Wawakilishi Zanzibar wachachamaa kuambiwa hakuna mafuta
Salma Said, Zanzibar
KAULI ya Mtaalamu kutoka Scotland, David Reading, kwamba kuna uwezekano mdogo wa kupata mafuta na gesi asilia katika visiwa vya Unguja na Pemba imewakera mawaziri na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na kumta aifute.
Lakini mtaalamu huyo alisisitiza kwamba yeye akiwa mshauri ni lazima awaeleze ukweli wa mambo, kwani hata makampuni yaliofanya utafiti siku za nyuma kuhusu mafuta walitoa ripoti ambayo haikueleza uhakika wa kuwepo kwa nishati hiyo.
Reading pia alisema kuwa gharama za utafutaji wa mafuta hayo ambayo hayana uhakika ni kubwa mno.
Mtaalamu huyo alikuwa akizungumza katika semina ya siku moja kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi iliyofanyika jana mjini Ugunja.
Reading alisema katika sehemu nyingi zilizogunduliwa mafuta au kuwepo kwa fununu za kuwapo kwa nishati hiyo, gharama yake ilikuwa ni kubwa ambapo ililazimu makampuni kusitisha kazi kwa sababu hiyo.
Matamshi hayo yalionekana kuwachukiza zaidi wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ambapo walimtaka mtaalamu huyo kufuta matamshi yake kwa maelezo kuwa tafiti nyingi zilizofanywa katika miaka ya mwanzoni mwa 1950 zilionesha kuwa yapo mafuta ya kutosha ya kibiashara Zanzibar.
Hoja hiyo iliibua hisia za wajumbe hao za siku nyingi na waalipopata nafasi ya kuchangia, walisema kuwa mafuta ya Zanzibar ni kwa Wazanzibari na kamwe yasifanywe kuwa ya Muungano na kusisitiza msimamo wa kutaka kuondolewa kwa sheria inayoelezea kuwa mafuta na gesi asilia kuwamo katika orodha ya mambo ya Muungano.
Wajumbe hao walisema kuwa huenda suala hilo la mafuta linaweza kusababisha machafuko visiwani, kwani uozefu unaonyesha kwamba nchi nyingi zenye mafuta kuzuka mapigano, hivyo wakashauri suala hilo lisiwe chanzo cha machafuko kwa Wazanzibari.
Waziri wa Utalii, Biashara na Uwekezaji, Samia Suluhu Hassan, alionekana kushangazwa na taarifa za Mshauri Mwelekezi na kuhoji: “Kama uwezekano wa kupatikana mafuta Zanzibar ni mdogo kwa nini serikali ya Muungano ilikataa wazo la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwenye kamati ya Waziri Mkuu na Waziri Kiongozi katika kugawana mapato ya mafuta?”
Hata hivyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Kiongozi, Hamza Hassan Juma, aliwataka wananchi kuipuuza kauli hiyo ya Mshauri Mwelekezi na kuongeza kuwa ikiwa mafuta hayataondolewa katika orodha ya mambo ya Muungano hatajutia kuona Muungano unayumba.
“Kuna msemo wa kihindi…ipasuke ngoma au ichanike lakini tujue moja kuwa mafuta ya Zanzibar ni kwa Wazanzibari na sio ya Muungano,” alisisitiza waziri huyo.
Kiongozi wa Upinzani katika Baraza la Wawakilishi, Abubakar Khamis Bakari kama walivyo wajumbe wengine waliochangia alisema mafuta yasiwe mambo ya Muungano kwani hata kuingizwa kwake haukufuatwa utaratibu unaofaa.
Mwakilishi wa Jimbo la Gando, Said Ali Mbarouk alisema kwamba Wazanzibari wamezoea kukosa, hivyo haitokuwa jambo la kushangaza ikiwa hakutakuwa na mafuta wakati jambo hilo litakapoondolewa katika orodha ya Muungano, kwani hivi sasa hainufaiki na lolote katika suala la gesi asilia.
Waziri Kiongozi Shamsi Vuai Nahodha akifungua semina hiyo aliwasihi wajumbe hao kutumia busara katika kumpa ushauri mtaalamu huyo ili aweze kupata maoni mwafaka na aweze kuzishauri serikali mbili namna bora ya kugawana mapato yatokanayo na utafutaji na ushimbaji wa mafuta.
Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi, Ali Mzee Ali alisema Wazanzibari wanapochangia kwa ajili ya kutetea nchi yao wasionekane kama ni wasaliti au wana nia ya kugombea urais bali wanatelekeza ahadi yao kwa wananchi ya kuwatetea katika baraza hilo.
Akifunga semina hiyo Waziri wa Maji, Ujenzi Nishati na Ardhi, Mansoor Yussuf Himid aliungana na wajumbe wengine wote kwa kutaka kuwa mafuta yaondolewe katika orodha ya Muungano kwani tokea asili hayakuwa hivyo.
Na leo tena,gazeti hilo linaripoti vituko zaidi vya Wazenji
Mafuta Zanzibar: Hata kidogo katika kinibu tutagawana na mengine kujipaka
Na Salma Said, Zanzibar
Wawakilishi wa Zanzibar wamesema "hata kama ujazo wa mafuta yanayoweza kupatikana Zanzibar ni sawa na glasi ndogo ya kupimia pombe (kinibu), mafuta hayo ni mali ya Wazanzibari watagawana ili watakaoweza wajipake mwilini".
Kauli hiyo ilitolewa jana baada ya mshauri, David Reading, kueleza kuwa mafuta yanayowezekana kupatikana kisiwani humo ni kidogo na kupatikana kwake ni kwa gharama kubwa.
Mtaalamu huyo kutoka Uingereza aliitwa kwa ajili ya kuishauri Serikali ya Mapinduzi (SMZ) na serikali ya Muungano namna bora ya kugawana rasilimali itokanayo na gesi na mafuta.
Kauli hiyo ya Reading pia imesababisha wawakilishi kuingiwa na chuki dhidi ya Wazanzibari walio kwenye serikali ya Muungano, wakiwaita kuwa ni vigeugeu mithili ya vinyonga na wasiojali maslahi ya Wazanzibari.
Akitoa maoni yake kuhusu suala la mafuta na gesi asilia kwa mshauri huyo mwelekezi, mwakilishi kutoka Chama cha Wananchi (CUF), Najma Khalfan Juma alisema kuwa hata kama mafuta ya Zanzibar yatakuwa madogo kiasi cha ujazo wa glasi ndogo ya kupimia pombe ya haramu ya gongo (kinibu), Wazanzibari watagawana hata ikiwa kwa ajili ya kujipaka mwilini.
"Hata kama watajipaka mwilini au wengine watatumia kama dawa ya kuchulia misuli, itakuwa bora zaidi kuliko suala la mafuta kuwa la Muungano," alisema.
Naye mwakilishi wa kuteuliwa na rais, Ali Mzee Ali, ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi, alisukumia shutuma zake kwa mawaziri walio kwenye serikali ya Muungano ambao ni Wazanzibari, akiwaita kuwa ni wanafiki na wanaobadilika kama kinyonga.
“Mheshimiwa mwenyekiti kuna wenzetu ambao wamo katika serikali ya Muungano. Wakija hapa (Zanzibar) wanajifanya ni watetezi sana wa Zanzibar, lakini kumbe ni wanafiki,” alilalamika mwakilishi huyo.
"Tabia ya viongozi hao haiwanufaishi Wazanzibari. Viongozi wa Zanzibar wasiwatilie maanani watu wa aina hiyo kwa kuwa wanatanguliza maslahi binafsi.
Baadaye mwakilishi huyo mteule aligeukia vyombo vya habari vya Zanzibar na kusema:
"Kitu cha kushangaza ni gazeti la Asumini ambalo limesajiliwa hapa Zanzibar. Gazeti hili liliwahi kuandika makala ndefu kuelezea umuhimu wa nishati ya mafuta kuwa ya Muungano.
Jambo hili si sahihi kwani Zanzibar hainufaiki na lolote na mapato ya gesi inayozalishwa Tanzania Bara," alisema.
“Ninalo hapa, waheshimiwa wajumbe, gazeti la Zanzibar Leo ambalo limechapisha makala kama ile iliyotolewa katika gazeti la Asumini. Sijui makala hii imepenya vipi mpaka ikatolewa humu; hilo anajua mheshimiwa (Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Ali Juma) Shamhuna.”
Gazeti la Asumini na Radio ya Zenj Fm zinamilikiwa na Kampuni ya Zanzibar Media Corporation, ambayo Mkurugenzi wake ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano, Muhammad Seif Khatib.
Mwakilishi huyo alisema mara nyingi wanaojitokeza kutetea maslahi ya Zanzibar wanaonekana wanafanya kampeni ya urais kwa mwaka 2010, huku wengine wakishambuliwa kwa maneno kuwa hawautaki Muungano ama kuwa na ajenda ya siri jambo ambalo anaamini si sahihi.
Ali Mzee aliwataka wananchi na hasa wajumbe wa baraza la wawakilishi kuungana kuwa kitu kimoja katika kutetea maslahi ya Zanzibar na kuachana na watu aliowaita kuwa 'Wazanzibari Maslahi' kwenye serikali ya Muungano.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Kiongozi, Hamza Hassan Juma aliwataka viongozi wa Zanzibar kutoogopa kufukuzwa serikalini kwa kuitetea Zanzibar kwani mara nyingi mtu anapojitokeza kutetea maslahi ya visiwa hivyo, huambiwa kuwa amechafua hali ya hewa kama ilivyokuwa kwa rais wa zamani wa Zanzibar na Makamu wa Kwanza wa Rais, Aboud Jumbe Mwinyi.
“Waheshimiwa tusiogope kunyang'anywa magari," alisema. "Wakitunyang'anya sawa, tutatembea hata kwa miguu lakini lazima tuitetea nchi yetu kwa sababu sisi tumeapa kwa katiba hii (katiba ya Zanzibar) na sio ya Jamhuri ya Muungano.”
Akichangia hoja hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais- Fedha na Uchumi, Dk. Mwinyihaji Makame alishabihiana na wenzake, akieleza kuwa katika suala la mafuta hakuna dhamira njema kwa Wazanzibari.
Mwakilishi wa Viti Maalumu (CUF), Zakia Omar Juma alisema umefika wakati sasa kwa Wazanzibari kujikomboa kiuchumi kwa kuungana kutetea mafuta yao kwani mara nyingi Zanzibar inapotaka kujikwamua kiuchumi huwekewa vikwazo na serikali ya Muungano.
Mwakilishi wa Jimbo la Ziwani (CUF), Rashid Seif alisema kwamba inaonekana Zanzibar kuna mafuta ya kutosha na ndio maana watu wa Tanzania Bara (Tanganyika) wanang'ang'ania suala la mafuta kuwa la Muungano licha ya kuwa Wazanzibari wenyewe hawataki.
0 comments:
Post a Comment