaka Mkulo kusimama na kutoa majibu, waziri huyo alikuwa akiteta jambo na Waziri wa Tamisemi, George Mkuchika ambaye alisimama pia kutaka kutoa majibu lakini, Makinda alimzuia awali kabla ya kumruhusu kutolea ufafanuzi jambo hilo. Baada ya kuona hali hiyo, Majaliwa alilazimika kusimama na kusogelea kipaza sauti na kulieleza Bunge kuwa zaidi ya Sh18 bilioni zitapelekwa huko kwa ajili ya kununulia madawati. Alipotafutwa baadaye na gazeti hili ili aeleze kwa nini hakutii amri ya Spika ya kusimama na kujibu swali hilo, Mkulo alisema: “Sikumsikia na kwa kuwa maswali yanaulizwa bungeni basi subiri kesho (leo) nitajibu ili irekodiwe.” Makinda alishawahi kutangaza bungeni kuwa Mawaziri wanatakiwa kuwa makini kwa kila swali au jibu linalotolewa ndani ya ukumbi kwani wakati wowote anaweza kumtaka yeyote kujibu swali au kutoa ufafanuzi. Serikali ya Uingereza ilikubali kuilipa Tanzania Pauni 29.5 milioni wastani wa Sh75bilioni, ambazo zilizidi katika biashara ya rada kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya BAE Systems. BAE Systems ilikiri mahakamani kwamba pamoja na kupoteza kumbukumbu, lakini rada hiyo iliuzwa kwa bei kubwa ikilinganishwa na thamani halisi. Fedha hizo ziliwahi kuibua mvutano kati ya Serikali ya Tanzania na Uingereza, baada ya kutaka fedha hizo zipelekwe kwa asasi za zisizo za kiserikali nchini. Baadaye Uingereza ilikubali kuzikabidhi fedha hizo zifikie mikononi mwa Serikali ya Tanzania na kuelekezwa katika sekta ya elimu, ikiwa ni pamoja na kununulia vitabu na vifaa vingine ikiwemo madawati. Sakata hilo la rada bado linaendelea kuitikisa nchi baada ya uchunguzi wa Taasisi ya Makosa Makubwa ya Jinai ya Uingereza (SFO), kuchunguza baadhi ya vigogo wa Serikali ya Awamu ya Tatu akiwemo aliyekuwa Mwanasheria Mkuu, Andrew Chenge ambaye anadaiwa kukutwa na kiasi cha Dola za Marekani 1.2 milioni katika Kisiwa cha Jersey. CHANZO: Mwananchi |
0 comments:
Post a Comment