Tuesday, 23 September 2008













Kwa mujibu wa Mwananchi

Mahakama Kuu yaamru wafanyakazi NMB kurudi kazini mara moja
Na Kizitto Noya

JAJI wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi, Jaji Mfawidhi Ernest Mwipopo, jana alibatilisha mgomo wa wafanyakazi wa Benki ya NMB na kuwataka warejee kazini ndani ya muda wa saa tatu, uamuzi ambao umeridhiwa na wafanyakazi.

Wafanyakazi hao kutoka karibu matawi yote zaidi ya 120 nchini kote, waliamua kugoma kwa muda usiojulikana wakiishinikiza serikali kusaini makubaliano ya malipo ya mkupuo wa fedha ambazo walistahili kulipwa wakati benki hiyo ikichukuliwa na mwekezaji mpya, kutengewa asilimia tano ya hisa na pia fedha za mfuko wa kujikopesha.

Akitoa hukumu hiyo jana, Jaji Mwipopo alizitaka pande mbili zinazopingana kutoa matangazo kwenye vyombo vyote vya habari kuwajulisha wafanyakazi hao kuwa wanatakiwa kurejea kazini kuanzia saa 11:25 jioni jana hadi leo 2:00 asubuhi.

Katika hukumu hiyo iliyodumu kwa muda wa saa mbili kuandaliwa na kusomwa, Jaji Mwipopo alisema Mahakama imefikia uamuzi huo baada ya kuona upungufu katika hoja tatu za wafanyakazi hao walizozitoa kutetea mgomo wao.

Akichambua hoja moja baada ya nyingine, Jaji Mwipopo alisema aya ya kwanza na ya pili za notisi ya mgomo huo, zimeiingiza serikali katika mgogoro huo kwa kueleza kuwa imechangia kwa kugoma kusaini makubaliano yaliyofikiwa kati ya wafanyakazi wa NMB na uongozi wa benki hiyo.

"Aya hizo zinagongana na nafasi ya serikali kwenye madai ambayo ni msingi wa ugomvi," alisema. "Aya ya kwanza imeitaja serikali kuwa ndio iliyogoma kusaini makubaliano. Kutokana na hali hiyo kuna uwezekano kuwa mgogoro huo umeelekezwa kwa NMB kwa sababu ndio taasisi pekee mnayoweza kuigomea."

Alisema hoja ya pili inayofanya mahakama isiutambue mgomo huo na kuuita haramu na batili, ni muda wa kutolewa kwa nositi ya kuanza kwake.

Alifafanua kuwa, notisi hiyo ya saa 48 iliyotolewa Ijumaa ilimaanisha kuwa mgomo huo ulitakiwa uanze saa 10:45 Jumapili, muda ambao saa hizo 48 ulikuwa unaisha. Lakini badala yake wafanyakazi walianza mgomo huo saa 2:00 asubuhi Jumatatu.

Hali kadhalika jaji huyo alifahamisha kuwa mgomo huo ulipaswa kuanza jana na sio juzi endapo notisi yake ingetolewa kwa kutumia siku za kazi badala ya saa kwani sheria ya kazi, haitambui siku za Jumamosi na Jumapili kuwa ni siku za kazi.

"Hoja ya pili ni timing (muda), kama notisi hiyo ni ya saa 48 na ilipokewa Ijumaa saa 10:45 jioni, muda wake ungeisha saa 10:45 Jumapili. Kwa nini hamkugoma siku hiyo na mkaamua kusubiri hadi Jumatatu?" alihoji Jaji Mwipopo na kuongeza:

"Lakini ikumbukwe kwamba, sura ya kwanza ya Sheria ya Kazi... haitambui Jumamosi na Jumapili kuwa ni siku za kazi, hivyo kuhesabu siku hizo kuwa siku za kazi sio sahihi."

Kwa mujibu wa Jaji Mwipopo ni jukumu la mahakama kutafsiri notisi ya saa 48 inaisha lini, kwa kuwa sheria haikutoa tafsiri kuhusu notisi ya masaa hasa endapo notisi hiyo inatolewa mwishoni mwa juma.

Alisema hoja ya tatu iliyotumika kuwaamuru wafanyakazi hao warejee kazini ni udhaifu uliopo katika notisi ya mgomo huo iliyoeleza kuwa mgomo utaendelea kwa muda usiojulikana mpaka mwajiri atakaposaini makubaliano.

Alisema maelezo hayo sio sahihi kwani hayatoi fursa kwa mwajiri kujadili suala hilo na ingekuwa vema mgomo ungeeleza muda maalumu ili kumpa fursa hiyo mwajiri.

"Kutokana na mambo hayo, mahakama imetengua mgomo huo na kuutangaza kuwa ni haramu na batili hivyo hautakiwi kufuatwa. Kwa mujibu wa kifungu 84 cha sheria za ajira, naamuru ndani ya masaa matatu, kuanzia sasa, wafanyakazi wote warejee kazini," alisema Jaji Mwipopo na kuongeza:

"Nimeangalia kwa makini na kugundua udhaifu wa mambo matatu ambayo yanafanya mgomo huo uonekane batili na haramu, hivyo ninatoa amri na maagizo kuhusu suala hilo.

"Naamuru mfanyakazi ambaye hakuweza kuripoti kazini leo (jana) awe ameripoti kazini kwake kesho (leo) saa 2:00 asubuhi na naagiza uongozi wa NMB uwapokee wafanyakazi hao wote bila masharti na usiwape adhabu kwa kushiriki mgomo huo."

Saa chache baadaye, wafanyakazi waliokuwa wamekutana kwenye Ukumbi wa Msimbazi Centre, walitaarifiwa kuhusu uamuzi huo na baadaye kukubaliana kuwa wataripoti kazini leo kama ilivyoamriwa na mahakama hiyo, anaripoti Jackson Odoyo.

Baada ya Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwandani na Taasisi za Benki (Tuico), Boniphace Nkakatisi kuwaeleza uamuzi huo, waliweka msimamo kuwa wasingerejea kazini na kumpa kiongozi huyo wakati mgumu wa kuwaelewesha.

"Nina waomba mrudi kazini kwa moyo mkunjufu tena kwa kujituma kama awali na kutii amri ya mahakama wakati sisi tunarudi mezani kwa majadiliano zaidi," alisema Nkakatisi.

Hata hivyo, baada ya majadiliano ya muda mrefu wafanyakazi hao waliamua kukubaliana na uamuzi huo, lakini wakawaagiza viongozi wao wa Tuico kuhakikisha suala hilo linatatuliwa haraka iwezekanavyo ndani ya wiki moja vinginevyo watagoma tena.

Hukumu ya Jaji Mwipopo ilitolewa baada ya saa mbili na nusu ya mvutano mkali wa hoja za kupinga na kutetea mgomo huo baina ya mawakili wa NMB na wafanyakazi, huku Jaji Mwipopo akilazimika kuingilia kati kwa kuwahoji maswali mawakili hao kwa nyakati tofauti.

Hoja iliyoibua hisia kali kwa pande zote mbili ni ile iliyoanzishwa na upande wa mlalamikaji (NMB) kupitia wakili wake, Rason Mbwambo kwamba mgomo huo umeandaliwa kwa hila ili kumkomesha mwajiri.

Mbwambo aliieleza Mahakama kuwa, hila imejitokeza kutokana na notisi ya kuanza kwake kutolewa Ijumaa jioni na anaamini imefanywa hivyo ili kutompa fursa mwajiri kuuzuia.

Hata hivyo, wakili wa wafanyakazi hao, Amour Khamis alisema mwenye hila ni mwajiri (NMB) kwa kutaka viongozi wa wafanyakazi hao wapelekwe gerezani kama wafungwa wa madai ya kuandaa mgomo badala ya kutaka kuwe na mazungumzo ya kufikia mwafaka.

"Mwajiri ndiye mwenye hila kwani anaweza kueleza sababu gani hapa (mahakamani) ya kuomba viongozi hao wakamatwe, wafilisiwe mali zao na kufungwa kama wafungwa wa madai badala ya kutaka mazungumzo," alihoji wakili huyo.

Kabla ya mahojiano hayo, Wakili Mbwambo aliiomba mahakama itoe amri na maelekezo mwafaka kwa wafanyakazi hao ili kukabiliana na mgomo huo ambao sasa umefikia katika hatua mbaya.

Mbwambo alitaka wafanyakazi hao warejee kazini huku utaratibu mwingine wa kimahakama ukiendelea ili kunusuru hasara itakayopatikana kutokana na mgomo huo unaofanyika nchi nzima.

Hata hivyo, hoja ya Wakili Mbwambo ilipingwa na wakili wa wafanyakazi, Khamis aliyesema: "Mheshimiwa jaji, Mbwambo hakuwa mkweli na hataki kuwa muwazi. Kutaka wafanyakazi hao warejee kazini ni kuendeleza mgogoro. Njia mwafaka ni watu kukutana na kufikia mwafaka."

Kabla ya majibizano hayo, Jaji Mwipopo alitumia muda mwingi kuwauliza maswali mawakili hao na ifuatayo ni sehemu ya mahojiano yao:

Jaji: Kwa nini, msomi Khamis, mahakama isiamini kuwa mgomvi wa Tuico ni serikali iliyokataa kusaini mabaliano yenu na sio NMB?

Wakili Khamis: Ndio maana nilisema kuna haja ya sisi kupata muda wa kuwasilisha nyaraka zetu kwa maandishi kwani makubaliano yalihusu pande tatu, wafanyakazi, NMB na serikali. Kabla ya serikali, NMB ilitakiwa iwe imesaini kwanza.

Jaji: Baada ya kutoa notisi ya saa 48 Ijumaa saa 10:45 jioni, kwa nini msingegoma Jumapili siku ambayo notisi yenu iliisha badala yake mkachagua Jumatatu?

Wakili Khamis: Sheria inataka watu wagome baada ya notisi, na kwa mujibu wa sheria hiyo hakuna ubaya watu kugoma muda wowote baada ya muda wa notisi hiyo kumalizika.

Jaji: Kwa nini masaa hayo 48 hayakuwa ya siku za kazi na hivyo kuishia Jumatatu na mgomo mkaanza leo (jana)?

Wakili Khamis: Siku za kazi sio za tarehe za mwezi, ni siku ambazo wafanyakazi wa taasisi wanatakiwa kufanya kazi na kwa NMB ni siku zote kwani ATM zinafanya kazi masaa 24, hivyo ni sahihi kuhesabu Jumamosi na Jumapili kuwa ni siku za kazi kwa NMB.

Baada ya mahojiano na wakili wa wafanyakazi, Jaji Mwipopo alimgeukia wakili wa NMB na sehemu ya mahojiano yao ni kama ifuatavyo:

Jaji: Kwa nini nyie (NMB) msionekane pia kuwa mna hila na mnashirikiana na wafanyakazi hao kuishinikiza serikali isaini makubaliano kwa kutotoa taarifa mapema kwamba Jumatatu mgomo unaanza?

Wakili Mbwambo: Tunashukuru kwamba unatukumbusha uwezekano wa kuwasiliana na ofisi yako hata siku za mwisho wa juma, lakini katika hali ya kawaida isingeweza kuwaza kwamba tungeweza kukupata siku hiyo.

Jaji: Kwa nini mnaomba viongozi hawa wakamatwe, wafilisiwe na wafungwe kama wafungwa wa madai badala ya kuomba mahakama izuie mgomo?

Wakili Mbwambo: Hili ni ombi moja tu, kumbuka pia tumeiomba mahakama ichukue hatua nyingine yoyote inayoona inafaa kunusuru hali hiyo.

Baada ya maswali na majibu hayo yaliyodumu kwa takriban saa 1:30 Jaji Mwipopo alisema: "Kuhusu maombi ya NMB kwamba viongozi wakuu wanne wasikilizwe leo na amri itolewe ya kukamatwa, kufilisiwa na kufungwa kama wafungwa wa madai, natoa amri kwamba mahakama imewapa muda ili waweze kujitetea kwa maandishi na vielelezo na kuwasilisha pingamizi la kiapo kesho, (leo) kesho kutwa wampe nakala ya hati hiyo wakili wa mwajiri na Septemba 26 tukutane hapo saa 4:00 asubuhi kuendelea na shauri hili."

Naye Boniface Meena anaripoti kuwa, menejimenti ya Benki ya NMB, imewataka wafanyakazi wote wa benki hiyo waliogoma kurejea kazini leo kama amri ya mahakama ilivyowataka.

Mkurugenzi Mkuu wa NMB, Ben Christiaanse alisema anategemea wafanyakazi hao watafika ofisini kwani serikali inayafanyia kazi madai yao.

Alisema si vizuri kwa wafanyakazi kugomea menejimenti ya benki kwa kuwa wafanyakazi hawaidai benki, bali serikali.

"Ninaamini kuwa, watafika ofisini kama kawaida na sidhani kama nitachukua hatua zozote za kisheria dhidi yao kutokana na mgomo uliotokea," alisema Christiaanse.


0 comments:

Post a Comment

Categories

Unordered List

Sample Text

Blog Archive

Labels

Follow Us on FaceBook

Popular Posts

Recent Posts

Recent Comments

Recent Premium Themes

Your Links

Flickr

Powered by Blogger.

Blog Archive

Followers

Download

Your Links

Blogger Tricks

Popular Posts

Recent Posts

Text Widget