Familia ya JK yamkana aliyetoweka na mamilioni UVCCM |
Monday, 20 February 2012 07:38 |
FAMILIA ya Rais Jakaya Kikwete imekana kuwa na nasaba na aliyekuwa Katibu wa Jumuiya ya Umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), wilayani Simanjiro, Alhaj Omar Yufus Kariaki, anayetuhumiwa kutokomea na zaidi Sh26 milioni, mali ya jumuiya hiyo. Dada wa Rais Kikwete aliyehudhuria harambee ya kuchangisha fedha hizo kwa mwaliko wa Alhaj Kariaki, Tausi Kikwete aliliambia gazeti hili mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa kitendo cha kijana huyo kujinasibu kuwa na undugu na familia yao, kililenga katika kujinufaisha isivyo halali. “Ukweli ni kwamba kijana huyo siyo ndugu yetu hata kwa mbali. Kwanza yeye anatoka Kondoa, wapi na wapi na sisi Wakwere wa Bagamoyo, mkoani Pwani, Hatumfahamu kabisa kwenye ukoo wetu zaidi ya kufahamiana naye tulipokutana Hija,” alisema Tausi. Alisema yeye na ndugu yake Mwanaisha Kikwete, walikutana na mtuhumiwa walipokwenda kuhiji Mecca, Saudi Arabia na baadaye kupeana mawasiliano yaliyowawezesha kuendelea kuwa karibu hata baada ya kurejea nchini. Alisema baada ya kurejea, yeye na Mwanaisha waliendelea kuwasiliana na Alhaj Kariaki aliyeonyesha kuwa kijana mwenye upendo na busara zilizowavutia wao kutembelea nyumbani kwao, Kondoa kwa mwaliko wake. “Ukaribu wetu ulifikia hatua ya sisi kutembelea nyumbani kwao Kondoa baada ya yeye kutualika. Lakini ukweli unabaki pale pale kwamba kijana huyo si ndugu yetu wala hana nasaba yoyote na kina Kikwete.” alisisitiza Tausi. Alisema ilipofika wakati wa harambee ya kutunisha Mfuko wa Mradi wa Maendeleo ya Vijana wa Wilaya ya Simanjiro, kijana huyo akiwa Katibu wa UVCCM wilayani humo, aliwaalika yeye na Mwanaisha kwenda kutoa semina kwa vijana kuhusu mbinu za ujasiriamali na miradi midogo. Kwa mujibu wa Tausi, semina hiyo ilifanyika katika ukumbi wa mikutano ya Hoteli ya Manyara Inn, iliyoko Mererani siku mbili kabla ya harambee iliyoongozwa na aliyekuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Shamsi Vuai Nahodha, ambaye sasa ni Waziri wa Mambo ya Ndani katika Serikali ya Muungano. Hata hivyo kauli hiyo ya Tausi inapinga na kauli yake ya awali kupitia simu mwaka jana, ambapo licha ya kukiri kumfahamu Alhaj Kariaki, pia alisema wana unasaba naye. “Ni kweli mimi na Mwanaisha ni dada wa mheshimiwa Rais (Kikwete) pia ni ndugu wa karibu wa kijana huyo (Alhaj Kariaki). Lakini binafsi sina mawasiliano naye tangu awe diwani huko kwako Kondoa. Kwa kifupi sijawasiliana naye tangu tuachane Mererani,” alisema Tausi mwaka jana alipoulizwa kuhusu mtuhumiwa huyo. Katika harambee hiyo iliyohudhuriwa na viongozi na watu kadhaa maarufu kutoka Mikoa ya Manyara na Arusha, Nahodha alichangia Sh2 milioni fedha taslimu wakati aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara Henry Shekifu akichangia 500,000. Kwa sasa Shekifu ni Mbunge wa Lushoto. Mwenyekiti wa UVCCM wa Wilaya ya Simanjiro, Kiria Laizer, alisema baada ya yeye kukabidhiwa mfuko wenye fedha mara baada ya harambee ambayo mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka naye alichangia Sh1.5 milioni, alikabidhi mfuko huo kwa katibu wake Alhaj Kariaki ambaye hadi juzi alipojitokeza baada ya gazeti hili kuripoti suala hilo. Mwenyekiti huyo aliwataja wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya UVCCM wilaya walioshuhudia makabidhiano kati yake na katibu wake kuwa ni Bonny Shongo na Paul Sipitet. Laizer aliyetoa pongezi na shukrani kwa mwandishi na gazeti la Mwananchi kwa kufanikisha mtuhumiwa kujitokeza, alisema awali walikuwa wakihofia kufuatilia suala hilo kwa karibu kwa hofu kwamba mtuhumiwa ana undugu na familia ya Rais. Alhaj Kariaki ambaye sasa ni Diwani wa Kata ya Kwa Delo wilayani Kondoa, aliibuka wiki iliyopita baada ya habari zake kuripotiwa katika gazeti hili. Alikiri kutokabidhi fedha zilizopatikana kwenye harambee hiyo iliyofanyika Mei 9 mwaka juzi akidai sehemu ya fedha hizo amezitunza kwenye akaunti yake, akisubiri kumalizika kwa kile alichodai kuwa mgogoro baina ya viongozi wa CCM mkoani Arusha ili azikabidhi CHANZO: Mwananchi |
0 comments:
Post a Comment